STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 9, 2014

Kiemba yupo kikazi zaidi Msimbazi

http://4.bp.blogspot.com/-TTjBvlaY9Hg/UYeEmUfOZEI/AAAAAAAAhoU/eRmNzAsJ9U0/s640/AMRIKIEMBASIMBA.jpg
Amri Kiemba kishangilia moja ya mabao yake
 KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Amri Kiemba, amesema kwa sasa hana muda wa kupiga blabla kwenye vyombo vya habari na badala yake anaelekeza ngumu na kuwaonyesha mashabiki wa kandanda kipi anachokifanya uwanjani.
Akizungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu toka Zanzibar, Kiemba alisema anaamini wote ambao walikuwa na maoni tofauti dhidi yake watakuwa wamepata salama kutokana na kile anachokifanya.
Kiemba alisema kutokana na hilo kwa sasa ameamua kufunga mdomo wake kuzungumza lolote badala yake kufanya kazi kwa manufaa ya klabu yake.
"Dah kwa sasa nimeamua kukaa kimya ili nifanye kazi, naamini hivi ndivyo inavyotakiwa ili kuwafanya watu wapime kazi yangu uwanjani na siyo kwenye vyombo vya habari," alisema Kiemba.
Mchezaji huyo ambaye magoli yake mawili aliyoyafunga kwenye mechi mbili tofauti yaliisaidia Simba kuvuka hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.
Kiemba alifunga bao la kwanza wakati Simba ikiilaza AFC Leopards katika mechi ya kwanza ya kundi B kabla ya kuifunga pia KMKM ya Zanzibar.
Nyota huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga, Miembeni na Moro United, alikuwa katika hatihati msimu huu kuondoka Simba kabla ya kupewa mkataba wa miaka miwili baada ya kuzima uvumi alikuwa akielekea Yanga.
Klabu hiyo ya Simba jana ilifanikiwa kuinyuka Chuoni katika mechi yao ya Robo Fainali ya Mapinduzi kwa mabao 2-0 na sasa wanakutana na timu inayowasumbua kwa muda mrefu ya URA toka Uganda.
Simba kwa miaka zaidi ya miwili ikikutana na URA imekuwa ikitepeta, japo ukali wa kocha Zdrakov Logarusic na msaidizi wake, Suleiman Matola wanatoa matumaini ya kupata dawa ya kuizima URA kab la ya kujua itavaana na nani kati ya Azam na KCC ya Uganda.

Tom Olaba akimwagia sifa kikosi cha Ruvu Shooting

http://images.supersport.com/AFC-Tom-Olaba-300.jpg
Tom Olaba

KOCHA Mpya wa klabu ya Ruvu Shooting, Mkenya Tom Olaba amekimwagia sifa kikosi cha timu yake akidai kina wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa wa soka na kudai wanampa imani ya kufanya nao vema katika Ligi Kuu.
Aidha kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar, alisema amebaini udhaifu wa aina tatu katika kikosi hicho na kueleza ameanza kurekebisha ili kuwahi pambano lao la kwanza la duru la pili la Ligi Kuu dhidi ya Prisons.
Akizungumza na MICHARAZO, Olaba aliyetua Ruvu Shooting kuziba nafasi ya kocha Charles Boniface aliyehamia Yanga, alisema kwa siku chache tangu aanze kukinoa kikosi chake amebaini kimejaliwa 'vijana wa kazi'.
Olaba alisema asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hiyo wana vipaji na uwezo mkubwa wa soka kitu kinachomtia moyo kwamba watafanya kazi kwa ufanisi na kuipaisha Ruvu kwenye duru la pili la ligi kuu.
"Kwa kweli ndiyo kwanza nina siku kama tata au nne tangu nianze kuinoa timu yangu, nimebaini vipaji na vijana wenye uwezo wa soka kitu kinachonitia moyo na kuamini tutafanya kazi vyema," alisema.
Olaba alisema pamoja na vipaji na uwezo wa kisoka, amebaini mapungufu matatu katika kikosi hicho na tayari ameanza kuyafanyia kazi kuyarekebisha.
"Wachezaji hawana uwezo wa kukaa na mipira, kutoa pasi na kunyang'anya mipira, kitu ambacho nimeanza kufanyia kazi mapema ili hata tukienda Mbeya kuvaana na Prisons tuwe tumekamilika, ila nimevutiwa na aina ya wachezaji walipo Ruvu kwani wanajua soka na wana vipaji," alisema.
Ruvu Shooting iliyomaliza duru la kwanza ikiwa kwenye nafasi ya saba kwa kujikusanyia pointi 17 kutokana na mechi 13, imemnyakua Olaba kwa mkataba wa muda mfupi wa miezi sita kwa ajili ya mechi za duru la pili.

TASWA kuchaguana Februari 16

KATIBU wa TASWA, Amir Mhando 'Mgosi'
UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), utafanyika Februari 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam. 
Uamuzi huo ulifikiwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika Dar es Salaam jana kujadili masuala mbalimbali ya chama na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla. 
Kikao kilikubaliana kuwa uchaguzi ufanyike kwa katiba ya zamani, kwani mchakato wa katiba mpya unaweza kuchukua muda mrefu, hivyo kusababisha viongozi waliopo madarakani kuendelea kukalia viti kinyume cha katiba, jambo ambalo si sahihi. 
Kutokana na hali hiyo viongozi wapya watakaochaguliwa moja ya kazi yao kubwa itakuwa kuifanyia marekebisho makubwa katiba ya chama chetu ili iende na wakati. 
Fomu za kuwania uongozi zitaanza kutolewa Februari 10 hadi Februari 14 mwaka huu saa kumi alasiri, masuala mengine yahusiyo uchaguzi huo, ikiwemo mahali utakapofanyika yatatangazwa baada ya kikao cha sekretarieti ya TASWA na Kamati ya Uchaguzi kitakachofanyika Februari 3.

Jennifer Mgendi aachia video mpya iitwayo 'Hongera Yesu'

MUIMBAJI nyota wa muziki wa nyimbo za Injili, Jennifer Mgendi ameibuka na albamu mpya ya video iitwayo 'Hongera Yesu' yenye nyimbo saba.
Akizungumza MICHARAZO, Mgendi alisema kuwa albamu hiyo tayari imeshatua madukani na aliwataka wapenzi wa muziki huo kutonunua CD 'feki' kwani kufanya hivyo kunawavunja moyo wasanii.
Video hiyo mpya mbali na kibao cha 'Hongera Yesu' kilichobeba jina la albamu, pia ina nyimbo kama 'Nikufanyie Nini?', 'Kikulacho', 'Mimi ni Wako', 'Baraka Zangu', 'Fumbua Macho' na 'Msimamo'.
Katika nyimbo za albamu hiyo Mgendi amewashirikisha nyota wengine wa muziki wa Injili kama Bahati Bukuku, Bonny Mwaitege, Christina Matai na Martha Ramadhani.
Mbali na kutoa video, Mgendi pia ametoa albamu ya audio ya vibao hivyo, ambayo nayo tayari iko madukani.
Muimbaji huyo amewahi kutamba na albamu kadhaa zilizomtangaza vyema kwenye ulimwengu wa muziki wa miondoko hiyo ikiwamo ile ya 'Mchimba Mashimo' iliyokuwa na nyimbo kama 'Moyo Tulia', 'Nalia', 'Baba ni Wakuaminiwa', 'Niongoze Safarini' na 'Rudi Nyumbani'.
Aidha, Mgendi alisema kuwa mwaka huu anatarajia pia kuzindua filamu yake mpya ambayo hata hivyo hakupenda kuitaja jina kwa sasa kwavile bado ni mapema.

Steve Nyerere aomba kukutana na serikali, wasambazaji