STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, June 2, 2012

Mr Blue, Malaki wachanganywa na Msichana Mzuri

Malaki MSANII anayekuja kwa kasi nchini, Sela Myovela 'Malaki' ameachia ngoma mpya iitwayo 'Msichana Mzuri' aliyoimba akishirikiana na mkali wa R&B, Khery Sameer Rajab maarufu kama Mr Blue au 'Kabaysa'. Akizungumza na MICHARAZO, Malaki aliyewahi kufyatua ngoma nyingine kali iitwao 'Maisha' aliyoimba na mkali wa Bongofleva nchini, Juma Kassim Kiroboto 'Sir Juma Nature' alisema wimbo huo mpya ameurekodia katika studio za Fishcrab chini ya prodyuza matata, Lamar. Malaki alisema wimbo huo uliopo katika miondoko ya R&B ni maalum ya ujio wake mpya chini ya usimamizi wa kaka yake, Mfaiswa Myovela 'Mzee wa FilamuCentral'. "Baada ya kimya kirefu cha miaka kama mitano, nimekuja na ngoma mpya kabisa iitwayo 'Msichana Mzuri' niliyopigwa tafu na Mr Blue, ikifanywa chini ya Lamar wa Fishcrabs Studio," alisema. Alisema, tayari wimbo huo ameshausambaza katika vituo vya redio na kuanza kurushwa hewani, huku mwenyewe nakijipanga kwa ajili ya kuitolea video yake. Aliongeza, lengo lake ni kufyatua albamu hapo baadae ingawa alisema kwa sasa ataendelea kudondosha wimbo mmoja mmoja kwa ajili ya kuweza kujitangaza na kupata shoo zitakazomwezesha kupata fedha za kukamilishia albamu hiyo. Malaki alitumbukia kwenye muziki wa kizazi kipya tangu mwaka 2005 na kutoa kazi yake ya kwanza kabisa akiwa na Juma Nature mwaka 2007 kabla ya kuwa kimya hadi mwaka huu alipotoka na 'ngoma' hiyo mpya.
Mr Blue katika pozi zake.

'Maafande' wamnyemelea Ngassa

KLABU nne tofauti zimekuwa zikimnyatia mshambuliaji mahiri wa timu ya Moro United, Benedict Ngassa, kwa ajili ya kutaka kumnasa ili wazichezee timu zao katika msimu moya wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Akizungumza na MICHARAZO, Ngassa alizitaja klabu hizo zinazomnyemelea kuwa ni JKT Ruvu, Ruvu Shooting, African Lyon na timu iliyopanda daraja ya Prisons ya Mbeya. Ngassa alisema viongozi wa klabu hizo kwa nyakati tofauti wamekuwa wa kiwasiliana nae na kufanya mazungumzo ingawa alikiri bado hajaafikiana nao mpaka sasa. "Licha ya kufuatwa na viongozi wa klabu hizo, bado sijaamua niende wapi, nitaangalia kwanza masilahi," alisema. Aliongeza kuwa, ingawa anafurahia kunyatiwa na timu hizo, lakini roho yake inamuuma kwa timu yake ya Moro United kushuka daraja akielekeza lawama zake kwa wachezaji walioichezea timu hiyo kwa mkopo. Ngassa, alisema wachezaji waliotua katika timu hiyo kwa mkopo toka klabu mbalimbali nyingine za ligi kuu walikuwa wakiihujumu timu yao ambapo licha ya wachezaji halisi wa Moro kujituma na kuifungia mabao, magoli hayo yalikuwa yakirejeshwa kitatanishi. "sio siri tumeshushwa daraja na wachezaji waliokuja Moro kwa mkopo, inauma sana," alisema. Moro United iliyokuwa imerejea tena Ligi Kuu imejikuta ikishuka daraja ikiungana na timu za Villa Squad na Polisi Dodoma kutokana na kujikusanyia pointi chache katika mechi 26 ilizocheza msimu huu ambapo Simba waliibuka mabingwa.

Bondia Magoma Shaaban afariki, azikwa kwao Tanga

ALIYEKUWA Bingwa wa Dunia wa WBU uzani wa Super Fly, Magoma Shaaban amefariki dunia na kuzikwa kwao mkoani Tanga. Kwa mujibu wa mdau mkubwa wa mchezo wa ngumi ambaye pia ni promota, Ibrahim Kamwe, Magoma alikumbwa na umauti juzi kwenye hospitali ya Bombo mkoani Tanga. Magoma alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo siku nne zilizopita kutokana na kuzidiwa na maradhi aliyokuwa nayo siku nyingi na kufariki majira ya jioni na alizikwa jana nyumbani kwao Mabovu Mwembesamaki, mjini Tanga. Marehemu aliyeacha mjane na watoto wawili Sudi,10 na Almasi,7 alizaliwa Oktoba 21, 1980 mjini Tanga na alianza kucheza ngumi tangu akiwa kinda akipitia klabu mbalimbali za ngumi za ridhaa kabla ya kuingia za kulipwa mwaka 1996 alipopanda ulingoni kuzipiga na Athumani Omari na kushinda kwa pointi. Hadi mauti yanamkuta bondia huyo aliyekuwa mfupi lakini machachari, alikuwa amepigana mapambano 16 na kushinda 13 kati ya hayo mapambano manne akishinda kwa KnockOut (KO) na kupigwa matatu pia kwa KO. Mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Julai 21 mwaka 2006 na Eugen Sorin Tanasie mjini Timisoara, Romania katika pambano ambalo alipigwa kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya pili. Taji lake la kwanza kutwaa lilikuwa ni la IBF Afrika, Septemba 12, mwaka 1998 akimpiga Mkenya Joseph Waweru kwa KO raundi ya kwanza, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Mei 11, mwaka 2000 alimpiga bondia ‘matata sana’ Totin Lukunim wa Thailand na kutwaa taji la IBF Intercontinental, uzito wa Super Fly kwenye ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam. Agosti 3, mwaka 2001 ndipo alitwaa ubingwa wa dunia wa WBU baada ya kumpiga Ferid Ben Jeddou wa Tunisia kwa TKO raundi ya sita mjini Avezzano, Abruzzo, Italia, kabla ya kupoteza taji hilo kwa kupigwa na Gabula Vabaza Julai 26, mwaka 2002 katika ukumbi wa Hemingways Casino, East London, Eastern Cape, Afrika Kusini kwa KO raundi ya kwanza. Mei 25, mwaka 2003 alipigwa na Mtanzania mwenzake, Mbwana Matumla kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kwa TKO raundi ya nne. Wadau mbalimbali wa ngumi wameelezwa kusikitishwa na kifo cha Magoma, wakiitaka familia, ndugu, jamaa na rafiki zake kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu wakiwakumbusha kuwa kazi ya Mola huwa haina makosa.