STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, September 23, 2013

Yathibitishwa Mtanzania ajeruhiwa tukio la ugaidi Kenya

36
WIZARA ya Mambo ya Nchi za Nje ya Tanzania imesema kuwa hadi kufikia leo Septemba 23, 2013 ni Mtanzania mmoja tu aliyetambulika kwa jina la Bwana Vedastus Nsanzugwanko mwenye cheo cha Umeneja katika kitengo cha Ulinzi wa Watoto, cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Hazina ya Kuhudumia Watoto (Child Protection, UNICEF) ambaye taarifa zake ziliifikia Ofisi ya Balozi kuwa amejeruhiwa kwa risasai na milipuko ya maguruneti kwenye miguu yake yote miwili.

Taarifa hiyo inasema kuwa kwa sasa hali Bwana Vedastus inaendelea vizuri akiwa anapatiwa matibabu alikolazwa katika hospitali ya Aga Khan ya jijini Nairobi, Kenya.

Imetaarifiwa kuwa Ubalozi unaendelea kufuatilia kwa lengo la kupata taarifa zaidi endapo kutakuwepo Watanzania wengine waliodhurika katika tukio hilo.

Ofisi ya Ubalozi kwa kushirikiana na Uongozi wa Chama cha Watanzania nchini Kenya (TWA) unaandaa utaratibu maalumu utakaowezesha TWA kuitikia wito uliuotolewa wa kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wahanga.


Chanzo: Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje

Askari wa Operesheni Kimbunga wafa ajalini


ASKARI Polisi watatu wa operesheni Kimbunga ya kusafisha wahamiaji haramu nchini, wamefariki dunia mjini Kahama kufutia ajali ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Muleba mkoani Kagera kuelekea makambako mkoani Njombe. 
Marehemu hao waliotambulika kwa majina ya Kopolo Fred,PC Subian na PC Michael wote ni askari wa kituo cha Polisi Makambako, na mauti yamewafika baada ya gari nambari PT 0776 Land Rover Diffender kuacha njia na kupinduka. 

MIILI YA ASKARI  IKIWA KATIKA HOSPITALI YA WILAYA YA KAHAMA
Ajali hiyo imetokea katika eneo la Sungamile Kata ya Kagongwa wilayani Kahama wakati dereva wa gari hilo PF3270 PC Yusuph, akijaribu kumkwepa Bibi Kizee mmoja huku gari likiwa kwenye mwendo kasi hali iliyosababisha kumshinda na kupinduka. 
Kijukuu Blog imeshuhudia Majeruhi wanane wakilazwa katika Hospitali ya wilaya ya Kahama wakiwemo askari polisi sita na Afisa uhamiaji wawili, huku magari yanayosafirisha askari kurudi vituoni kwao yakizuiliwa kuendelea na safari na kulala Kahama. 
Kumbukumbu za kipolisi pia zimeonesha kuwa hapo jana jioni askari wengine walipata ajali katika kijiji cha Igusule wilayani nzega ambapo askari 4 wamelazwa katika hospitali ya wilaya Kahama huku mmoja akiwa na hali mbaya. 
Oparesheni Kimbuga ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete, la kuwaondoa wahamiaji haramu nchini, ambapo vikosi vya ulinzi kwa pamoja viliunda kikosi kimoja na kufanya kazi nchini kote.
Kwa hisani ya Kijukuu blog

Mwanamke atajwa kuongoza tukio la kigaidi la Kenya

MWANAMKE raia wa Uingereza, Samantha Lewthwaite aka The White Widow, *anahisiwa* kuongoza kundi la magaidi wa Al-Shabaab walioivamia mall maarufu ya Westgate ya jijini Nairobi nchini Kenya jana na kuwaua watu zaidi ya 68 na kujeruhi wengine zaidi ya 175.



Tayari mashirika makubwa ya habari duniani yakiwemo, CNN, The Sun na IBTimes yameandika habari kuhusu uwezekano wa mwanamke huyo kuwa kiongozi wa magaidi hao walioshambulia Westgate.

Nayo akaunti ya Twitter ya American Jihad Watch ‏@watcherone, imepost picha ya gaidi wa kike iliyedai ilipigwa na camera za ndani ya mall huyo na kudai kuwa ‘huenda’ akawa ni The White Widow. “Female jihadi caught on mall camera at Westgate Centre Shopping mall earlier yesterday may be infamous ‘White Widow’, imesomeka tweet hiyo.


Picha ya gaidi akiwa ndani mall hiyo

Kwa mujibu wa baadhi ya watu waliokolewa kwenye mall hiyo, miongoni mwa magaidi hao alikuwepo mwanamke wa kizungu.

Kwa mujibu wa CNN, magaidi watatu ni wa Marekani, mmoja wa Kenya, Uingereza, Finland na wawili wa Somalia. Bado wamo ndani ya mall hiyo.

