STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 3, 2011

Mtenda Akitendewa ya Extra Bongo videoni



WIMBO mpya wa bendi ya Extra Bongo unaotarajiwa kutambulishwa rasmi leo kwa mashabiki sambamba na vibao vingine na wanamuziki wapya uitwao, Mtenda Akitendewa umefyatuliwa video yake.
Video ya kibao hicho ambacho awali lilipangwa kufahamika kama 'Under 18' kimefyatuliwa na wanamuziki wa bendi hiyo wakiwa kambini kupitia kampuni ya Sophia Records ya jijini Dar es Salaam na utaanza kuonekana hewani wakati wowote kuanzia sasa.
Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki 'Kamarade' aliiambia Micharazo kuwa, waliamua
kurekodi video ya wimbo huo wakiwa kambini kama njia ya kuwapa burudani mashabiki wao kuwaonyesha hawakuwa bure kambini bali walikuwa wakiwaandalia mambo mapya.
"Pamoja na kuandaa kazi mpya, lakini pia tumefyatua video ya moja ya vibao hivyo kiitwacho Mtenda Akitendewa ambacho kitaanza kuonekana wakati wowote,tumeshasambaza, kibao hicho na vingine pamoja na wanamuziki wapya tutawatambulisha rasmi Ijumaa," alisema.
Choki alisema onyesho la utambulisho kwa bendi yao litafanyika leo kwenye ukumbi wa New Msasani Club kabla ya kufuatiwa na maonyesho mawili ya TTC Chang'ombe litakalofanyika Jumamosi kisha Jumapili pale Mango Garden kabla ya kujiandaa kwenda Zanzibar.
Mtunzi na muimbaji huyo alizitaja nyimbo nyingine zitakazotambulishwa sambana na
wanamuziki sita waliowanyakua wakienda kambini kutoka Twanga Pepeta ni Neema, Nguvu
na Akili na Fisadi wa Mapenzi vinavyoandaliwa kwa ajili ya albamu mpya na ya pili.
Alipoulizwa kama kibao hicho ni 'dongo' mahasimu wao, African Stars 'Twanga Pepeta', Choki alisema sio kweli kibao cha Mtenda Akitendewa ni kijembe, ila alisema kama kuna mtu atakayeguswa nao na kulalamika ujue ndiye mhusika.
"Staili yetu ni kama ile ya zamani ya kurusha jiwe kwenye kiza, atakasema mmh, hujue limempata, ila sio kweli kama nimetunga mahususi kwa ajili ya mtu yeyote," alisema Choki.
Mkurugenzi huyo aliwataja wanamuziki watakaotambulishwa kwenye maonyesho hayo ya mwishoni mwa wiki ni mtunzi na muimbaji nyota nchini, Rogert Hegga 'Caterpillar', Rapa Saulo John 'Ferguson', mpiga besi, Hoseah Mgohachi na wanenguaji Hassani Mohammed 'Super Nyamwela', Isaac Burhan 'Super Danger' na Otilia Boniface waliotoka African Stars 'Twanga Pepeta'.

No comments:

Post a Comment