STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 24, 2013

Baada ya kung'ara Gor Mahia, Ivo Mapunda awindwa na Tusker

http://4.bp.blogspot.com/_JI2CjMwyBpw/RuQM81wihfI/AAAAAAAAAqU/fNdStm7uFF0/s400/IVO-MAPUNDA.jpg
Ivo Mapunda
KIPA nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda anayeidakia Gor Mahia ya Kenya, amesema yupo katika harakati ya kuhamia kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya, Tusker.
Hata hivyo kipa huyo aliyewahi kuichezea Bandari-Kenya kabla ya kutua Gor Mahia, alisema anasubiri kwanza kumalizika kwa mkataba wake mwishoni mwa mwaka huu kuamua hatma yake.
Alisema kocha wa Tusker, Robert Matano alimpigia simu mara baada ya kung'ara katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya 8 Bora ili kujua mkataba wake ukoje kabla ya kumvuta Tusker.
Mapunda aliyechaguliwa Mchezaji Bora wa pambano hilo lililoisha kwa suluhu ya kutofungana, lakini Tusker ikisonga mbele kwa ushindi wa bao 1-0 iliyopata katika mechi ya awali, alisema iwapo Tusker itamvutia kimasilahi atahamia kwa mabingwa hao wa ligi.
"Nitaangalia masilahi kwanza kama jamaa nibaki Gor Mahia au kujiunga na Tusker, ila nasubiri kwamba mkataba wangu na klabu yangu ya sasa uishe Desemba mwaka huu," alisema Mapunda.
Kuhusu mafanikio anayoyapata akiwa Kenya, kipa huyo aliyewahi kuidakia Prisons Mbeya na St George ya Ethiopia alisema yanamfariji mno baada ya kupuuzwa nyumbani akionekana kaisha.
"Nafurahia mno kupata mafanikio ugenini na kuthaminika naamini Mungu ataendelea kunisaidia zaidi na kutamba," alisema.
Mapunda ambaye amekuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Gor Mahia anatarajiwa kuiongoza timu yake Jumapili ikiwa ugenini katika mji wa Mumias dhidi ya Western Stima katika mechi ya Ligi.

HATIMAYE HARUNA NIYONZIMA ASAINI MIAKA MIWILI YANGA SC


Uongozi wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom  klabu ya Young Africans leo umekata mzizi wa fitina kwa kiungo mchezeshaji kutoka nchini Rwanda Haruna Niyonzima kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili kufuatia kumalizika kwa mkataba wake awali.
Akiongea na waandishi wa habari makao ya klabu ya Yanga, katibu mkuu Lawrence Mwalusako amesema wameamua kumuongezea mkataba mchezaji huyo kufuatia kuuhitaji mchango wake kwani katika kipindi chake cha miaka miwili ameonyesha kiwango cha hali ya juu na kutoa mchango mkubwa.
 Mwalusako amesema kumekua yakiongelewa mengi juu ya mchezaji wetu Niyonzima, baadhi ya vyombo vya habari vimekua vikitoa taarifa za kupotosha juu yake ukweli leo umedhihirika kwamba Niyonzima ni mchezaji wa Yanga na ataendelea kuitumikia kwa miaka miwili.
Haruna Niyonzima alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza Julai 2011 akitokea katika timu ya APR nchini Rwanda ambapo katika miaka yake miwili aliyoichezea timu ya Yanga amefanikiwa kuisadia kupata makombe mawili ya ubingwa wa Ligi Kuu 2012-2013 na Kombe la Kagame 2011-2012.
Naye Niyonzima amesema anawashukuru wanachama, washabiki na wapenzi wa klabu ya Yanga kwa kuwa naye muda wote, Yanga ni nyumbani kwangu kwani najisikia furaha kuichezea timu hii na malengo yangu ni kuisadia ili iweze kufanya vizuri katika upatashindano ya kimataifa.
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya klabu ya Yanga Abdallah BinKleb amesema palikua na propaganda nyingi juu ya Niyonzima, lakini ukweli ndio huu Niyonzima ataendelea kuitumikia klabu ya Yanga kwa miaka miwili.
"Tunautambua mchango wake alioutoa kwa miaka mwili kwani ameweza kutupatia vikombe viwili vya Ligi Kuu ya Vodacom na Kombe la Kagame hivyo tumemuongezea mkataba wa miaka miwili tena ili aendelee kutoa mchango wake na kuisadia timu katika michezo ya kimataifa" alisema BinKleb.

Credit:Global Publishers

Banana Zorro, Khadija Kopa kupamba Miss Ukonga kesho

http://1.bp.blogspot.com/_GKcbi1xLxZk/TSxkdhS4gjI/AAAAAAAAH0U/FmAGrzZ0XLc/s400/IMGP0489.JPG
Banana Zorro na mmoja wa waimbaji wake wa B-Band wakitumbuiza

http://1.bp.blogspot.com/-Jqs6ERoQU2M/TvC57BGBQ_I/AAAAAAAAGQw/A8s-FsEMnZs/s1600/kopa.jpg
Khadija Kopa
WASANII nyota nchini Banana Zorro na bendi yake ya B-Band pamoja na Malkia wa Mipasho, Khadija Kopa kesho wanatarajiwa kuwasinidikiza warembo 17 watakaochuana kuwania taji la urembo la Redd's Miss Ukonga 2013, litakalofanyika jijini Dar es Salaam.
Warembo hao watachuana kwenye shindano litakalofanyika kwenye ukumbi wa Wenge Garden na kusindikizwa na burudani ya wasanii hao wanaotamba nchini na nyimbo mbalimbali.
Mratibu wa shindano hilo, Rashid Kazumba aliiambia MICHARAZO kuwa jumla ya warembo 17 watachuana kuwania taji hilo sambamba na kuwania nafasi ya kuwania ushiriki wa shindano la Miss Ilala litakalofanyika baadaye.
Kazumba alisema maandalizi kwa ujumla kwa ajili ya kinyang'anyiro hicho yamekamilika na kwamba inasubiriwa tu kuona nani atakayeibuka kidedea usiku wa kesho.
Aliwataja baadhi ya warembo watakaochuana katika shindano hilo lililodhaminiwa na makampuni kadhaa nchini ni pamoja na Glory Jigge, Happiness Jackson, Flosek Mwakanyamale, Annatolia Raphael, Musnat Hassan, Gift Swai, Natasha Mohamed, Vanessa Magule, Queen John, Martha Gewe, Nancy Obasi, Mwanamkasi Bakari na Diana Joachim.Klabu za Ligi Kuu kupigwa msasa kuhusu usajili wa TMS
Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina ya usajili kwa njia ya mtandao (Transfer Matching System-TMS) kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kwa ajili ya msimu wa 2013/2014.

Semina hiyo itafanyika Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF saa 3 kamili asubuhi ikishirikisha watu wawili kutoka kila klabu ambao ni TMS Manager, na ofisa mwingine wa klabu.

Klabu za ligi hiyo zinazotakiwa kuhudhuria semina ya usajili ni Ashanti United, Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Kagera Sugar, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, Oljoro JKT, Rhino Rangers, Ruvu Shooting, Simba, Tanzania Prisons na Yanga.

Semina hiyo huenda ikazisaidia klabu za ligi hiyo ambao mara kadhaa wamekuwa wakiingia mkenge katika zoezi la usajili wa wachezaji kutokana na mfumo huo mpya kuwakanganya kama ilivyojitokeza msimu huu ulioisha katika usajili wa mchezaji Mbuyi Twitte aliyegombewa Simba na Yanga.

Banka kuitema Bandari-Kenya, huenda akarejea nyumbani au....!


