STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, April 7, 2012

MAMIA WAFURIKA MSIBA WA STEVEN KANUMBA

MEYA wa Manispaa ya Kinondoni na Ilala, Yusuf Mwenda na Jerry Slaa ni miongoni
mwa viongozi waliojitokeza kwenye msiba wa nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba aliyefariki juzi usiku nyumbani kwake baada ya kuanguka katika mzozo na mpenzi wake.
Aidha umati mkubwa ulijitokeza kwenye msiba wa msanii huu uliopo nyumbani kwake
Sinza Vatican, jana ulisababisha msongamano mkubwa kiasi cha kuziba barabara ya
Makanya na kuwalazimisha askari polisi kufanya kazi ya ziada kuweka mambo sawa.
MiCHARAZO lililokuwepo msibani hapo, liliwashuhudia mameya hao na viongozi wengine kama Katibu wa Kamati ya Uchumi na Fedha CCM-Taifa, Mwigulu Nchemba na Diwani wa Kata ya Sinza, Renatus Pamba wakiwa na nyuso za huzuni wakitoa pole zao.
Viongozi hao kila mmoja alikuwa akiwapa pole wasanii waliofanya kazi na Kanumba
pamoja na watu wengine kabla ya baadhi yao kuondoka na kuwaacha mamia ya watu
wakiwemo wasanii nyota wa filamu wakiendelea na msiba huo.
Kutokana na wingi wa watu waliojitokeza kwenye msiba huo, iliwalazimisha waratibu wa msiba huo, kuwahamishi waombelezaji hao kwenye ukumbi wa Vatican Hoteli, huku wakiwazuia wengine kuingia ndani na kuleta tafrani za hapa na pale.
Mratibu wa Bongo Movie, Steven Mengele 'Steve Nyerere' alisema waliamua kuhamishia watu hotelini hapo kutokana eneo la nyumba ya marehemu Kanumba kutotosha kwa wingi wa waombolezaji waliojitokeza waliosababisha msongamano mkubwa.
Msongamano huo wa waombelezaji ulisababisha hata magari yanayotumia barabara ya
Makanya kushindwa kupita vema na kuwapa kazi ya ziada askari polisi wa kawaida na
wale wa barabarani kuyaongoza magari hayo.
Wasanii mbalimbali walikielezea kifo cha Kanumba kama pengo litakalochukua muda
mrefu kuziba katika tasnia ya sanaa hasa uigizaji wa filamu ambayo marehemu aliifanya kwa muda mrefu wa maisha yake tangu akiwa shuleni.
Mayasa Mrisho anayefanya kazi nyingi na Kanumba, alisema mpaka sasa haamini kama
Kanumba kafariki kwa namna kifo chake kilivyokuwa cha ghafla.
'Siamini, kama ni kweli Kanumba kafa," alisema huku akilia. Aliongeza Kanumba
amefariki wakati wakitoka kumalizia kazi yao mpya iitwayo 'Mr Price', huku pia
wakijiandaa kuingiza sokoni filamu yao mpya iitwayo 'Ndoa Yangu'.
Wasanii wengine kama Patcho Mwamba, Rajabu Jumanne 'Chilli', Issa Kipemba, Fatuma Makongoro 'Bi Mwenda' walisema itawachukua muda mrefu kumsahau mwenzao ambaye alikuwa mtu wa watu, asiye na makuu licha ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao.
Nalo Baraza la Sanaa la Taifa, kupitia Katibu Mkuu wake, Ghonce Materego, walitoa
salamu za rambirambi kutokana na kifo hicho cha Kanumba wakidai kimeshtua na
kuwaachia pengo kubwa katika fani ya sanaa nchini.
"BASATA inaungana na familia za wafiwa na wasanii wote nchini kwa maombolezo ya msiba huu mkubwa na wa kihistoria. Kufiwa na msanii huyu mahiri kwenye tasnia ya filamu ni pengo kubwa kwa familia, Sekta ya sanaa na Taifa kwa ujumla kutokana na
ukweli kuwa, aliweza kuutangaza utamaduni na sanaa yetu nje ya mipaka," sehemu ya
rambirambi hiyo ya Basata inasomeka hivyo.
Steven Charles Kanumba, aliyezaliwa Januari 8, 1984 huko Shinyanga, alifariki usiku wa kuamkia jana kwa kile kinachoelezwa alisukumwa na kuanguka sakafuni na aliyekuwa
mpenzi wake, Elizabeth Michael 'Lulu' ambaye kwa sasa anashikiliwa na jeshi la Polisi.
Msanii huyo, aliyesoma Shule ya Msingi Bugoyi na Shule za Sekondari Mwadui, Dar
Christian Seminary na Jitegemee kabla ya kuanza kutamba kwenye sanaa kupitia kundi la Sanaa alilojiunga nalo mwaka 2002 hadi 2006 alipojiengua na kucheza filamu mbalimbali.
Baadhi ya kazi zake ni 'She is My Sister', 'Dar to Lagos', 'Cross My Sin', 'The Director', 'Hero of the Church', Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Dar to Lagos, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears, Unfortunutes Love, My Valentine, The Shock, Deception na kazi ya mwisho kuitoa sokoni ni 'Kijiji Chatambua Haki'.

