STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, June 2, 2012

Bondia Magoma Shaaban afariki, azikwa kwao Tanga

ALIYEKUWA Bingwa wa Dunia wa WBU uzani wa Super Fly, Magoma Shaaban amefariki dunia na kuzikwa kwao mkoani Tanga. Kwa mujibu wa mdau mkubwa wa mchezo wa ngumi ambaye pia ni promota, Ibrahim Kamwe, Magoma alikumbwa na umauti juzi kwenye hospitali ya Bombo mkoani Tanga. Magoma alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo siku nne zilizopita kutokana na kuzidiwa na maradhi aliyokuwa nayo siku nyingi na kufariki majira ya jioni na alizikwa jana nyumbani kwao Mabovu Mwembesamaki, mjini Tanga. Marehemu aliyeacha mjane na watoto wawili Sudi,10 na Almasi,7 alizaliwa Oktoba 21, 1980 mjini Tanga na alianza kucheza ngumi tangu akiwa kinda akipitia klabu mbalimbali za ngumi za ridhaa kabla ya kuingia za kulipwa mwaka 1996 alipopanda ulingoni kuzipiga na Athumani Omari na kushinda kwa pointi. Hadi mauti yanamkuta bondia huyo aliyekuwa mfupi lakini machachari, alikuwa amepigana mapambano 16 na kushinda 13 kati ya hayo mapambano manne akishinda kwa KnockOut (KO) na kupigwa matatu pia kwa KO. Mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Julai 21 mwaka 2006 na Eugen Sorin Tanasie mjini Timisoara, Romania katika pambano ambalo alipigwa kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya pili. Taji lake la kwanza kutwaa lilikuwa ni la IBF Afrika, Septemba 12, mwaka 1998 akimpiga Mkenya Joseph Waweru kwa KO raundi ya kwanza, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Mei 11, mwaka 2000 alimpiga bondia ‘matata sana’ Totin Lukunim wa Thailand na kutwaa taji la IBF Intercontinental, uzito wa Super Fly kwenye ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam. Agosti 3, mwaka 2001 ndipo alitwaa ubingwa wa dunia wa WBU baada ya kumpiga Ferid Ben Jeddou wa Tunisia kwa TKO raundi ya sita mjini Avezzano, Abruzzo, Italia, kabla ya kupoteza taji hilo kwa kupigwa na Gabula Vabaza Julai 26, mwaka 2002 katika ukumbi wa Hemingways Casino, East London, Eastern Cape, Afrika Kusini kwa KO raundi ya kwanza. Mei 25, mwaka 2003 alipigwa na Mtanzania mwenzake, Mbwana Matumla kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kwa TKO raundi ya nne. Wadau mbalimbali wa ngumi wameelezwa kusikitishwa na kifo cha Magoma, wakiitaka familia, ndugu, jamaa na rafiki zake kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu wakiwakumbusha kuwa kazi ya Mola huwa haina makosa.

No comments:

Post a Comment