STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, March 3, 2011

Maugo atamba atatumia siku 16 kumchapa Kaseba




WAKATI Japhet Kaseba akiwa ameshaanza mazoezi kujiandaa na pambano lao itakalochezwa mwezi ujao, bondia Mada Maugo, amesema hana haraka ya kufanya hivyo badala yake ataanza rasmi April Mosi, akidai siku 16 zitamtosha kujiandaa kumchakaza mpinzani wake huyo.
Kaseba na Maugo watapigana kwenye pambano maalum la 'Nani Zaidi' litakalofanyika April 16, kwenye ukumbi wa PTA, Dar es Salaam kwa ajili ya kusaka mshindi atakayepigana na bingwa wa dunia, Francis Cheka.
Kaseba ameshatangaza ameshaanza maandalizi ili kujiweka sawa kumpiga Maugo, ambaye kama yeye ameshawahi kujeruhiwa na Cheka siku za nyuma, lakini Maugo akizungumza na Micharazo alisema yeye bado hajaanza.
Maugo alisema yeye bao yupo yupo kwa sasa na ataanza rasmi April Mosi na kutumia siku 16 kabla ya kuvaana na Kaseba kujiweka fiti na kutamba siku hizo zinatosha kumchakaza bingwa huko wa dunia wa Kick Boxing.
"Sijaanza na wala sitarajii kuanza kwa sasa kwa vile pambano lenyewe ni jepesi sana kwangu, nitatumia siku 16 kabla ya pambano hilo kuanza mazoezi na nina uhakika wa kumchakaza Kaseba bila tatizo," alisema Maugo.
Maugo alisema pamoja na kwamba mpinzani wake kuanza kujinadi kuwa atampiga, yeye hataki kupiga domo na badala yake kuwaomba mashabiki wa ngumi kujitokeza ukumbini siku ya April 16 kushuhudia ukweli huo.
"Sitaki kujibishana maneno na Kaseba, sio kawaida yangu, mie ni mtu wa vitendo zaidi na hivyo nawasihi mashabiki waje ukumbi kuona kama Kaseba atamaliza raundi nane la pambano hilo ni hayo tu," alisema Maugo.
Mabondia hao wenye majina makubwa nchini watapambana katika pambano la raundi nane la uzani wa Kilo 72 lililoandaliwa na mratibu Kaike Siraju kupitia kampuni ya Kaike Promotion chini ya usimamizi wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBO.

Mwisho

No comments:

Post a Comment