Hata hivyo Kwa mujibu wa mtandao wa Telegraph, jana usiku ofisa wa shirika la kupambana na ugaidi Kenya alikanusha taarifa kuwa Samantha Lewthwaite anaweza kuhusika na shambulio la jana.

Samantha Lewthwaite aka The White Widow ni nani?

Ni mwanamke anayetafutwa kwa udi na uvumba kwa kuhusika kwake kwenye matukio mbalimbali ya kigaidi nchini Uingereza na Afrika Mashariki. Yeye ndiye aliyepanga shambulio la kigaidi jijini London la mwaka 2005 lililosababisha vifo vya watu 52 ambapo mume wake Jermaine Lindsay alijitoa muhanga.

Akitokea Aylesbury, Buckinghamshire, nchini Uingereza, The White Widow kwa sasa ni kiongozi wa juu wa mashambulio ya Al Shabaab nchini Kenya na Somalia. Mwanamke huyo anadaiwa kuwa mfadhili mkuu wa shughuli za kundi hilo la kigaidi.

Mwezi May hati ya kumkamata ilitolewa baada ya kushindwa kufika mahakamani nchini Kenya kwa kesi ya kutengeneza bomu.

*anahisiwa* – Habari haijathibitishwa

Msiba! Ajali zaua watu zaidi ya 20 Mbeya, Dodoma

WATU  13 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa vibaya katika matukio mawili ya ajali za barabarani zilizotokea katika mikoa ya Mbeya na Dodoma usiku wa kuamkia leo.

Habari toka Dodoma zinasema watu sita watatu wanaotajwa kuwa na uhusiano wa kidugu wamefariki baada ya basi ya Al Saedy linalofanya safari zake kati ya Dar na Dodoma kugongana uso kwa uso na lori eneo la Chalinze mkoani humo  majira ya saa 4 usiku.

Nako Mbeya watu wengine saba nao walipoteza maisha katika ajali mbaya huku watu zaidi ya 10 wakiwaachwa hoi kwa majeraha mabaya katika ajali iliyohusisha daladala aina ya Toyota Hiace kwa kilichoelezwa mwendo kasi na kufeli kwa breki.

Kwa tukio la Dodoma lililotokea usiku wa saa 4 inaelezwa watu waliofariki ni waliokuwa ndani ya lori hilo ambapo wanandugu watatu akiwamo dereva walipoteza maisha papo hapo sambamba na utingo wa gari hilo na wengine ni wale waliokuwa kwenye basi hilo la Al Saedy.

Kwa ajali ya Mbeya wengi wa waliofariki ni abiria wa 'kipanya' na kondakta wake na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Diwani Athuman amewakumbusha madereva kuwa waangalifu wawapo barabarani.

Ajali hizo zimetokea wakati Tanzania ikiwa ndani wa Wiki ya Nenda kwa Usalama.

 Lori la mizigo lililogongana uso kwa uso na basi la Al - Saedy lililokuwa likitoka Dar Es salaam kuelekea Mkoani Dodoma jana usiku linavyofanana baada ya kugongana na basi hilo uso kwa uso
 Basi la Al Saedy linavyoonekana mara baada ya kugongana na lori la Mizigo Maeneo ya Chalinze Mkoani Dodoma Jana Usiku
Basi la Al Saedy linavyoonekana mara baada ya kugongana na lori la Mizigo Uso Kwa Uso jana usiku eneo la Chalinze Mkoani Dodoma.

Mateka wazidi kuokolewa Kenya, ila hali bado tete


KENYA imesema mateka wachache wamebaki ndani ya maduka ya kifahari ya Westage Mall yaliyovamiwa na wanamgambo wa kiislamu wa Al- shabab Jumamosi ambapo dazani za watu wameuwawa.

Kundi la kigaidi la wanamgambo la Al- shabab limedai kuhusika na shambulizi likisema kuwa linajibu kuhusu majeshi ya Kenya yaliyoko katika operesheni nchini Somalia.

Majeshi ya Kenya yalianza kufanya mashambulizi Jumapili  jioni katika maduka hayo ya kifahari ya Westage Mall kuokoa watu waliokuwa wamejificha au kushikiliwa mateka na watu wenye silaha.

Waziri wa mambo ya ndani Joseph Ole Lenku, aliuambia mkutano wa waandishi wa habari Jumatatu kwamba vikosi vya Kenya sasa vinadhibiti kila ghorofa la jengo hilo na tayari yameokoa takriban mateka wote waliokuwa wamebaki ndani.

Amesema watu wawili waliokuwa na silaha waliuwawa katika operesheni za kijeshi zinazoendelea na wanajeshi 10 wa vikosi vya usalama wamejeruhiwa.

Lenku alizungumza kwa karibu dakika 90 baada ya mashahidi kusikia milipuko mikubwa iliyokuwa inatokea kwenye Mall ikifuatiwa na milio ya bunduki. Moshi mkubwa mweusi bado unaendelea kufuka kutoka kwenye Mall baada ya milipuko hiyo. Lenku anasema wanamgambo walichoma moto magodoro ili kuvuruga hali.

Amesema watu 62 wameuwawa tangu shambulizi hilo lilipozuka Jumamosi ambapo
Shirika la msalaba mwekundi la Kenya limetoa idadi ya vifo kuwa ni 69 huku 175 wakiwa wamejeruhiwa na takriban watu wengine 65 hawajulikani walipo.


Hizi ndizo filamu zitakazoonyeshwa katika Tamasha la Filamu Dar linaloanza kesho




Yanga, Azam yafunika mapato ya Simba, Mbeya City


Simba
Yanga
Na Boniface Wambura
PAMBANAO la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Azam na Yanga lililochezwa jana (Septemba 22 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 138,188,000, ikifunika yake ya mechi ya Simba na Mbeya City iliyoingiza Sh..

sh. 123,971,000.
Katika pambano la Yanga na Azam, jumla ya watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 33 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 walikuwa 24,020.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 33,065,409.1 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 21,079,525.42.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 16,812,919.89, tiketi sh. 5,022,342, gharama za mechi sh. 10,087,751.93, Kamati ya Ligi sh. 10,087,751.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,043,875.97 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,923,014.64.

Mechi iliyopita ya VPL kwenye uwanja huo kati ya Simba na Mbeya City iliingiza sh. 123,971,000.

Katika mechi ya Jumamosi kati ya Simba na Mbeya City, jumla ya

watazamaji 21,936 ndiyo waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 32 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 30,064,741.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 18,910,830.51.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 15,287,156.92, tiketi sh. 3,145,790, gharama za mechi sh. 9,172,294.15, Kamati ya Ligi sh. 9,172,294.15, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 4,586,147.08 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,567,003.28.

Issa Matumla anyukwa kwa KO


Bondia Adamu Ngange (kushoto) akichapana na Issa Matumla,  wakati wa pambano lao lililofanyika jana jumapili katika ukumbi wa Kilimahewa uliopo Chanika Kigogo Fresh. Katika pambano hilo, Ngange alishinda kwa KO katika raundi ya pili.  
Mwamuzi, Saidi Chaku (kulia) akimpa huduma ya kwanza bondia Issa Matumla, baada ya kugaragazwa kwa ngumi na bondia Adamu Ngange.
Bondia Antony Mathias (kulia) akimpiga ngumi mfululizo bondia Ismail Ninja, wakati wa mpambano wao.
Bondia Antony Mathias akiwa amebebwa juu baa ya kupata ushindi wa KO
Mdau wa mchezo wa masumbwi, Halima Kaubanika, akiwa ni mmoja kati ya wadau waliojitokeza kufuatilia mchezo huo jana.

Tamasha la Filamu Dar es Salaam kuzinduliwa rasmi kesho Dar

Dar Films Festival hiyooooo!
TAMASHA la siku tatu la filamu lifahamikalo kama 'Dar Filamu Festival (DFF)-2013' linatarajiwa kuzinduliwa kesho kwa semina ya mafunzo ya uigizaji, utayarishaji, uongozaji na uandishi wa miswada wa filamu inayofanyika Chuo Kikuu Idara ya Sanaa.
Mabalozi wa tamasha hilo, Vincent Kigosi 'Ray'  na Elizabeth Michael 'Lulu' ndiyo watakaonogesha tamasha hilo kwa siku hizo tatu kabla ya kufungwa Alhamisi ambapo  mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Dk Funella Mukangara.
Akizungumza na MICHARAZO mapema leo, mmoja wa waratibu wa tamasha hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano wa mtandao wa filamucentral na kampuni ya Haak Neel Production. Myovela Mfwaisa, alisema tamasha hilo litafanyikia viwanja vya Chuo cha Posta.
Mfwaisa alisema mbali na semina hiyo ya mafunzo pia leo kwenye uzinduzi kutakuwa na uonyeshwaji wa filamu nne za kibongo na utaratibu huo utafanyika siku zote tatu.
"Tamasha letu la DFF litazinduliwa rasmi Jumanne kwa semina ya mafunzo juu ya uigizaji, uandishi wa miswada, utayarishaji na uongozaji wa filamu chini wa wakufunzi toka Chuo Kikuu na jioni kutakuwa na uonyeshwaji wa filamu nne tofauti," alisema.
Mfwaisa alisema mabalozi wa tamasha hilo ni Mtayarishaji na Muongozaji Bora wa 2011-2012, Vincent Kigosi 'Ray' na Elizabeth Michael 'Lulu' ma kwamba watatumia kuonyesha kazi za kitanzania za lugha ya Kiswahili tu kwa mwaka huu .
Alisema keshokutwa itakuwa zamu ya makampuni ya kuzalisha na kusambaza filamu nazo zitakuwa na wasaa wao wa kutangaza kazi zao kwa wadau kabla ya siku ya mwisho kutakuwa na mjadala wa mustakabali wa filamu nchini utakaohusisha taasisi kama TRA, Bodi ya Ukaguzi wa Filamu, wasambazaji wa filamu na taasisi nyingine.