STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 17, 2010

Jane Misso kuzindua albamu yake Diamond Jumapili







MSANII nyota wa muziki wa Injili nchini, Jane Misso kesho anatarajia kuzindua albamu yake mpya na ya pili ya 'Uinuliwe' akisindikizwa na wasanii mbalimbali wa miondoko hiyo wa ndani na nje ya nchi.
Uzinduzi wa albamu hiyo utakaoenda sambamba na kuachiwa hadharani video yake, umepangwa kufanyika mchana wa kesho kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Micharazo, Misso, ambaye ni mchungaji na mwalimu aliyewahi kufanya kazi nchini Uganda kabla ya kujikita kwenye miondoko hiyo na kuachia albamu yake ya kwanza ya 'Umoyo', alisema wasanii karibu wote watakaomsindikiza kesho wameshawasili jijini Dar es Salaam.
Misso aliwataja wasanii waliotua kwa ajili ya kumsindikiza katika uzinduzi wake ni pamoja na Mcongo, David Esengo, Peace Mhulu kutoka Kenya watakoshirikiana na nyota wa Kitanzania wa muziki huo na kwaya mbalimbali kumpambia onyesho lake.
Mwanamama huyo aliwataja wasanii wa Injili wa Tanzania watakaompiga tafu kesho ni Christina Shusho, Upendo Nkone, Martha Mwaipaja, Steve Wambura na Joseph Nyuki.
"Kwaya zitakazonisinidkiza ni pamoja na Joy Bring'res, The Whispers Band, AIC Chang'ombe na kwaya ya Watoto Yatima kutoka Dodoma inayoongozwa na mlemavu wa ngozi, Timotheo Maginga," alisema Misso.
Misso alisema albamu hiyo ina nyimbo sita na baadhi yake zinahamasisha wananchi juu ya ushiriki wao katika Uchaguzi Mkuu wa Taifa wa Urais, Ubunge na Udiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31.
Nyimbo zilizoibeba albamu hiyo ni 'Pokea Sifa', 'Motema', 'Nyosha Mkono Wako', 'Uinuliwe', 'Unaweza Yote' na 'Mimi Najua Neno Moja'.

No comments:

Post a Comment