STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 17, 2010

Super Nyamwela na safari yake kimuzikiKUJITUMA kwake na kiu kubwa ya mafanikio aliyokuwa nayo wakati akichipukia kwenye sanaa ndio silaha kubwa ya mafanikio ya dansa, Super Nyamwela, mmoja wa madansa wakongwe waliodumu katika fani hiyo kwa muda mrefu nchini.
Nyamwela ambaye majina yake kamili ni Hassani Mussa Mohammed, alisema juhudi za mazoezi na kujituma bila kuchoka ndivyo vilivyomfikisha alipo, akimiliki kundi lake binafsi la sanaa pamoja na kuendesha miradi kadhaa ya maduka mbali magari na nyumba ya kuishi.
Nyamwela aliyerejea nchini hivi karibuni akitokea nchi kadhaa za kiafrika kwa ajili ya 'shoo' za kundi lake binafsi, anasema katu hawezi kuidharau sanaa hiyo kwa kuwa imemfanya awe mtu katika watu tofauti na mtazamo wa watu wengi juu ya muziki na sanaa kwa ujumla.
"Leo hii kama sio sanaa hii ya kunengua, pengine nisingefika huko Namibia, Liberia, Afrika Kusini, Botswana na kwingineko kama ilivyokuwa miezi 11 ya ziara yangu katika nchi hizo acha zile ninazoambatana na bendi yangu ya African Stars 'Twanga Pepeta," alisema.
Dansa huyo aliyeanza fani hiyo tangu akiwa kinda, hajutii kwake kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari kwa kuwa hakuna anachokikosa kwa sasa, ingawa mipango yake ni kujiendeleza pale alipoishia.
Akiwa amejinyakulia mataji mbalimbali ya mashindano ya disko nchini likiwemo lile la Mkoa wa Dar es Salaam, alisema safari yake ilianzia alipomaliza elimu ya msingi alipojitosa jumla kwenye fani hiyo aliyokuwa huku akiendelea na 'kitabu'.
Baadae aliungana na wasanii wenzake kadhaa kuunda kundi la Top Family lililotamba pale 'Kwa Macheni' kabla ya kwenda kuasisi kundi la Billbums ambalo lilisheheni wasanii wakali waliokuja kunyakuliwa na bendi ya African Stars.
Tangu awe Twanga Papeta, Nyamwela hajawahi kuhama hata mara moja licha ya kuwepo kwa majaribio kadhaa ya kutaka kumng'oa ASET bila ya mafanikio.
"Sidhani kama nitaondoka Twanga kirahisi, labda kama nitaenda kwenye bendi yangu binafsi ambayo naipigia mahesabu kuja kuunda siku za usoni wakati mambo yangu yamekaa vema, lakini si kwenda bendi zingine za hapa nchini," alisema.
Mkali huyo ambaye amejitumbukiza katika uimbaji na upigaji tumba na dramu, alisema kwa sasa akili zake zote ni kuhakikisha anaiboresha kampuni yake binafsi ya SN Stars Entertainment, ili iendeshwe kisasa na kujitanua nje ya Dar es Salaam.
Nyamwela aliyemaliza kuikarabati nyumba yake iliyopo Mbezi Beach ambayo iliunguzwa kwa moto na watu aliodai 'maadui' zake, alisema mbali na kuiboresha kampuni yake pia malengo yake ni kugeukia kazi ya kurapu na kufyatua filamu izungumziayo maisha yake.
Alisema filamu hiyo itafahamika kwa jina la My Talent ambayo itaanza kurekodiwa mara baada ya kumalizika kwa mfungo wa Ramadhani ikienda sambamba na maandalizi ya albamu yake mpya ya tatu ambayo imeshakilishika wimbo mmoja wa Tumechete.
Albamu yake ya kwanza iliyouza sana ilifahamika kwa jina la Master of the Tample na ile ya pili ni Afrika Kilomondo aliyoiingiza sokoni hivi karibuni ikiwa na nyimbo sita alzioshirikiana na waimbaji mbalimbali akiwemo Ally Choki, Richard Maalifa na Juma Nature.
Kuhusu matukio ambayo hataondoka akilini mwake hadi anaingia kaburini, Nyamwela alisema ni kuunguliwa kwa nyumba yake na kumpoteza mzazi mwenzie, marehemu Halima White.
"Aisee hili la kuunguliwa nyumba na lile la kumpoteza mzazi mwenzangu, marehemu Halima White, ni vigumu kuyasahau," alisema.
Aliongeza, amefarijika baada ya kumpata mwandani wake mpya Upendo Merere ambaye anatarajia kuuona nae hivi karibuni mipango yake ikienda vema, ili waweze kuwalea watoto watatu alionao.
Dansa huyo asiyependa majungu na uvivu kazini alisema atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatamshukuru Mkurugenzi wa ASET Asha Baraka na uongozi na wasanii wote wa bendi ya Twanga Pepeta kwa kushirikiana naye kwa hali na mali.
"Siwezi kumsahau Da Asha Baraka kwa jinsi nilivyokaa naye tangu alipotuchukua toka Billbums hadi leo hii, pia uongozi mzima wa Twanga Pepeta, wasanii na vyombo vya habari vinavyonipa sapoti katika tangu nikiwa kinda katika sanaa hadi leo hii,"
Aliwaasa wenzake kujituma kama yeye na kutokubali kukata tamaa ili waweze kufanikiwa na kubwa ni kuipenda kazi zao na kujithamini wenyewe wakijilinda na ugonjwa wa Ukimwi.
Mkali huyo aliyezaliwa karibu miaka 30 iliyopita huko Zanzibar, alisema kutojidhamini kwa ujumla ndiko kunakopelekea wasanii wengine kutumbukia kwenye maambukizo ya ugonjwa huo.

Mwisho

Jane Misso kuzindua albamu yake Diamond JumapiliMSANII nyota wa muziki wa Injili nchini, Jane Misso kesho anatarajia kuzindua albamu yake mpya na ya pili ya 'Uinuliwe' akisindikizwa na wasanii mbalimbali wa miondoko hiyo wa ndani na nje ya nchi.
Uzinduzi wa albamu hiyo utakaoenda sambamba na kuachiwa hadharani video yake, umepangwa kufanyika mchana wa kesho kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Micharazo, Misso, ambaye ni mchungaji na mwalimu aliyewahi kufanya kazi nchini Uganda kabla ya kujikita kwenye miondoko hiyo na kuachia albamu yake ya kwanza ya 'Umoyo', alisema wasanii karibu wote watakaomsindikiza kesho wameshawasili jijini Dar es Salaam.
Misso aliwataja wasanii waliotua kwa ajili ya kumsindikiza katika uzinduzi wake ni pamoja na Mcongo, David Esengo, Peace Mhulu kutoka Kenya watakoshirikiana na nyota wa Kitanzania wa muziki huo na kwaya mbalimbali kumpambia onyesho lake.
Mwanamama huyo aliwataja wasanii wa Injili wa Tanzania watakaompiga tafu kesho ni Christina Shusho, Upendo Nkone, Martha Mwaipaja, Steve Wambura na Joseph Nyuki.
"Kwaya zitakazonisinidkiza ni pamoja na Joy Bring'res, The Whispers Band, AIC Chang'ombe na kwaya ya Watoto Yatima kutoka Dodoma inayoongozwa na mlemavu wa ngozi, Timotheo Maginga," alisema Misso.
Misso alisema albamu hiyo ina nyimbo sita na baadhi yake zinahamasisha wananchi juu ya ushiriki wao katika Uchaguzi Mkuu wa Taifa wa Urais, Ubunge na Udiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31.
Nyimbo zilizoibeba albamu hiyo ni 'Pokea Sifa', 'Motema', 'Nyosha Mkono Wako', 'Uinuliwe', 'Unaweza Yote' na 'Mimi Najua Neno Moja'.