STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, October 21, 2013

Pambano la Twiga Stars lapangulia ratiba Ligi Kuu

KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imefanya marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ili kupisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania na Msumbiji.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza kwa mashindano ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 itachezwa Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni.
U20 tayari imehamishia kambi yake hosteli ya Msimbazi Center, Dar es Salaam kutoka JKT Ruvu mkoani Pwani tangu wiki iliyopita kujiandaa kwa mechi hiyo. Fainali za Kombe la Dunia kwa U20 wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada.
Marekebisho ya ratiba ya VPL yamegusa raundi zote tatu zilizobaki kukamilisha mzunguko wa kwanza. Kutokana na marekebisho hayo mechi za raundi ya 11 zitakuwa ifuatavyo; Oktoba 28 mwaka huu ni Coastal Union vs Mtibwa Sugar, Oljoro JKT vs Ashanti United, Ruvu Shooting vs Kagera Sugar na Simba vs Azam. Oktoba 29 mwaka huu ni Tanzania Prisons vs Mbeya City, Yanga vs Mgambo Shooting na Rhino Rangers vs JKT Ruvu.
Raundi ya 12 ni kama ifuatavyo; Oktoba 31 mwaka huu ni Simba vs Kagera Sugar, Novemba 1 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Yanga. Novemba 2 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Coastal Union, Tanzania Prisons vs Oljoro JKT, Azam vs Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar vs Rhino Rangers na Mbeya City vs Ashanti United.
Raundi ya 13 ni kama ifuatavyo; Novemba 6 mwaka huu ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashanti United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar. Novemba 7 mwaka huu ni Azam vs Mbeya City.
Mechi za kufunga raundi ya 10 zitachezwa keshokutwa (Oktoba 23 mwaka huu) kama ratiba inayoonesha. Mechi hizo ni kati ya Coastal Union vs Simba, Tanzania Prisons vs Kagera Sugar na Yanga vs Rhino Rangers.

Winta: Kisura wa Jumba la Dhahabu aliyepona kufa kwa Risasi

Msanii Angel John Komba 'Winta' katika pozi
LICHA ya kipaji cha kuzaliwa alichoanza kukionyesha tangu akiwa kinda wakati akisoma Shule ya Msingi Mgulani, msanii Angel John Komba 'Winta' anakiri kuwapenda na kuvutiwa kupita kiasi na Genevieve Nnaji wa Nigeria na Yvonne Cherly 'Monalisa' kulichangia kuingia kwake katika fani ya uigizaji.
Winta, mmoja wa waigizaji wa kike mahiri nchini aliyetamba na kazi mbalimbali kama tamthilia na filamu anasema nyota hao walikuwa wakimkosha kila alipoziona kazi zao na kuapa kuwa ni lazima na yeye aje kuwa staa kama wao.
"Nnaji na Monalisa ndiyo walinipa mzuka wa kujibidiisha katika sanaa ya uigizaji kwani walinikosha na mpaka sasa navutiwa nao," anasema.
Anasema kabla ya kuvutiwa na umahiri wa wanadada hao alikuwa amejikita kwenye sanaa ya kupiga na kucheza ngoma enzi akiwa darasa la sita na kuendelea hata alipojiunga na Sakhafa Sekondari ambapo tayari alishaanza kuigiza.
Hata hivyo anasema kujitosa kwake rasmi katika uigizaji, ilikuwa mwaka 2001 alipokutana na Jumanne Kihangale 'Mr Chuz' anayemtaja kama mmoja wa watu asiyoweza kuwasahau kwa alivyomsaidia kufika mahali alipo sasa na kuwa miongoni mwa waasisi wa kundi maarufu ya uigizaji la Fukuto Arts Professional.
"Kiukweli nilitumbukia rasmi kwenye uigizaji mwaka 2001 nikiwa miongoni mwa waasisi wa kundi la Fukuto na kazi ya kwanza kuicheza ilikuwa ni igizo lililokimbiza nchini la Jumba la Dhahabu na mingine iliyokuja baadaye kabla ya kuhamia kwenye filamu kwa kucheza kazi mbalimbali zilizonipaisha ndani na nje ya nchi," anasema.
Mrembo huyo anayeishabiki Simba na mabingwa watetezi wa England klabu ya  Manchester United, anasema tangu ameingia kwenye fani hiyo anashukuru amepata mafanikio mengi ya kujivunia baadhi hapendi yaanikwe gazetini.
Winta anadai mbali na manufaa ya kiuchumi, sanaa imemfanya afahamiane na watu wengi na kupata rafiki na kutembea sehemu mbalimbali.
"Nashukuru sanaa imenisaidia kwa mambo mengi ya kujivunia, japo sijaridhika kwa vile ndoto zangu ni kuja kumiliki kampuni binafsi itakayozalisha na kusambaza kazi zangu na za wasanii wenzangu," anasema.

