STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 19, 2012

Dar Modern kuzindua tatu kwa mpigo



KUNDI linalokimbiza kwenye miondoko ya mwambao nchini, Dar Modern Taarab 'Wana wa Jiji' wanatarajia kuzindua kwa mpigo albamu zao tatu mpya katika onyesho litakalofanyika mwezi ujao jijini Dar es Salaam.
Albamu hizo tatu za kundi hilo ni 'Sikukuchagua kwa Mapesa', 'Ndugu wa Mume Mna Hila' na 'Toto la Kiafrika' ambazo kila moja ina nyimbo nne.
Akizungumza na MICHARAZO jana, Mkurugenzi wa kundi hilo, Mridu Ally Mridu 'Tx', alisema uzinduzi huo utafanyika mwishoni mwa Februari, mara baada ya kuwasili kwa kanda za kaseti za albamu hizo ambazo zinatengezwa kwa sasa nchini Kenya.
Mridu, alisema uzinduzi wao wamepanga kuufanya katika ukumbi wa Hoteli ya Travertine-Magomeni ama Diamond Jubilee yote ya jijini Dar es Salaam.
"Tupo katika mipango ya kufanya uzinduzi wa albamu zetu tatu kwa mpigo utakaofanyika ama Travertine au Diamond. Kwa sasa tunasubiri kaseti za albamu hizo zinazotengenezwa Kenya, kuwasili nchini ili tupange tarehe rasmi ya kufanyika kwa uzinduzi huo, ila utafanyika mwishoni mwa Februari," alisema.
Mridu alisema katika onyesho hilo la uzinduzi watawatambulisha wasanii wao wapya waliowanyakua hivi karibuni katika kuliimarisha kundi lao ambalo liliondokewa na mastaa wao kadhaa akiwemo Hammer Q, Hashim Said 'Big Sound' na wengineo.
Pia alisema mbali na kuzindua albamu mpya kwa kupiga nyimbo 12 za albamu hizo, pia watakumbushia nyimbo za albamu zao za zamani kama 'Ni Vijimambo Tu', 'Sote Twasaka Riziki', 'Kitu Mapenzi' na 'Gharika ya Moyo' maarufu kama 'Pembe la Ng'ombe'.
"Yaani itakuwa full burudani kwa namna tukavyowapa mashabiki wetu vitu mchanganyiko, kuanzia vile vya awali hadi hivyo vipya pamoja na kuutambulisha mtindo wetu mpya wa kunengua," alisema Mridui.
Kundi hilo la Dar Modern lilianzishwa rasmi mwaka 2006 likiundwa na wasanii mchanganyiko waliotoka kundi la Babloom Modern Taarab na mengine ya jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment