STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 24, 2013

JK awatia moyo Stars kwa Morocco

Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Taifa Stars jana Ikulu

Wachezaji wa Stars wakijifua kwa mazoezi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amewaambia wachezaji wa timu ya taifa ya soka (Taifa stars) kwamba wanaweza kuwafunga tena Morocco katika mechi yao ya marudiano ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 mjini Marrakech kama walivyowafunga jijini Dar es Salaam katika mechi yao ya awali.
Stars watarudiana na Morocco Juni 7 katika mechi yao ya nne ya hatua ya makundi baada ya kuwashushia kipigo kilichoishangaza "dunia ya soka" cha magoli 3-1 katika katika mechi yao ya awali jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na timu hiyo wakati alipoialika Ikulu kwa ajili ya mlo wa mchana jana, Rais Kikwete alisema: "Maadamu mliwashinda mara ya kwanza, hakikisheni mnawashinda tena kwa kuwa mkishinda tunafurahi sana na mkishindwa tunanyong’onyea sana."
Rais Kikwete aliiambia timu hiyo kuwa uwezo waliouonesha katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu kwa fainali hizo dhidi ya Gambia ambayo walishinda 2-0, na kisha kuisambaratisha Morocco 3-1, zinathibitisha uwezo mkubwa walionao Watanzania katika mchezo huo na kwamba cha muhimu ni kujiamini.
Aidha, amempongeza kocha wa timu hiyo Kim Poulsen pamoja na Kamati ya Ushindi ya Taifa stars kwa kuisaidia timu hiyo kwa hali na mali ili iweze kushinda na hatimaye iweze kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia kucheza fanali za Kombe la Dunia. Stars itahitaji kucheza mechi tano kishujaa ili kwenda Brazil 2014.
Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo nchini ili kupambana na changamoto zinazoikabili timu hiyo ili kuiwezesha kufanya vizuri.
Kwa upande wake kocha Poulsen alimshukuru Rais Kikwete kwa kuwakaribisha na kuwatia moyo ambapo aliahidi kuifundisha vizuri timu hiyo ili kuhakikisha kuwa wanafanya makubwa.
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, nahodha wa  timu hiyo, Juma Kaseja alimshukuru Rais Kikwete na kuahidi kuhamasishana kujituma kwenye mazoezi na hatimaye kutimiza ndoto za Watanzania.
Taifa Stars iko Kundi C la kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014, ikiwa na pointi 6, moja nyuma ya vinara, Ivory Coast. Morocco ni ya tatu kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi mbili na Gambia inaburuta mkia ikiwa na pointi moja.

No comments:

Post a Comment