MKASA
Kisura huyo anayependa kula ugali kwa mlenda na dagaa mchele wa kukaangwa, anasema sanaa ya Tanzania imezidi kupiga hatua kubwa kulinganisha na siku za nyuma japo anadai wizi na unyonyaji unawafanya wasanii washindwe kunufaika.
Anasema, lazima serikali na mamlaka zinazosimamia fani hiyo kutoa makucha yake ili kuwabana wanyonyaji na wezi wa kazi za wasanii ili kuinua maisha ya wasanii tofauti na sasa wengi wao wakiishi maskini tofauti na jasho lao.
Msanii Winta katika pozi
Pia anataka watengeneze miundo mbinu itakayowasaidia chipukizi kuendeleza vipaji vyao ili kusaidia kuondoa tatizo la ajira sambamba na serikali kuvuna pato kupitia fani hiyo.
Juu ya tukio la furaha, Winta anasema ni siku alipojaliwa kujifungua mtoto wa kiume aliyenaye, huku akidai hawezi kuusahau mkasa uliowahi kumkuta hivi karibuni alipokuwa na rafikize 'wakila bata' na kubadilishana mawazo baa.
Anasema akiwa na wenzake hawana hili wala lile, ghafla Pub waliyokuwepo (jina limehifadhiwa) ilivamiwa na majambazi ambao waliwamrisha wateja wote kulala na yeye kwa ubishi alikurupuka ili kukimbia na kufyatuliwa risasi iliyomkosakosa sentimita chache na kwa kiwewe alijikuta akitumbukia kwenye mtaro wa maji machafu yaliyochanganyika na kinyesi.
Winta anasema kila anapolikumbuka tukio hilo la kusalimika kufa kwa risasi na jinsi alivyokoga uchafu huo hukosa raha.
"Siwezi kulisahau tukio hilo kwa jinsi nilivyonusurika kifo cha risasi na kutumbukia kwenye mtaro wa kinyesi, yaani ilikuwa balaa. Ila nashukuru  Mungu aliinusuru roho yangu," anasema.
Winta ambaye hajaolewa japo ana mtoto mmoja, anasema hakuna msanii wa kiume anayemkuna nchini kama mkongwe Amri Athuman maarufu kama Mzee Majuto.
"Huyu mzee noma, hana mpinzani na anajua kitu anachokifanya katika fani," anasema mwanadada huyo anayejikubali mwenyewe kwa uwezo alionao.

ALIPOTOKAAngel John Komba 'Winta' alizaliwa mwaka 1982 katika hospitali ya Temeke, Dar es Salaam kabla ya kuanza Shule ya Msingi Mgulani kabla ya kujiunga na Sakhafa Sekondari ambapo tayari alishaanza kujishughulisha na sanaa akicheza, kupiga ngoma na kuigiza.
Winta anayependa kunywa Fanta Passion na Castle Light, baada ya kumaliza shule alitumbukia rasmi kwenye sanaa hiyo akianzia kundi la Fukuto Arts Professional na kutamba nalo na tamthilia kadhaa kabla ya kuangukia kwenye filamu.
Baadhi ya filamu alizoigiza mwanadada huyo anayependa kutumia muda wa ziada kuangalia 'muvi' kuchati na kusoma vitabu na magazeti ni pamoja na 'Shock' aliyoigiza na marehemu Steven Kanumba, 'I Hate My Birthday', 'Pigo la Yatima', 'Kovu la Laana' na nyingine.
Winta akiwa na marehemu Kanumba walipokuwa wakiigiza filamu ya The Shock
Winta anayewataka wasanii wenzake kutegemea vipaji walivyonavyo na kuvitumikia kwa ufanisi badala ya kujihusisha na skendo au vitendo vya ushirikiana.
"Hakuna siri kwa sasa wasanii wanaendekeza sana mambo ya kishirikiana kwa kushinda kupishana kwa waganga ili kuroga na kutembelea nyota za wenzao, ila ukweli mtu anayejiamini na kutegemea kipaji hawezi kufanya upuuzi huo ambao hausaidii zaidi ya kujidhalilisha," anasema.
Mwanadada huyo anayemshukuru mno Mr Chuz na watu wengine waliomsaidia kwa namna moja au nyingine kufika alipo, anaiomba jamii iwachukulie wasanii kama watu wengine na pale wanapokosea wasiwahukumu wote au kuwaona watu wa ajabu kwa sababu hakuna binadamu aliyekamilika.
"Pia watuunge mkono kwa kununua kazi zetu sambamba na kutusaidia kupambana na maharamia kwa kuacha kununua kazi feki badala yake wazinunue kazi halisi ili tuweze kuendelea kuwapa burudani," anasema.

Simba, Yanga waingiza Mil. 500

Wachezaji wa Simba na Yanga walipokuwa wakiumana jana
Na Boniface Wambura
PAMBANO la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana baina ya watani wa jadi Simba na Yanga lililochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao 3-3 limeingiza jumla ya Sh. Milioni 500.7.
Mashabiki 57,422 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 63 kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Ni tiketi 131 tu ndizo hazikuuzwa ambazo ni 90 za VIP A, 40 za VIP B na moja ya VIP C. Tiketi zilizochapwa kwa ajili ya mechi hiyo ni 57,558 ambayo ndiyo idadi ya viti vilivyopo kwenye uwanja huo. Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,025,564.32 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,382,084.75.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 62,555,371.69, tiketi sh. 7,309,104, gharama za mechi sh. 37,533,223.01, Kamati ya Ligi sh. 37,533,223.01, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,766,611.51 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,596,253.39.

