STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 19, 2012

Asilimia 80 ya waandishi wa habari hawajaajiriwa

RAIS wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Kenneth Simbaya, amesema zaidi ya asilimia 80 ya waandishi wa habari nchini hawajaajiriwa na hawana mikataba ya aina yoyote ya kazi na wamiliki wa vyombo vya habari, licha ya kwamba wanafanya kazi katika mazingira magumu .
Simbaya aliyasema hayo jana, baada ya kutembelea Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoani Kilimanjaro (MECKI) na kuzungumza na wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo iliyopo mjini Moshi.
Alisema utafiti uliofanywa na UTPC, umebaini zaidi ya asilimia 80 ya waandishi wa habari hapa nchini wanajitegemea kutafuta habari katika maeneo ya mjini na vijijini na hata kwenye maeneo ya hatari bila kuajiriwa ama kuwa na mikataba na wamiliki wa vyombo wanavyovifanyia kazi.
Alisema mwandishi pia amekuwa akilipwa ujira mdogo wa Sh. 5,000 na 3,000 hadi Sh. 1,500 kwa habari moja inayotoka gazetini, licha ya gharama kubwa anazotumia kutafuta habari hizo na kuwafikishia wenye vyombo vya habari.
Alisema kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa, UTPC inafanya jitihada za makusudi kuwasiliana na wamiliki wa vyombo vya habari ili kuangalia namna waandishi wa habari wanakuwa na mikataba ya ajira kazini na hata kuendelezwa kitaaluma pindi wanapokuwa kazini kwa muda mrefu.
Alisema UTPC pia inakusudia kuanzisha vyombo huru vya habari yakiwemo magazeti, redio na televisheni, vitakavyowawezesha waandishi wa habari kuwa na vyombo vyao vinavyotumia habari sahihi na zilizofanyiwa utafiti na uchunguzi wa kina bila upendeleo.
Alitoa wito kwa waandishi wa habari pamoja na kufanyakazi katika mazingira magumu nay a hatari, kuzingatia maadili ya kazi zao na kuepuka kutumiwa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari kwa malengo yao binfsi.
Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema waandishi wengi wa habari wamekuwa wakifanya kazi kubwa na hata kuhatarisha usalama wa maisha yao, lakini hawalipwi mishahara kulingana na kazi wanazozifanya na badala yake wamegeuka kuwa ombaomba .
Mkuu huyo wa mkoa alisema waandishi wengi wamekuwa wakiishi kwa njia za kiujanja ujanja ili kusukuma maisha yao.

NB:Imeandikwa na Jackson Kimambo, NIPASHE-Moshi

No comments:

Post a Comment