Banka (kushoto) akiwa na wachezaji wenzake wa Kitanzania wanaocheza wote Bandari-Kenya
KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa nchini Kenya, Mohammed Banka amesema hafikirii kuongeza mkataba mpya na timu yake ya Bandari Kenya bila kueleza sababu.
Banka, alisema kuna mambo mawili kichwani mwake baada ya kuisha kwa mkataba wake na klabu hiyo yenye maskani yake Mombasa, ama arejee nyumbani au kujiunga na timu nyingine.
Kiungo huyo alisema mkataba wake unatarajiwa kuisha miezi miezi mwili ijayo na hivyo hajaamua kuongeza mkataba mpya zaidi ya kutaka kuondoka klabuni hapo.
"Tunamalizia duru la kwanza Jumapili kwa kuumana na Sofapaka na mimi ndiyo namalizia mkataba wangu na sifikirii kuongeza tena zaidi ya kurudi nyumbani au kusonga mbele," alisema Banka.
Mchezaji huyo aliyekuwa miongoni mwa walioipandisha Ligi Kuu timu hiyo ambayo kwa sasa ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa timu 16, alisema haoni sababu ya kubaki Bandari bila kufafanua.
Hata hivyo hivi karibuni mchezaji huyo alidokeza kuna mambo hayapo sawa hasa suala la masilahi tofauti na makubaliano yaliyokuwepo kati yake na uongozi wa timu hiyo ilipopanda daraja.


TFF yasisitiza wenyeviti wa FA ndio wasimamizi wa RCL
Na Boniface Wambura
WAKATI mechi za kwanza za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zinachezwa wikiendi hii, Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesisitiza kuwa wasimamizi wa mechi za ligi hiyo ni wenyeviti wa mikoa wa vyama vya mpira wa miguu.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Ramadhan Nassib ilikutana jana (Mei 23 mwaka huu) kupitia ripoti za makamishna kwa mechi za raundi ya kwanza ya RCL iliyomalizika wikiendi ya Mei 18 na 19 mwaka huu.

Kuhusu viwanja vinavyotumika kwa ligi hiyo, Kamati imesema vitaendelea kuwa vile vya makao makuu ya mikoa, na kwa vile vilivyokuwa vimeombwa vifanyiwe marekebisho ili viweze kukaguliwa kwa ajili ya RCL msimu ujao. Pia imeitaka mikoa kuendelea kuboresha viwanja vinavyotumika sasa, lakini vina upungufu.

Vilevile Kamati imebaini kuwa zimekuwepo pingamizi kuhusu usajili wa wachezaji ambapo imesema haiwezi kujadili pingamizi hizo kwa vile mikoa yote haikuwasilisha usajili wa wachezaji wa klabu husika uliofanyika mikoani kama ilivyoagizwa na kuelekezwa na TFF.

Hata hivyo, Kamati imeitaka mikoa ambayo klabu zao zimefanikiwa kuingia raundi ya pili kuwasilisha usajili huo haraka.

Pia Kamati imebaini kuwa zipo baadhi ya klabu ambazo zimekata rufani kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji, na kusisitiza kilichowasilishwa ni pingamizi kwa vile kwa mujibu wa kanuni masuala ya uwanjani hayakatiwi rufani. Hivyo, Kamati imeshauri klabu zilizokata rufani zilirejeshewe ada zilizolipa kwa ajili hiyo.

Makamishna na waamuzi wanaosimamia mechi za RCL wamekumbushwa kuwa ili mchezaji aruhusiwe kucheza mechi ni lazima awe na leseni yake (kadi ya usajili), vinginevyo asiruhusiwe kucheza mechi husika.

Mechi za RCL zinaendelea wikiendi hii ambapo zote zitachezwa Jumapili (Mei 26 mwaka huu) isipokuwa mechi kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na African Sports ya Tanga itakayochezwa Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi.

Nayo mechi kati ya Abajalo ya Dar es Salaam na Kariakoo ya Lindi iliyokuwa ichezwe Jumamosi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam sasa itachezwa Jumapili kwa vile siku hiyo uwanja huo utatumika kwa mazoezi ya Taifa Stars.

Mechi nyingine za RCL zitakazochezwa Mei 26 mwaka huu ni Machava FC ya Kilimanjaro dhidi ya Mpwapwa Stars ya Dodoma kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara na Biharamulo FC ya Kagera zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ni kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya Katavi.