Abdallah Juma: Aliyerudisha heshima ya hat-trick kwa wazawa Bara

Abdallah Juma alipokuwa Simba
 HALI aliyokumbana nayo akiwa na timu ya Simba msimu uliopita, ilimfanya mshambuliaji Abdallah Juma, kukaribia kutundika daluga na kuachana na soka.
Anasema alishaamua kuachana na soka na kwenda kufanya kazi za ufundi magari kutokana na alivyokatishwa tamaa na Simba iliyomsajili kutokea Ruvu Shooting.
Hata hivyo, baada ya ushauri wa watu wake wa karibu na mzuka wa soka alionao tangu utotoni, ulimbadili mawazo yake na kuamua kujiunga na Mtibwa Sugar.
Kitendo cha kujiunga Mtibwa kimeweza kumrejeshea furaha na hasa baada ya wiki iliyopita kufunga mabao matatu (hat-trick) na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mzawa kufanya hivyo tangu Juma Semsue aliyekuwa Polisi Dodoma kupiga hat-trick.
Semsue aliweka rekodi hiyo ya kufunga hat-trick msimu wa 2010-2011 wakati Polisi ilipoishindilia Villa Squad mabao 5-3, baada ya hapo ligi hiyo ilishuhudiwa ikiisha kwa misimu miwili mfululizo bila hat-trick nyingine.
Mwezi uliopita Mrundi Amisi Tambwe wa Simba ndiye aliyekuja kuvunja mwiko huo kwa kufunga mabao manne wakati timu yake ikiizabua Mgambo JKT 6-0 na ndiyo Juma akaifikia rekodi yake wakati Mtibwa ikiifunga Oljoro JKT 5-2.
"Nimejisikia furaha, sikutegemea na hii ni hat-trick yangu ya kwanza, pia imekuja nikitoka katika kipindi cha kukata tamaa cha kucheza soka," anasema.
Juma ambaye hufananishwa na wengi na Abdallah Juma mwenye asili ya Unguja aliyewahi kutamba Mtibwa akiweka rekodi ya kufunga mabao 25 katika msimu mmoja, yote ndani ya Uwanja wa Manungu, anasema tukio hilo litabaki kuwa historia kwake.
Anasema kinachomfanya achekelee ni namna alivyoweka rekodi katika Ligi Kuu Bara akiwa mzawa wa kwanza 'kutupia' hat-trick baada ya misimu miwili, pia namna alivyoibuka akiwa keshakata tamaa ya soka kwa mambo aliyofanyiwa Simba.
"Kitendo cha kuchezeshwa mechi mbili tena kwa muda usiozidi robo saa kwa msimu mzima Simba, kutokana na kutoaminiwa na kocha, kinanitia simanzi na siwezi kusahau maishani," anasema.
Mkali huyo aliyeanza kujipatia umaarufu wa kufumania nyavu akizichezea FC Kambarage, Polisi-Shinyanga na Mwanza Utd kabla ya kutua katika Ligi Kuu kupitia AFC Arusha, Kagera Sugar na Ruvu Shooting, anawashukuru makocha wa Mtibwa Sugar kwa kumrejeshea furaha yake.
"Wananiamini na wamenisaidia kurejea katika kiwango changu, nimecheza mechi tatu tu, lakini tayari nimeweka rekodi naamini nitaendelea kufanya vema zaidi," anasema.
Anaeleza kuwa, wakati mwingine makocha huchangia 'kuua' vipaji vya wachezaji kwa kuwakatisha tamaa kwa kutokana na kutowaamini na kushindwa kuwasaidia pale wanapotokea kukosea kutekeleza maagizo yao uwanjani.
"Namshukuru Mungu. Huu ni mwanzo kwani naamini nitaendelea kufumania nyavu ili kufikia lengo la kuitwa Taifa Stars na pia kucheza soka la kulipwa nje ya nchi," anasema.

Bendera
Mkali huyo anayependa kula ugali kwa dagaa na mboga za majani huku akishushia na maji na soda, anasema mafanikio yake kisoka licha ya kuchangiwa na makocha tofauti, lakini hawezi kumsahau Madaraka Bendera aliyemnoa akiwa AFC.
Anasema Bendera alimtengeneza akawa Juma 'Magoli' ndiyo maana alimezewa mate na kuhama timu moja hadi nyingine mpaka Msimbazi ambapo hata hivyo, waliishia 'kumchomesha mahindi'.
Shabiki huyo wa Arsenal  anayemzimia mshambuliaji wa zamani wa klabu hiyo ya England, Robin van Persie aliyepo Manchester Utd kwa sasa, anasema soka limemsaidia kwa mambo mengi japo hapendi yaanikwe gazetini.
"Nitakosa fadhila kama sitamshukuru Mungu jinsi soka lilivyonisaidia," anasema.
Juma analitaja pambano la Ligi Kuu Bara kati ya AFC Arusha dhidi ya Yanga misimu minne iliyopita kuwa ndilo gumu na asilolisahau.
"Mbali na kuwa la kwanza dhidi ya timu kubwa kama Yanga, lakini kitendo cha kuingia uwanjani dakika nane kabla ya mechi kwisha na kuisawazishia AFC bao, itabaki kumbukumbu ya milele kwangu" anasema.
Anasema katika pambano hilo Yanga ilitangulia kufunga mapema na kudumu hadi dakika ya 82 alipoingizwa na kocha Bendera na kufanikiwa kufunga bao la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 1-1.
Abdallah Juma
Msukuma
Abdallah Salum Juma, alizaliwa 1989 mkoani Shinyanga akiwa ni mtoto wa mwisho kwa tumbo la mama yake akitanguliwa na kaka yake kwenye familia ya watoto nane wa mzee Salum Juma.
Anasema soka lake lilianzia mkoani Shinyanga wakati akisoma Shule ya Msingi Mangejese. Anafafanua kuwa alikuwa akimudu nafasi nyingi uwanjani kuanzia ya ulinzi, kiungo, hadi ushambuliaji na timu yake ya 'chandimu' ikiwa ni Mwenge Stars kabla ya kusajiliwa Segese Stars ya Kahama kwa michuano ya Ligi.
Juma anasema alivutiwa kipindi hicho na Mashaka Ayoub aliyewahi kutamba timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara na alipotoka Segese alisajiliwa Kambarage kisha AFC Arusha iliyovutiwa naye.
Aliichezea AFC kwa misimu kadhaa kabla ya kusajiliwa Kagera Sugar kisha kurudi tena AFC na kuteuliwa timu ya Mount Meru Warriors kwa michuano ya Kombe la Taifa na kuivutia Ruvu Shooting iliyomsajili kabla ya kutua Simba.
Abdallah Juma (kulia) akiwajibika uwanjani
Anasema soka la Tanzania linazidi kupiga hatua kubwa kwa vijana kuonyesha uhai wa kurejesha heshima ya Tanzania kimataifa, japo aliiomba serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuongeza nguvu katika soka la vijana ili kuwaandaa mashujaa wa kesho.
Anasema hakuna kitu anachokitamani maishani mwake kama kulitumikia taifa lake kupitia timu ya taifa ambayo hajawahi kuinusa hata kidogo, huku akiota pia kucheza soka la kulipwa Ulaya na kuwataka wachezaji wenzake kujibidiisha kwenye mazoezi na kuzingatia nidhamu na miiko ya uchezaji wa soka.
Juma anayekiri kama siyo soka huenda angekuwa fundi magari mzuri kutokana na fani hiyo kuipenda na kuisomea kwa muda, anasema ligi kuu ya msimu huu ni ngumu na inayotoa changamoto kubwa kwa klabu pamoja na wachezaji wa timu shiriki.
"Ligi ya msimu huu kiboko, haitabiriki kutokana na ugumu wake, kitu ambacho ni kizuri kwa wachezaji na hata klabu kujipanga zaidi ili kupata matokeo mazuri," anasema.
Mchezaji huyo anasema anadhani timu bora itafahamika mwishoni mwa msimu pale itakapotwaa ubingwa na kupata uwakilishi wa mechi za kimataifa kwa sababu kwa sasa ni vigumu kutabiri kwa vile timu zote 14 zina nafasi sawa ya kutwaa taji hilo kwa kadri watakavyojipanga vema.

KR Mullar: Mkali wa Mapanga Shaa anayefananishwa na Gervinho



KR Mulla akikamua jukwaani
MASHABIKI wa muziki wanamuita 'Jibaba' CD 700' kutokana na kuwa na 'mapafu' ya kuhimili jukwaa akiimba na kucheza kwa muda mrefu, huku wale wa soka wamembatiza jina la Gervinho kutokana uwezo wake kisoka na kule kushabihiana kwake na nyota wa Ivory Coast aliyewahi kutamba Arsenal, Gervais Lombe Yao Kouassi maarufu kama 'Gervinho'.
Hata hivyo majina yake halisi ni Rashid Ziada 'KR Mullah', mmoja wa wasanii wakongwe wa muziki wa kizazi kipya aliyeasisi makundi kadhaa ambaye kwa sasa ametuliza 'mtima' wake katika kundi la Wanaume Halisi akiungana tena na 'swahiba' wake, Juma Kassim 'Sir Juma Nature'.
KR Mullah, ambaye kitaaluma ni fundi magari fani aliyoisomea Chuo cha VETA na kuifanya kwa muda kabla ya kutumbukia kwenye muzuki, ni kati ya vijana wachache waliojaliwa vipaji lukuki akimudu kuimba, kutunga, kucheza na kupanga muziki, huku pia akiwa mahiri katika soka akimudu nafasi mbalimbali uwanjani kuanzia nafasi ya beki, kiungo, winga hadi ile ya ushambuliaji.
Akiwa amewahi kuzichezea timu mbalimbali za mitaani katika maeneo yao ya Temeke akishiriki pia Ligi Daraja la Tatu na Nne, KR Mullah kwa sasa ni mmoja wa wachezaji anayeunda kikosi cha timu ya Golden Bush Veterani akiungana na wakali wa zamani za klabu za Simba, Yanga na Mtibwa Sugar.
Kupenda kwake soka na muziki kulimsababisha akaamua kuachana na kuchezea spana na 'oil' ili kutumikia fani hizo na kukiri kwamba kwa kiasi fulani zimemsaidia kiuchumi na kimaisha, japo hajaridhika na mahali alipo.
"Soka nalicheza kwa vile nalipenda na limenisaidia kufahamiana na watu wengi pamoja na kunisaidia kuwa pumzi kubwa jukwaani, lakini muziki ndiyo zaidi kwa kunisaidia kiuchumi, naishi na familia yangu kwa sababu ya muziki, japo sijaridhika," anasema.
Anasema japo anafarijika kuona muziki wa kizazi kipya ukikubalika mbele ya jamii tofauti na siku za nyuma, furaha yake itafikia kilele siku atakapoitwa kwenda kutumbuiza 'duniani' kama mastaa wengine wanaoletwa nchini.
"Siku nitakapoalikwa na kwenda kufanya kazi katika nchi zilizoendelea kimuziki sambamba na wakali wanaong'ara duniani, ndipo nitakapoona kweli sasa nipo juu na ndoto zangu za kuutangaza muziki wetu kimataifa imefanikiwa," anasema.
KR Mullah, aliyepewa jina hilo la Mullah akifananishwa na kiongozi aliyewahi kuvuma wa kundi la Taleban, Mullah Omar Mohammed kutokana na uwezo wa kutawala jukwaa na kuwaongoza wenzake kuwaburudisha mashabiki wao.
KR Mulla akionyesha umahiri waka katika soka
CHUJI
KR Mullah anayependa kula ugali kwa samaki na mboga za majani na kunywa maji na siku moja moja 'maji ya mende' anasema hakuna tukio la furaha kwake kama kukubalika kwa ubunifu wake wa staili ya kucheza ya 'Mapanga Shaa' inayotumiwa na kundi la TMK Wanaume Family.
"Hili ndilo tukio la furaha kuona ubunifu wangu ukitumika kama nembo ya kundi letu popote tulio na ninalizwa na matukio ya wasanii wenzetu kutangulia mbele ya haki wangali wadogo, inauma na kunitoa machozi," anasema.
Mkali huyo ambaye anajiandaa kupakua albamu yake ya pili binafsi itakayokuwa na zaidi ya nyimbo 10 ni shabiki mkubwa wa Yanga akimzimia kiungo mshambuliaji, Athuman Idd 'Chuji' na kimataifa anaishabikia Manchester United, japo anadai alijikuta akiipenda Arsenal kutokana na Gervinho, pia akidai anapenda soka la Cristiano Ronaldo.
"Kwa kweli Chuji ananikosha kwa soka lake, ni moja ya wachezaji wenye vipaji vikubwa vya soka ambao Tanzania tunapaswa kuwaringia, pia nakunwa na Ronaldo jamaa anakila kitu. Anastahili kuwa mchezaji bora wa dunia,"anasema.
Msanii huyo aliyetumbukia kwenye fani ya muziki miaka ya 1990  akianzia kwenye kundi la GMW- Mazimwi anasema lau kama siyo muziki huenda angebobea kwenye soka  kutokana na kuupenda mno mchezo huo akianza kucheza tangu akisoma Shule ya Msingi.
Anasema baada ya kutamba shuleni alizichezea timu kadhaa wakati huyo akifahamika kwa jia la utani kama 'Zico' baadhi ya timu hizo ni Sumu ya Mamba, Inter Milan, Gaza Fc katika michuano ya ligi na ile ya mchangani kabla ya sasa kutulia Golden Bush Veterani.

MUZIKI
KR Mullah aliyezaliwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, alianza kupenda muziki tangu akiwa kinda kwa kupenda kusikiliza nyimbo za wasanii nyota wa zamani kama akina MC Hammer, Kriss Kross kabla ya kujumuika na vijana wenzake kuunda kundi la GMW Mazimwi wakati huo akisoma chuo cha ufundi VETA.
Baadaye aliungana na Juma Nature na kuunda kundi la Wachuja Nafaka kabla ya mwaka 2003 kushirikiana pamoja kuasisi kundi la TMK Wanaume Family ambalo hata hivyo lilikuja kugawanyika na kuzaliwa makundi matatu tofauti, likianza la Wanaume Halisi, kisha Temeke Unity.
Katika mgawanyiko huo huo KR Mullah aliamua kusalia TMK Wanaume Family akiwa na akina Chegge, Mhe Temba, Stico na wengine kabla ya mwishoni mwa mwaka jana kuamua kumfuata Sir Juma Nature katika kundi la Wanaume Halisi na kutoa kazi moja iitwayo 'Umemponza Mdomo'.
Mkali huyo ameshiriki albamu kadhaa za karibu makundi yote aliyowahi kufanya kazi, lakini pia alishatoa albamu yake binafsi iliyofahamika kama 'Kamua kwa Uwezo' na sasa anajiandaa kupakua albamu yake ya pili ambayo imeshatambulishwa na nyimbo kama 'Choo cha Kike' na 'Kelele'.
Nyimbo mbili ambazo anatarajiwa kuzitoa hivi karibuni ni 'Wivu' na 'Masela na Machizi' ambazo zote zitakuwa kwenye albamu hiyo.
KR Mulla akiwa na Rais Jakaya Kikwete
KR Mullah, anasema wimbo huo wa Wivu ndiyo utakaokuwa wa kwanza kutoka amaurekodia katika studio ya kundi lao ya Halisi Records kabla ya baadaye kufuatiwa na Masela na Machizi.
Mkali huyo anayelia na wizi wanaofanyiwa wasanii na kuiomba serikali iwasaidie, anasema hakuna akichukiacho kama 'bifu' za kijinga zifanywazo na wasanii wenzake alizodai zinachangia kurudisha nyuma maendeleo ya muziki.
Anasema siyo vibaya ukawapo ushindani na changamoto za kukuza muziki na siyo bifu za kuwekeana uhasama na hata kufikia wasanii kupigana au kuwa maadui, kwani haisaidii ingawa alikiri jambo hilo lipo hata kwa nyota wa dunia.
Mkongwe huyo anaiasa jamii kupambana kwa vitendo na ugonjwa wa Ukimwi kwa madai mabango na juhudi za serikali na wahamasishaji yameshatosha, huku akiwataka wasanii wenzake kupunguza kutumia dawa za kulevya.
Anasema wasanii hawazuiwi kutumia vilevi kama pombe kiasi kujiburudisha, lakini siyo kuvuka mipaka na kubwia unga au kuvuta bangi kama wehu kwani huwafanya wakose umakini wa kazi yao na kujiingiza katika vitendo viovu.

Ushindi mfululizo waipa jeuri Mtibwa Sugar

Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime
USHINDI wa mechi tatu mfululizo ulioiwezesha kuingia kwenye Tano Bora, umeifanya klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro kujipa matumaini ya ubingwa.
Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania ambao wamekuwa wakitoa dozi nene kwa wapinzani wao kwa mechi zake za karibu, wamesema ligi ya msimu huu haina mwenyewe hivyo hata wao wanaamini wanaweza kutwaa taji mwishowe.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mecky Mexime, alisema ligi ya msimu huu ni ngumu na isiyotabirika na hivyo hawawezi kujiondoa kwenye ubingwa wakati wanazidi kufanya vyema katika mechi zao.
Mexime alisema anachoamini ni vijana wake wazidi kutekeleza maagizo yake na kupata ushindi katika mechi zao ili kurejea mafanikio iliyowahi kupata klabu hiyo kwa kutwaa ubingwa wa Tanzania mara mbili mfululizo.
"Tunashukuru tumepata matokeo mazuri katika mechi zetu za karibuni na hii ni baada ya kurekebisha makosa na sasa tuna matumaini zaidi ya kuwa miongoni mwa timu zinaweza kutwaa ubingwa," alisema.
Kocha huyo aliyewahi kuwa nahodha wa Mtibwa na Taifa Stars, alisema pamoja na ushindi mara tatu mfululizo kwa timu yake hauwafanyi wabweteke badala yake wanajipanga zaidi ili kupata matokeo mazuri zaidi kwa mechi zao zilizosalia.
Kikosi cha timu hiyo yenye maskani yake katika mashamba ya Manungu, Turiani Morogoro, kinatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi kwa kuumana na Coastal Union ya Tanga mechi itakayochezwa uwanja wa Mkwakwani na Mexime alisema wanajipanga ili wafanye vizuri katika mechi hiyo.
Kwa sasa Mtibwa inakamata nafasi ya tano ikiwa na pointi 16 sawa na za Yanga ila inazidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa na mabingwa watetezi hao waliopo nyuma ya mtani wao Simba yenye piointi 19.
Kileleni mwa msimamo mwa ligi hiyo kuna Azam na Mbeya City ambazo zote zina pointi 20 kila moja zikitofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Gaucho akiri 'gemu' kumkataa lakini akwepa mzigo wa lawama

Abdulhalim Humud 'Gaucho'
KIUNGO Mshambuliaji wa Simba, Abdulhalim Humud 'Gaucho' amekiri kwamba hakuwa katika kiwango kizuri katika pambano lao la juzi dhidi ya wapinzani wao wa jadi Yanga, akidai 'gemu' lilimkataa, lakini amesema hadhani kama anapaswa kubebeshwa mzigo wa lawama kwa namna timu ilipocheza katika kipindi cha kwanza.
Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah KIbadeni 'King' alikaririwa akimtupia lawama kiungo huyo kwa matoikeo ya 3-0 iliyopatya timu yake katika kipindi cha kwanza kabla ya kumtoa na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla na Simba kurejesha mabao yote matatu na kulazimisha sare ya mabao 3-3.
Akizungumza na MICHARAZO asubuhi hii Gaucho, alisema anamheshimu kocha wake na anaheshima kauli yake kutokana na Simba kucheza ovyo kipindi cha kwanza, lakini alisema kwake anaamini 'gemu' lilimkataa japo linaloweza kumtopkea mchezaji yeyote duniani.
Gaucho alisema anaamini kocha alimpanga kwa uwezo alionao na alioonyesha katika mechi kadhaa za nyuma, ila bahati mbaya gemu lilimkataa na hivyo kutocheza vyema, japo alisema hapaswi kulaumiwa pekee yake kwani karibu timu nzima ilishindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
"Sijamsikia kocha akiyasema unayoniambia ila kama amenitupia lawama, sidhani kama ni sawa kwa sababu timu nzima katika kipindi cha kwanza hatukucheza vyema na kutimiza wajibu wetu, ila namheshimu kauli yake, japo lazima nikiri kwamba nilijiandaa sana kwa mchezo huo ila 'gemu' lilinikataa," alisema Gaucho.
Mchezaji huyo alirejea Simba akitokea Azam msimu uliopita, alisema kama mchezaji anajisikia vibaya kunyooshewa vidole kwa sababu inaweza kutafisriwa vibaya na mashabiki ilihali amekuwa akijitolea kwa uwezo wake kuhakikisha Simba inafanya vyema.
Kibadeni alionyesha kukerwa na baadhi ya wachezaji akiwamo Gaucho kwa jinsi walivyocheza katika kipindi cha kwanza na Simba kulala mabao 3-0 kabla ya kufanya mabadiliko na kusaidia kurejea mabao yote matatu kupitia kwa Betram Mombeki, Joseph Owino na Kaze Gilbert na kuifanya timu hiyo ipumue katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 19.
Timu hiyo inatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa kuvaana na Coastal Union ya Tanga katika mfululizo wa ligi hiyo iliyopo raundi ya 10 kwa sasa. Mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga.