STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 3, 2011

Maugo atamba atatumia siku 16 kumchapa Kaseba
WAKATI Japhet Kaseba akiwa ameshaanza mazoezi kujiandaa na pambano lao itakalochezwa mwezi ujao, bondia Mada Maugo, amesema hana haraka ya kufanya hivyo badala yake ataanza rasmi April Mosi, akidai siku 16 zitamtosha kujiandaa kumchakaza mpinzani wake huyo.
Kaseba na Maugo watapigana kwenye pambano maalum la 'Nani Zaidi' litakalofanyika April 16, kwenye ukumbi wa PTA, Dar es Salaam kwa ajili ya kusaka mshindi atakayepigana na bingwa wa dunia, Francis Cheka.
Kaseba ameshatangaza ameshaanza maandalizi ili kujiweka sawa kumpiga Maugo, ambaye kama yeye ameshawahi kujeruhiwa na Cheka siku za nyuma, lakini Maugo akizungumza na Micharazo alisema yeye bado hajaanza.
Maugo alisema yeye bao yupo yupo kwa sasa na ataanza rasmi April Mosi na kutumia siku 16 kabla ya kuvaana na Kaseba kujiweka fiti na kutamba siku hizo zinatosha kumchakaza bingwa huko wa dunia wa Kick Boxing.
"Sijaanza na wala sitarajii kuanza kwa sasa kwa vile pambano lenyewe ni jepesi sana kwangu, nitatumia siku 16 kabla ya pambano hilo kuanza mazoezi na nina uhakika wa kumchakaza Kaseba bila tatizo," alisema Maugo.
Maugo alisema pamoja na kwamba mpinzani wake kuanza kujinadi kuwa atampiga, yeye hataki kupiga domo na badala yake kuwaomba mashabiki wa ngumi kujitokeza ukumbini siku ya April 16 kushuhudia ukweli huo.
"Sitaki kujibishana maneno na Kaseba, sio kawaida yangu, mie ni mtu wa vitendo zaidi na hivyo nawasihi mashabiki waje ukumbi kuona kama Kaseba atamaliza raundi nane la pambano hilo ni hayo tu," alisema Maugo.
Mabondia hao wenye majina makubwa nchini watapambana katika pambano la raundi nane la uzani wa Kilo 72 lililoandaliwa na mratibu Kaike Siraju kupitia kampuni ya Kaike Promotion chini ya usimamizi wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO.

Mwisho

Nyilawila awafunika Cheka, MaugoBINGWA wa Dunia wa Ngumi za Kulipwa anayeshikilia taji la WBF, Karama Nyalawila, ndiye Mtanzania anayeongoza kwa ubora miongoni mwa mabondia wa uzani wa Middle akiwafunika wakali kama Francis Cheka na Mada Maugo.
Kwa mujibu wa takwimu za ubora wa mabondia wa uzani huo duniani, kupitia mtandao wa Box Rec, Nyalawila anashikilia nafasi ya 74, wakati Cheka, Bingwa wa Dunia wa UBO, ICB na WBC yupo nafasi ya 142.
Maugo yeye anashika nafasi ya 196 akimzidi wakongwe Rashid Matumla 'Snake Man' na Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo' wanashika nafasi ya 327 na 370.
Nyalawila aliyetwaa taji hilo Desemba 3 mwaka jana huko Jamhuri ya Czech, ni miongoni mwa mabondia wanne wa kiafrika waliopo kwenye orodha wa mabondia 100 Bora Duniani wa uzani huo wa Middle.
Wengine waliopo kwenye orodha hiyo ni Mganda, Kassim Ouma anayeshika nafasi ya 32 akiwa ndiye kinara kwa mabondia wa Kiafrika, Assie Duran na Osumanu Adama wa Ghana waliopo nafasi ya 34 na 35 na Mnigeria, Eromosele Albert aliyepo anayeshikilia nafasi ya 38.
Bondia anayeongoza kwenye orodha ya wapiganaji wa uzani huo ni Sergio Gabriel Martinez wa Argentina anayefuatiwa na Felix Sturm wa Ujerumani na anmayeshikilia nafasi ya tatu duniani ni Danile Geale wa Australia.
Mabondia wa Kitanzania wanatengeneza 10 Bora yao wakiwafuata Nyalawila na Cheka ni, Mada Maugo (196), Thomas Mashali (212), George Dimoso (289), Maisha Samson (302), Rashid Matumla (327), Bagaza Mwambene (342), Stan Kessy (350) na Maneno Oswald 'Mtando wa Gongo' akiishika nafasi ya 370.

