STRIKA
USILIKOSE
Saturday, April 7, 2012
BREAKING NEWS: STEVEN KANUMBA 'THE GREAT' IS NO MORE
MUIGIZAJI nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba, 28, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa habari za kuaminika na kuthibitishwa na rafikie wa karibu, Patcho Mwamba, Kanumba alifariki nyumbani kwake baada ya kuanguka akitokea bafuni kutokana na kuteleza.
Chanzo hicho kinasema kwamba Kanumba alianguka baada ya kusukumwa na mpenzi wake (jina tunalo) aliyekuwa akizozana nae badaa ya kupishana kiswahili.
"Brother Kanumba kafariki usiku wa kuamkia leo na maiti yake kwa sasa ipo Mumhimbili, ikisubiri taratibu za mazishi, ni kama utani ila ndio hivyo. Alisukumwa na kuangukia kisogo na kufariki papo hapo," chanzo hicho kilisema.
Aliongeza kwa sasa walikuwa wakiwasiliana na mama yake ambaye inadaiwa yupo Bukoba pamoja na familia yake iliyopo Shinyanga kujua taratibu za mazishi yake.
Patcho Mwamba alipoulizwa juu ya kifo cha Kanumba, alithibitisha lakini hakuweza kuweka bayana chanzo zaidi ya kusisitiza kuwa alianguka sakafuni nyumbani kwake na kufariki akiwahishwa Muhimbili, ambako kwa sasa mwili wake umehifadhiwa.
Steven Charles Kanumba alizaliwa Januari 8, 1984 mkoani Shinyanga akiwa ni mmoja kati ya watoto wa nne wa mzee Charles Kanumba.
Alisoma Shule ya Msingi Bugoyi, huko huko Shinyanga kabla ya kuendelea na masomo ya Sekondari katika Shule ya Mwadui, kisha kuhamia Shule ya Dar Christian Seminary, alipohitimu kidato cha nne. Baadaer alijiunga na masomo ya juu ya Sekondari na kumaliza Kidato cha Sita katika Shule ya Jitegemee, ambapo tayari alishaanza kujishughulisha na sanaa kupitia kundi la Kaole Sanaa alilotamba nalo na michezo mbalimbali iliyokuwa ikionyesha kwenye kituo cha ITV.
Baadae aliamua kujiengua katika kundi hilo na kucheza filamu akishirikiana na wasanii wenzake, Blandina Chagula 'Johari' na Vincent Kigosi 'Ray'.
Hadi anafariki msanii huyo alikuwa ni Muigizaji, Mtunzi, Mtayarishaji na muongozaji, akimiliki kampuni ya Kanumba the Great Films ambayo ilikuwa ikizalisha filamu na kuibua wasanii wengi chipukizi.
Marehemu alikuwa hajaoa wala kuwa na mtoto. Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment