STRIKA
USILIKOSE
Thursday, January 19, 2012
'Ajuza' afyatua kibao na Mhe Temba
UNAWEZA kudhani ni utani, ila ukweli ni kwamba msanii chipukizi lakini mwenye umri mkubwa wa zaidi ya miaka 50, Mwanahija Cheka 'Bi Cheka' amefyatua kibao kipya cha miondoko ya kizazi kipya akishirikiana na nyota wa miondoko hiyo nchini, Mheshimiwa Temba.
Meneja wa msanii huyo, Said Fella, alisema kibao cha Bi Cheka kiitwacho 'Ni Wewe', kimerekodiwa katika studio za Poteza Records, chini ya utayarishaji wa Suleiman Daud 'Sulesh' au 'Mr India'.
Fella, alisema tofauti na umri wake wa miaka 51, Bi Cheka 'amechana' mno katika kibao hicho, kiasi kwamba hata Mheshimiwa Temba alimvulia kofia wakati wakirekodi.
"Huwezi amini, hajawahi kuimba kokote zaidi ya kuimba kaswida alipokuwa chuo, akimtaja mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Maalim Muhidin Gurumo ndiye aliyekuwa mwalimu wake, lakini kazi kubwa aliyofanya kwenye wimbo huo mpya inashangaza," alisema Fella.
Aliongeza, ndani ya kibao hicho Bi Cheka anamlilia Temba awe wake kimapenzi, huku Temba akijaribu kumtolea nje kitu kilichoufanya wimbo huo kuwa wa kusisimua ambapo wanatarajia kuusambaza katika vituo vya redio kwa ajili ya kurushwa hewani.
Fella alisema mbali na kujipanga kuusambaza wimbo huo, pia wameanza maandalizi ya kufyatua video yake, huku wakiendelea kumrekodiwa nyimbo nyimbo kwa ajili ya albamu yake ambayo alisema huenda ikawa na nyimbo nane au kumi.
"Video ya kibao hicho ambacho Bi Cheka ameimba hip hop na kuchana mistari kama Da Brat (msanii nyota wa miondoko hiyo wa nchi ya Marekani), tunatarajia kuanza kurekodi wakati wowote kuanzia sasa," alisema Fella.
Fella, alisema msanii huyo aliwasiliana nae kumuomba amsaidie kumtolea kazi baada ya kusikia ana kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji, ingawa alisitiza awali kwa umri alionao, lakini alimsihi ampe nafasi na mwenyewe ameridhika nae kwa uwezo mkubwa wa kuimba na upangiliaji wa sauti alionao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment