STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 9, 2014

Steve Nyerere aomba kukutana na serikali, wasambazaji


MWENYEKITI mpya wa Bongo Movie Unity, Steven Mengele 'Steve Nyerere' ameiangukia serikali akiomba kukutana nao pamoja na wasambazaji wa kazi za wasanii ili kujadili mambo mbalimbali yanayowakabili.
Steve Nyerere alisema kwa muda mrefu wasanii wamekuwa wakinyonywa jasho lao na yeye kama kiongozi mwenye dhamana wa kuwasaidia wasanii wenzake ameona ni vyema kukutana na serikali na wasambazaji kuweka mambo sawa.
Alisema wasanii wamekuwa wakinyonywa katika jasho lao, na kumekuwa na juhudi kubwa za kuwasaidian wasanii, lakini bila mafanikio hivyo anaamini mkutano wake na serikali na wasambazaji utaleta jibu zuri.
"Baada ya kuchaguliwa na wasanii wenzangu, nimepanga kuanza kuomba kukutana na serikali na wasambazaji ili kuweza kumaliza kilio cha muda mrefu cha unyonyaji wanaofanyiwa wasanii," alisema.
Steve aliyechaguliwa mwishoni mwa wiki katika uchaguzi mkuu wa umoja huo, alisema ni Tanzania pekee ambayo msanii na mtayarishaji ndani ya mwaka anaweza kutengenezea filamu kuanzia 6 mpaka zaidi ya 10.
"Duniani kote mtayarishaji anaweza kutengeneza filamu kati ya moja mpaka mbili, lakini hapa msanii mmoja anazalisha filamu zaidi ya 10 kwa mwezi na kuuza kazi hiyo kati ya Sh. milioni 10-20, huu ni wizi," alisema.
Alisema ni vyema msanii akaweza kutengeneza filamu angalau moja kwa mwaka na kuiuza pengine hata kwa Sh. milioni 200 kuliko mtindo wa sasa ambao unawanufaisha wasambazaji wanaouziwa 'master' na kuzalisha filamu maradufu tofauti na fedha walizonunulia kazi hizo.
Alisema Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40, lakini alisema kwa mauzo ya hata nakala 10,000 tu kwa bei ya Sh.5,000 kwa nakala, muuzaji anapata Sh. milioni 50 hivyo si sawa kuwapa wasanii waliotoka jasho Sh. milioni 10 wakagawane.
Mwenyekiti huyo aliyechukua nafasi ya Vincent Kigosi 'Ray' aliyekuwa akiiongoza Bongo Movie kabla ya uchaguzi huo, alisema anaamini serikali ikiweka mikakati mizuri kuwabana wasambazaji wasanii watanufaika na kulipa kodi itakayosaidia kuleta maendeleo ya nchi kuliko ilivyo sasa.

No comments:

Post a Comment