mwisho

SIMBA YATAKATA AFRIKA, LICHA YA KIPIGO YAFUZU 16 BORA KOMBE LA SHIRIKISHO
ANGURUMAPO SIMBA MCHEZA NANI? HAKUNAGA! Ndivyo tunavyoweza kusema baada ya klabu ya soka ya Simba kupenya kwenye hatua ya 16 Bora ya KOmbe la Shirikisho Afrika, licha ya kipigo cha mabao 3-1 ilichopewa usiku wa kuamkia leo na Entente Sportive de Setif ya Algeria.
Ikicheza wachezaji 10, Simba iliweza kupigana hadi dakika za nyongeza kupata bao pekee la kufutia machozi lililokuwa na faida kubwa kwao, kuwavusha hatua hiyo wakiwaduwaza waarabu wasiamini kilichowakuta baada ya kuamini wamemng'oa mnyama.
Shujaa wa Simba katika pambano hilo lililochezeshwa na waamuzi kutoka Tunisia alikuwa ni Mganda, Emmanuel Okwi aliyefunga katrika dakika ya 92 na kuifanya timu yake isonge mbele kwa faida ya bao la ugenini kutokana na matokeo ya jumla kuwa mabao 3-3.
Simba katika pambano lao la awali lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Machi 25, ilishinda mabao 2-0 na hivyo kwa sare hiyo wamevuka kwa matokeo ya kuwa mabao 4-3.
Beki wa kutumainiwa wa Simba Juma Said Nyosso alitolewa uwanjani mapema baada ya kulimwa kadi nyekundu kwa kuonyesha ubabe uwanjani dhidi ya mshambuliaji wa Setif.
Wenyeji walitumia mwanya wa kutolewa kwa Nyosso kupachika bao la kuongoza lililofungwa dakika ya 34 na Mohammed Aoudia na kurejea kipindi cha pili kwa kasi kwa kufunga bao jingine kupitia mshambuliaji huyo mkali.
Bao la tatu la Setif, iliyokuwa ikiyotawala vipindi vyote viwili, ingawa juhudi zao za kuvuna mabao mengi zilizimwa na kipa Juma Kaseka, lilifungwa katika dakika ya 52 kupitia kwa Mokhtar Benmoussa.
Baada ya kupata mabao hayo Setif ilirejea nyuma na kulinda bao wakiamini wameshamaliza kazi kabla ya Okwi kuwaduwaza baada ya kuwachambua mabeki wa timu hiyo kisha kufumua shuti kali la mbali lililomshinda nguvu kipa wa Setif na kutinga wavuni.
Kwa ushindi huo, Simba sasa itakutana na mshindi kati ya Ferroviário Maputo ya Msumbiji au Al Ahly Shendi ya Sudan ambazo zinatarajiwa kuumana kesho Jumapili, huku timu ya Sudan ikiwa na faida ya bao moja iliyopata katika mechi yao wiki mbili zilizopita ilipowafunga wenyeji wao bao 1-0.
Katika mchezo wa jana kikosi cha Simba kilichoaanza dhidi ya ES Setif kiliwakilishwa na Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah/Said Nassoro 'Chollo' , Juma Nyoso, Kelvin Yondani, Patrick Mafisango, Salum Machaku, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi 'Boban' na Emmanuel Okwi.

PICHA ZA BAADHI YA KAZI YA NDOA YANGU, MOJA YA FILAMU ZA MWISHO ZA KANUMBA INAYOTARAJIWA KUINGIA SOKONI KARIBUNI

ZA LEO LEO

BREAKING NEWS: STEVEN KANUMBA 'THE GREAT' IS NO MORE
MUIGIZAJI nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba, 28, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa habari za kuaminika na kuthibitishwa na rafikie wa karibu, Patcho Mwamba, Kanumba alifariki nyumbani kwake baada ya kuanguka akitokea bafuni kutokana na kuteleza.
Chanzo hicho kinasema kwamba Kanumba alianguka baada ya kusukumwa na mpenzi wake (jina tunalo) aliyekuwa akizozana nae badaa ya kupishana kiswahili.
"Brother Kanumba kafariki usiku wa kuamkia leo na maiti yake kwa sasa ipo Mumhimbili, ikisubiri taratibu za mazishi, ni kama utani ila ndio hivyo. Alisukumwa na kuangukia kisogo na kufariki papo hapo," chanzo hicho kilisema.
Aliongeza kwa sasa walikuwa wakiwasiliana na mama yake ambaye inadaiwa yupo Bukoba pamoja na familia yake iliyopo Shinyanga kujua taratibu za mazishi yake.
Patcho Mwamba alipoulizwa juu ya kifo cha Kanumba, alithibitisha lakini hakuweza kuweka bayana chanzo zaidi ya kusisitiza kuwa alianguka sakafuni nyumbani kwake na kufariki akiwahishwa Muhimbili, ambako kwa sasa mwili wake umehifadhiwa.
Steven Charles Kanumba alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga akiwa ni mmoja kati ya watoto wa nne wa mzee Charles Kanumba.
Alisoma Shule ya Msingi Bugoyi, huko huko Shinyanga kabla ya kuendelea na masomo ya Sekondari katika Shule ya Mwadui, kisha kuhamia Shule ya Dar Christian Seminary, alipohitimu kidato cha nne. Baadaer alijiunga na masomo ya juu ya Sekondari na kumaliza Kidato cha Sita katika Shule ya Jitegemee, ambapo tayari alishaanza kujishughulisha na sanaa kupitia kundi la Kaole Sanaa alilotamba nalo na michezo mbalimbali iliyokuwa ikionyesha kwenye kituo cha ITV.
Baadae aliamua kujiengua katika kundi hilo na kucheza filamu akishirikiana na wasanii wenzake, Blandina Chagula 'Johari' na Vincent Kigosi 'Ray'.
Hadi anafariki msanii huyo alikuwa ni Muigizaji, Mtunzi, Mtayarishaji na muongozaji, akimiliki kampuni ya Kanumba the Great Films ambayo ilikuwa ikizalisha filamu na kuibua wasanii wengi chipukizi.
Marehemu alikuwa hajaoa wala kuwa na mtoto. Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema.