STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, December 5, 2010

TAKUKURU-Kilosa yafichua kucha zake

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU, Wilaya ya Kilosa, imeanza makali yake kwa kuwafikisha mahakamani baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za rushwa na ubadhilifu wa fedha za halmashauri hiyo.
Kaimu Kamanda wa Takukuru wilayani humo, Heri Mwankusye, aliiambia Micharazo mjini humo kuwa, tangu ofisi yao ifanyiwe mabadiliko ya kupelekwa watendaji wapya, wameweza kufungua jumla ya kesi tano ambazo watuhumiwa wake wamefikishwa mahakamani.
Mwankusye alisema kesi hizo ni za kuanzia kipindi cha Januari na Desemba mwaka huu, ambapo moja inawahusisha watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Kilosa, ambayo ilifunguliwa mwezi uliopita ikihusisha utafunwaji wa Sh. Mil. 3.7.
Katika kesi hiyo inamhusisha pia karani wa benki ya NMB wilayani humo pamoja na maafisa wengine wakuu wa halmashauri hiyo (idadi na majina yao tunayo).
Mwankusye alizitaja kesi zingine ni ile inayomhusisha Afisa Mtendaji wa Kata ya Mbumi, aliyestakiwa kwa kosa la kupokea hongo ya Sh 5,000 ambapo kesi yake ipo hatua ya mwisho kabla ya kutolewa hukumu.
"Kesi hii ipo hatua ya mwisho na hukumu yake itatolewa Desemba 17 mwaka huu, kesi nyingi ni ile inayomhusu Mzee wa Baraza la Mahakama ya Mwanzo yta Msowelo, anayeshtakiwa kwa kupokea rushwa ya Sh 60,000," alisema.
Kamanda huyo alizitaja kesi zingine kuwa ni ile ya Afisa Mifugo wa Kata ya Kisanga aliyeshtakiwa pamoja na askari kwa tuhuma za rushwa ya Ng'ombe nane na fedha taslim, Sh.Mil. 1, huku kesi ya mwisho ikiwa inahusisha askari wawili, nao wakidaiwa kupokea rushwa ya ng'ombe katika kata hiyo hiyo ya Kisanga.
Mwankusye alisema kesi hizo ni mwanzo wa taasisi yao kushughulikia tuhuma zinazowasilishwa kwao kila kukicha juu ya kuwepo kwa ubadhilifu na vitendo vya rushwa vilivyokithiri kwa watendaji wa halmashauri hiyo ya Kilosa.
"Huu ni mwanzo wa kasi yetu ya kushughulikia vitendo vya rushwa na ubadhilifu, lengo ni kutaka kuthibitishia umma kwamba tupo kazini na hasa baada ya Rais kutupa meno," alisema Mwankusye.
Alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kuwapa ushirikiano kuweza kuwashughulikia watendaji hao na kuisaidia serikali katika kupambana na kukomesha vitendo hivyo vinavyochangia kurudisha maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Mwisho

Waziri Mkulo ataka Wezi wasipewe uongozi Kilosa





WAZIRI wa Fedha na Uchumi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkulo, amewaomba wananchi wa wilaya ya Kilosa kuwashawishi madiwani wao kutowachagua wenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, ambao ni wezi na wasio na uchungu fedha za umma.
Pia, Waziri Mkulo, amesema anajisikia aibu kwa wilaya hiyo ya Kilosa kupata hati chafu kutokana na kukithiri kwa wizi na ubadhilifu mkubwa wa fedha za miradi ya maendeleo zilizopelekwa katika halmashauri hiyo, akitishia kuzuia mabilioni ya fedha yaliyoidhinishwa kwa halmashauri hiyo.
Akiwahutubia wanachama wa CCM na wakazi wa wilaya hiyo katika mapokezi yake na hafla ya kumpongeza kwa kuteuliwa tena kuwa Waziri, Mkulo, alisema ili kuweza kuzuia wizi na ubadhilifu wa fedha za maendeleo za halmashauri yao ni vema wananchi wakawabana madiwani wao na kuwasihi wasiwachague wenyekiti wa kuiongoza halmashauri hiyo ambao ni wezi.
Uchaguzi huo wa Wenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Kilosa, unatarajiwa kufanyika ndani ya mwezi huu, ambapo wagombea wanne wamejitokeza kuomba nafasi za Uenyekiti wakisubiri kupitishwa kuwania wadhifa huo.
Ili kuifanya halmashauri hiyo kupata viongozi waadilifu, waaminifu na wenye uchungu wa kweli wa maendeleo ya wananchi, Waziri Mkulo, alisema ni vema wananchi wakawabana madiwani wao kuchagua wenyeviti safi.
Waziri Mkulo alisema, kwa deni kubwa alilonalo kwa wananchi wa Jimbo lake la kuwaletea maendeleo ni vema nao wamsaidie jambo moja la kuhakikisha halmashauri hiyo haiwaingizi madarakani wenyekiti ambao ni wezi, watakaoenda kutafuna fedha za miradi ya maendeleo.
"Kwanza nawashukuru kwa kuniwezesha kuwa Mbunge na kumfanya Rais Jakaya Kikwete kunirejeshea cheo hiki cha Uwaziri wa Fedha, kwa hakika nina deni kubwa kwenu la kuwapa maendeleo, ila nina ombi moja kwenu," alisema Waziri Mkulo.
"Naomba mshawishi madiwani wenu kunichagulia wenyekiti was halmashauri ya wilaya wasio wezi na wenye uchu wa kutafuna fedha za miradi ya maendeleo, bahati nzuri serikali imetuidhinishia Sh. Bil 6.83 kutoka Sh Mil 82 ilizokuwa ikipewa awali halmashauri yetu, hivyo tunataka watu wasafi ili Kilosa iwe na maendeleo na kutofautika na ile ya mwaka 2005," aliongeza.
Alisema katika watendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo wamekuwa kama 'mchwa' kwa jinsi wanavyotafuna fedha za miradi na kufanya wananchi waendelee kutaabika, kitu ambacho kama Waziri wa Fedha na Uchumi anaumia na ndio maana anawaomba wananchi wasimwangushe.
"Kama Waziri wa Fedha na Uchumi, najisikia aibu kuona halmashauri yetu ya Kilosa mimi nikiwa Mbunge wake, tukipewa hati chafu kutokana na utafunaji wa fedha za miradi, kama wezi watachaguliwa kuiongoza halmashauri hii nitazuia fedha zilizoidhinishwa zisije," alisema Mkulo.
Alisema kama kusingekuwa na ulaji wa fedha za miradi, wilaya ya Kilosa ingekuwa mbali kwa maendeleo na kusisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutorudia tena makosa kwa kuwarejesha madarakani madiwani ambao ni sehemu ya 'mchwa' wanatafuna fedha hizo.
Hafla ya kumpongeza Waziri Mkulo iliandaliwa na Baraza la Wazee wa wilaya hiyo chini ya Uenyekiti wa DC wa zamani, Raphael Chayeka na Katibu wake, Gervas Makoye, ambapo wanachama wa CCM na Jumuiya zake walimzawadiwa Mbunge huyo wa Kilosa.

Mwisho