Kanumba ana 'shock', Ray atamba

BAADA ya kuanza mwaka na filamu ya 'Deception', muigizaji nyota wa filamu nchini, Steven Kanumba 'The Great' ameibuka na filamu mpya iitwayo 'The Shock'.
Filamu hiyo ambayo imekamilika hivi karibuni na sasa ipo katika maandalizi ya kuachiwa mitaani, ni ya pili kwa msanii huyo kwa mwaka huu wa 2011.
Akizungumza na Micharazo, Kanumba alisema kama ulivyo utaratibu wake wa kuibua wasanii wapya katika fani hiyo, ndani ya 'The Shock' amemtambulisha muigizaji mpya mwanadada mrembo Shez Sadry ambaye amedai amefanya mambo makubwa kama mzoefu.
Kanumba alisema mbali na mwanadada huyo ambaye ndiye mhusika mkuu, pia kuna kuna muimbaji wa FM Academia Patcho Mwamba, Ben Braco, yeye mwenyewe na wengineo.
"Baada ya Deception sasa The Shock inakuja ambayo na kifaa kipya lakini kikali katika muigizaji, Shaz Sadry," alisema Kanumba.
Alisema filamu hiyo inatarajiwa kuachiwa mitaani ndani ya mwezi huu na itasambazwa na kampuni ya Steps Entertainment.
Katika hatua nyingine, mpinzani mkubwa wa Kanumba, Vincent Kigosi 'Ray' amesema filamu yake mpya ya 'Second Wife' inatarajiwa kuingia mitaani wiki ijayo na kuwataka mashabiki wa fani hiyo kukaa mkao wa kula kupata uhondo.
Katika filamu hiyo mpya, Ray ameigiza na wakali kama Riyama Ally, Coleta Raymond, Aisha Bui, muigizaji mpya mwanadada Skyner Ally na mtoto Aisha.
Ray amesema filamu hiyo ni 'funika bovu' kutokana na jinsi alivyoigiza kwa kushirikiana na wenzake na kusisitiza kuwa, hizo ni salamu kwa wapinzani wao kuwa RJ Production imekuja kivingine ndani ya mwaka 2011.

Madee asikitika Dogo Janja kuzinguliwa shuleni

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya, Hamad Ally 'Madee' amedai kusikitishwa na kitendo ambacho amekuwa akifanyiwa msanii chipukizi anayemfadhili, Abdul-Aziz Chende 'Dogo Janja' na mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Makongo anayosoma kwa sasa.
Akizungumza na Micharazo, Madee alisema kuwa, amesikitishwa na taarifa kwamba mmoja wa walimu wa shule hiyo amekuwa akimpa wakati mgumu Dogo Janja, jambo analohofia linaweza kushuka kiwango chake cha elimu darasani.
Hata hivyo Madee alisema tayari suala la mwalimu huyo ambaye hakumtaja jina, limeshafikishwa kwa mkuu wa shule hiyo, na Dogo Janja anaendelea kusoma kwa vile hana mpango wa kuhama.
"Kwa walimu wa namna hii wanaharibu viwango vya wanafunzi darasani, ila nashukuru mambo yameshamalizwa kwa Dogo kwenda kwa Mkuu na kulalamika na ticha huyo kuonywa," alisema.
Aliongeza ni vema walimu wakatambua kuwa wao ni walezi kwa wanafunzi na hivyo waishi
kama watoto wao na wanapokosea wawaelekeze hata kama kwa bakora, lakini wakizingatia
miiko na taaluma zao za kazi.
Dogo Janja, alinukuliwa na kituo kimoja akisema kuwa alikung'utwa na mwalimu wake huyo baada ya kutofautiana nae kiswahili, huku akidai mara kwa mara amekuwa akimzingua akimuita 'Dogo Jinga' badala ya jina lake la Dogo Janja, kitu kilichokuwa kikimnyima raha shuleni.
Madee, aliamua kumsaidia Dogo Janja mwenyeji wa Arusha kutokanan na kuvutiwa na kipaji chake na tayari ameshamkamilishia albamu mpya iitwayo Ngarenaro, akiwa pia ndiye anayemlipia ada shuleni hapo akijiandaa kumfyatulia video ya albamu hiyo yenye nyimbo 10.

Mtenda Akitendewa ya Extra Bongo videoniWIMBO mpya wa bendi ya Extra Bongo unaotarajiwa kutambulishwa rasmi leo kwa mashabiki sambamba na vibao vingine na wanamuziki wapya uitwao, Mtenda Akitendewa umefyatuliwa video yake.
Video ya kibao hicho ambacho awali lilipangwa kufahamika kama 'Under 18' kimefyatuliwa na wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa kambini kupitia kampuni ya Sophia Records ya jijini Dar es Salaam na utaanza kuonekana hewani wakati wowote kuanzia sasa.
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki 'Kamarade' aliiambia Micharazo kuwa, waliamua
kurekodi video ya wimbo huo wakiwa kambini kama njia ya kuwapa burudani mashabiki wao kuwaonyesha hawakuwa bure kambini bali walikuwa wakiwaandalia mambo mapya.
"Pamoja na kuandaa kazi mpya, lakini pia tumefyatua video ya moja ya vibao hivyo kiitwacho Mtenda Akitendewa ambacho kitaanza kuonekana wakati wowote,tumeshasambaza, kibao hicho na vingine pamoja na wanamuziki wapya tutawatambulisha rasmi Ijumaa," alisema.
Choki alisema onyesho la utambulisho kwa bendi yao litafanyika leo kwenye ukumbi wa New Msasani Club kabla ya kufuatiwa na maonyesho mawili ya TTC Chang'ombe litakalofanyika Jumamosi kisha Jumapili pale Mango Garden kabla ya kujiandaa kwenda Zanzibar.
Mtunzi na muimbaji huyo alizitaja nyimbo nyingine zitakazotambulishwa sambana na
wanamuziki sita waliowanyakua wakienda kambini kutoka Twanga Pepeta ni Neema, Nguvu
na Akili na Fisadi wa Mapenzi vinavyoandaliwa kwa ajili ya albamu mpya na ya pili.
Alipoulizwa kama kibao hicho ni 'dongo' mahasimu wao, African Stars 'Twanga Pepeta', Choki alisema sio kweli kibao cha Mtenda Akitendewa ni kijembe, ila alisema kama kuna mtu atakayeguswa nao na kulalamika ujue ndiye mhusika.
"Staili yetu ni kama ile ya zamani ya kurusha jiwe kwenye kiza, atakasema mmh, hujue limempata, ila sio kweli kama nimetunga mahususi kwa ajili ya mtu yeyote," alisema Choki.
Mkurugenzi huyo aliwataja wanamuziki watakaotambulishwa kwenye maonyesho hayo ya mwishoni mwa wiki ni mtunzi na muimbaji nyota nchini, Rogert Hegga 'Caterpillar', Rapa Saulo John 'Ferguson', mpiga besi, Hoseah Mgohachi na wanenguaji Hassani Mohammed 'Super Nyamwela', Isaac Burhan 'Super Danger' na Otilia Boniface waliotoka African Stars 'Twanga Pepeta'.

Akudo Impact yanyakua wanenguaji wapya

BENDI ya Akudo Impact imeongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji wa jukwaa baada ya
kuwanasa wanenguaji watatu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Kwa mujibu wa meneja wa bendi hiyo George Kyatika, wanenguaji hao ni Mariam Sangwa,
Francine Bozi na Mary Sheli ambao tayari wameshatambulishwa kwenye maonyesho mbalimbali ya Akudo.
Meneja huyo alisema ujio wa wanenguaji hao unaifanya Akudo kuwa na jumla ya madansa sita wengine wakiwa ni Fanny Bosawa, Raissa Sangwa na Nadine Issala.
"Tumeongeza wanenguaji wakati huu ambao tuko kwenye maandalizi ya uzinduzi wa albamu
yetu ya History no Change ambayo itazinduliwa mwezi wa ujao," alisema Kyatika.
Alisema kuwa awali safu yao ya ushambuliaji wa jukwaa ilikuwa inapwaya hasa baada kupunguza baadhi ya wanenguaji ambao makali yao ya kufanya kazi yalikuwa yamepungua lakini sasa wamepata wapya.
Kyatika alizitaja baadhi ya nyimbo za albamu hiyo wanayojiandaa kuzindua kuwa ni 'Ubinafsi', 'Umefulia', 'Pongezi kwa Wanandoa' na 'Umejificha Wapi'.
Aliongeza kusema kuwa sasa Akudo imejipanga upya kuanzia kwenye uongozi wa bendi na
hivyo ana uhakika itaendelea kufanya vizuri kwa kuwaburudisha mashabiki na wapenzi wake.
Akudo imekuwa ikitamba na albamu yake ya kwanza ya Impact ambayo ilichangia kuipandisha chati bendi hiyo inayojiita Vijana wa Masauri ikiwa chini ya rais wake Christian Bella.