Nayo Kimondo SC ya Mbeya itakuwa mgeni wa Njombe Mji ya Njombe katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe. Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.

Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.

Sasa ruksa kwa Dk Slaa kuoana na mchumba wake Josephine Mushumbuzi

http://1.bp.blogspot.com/-X80Lpg2l-A8/TxjnMk-zMpI/AAAAAAAASwo/6mhA0f67CBQ/s640/dkt+slaa.jpg
Dk Slaa (kulia) na mchumba wake, Josephine Mushumbuzi


HATIMAYE Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, imetupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na aliyekuwa mume wa Josephine Mshumbusi, ambaye ni mchumba wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbroad Slaa, Mahimbo baada ya kuiona rufaa hiyo haina msingi wowote kisheria.Hukumu hiyo ya rufaa ya  madai ya ndoa Na.32/2012 ilitolewa jana na Hakimu Aniseth Wambura ambapo alisema mahakama yake imefikia uamuzi huo wa kuitupa rufaa hiyo kwasababu haina mantiki ya kisheria.Hakimu Wambura alisema mahakama yake imekubalina na hukumu iliyotolewa Aprili 2012 na Mahakama ya Mwanzo Sinza katika kesi ya madai talaka iliyokuwa imefunguliwa na Mshumbusi anayetetewa na wakili wa kujitegemea Philemon Mutakyamilwa  dhidi ya Maimbo ambapo mahakama hiyo ya chini ilitangaza kuwa hakukuwa na ndoa baina ya watu hao kwasababu Maimbo alikuwa ni mzinzi, simwaminifu katika ndoa yake na alikuwa akimtesa mkewe.“Baada ya mahakama yangu kusikiliza hoja za mwomba rufaa na mjibu rufaa ,mahakama hii imefikia uamuzi wa kukubali hoja za Mshumbisi kuwa kwa tabia ile ya mbaya ya uzinzi na ukosefu wa uaminifu katika ndoa yake hapakuwepo na ndoa baina yao hivyo mahakama yake inatangaza kuwa hukumu ya mahakama ya Mwanzo Sinza ambayo iliivunja ndoa hiyo ilikuwa hukumu sahihi “alisema hakimu Wambura.Akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo wakili Mutakyamilwa alisema amefurahishwa na hukumu hiyo kwani mahakama imetenda haki  kwasababu kesi hiyo ya madai ya talaka ilikuwa na msukumo wa siasa chafu zilizokuwa na lengo chafu la kumchafulia jina mteja wake(Mshumbusi) ambaye kwa sasa ni mzazi mwenzie Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.Wilbroad Slaa.
Kutokana na hali ni wzi kwamba Dk Slaa sasa wanaweza kuoana na mpenzi wake huyo waliyezaa naye mtoto mmoja.

Chegge, Mhe Temba wanaswa na Maringo 7


Mhe Temba na Chegge

Maringo Saba katika pozi
MCHEKESHAJI anayetamba kwenye kipindi cha Mizengwe, Rashid Costa 'Maringo 7' amewajumuisha wakali wa muziki wa kizazi kipya nchini, Said Chegge, Mheshimiwa Temba na 'bosi' wao Saidi Fella kwenye filamu yake anayotarajia kuitoa hivi karibuni.
Maringo 7 aliyewahi kutamba na michezo ya kuigiza ya kwenye runinga akiwa na kundi la Shirikisho Msanii Afrika, alisema filamu hiyo itafahamika kwa jina la 'Papaa' na atawashirikisha wakali hao na nyota wengine wa filamu nchini.
"Nipo katika maandalizi ya mwisho ya kukamilisha filamu yangu mpya itakayoitwa 'Papaa' ambayo mbali na kucheza mimi na nyota wengine wa filamu, pia ndani mwake kutakuwa na Said Fella, Mhe. Temba, Said Chegge na YP," alisema Maringo 7.
Maringo 7, alisema ana imani kazi hiyo itathibitisha kipaji alichonacho katika sanaa ya uigizaji na muziki, fani anazozifanya kwa wakati mmoja kwa sasa.

Salha, Hammer Q watoa albamu ya Mke na Mume

Salha Abdallah na mumewe Hammer Q
MUIMBAJI nyota wa taarab wa kundi la Dar Modern, Salha Abdallah akishirikiana na mumewe Husseni Mohammed 'Hammer Q' wamekamilisha kurekodi nyimbo tatu mpya kwa ajili ya kutoa albamu yao.
Akizungumza na MICHARAZO, Salha ambaye 'amelitosa' kundi la Five Star lililokuwa limetangaza kumnyakua hivi karibuni, alisema nyimbo mbili kati ya hizo zipo katika miondoko ya taarab na wimbo mwingine upo katika mahadhi ya mchiriku.
Salha aliyeripotiwa kupewa kipigo kikali na mumewe huyo kiasi cha kulazwa hospitalini kabla ya kusameheana, alizitaja nyimbo hizo tatu kati ya nne walizopanga kuwamo katika albamu hiyo kuwa  ni 'Tunaoana', 'Safiri Salama' na 'Nisamehe Tusonge Mbele'.
"Wimbo wa 'Nisamehe Tusonge Mbele' upo katika mahadhi ya Mchiriku na nyingine zipo katika miondoko ya taarab na kibao cha mwisho ambacho tutakirekodi baadaye ni ule wa 'Subhana Heri'," alisema Salha.
Muimbaji huyo aliyeingia kwenye fani hiyo mwaka 2008 kwa kuvutiwa na sauti tamu ya marehemu Mariam Khamis, alisema wameanza kutoa albamu hiyo lakini mipango yao ya baadaye kuja kuanzisha kundi lao ili kuepuka kuwatumikia watu.
"Tuna mipango ya kuja kuanzisha kundi letu wenyewe baada ya kufanya kazi kwa watu kwa kipindi kirefu bila ya kupata mafanikio yoyote ya maana," alisema Salha

TP Mazembe yamnyakua kocha wa Mali


https://lh6.googleusercontent.com/-VEtRhDY7qrI/UZzx8PeR2fI/AAAAAAAAlAE/izjc83pUpI8/patrice-carteron-dijon5.jpg?imgmax=800
Kocha Patrice Carteron

LUBUMBASHI, Congo DR
KAMPENI za Mali za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zilipaa juzi Jumatano wakati kocha wao Patrice Carteron  aliposaini mkataba wa miaka miwili na klabu ya TP Mazembe ya Congo.
Mali, ambayo chini ya kocha huyo Mfaransa ilimaliza ya tatu katika fainali ya Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini, ina mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Rwanda na Benin Juni 9 na Juni 16.
"Tunamtambua Patrice Carteron kama kocha wa Mali," rais wa shirikisho la soka la nchi hiyo Hamadoun Kola Cisse alisema katika mahojiano na kituo cha radio cha Ufaransa.
"Yuko katika mkataba hadi mwakani lakini kwa kwenda kusaini mkataba mwingine anajiweka matatani," Cisse alisema.
Katika muda huo huo wa mahojiano, beki wa zamani wa klabu za St Etienne na Sunderland, Carteron (42) alikuwa alikuwa akitambulishwa hadharani kwenye Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi.
"Hatuna pingamizi kwa Carteron kuiongoza Mali katika mechi zao mbili zijazo Juni licha ya kusaini mkataba nasi," mwenyekiti Moise Katumbi alisema.

JK awatia moyo Stars kwa Morocco

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Taifa Stars jana Ikulu

Wachezaji wa Stars wakijifua kwa mazoezi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amewaambia wachezaji wa timu ya taifa ya soka (Taifa stars) kwamba wanaweza kuwafunga tena Morocco katika mechi yao ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 mjini Marrakech kama walivyowafunga jijini Dar es Salaam katika mechi yao ya awali.
Stars watarudiana na Morocco Juni 7 katika mechi yao ya nne ya hatua ya makundi baada ya kuwashushia kipigo kilichoishangaza "dunia ya soka" cha magoli 3-1 katika katika mechi yao ya awali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na timu hiyo wakati alipoialika Ikulu kwa ajili ya mlo wa mchana jana, Rais Kikwete alisema: "Maadamu mliwashinda mara ya kwanza, hakikisheni mnawashinda tena kwa kuwa mkishinda tunafurahi sana na mkishindwa tunanyong’onyea sana."
Rais Kikwete aliiambia timu hiyo kuwa uwezo waliouonesha katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu kwa fainali hizo dhidi ya Gambia ambayo walishinda 2-0, na kisha kuisambaratisha Morocco 3-1, zinathibitisha uwezo mkubwa walionao Watanzania katika mchezo huo na kwamba cha muhimu ni kujiamini.
Aidha, amempongeza kocha wa timu hiyo Kim Poulsen pamoja na Kamati ya Ushindi ya Taifa stars kwa kuisaidia timu hiyo kwa hali na mali ili iweze kushinda na hatimaye iweze kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia kucheza fanali za Kombe la Dunia. Stars itahitaji kucheza mechi tano kishujaa ili kwenda Brazil 2014.
Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo nchini ili kupambana na changamoto zinazoikabili timu hiyo ili kuiwezesha kufanya vizuri.
Kwa upande wake kocha Poulsen alimshukuru Rais Kikwete kwa kuwakaribisha na kuwatia moyo ambapo aliahidi kuifundisha vizuri timu hiyo ili kuhakikisha kuwa wanafanya makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa  timu hiyo, Juma Kaseja alimshukuru Rais Kikwete na kuahidi kuhamasishana kujituma kwenye mazoezi na hatimaye kutimiza ndoto za Watanzania.
Taifa Stars iko Kundi C la kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014, ikiwa na pointi 6, moja nyuma ya vinara, Ivory Coast. Morocco ni ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi mbili na Gambia inaburuta mkia ikiwa na pointi moja.

Yanga kujipima kwa Rayon kabla ya kwenda Darfur kutetea Kagame


Kikosi cha Yanga
MABINGWA watetezi wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), Yanga wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Rwanda, Rayon kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mwezi ujao.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, alisema kuwa wamepokea barua ya mwaliko huo kutoka kwa mratibu wa mechi hiyo lakini bado hawajathibitisha hadi kocha Mholanzi Ernie Brandts atakapotoa maelekezo.
Mwalusako alisema kwamba mechi hiyo wakiipata itakuwa ni nzuri kwa kuwaandaa wachezaji kuelekea Sudan na vile vile ni nafasi kwa Yanga kuwapa heshima mashabiki wake wa kanda ya ziwa kuiona timu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara.
"Ni kweli taarifa za mechi hiyo tunayo, lakini majibu rasmi hatutawapa na siku ya mchezo pia haijapangwa ila wamependekeza iwe mapema mwezi ujao," alisema Mwalusako.
Naye mmoja wa viongozi wa Rayon, Clever Kazungu, alithibitisha timu yake kupokea mwaliko huo na kusema kwamba wako tayari kuja nchini endapo watafikia makubaliano na waandaaji wa mchezo.
Kazungu alisema tayari wameambiwa kuwa watalipiwa gharama ya malazi, chakula na posho ya wachezaji kwa siku watakazokuwa hapa nchini.
Yanga itaanza kampeni za kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame kwa kuivaa Express ya Uganda katika mechi ya kundi C itakayofanyika Juni 20 kwenye Uwanja wa Elfasher saa nane mchana wakati Simba iliyopangwa kundi A itashuka dimbani siku inayofuata kuivaa El Mereikh.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Bara watashuka tena dimbani Juni 22 mwaka huu kuikabili Ports na watakamilisha mechi za hatua ya makundi Juni 25 kwa kuvaana na Vital'O.
Simba watashuka tena kusaka ubingwa wa michuano hiyo Juni 23 kwa kupambana na APR na watamaliza dhidi ya Elman Juni 26.
Yanga pia huenda ikawavaa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Zanzibar, KMKM, katika mechi nyingine ya kirafiki inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.