STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, July 31, 2011

Uongozi wakana kumpa Nyagawa umeneja SimbaUONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umekanusha taarifa kwamba umempa cheo cha umeneja kiungo wake iliyomtema kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania, Nico Nyagawa.
Nyagawa, aliyekuwa nahodha wa klabu hiyo ametemwa kwenye usajili wa kikosi kipya kitakachoitumikia timu hiyo msimu ujao, huku kukiwepo na taarifa kwamba kiungo huyo amekula shavu la kuteuliwa kuwa meneja wa timu hiyo.
Klabu ya Simba kupitria Afisa Habari wake, Ezekiel Kamwaga, alikanusha madai hayo ya kumpa Nyagawa umeneja, akisema cheo hicho bado kipo kwa King Abdallah Kibadeni, licha ya kukiri ni kweli wamemuacha mchezaji huyo kwa msimu ujao.
"Nyagawa hajapewa umeneja, ingawa ni kweli ametemwa kwenye orodha mpya ya kikosi cha Simba kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara," alisema Kamwaga.
Alisema kwa sasa uongozi wao unaangalia namna ya kumpa kazi nahodha wao huyo, kwa vile bado anaye mkataba na klabu hiyo hadi mwakani.
Alipoulizwa madai kwamba mchezaji huyo amekuwa akitaka kulipwa haki zake ili atimke zake kimoja Msimbazi, Kamwaga alisema hizo ni taarifa za uzushi kwa vile Nyagawa mwenyewe hajawahi kuueleza chochote uongozi juu ya jambo hilo hadi alipoongea na Sema Usikike.
"Hizo ni taarifa za uzushi tu, tulishazungumza na Nyagawa na ndio maana tunasema tupo katika mipango ya kumpa majukumu ndani ya Simba, " alisema.
Nyagawa aliyesajiliwa na Simba msimu wa 2005-2006 akitokea Mtibwa Sugar anatajwa kama mmoja wa wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu wa soka nchini, ingawa amekuwa na bahati mbaya ya kutoitwa mara kwa mara katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.


Mwisho

Yanga yawatoa hofu mashabiki *Ni juu ya kutoweka kwa 'Diego'
UONGOZI wa klabu ya soka ya Yanga umewatoa hofu wanachama na mashabiki wake juu ya taarifa kwamba mshambuliaji wao nyota kutoka Uganda, Hamis Kizza 'Diego' ametoweka.
Kiza aliyeng'ara kwenye michuano ya Kombe la Kagame na kuibebesha taji mabingwa hao wa Tanzania Bara, ndiye aliyekuwa hajaripoti katika kambi ya timu hiyo inayojiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Simba.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema hakuna ukweli kuwa Kizza 'amepeperuka' Jangwani kama inavyovumishwa, ila nyota huyo alikuwa na matatizo ya kifamilia na kwamba angewasili mwishoni mwa wiki.
Sendeu, alisema kama mshambuliaji huyo asingekuwa mali yao jina lake lisingekuwa kwenyue orodha ya wachezaji wapya wa kikosi chao, pamoja na kuitumikia Yanga kwenye michuano ya Kombe la Kagame ambapo walifanikiwa kutwaa taji ikiwa ni mara yao ya nne tangu 1974.
"Ni kweli Kizza amechelewa kuja, lakini haina maana ndio kaingia mitini kama baadhi ya vyombo vya habari vinavyotaka kupotosha, tunadhani atawasili kabla ya Jumapili," alisema.
Aidha, Sendeu, alisema wameamua kukacha kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya timu za Coastal Union na Azam kutokana na walioziratibu kushindwa kufanya mawasiliano na uongozi wao kulingana na programu za benchi lao la ufundi.
"Hizo mechi tulikuwa tukizisikia tu redio na kwenye vyombo vingine vya habari, lakini uongozi haukuwa na taarifa nazo na ndio maana tumeamua kuachana nazo, kwani tunahisi kuna ujanja ujanja uliokuwa ukifanyika hasa mechi ya Coastal," alisema Sendeu.
Yanga wanaoendelea kujinoa jijini Dar chini ya makocha wake, Sam Timbe na Fred Felix 'Minziro' walitangaza kufuta mechi hizo zilizokuwa zichezwe mwishoni mwa wiki katika miji ya Tanga na Dar es Salaam.

Tamasha la Simba Day usipime!
BURUDANI mbalimbali za muziki na pambano la kirafiki la kimataifa litakaloihusisha wawakilishi wa Uganda kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika zinatarajiwa kupamba tamasha la soka la klabu ya Simba, 'Simba Day' litakalofanyika Agosti 8 jijini Dar es Salaam.
Wawakilishi hao wa Uganda, Simba Fc inayomilikiwa na Jeshi la nchi hiyo ndiyo watakaokuja kupamba tamasha hilo, ambalo pia litashuhudia timu ya Simba U23, ikikwaruzana na Azam katika kunogesha shamrashamra hizo.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliiambia MICHARAZO kuwa, tamasha lao litapambwa na burudani za muziki toka kwa bendi mbalimbali za muziki wa dansi na wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao hata hivyo hakuwataja.
Kamwaga alisema shamrashamra hizo za burudani ya muziki zitafuatiwa siku hiyo na utoaji wa tuzo za heshima kwa wadau wa Simba wakiwemo wachezaji, makocha na viongozi wa zamani walioisaidia klabu yao tangu ilipoanzishwa pamoja na wale wanaoisaidia sasa klabu hiyo.
"Karibu kila kitu kimekaa vema kwa sasa ikiwemo kuthibitishwa kwa Simba ya Uganda kuja nchini kucheza nasi katika tamasha hilo, ambalo kabla ya pambano hilo kutakuwa na burudani za muziki na pambano la timu za vijana za Simba na Azam," alisema Kamwaga.
"Mbali na burudani hizo pia tutatoa tuzo za heshima kwa wadau wetu katika namna ya kukumbuka na kushukuru mchango wao," alisema Kamwaga.
Kuhusu maandalizi yao ya mechi yao ya Ngao ya Hisani iliyoapngwa kucheza Agosti 17, Kamwaga alisema yanaendelea vema ikiwemo kikosi chao kuendelea kujifua kwa mazoezi pamoja na kucheza kadhaa za kirafiki visiwani Zanzibar.
Alisema wana imani kubwa ya kufanya vema kwenye pambano hilo dhidi ya Yanga pamoja na kwenye msimu mpya wa ligi kuu utakaoanza wiki moja baada ya pambano hilo la Ngao ya Hisani.
Simba ina deni la kulipa kisasi kwa Yanga iliyowafunga kwenye mechi kama hiyo msimu uliopita kwa mikwaju ya penati na kipigo ilichopata kwenye fainali za Kombe la Kagame lililochezwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambapo Mghana Kenneth Asamoah waliwaliza.
"Hatuna shaka na mechi zetu zijazo kutokana na maandalizi tuliyofanya huko Zanzibar," alisema Kamwaga aliyechukua nafasi hiyo hivi karibuni akimrithi, Clifford Ndimbo.

Mwisho

Kalapina ahubiri Uzalendo nchini

MSANII nyota wa muziki wa hip hop nchini, Karama Masoud 'Kalapina' ametaka somo la uzalendo lifunzwe rasmi shuleni kwa nia ya kuwapika viongozi na wananchi watakaokuwa na uchungu wa kweli dhidi ya nchi yao kitu kinachoweza kupunguza ufisadi.
Kalapina, alisema somo hilo la uzalendo mbali na kusaidia kuondoa ufisadi, pia itawafanya hata wasanii kujipenda na kujithamini kwa kutanguliza utanzania kwanza tofauti na sasa kukosa kujiamini na kuendelea kuwatukuza wasanii wa kigeni na kushindwa kuwika kimataifa.
Akizungumza na blog hii mwishoni mwa wiki, Kalapina alisema mambo yanayoendelea nchini kuanzia kwa wananchi wa kawaida hadi viongozi na wanasiasa kuwa wabinafsi, wenye uchu na kutokuwa na uchungu wa nchi yao imetokana na kukosekana kwa somo la uzalendo.
"Nadhani watanzania tangu utotoni wakianza kufunzwa uzalendo na kujithamini wenyewe, vitendo vya ufisadi, uharamia na wasanii kupenda kuwaiga wasanii wa kimataifa badala ya kubuni kazi zao litaondoka na nchi itaenda vema," alisema.
Kalapina, alisema hata vitendo vya wanajamii kuwaibia kazi wasanii unatokana na ukosefu wa uzalendo na kuzidi kuwafanya wasanii kuendelea kuishi maisha ya dhiki kinyume na wenzao wa kimataifa wanaoongoza kwa utajiri kuliko hata viongozi wao wa serikali.
Kiongozi huyo wa kundi la muziki wa hip hop la Kikosi cha Mizinga, alisema hapendi hali ya mambo inayoendelea nchini kwa watanzania kuwa maskini wakati inafahamika nchi ina rasilimali zinazoweza kuwafanya waishi maisha ya kitajiri kuliko taifa lolote barani Afrika

Coastal 'yamrudisha' Mwalala kwao

MSHAMBULIAJI mpya wa timu ya Coastal Union ya Tanga, Ben Mwalala 'amerejeshwa' kwa nchini Kenya, baada ya timu yake iliyorejea Ligi Kuu Tanzania Bara, kuamua kupiga kambi ya kudumu nchini humo.
Coastal iliyowahi kuwa mabingwa wa soka nchini mwaka 1988, imeamua kuweka kambi ya kudumu mjini Mombasa, kujiandaa na msimu mpya wa ligi utakaoanza mwezi ujao hali inayowafanya nyota wao wapya Mwalala na mkenya mwenzie Abubakar Husseni kurejea kwao.
Afisa Habari wa timu hiyo, Eddo Kumwembe, alisema uongozi wao umeamua kuweka kambi ya kudumu Kenya, ikicheza mechi kadhaa za kirafiki za kujipima nguvu kujiweka fiti kabla ya kuanza kwa mikikimikiki ya ligi iliyokuwa ianze rasmi Agosti 20.
Kumwembe, alisema awali walikuwa wamepanga kurejea kwa muda Tanzania kwa ajili ya kuja kucheza pambano la kirafiki na Yanga lililokuwa lichezwe jana, lakini kutokana na uongozi wa Jangwani 'kuchomoa' kucheza nao wameamua kusalia Kenya hadi msimu utakapoanza.
"Kutokana na Yanga kuchomoa kucheza na sisi, tumeamua kubaki Kenya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kwa kujipima nguvu na timu za huko," alisema.
Coastal inayonolewa na kocha Hafidh Badru, imefanya usajili unaoonekena wa kutisha kwa kuwajaza nyota wa kigeni kama Mwalala, Husseni na wanigeria wawili, Felix Amechi na Samuel Temi huku ikiwa na nyota wengine wa Tanzania akiwemo Aziz Salum Gilla aliyetoka Simba.

Mwisho

Super D aachia DVD nyingine za kufunzia ngumi
KOCHA maarufu wa mchezo wa ngumi nchini, Rajab Mhamila 'Super D' aliyeamua kutumia njia ya DVD kuwafunza watu ngumi, ameachia kazi nyingne tatu mpya.
Kazi hizo tatu zinahusisha mapambano kadhaa ya nyota na mabingwa wa ngumi za kulipwa duniani, ziachiwa sokoni zaidi ya wiki moja sasa.
Akizungumza na MICHARAZO, Super D, alisema tofauti na kanda yake ya awali, DVD za sasa zimeandaliwa kisasa na zikiwa na mchanganyiko wa 'clips' za michezo ya nyota wa dunia katika kuwafunza watu namna ya kupigana ngumi.
Super D, alisema mbali na michezo ya nyota hao wa dunia akiwemo Manny Pacquiao, Floyd Maywather, Roy Jones na wakali wengine DVD hizo pia zina michezo ya tamasha lao la ngumi wanaloendesha kwa kushirikiana na kocha Habib Kinyogoli.
"Katika muendelezo wa kuwafunza watu ngumi kwa njia rahisi, nimetoa dvd pamoja na cd nyingine tatu tofauti zilizokusanya michezo ya mabingwa wa dunia na mafunzo ya ngumi tunayoendesha kupitia tamasha letu na Kinyogoli Foundation," alisema.
Super D, ambaye ni kocha wa klabu ya ngumi ya Ashanti, alisema anaamini kupitia njia hiyo watu wengi wenye kupenda kujifunza mchezo wa ngumi kwa kuangalia mbinu na ufundi katika mchezo huo kupitia michezo ya mabondia waliopo kwenye dvd hizo.
Aliongeza kuwa, mbali na dvd hizo bado vijana wenye vipaji vya ngumi wanaweza kujiunga na klabu zao za Ashanti na Amana kujifunza 'live' chini ya makocha Habib Kinyogoli, Kondo Nassor, yeye Super D na wengine wanaowanoa vijana mbalimbali.

Mwisho

Siujasaini kokote-Nsa Job

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Yanga, Nsa Job, amedai hajasaini kokote hadi sasa licha ya jina lake kuwepo kwenye orodha ya wachezaji wa klabu ya Villa Squad.
Hata hivyo mchezaji huyo, alisema kama uongozi wa Villa utakaa nae mezani na kukubaliana juu ya masilahi atakubali kuichezea kwa vile imeonyesha nia ya kumhitaji.
Akizungumza na MICHARAZO, Job, aliyeachwa na Yanga msimu huu baada ya kuitumikia msimu uliopita akitokea Azam, alisema hakuna mazungumzo yoyote aliyofanya na Villa waka kusaini kuichezea klabu hiyo.
Alisema, mara alipoachwa na Yanga alikuwa kwenye mipango ya kwenda Sweden kucheza soka la kulipwa, hivyo hakuwahi kufanya mazungumzo na klabu yoyote, ila kama ni kweli Villa inamhitaji ataweza kuwasaidia wakielewana juu ya suala la masilahi.
"Sijasaini kokote ndugu yangu, sio Villa wala klabu nyingine niliyofanya nao mazungumzo, ila kama klabu hiyo inanitaka sioni tatizo kuichezea kama tutaelewana juu ya masilahi, si unajua soka ni ajira bwana," alisema Job.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kuzichezea Moro United na Simba, alisema hata kama atakubaliana na Villa kuichezea, bado mipango yake ya kwenda kucheza soka la kulipwa ipo pale pale kwani anaendelea kuwasiliana na wakala wake Nyupi Mwakitosa.
Job, alisema wakala huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa soka Tanzania mwenye uraia wa Sweden kwa sasa, amemhakikishia kumhangaikia kupata timu ya kwenda kufanya nanyo majaribio baada ya ile ya awali kushindwa kukubaliana nao baadhi ya mambo.

Mwisho

Pondamali awachanganya Villa Squad

UONGOZI wa klabu ya soka ya Villa Squad, umedai kuchanganywa na kitendo cha aliyekuwa kocha wao, Juma Pondamali kujiondoa kikosi, huku wakikanusha kumteua Rachel Mwiligwa kuwa msemaji mpya wa klabu yao.
Makamu Mwenyekiti wa Villa, Ramadhani Uledi, aliambia MICHARAZO juzi kuwa, kujiondoa kwa Pondamali kumewapa wakati mgumu kutokana na ukweli alikuwa sehemu ya mipango yao ya kuisaidia timu hiyo kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Uledi alisema kinachowachanganya zaidi ni hatua ya kocha huyo aliyekuwa pia Mkurugenzi wa Ufundi, kuondoka kimyakimya bila kuwaambia zaidi ya kusoma taarifa zake kwenye vyombo vya habari.
"Tumeshtushwa na kuchanganywa na Pondamali kujiondoa tukielekea kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu Tanzania Bara tuliyoirejea msimu huu, hatujui kitu gani kilichomkimbiza, ila kutakutana kujadili tuone tunafanyaje," alisema.
Uledi anayekaimu pia nafasi ya Mwenyekiti, ambayo ipo wazi baada ya TFF kusitisha kuwaniwa kwenye uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Juni, mwaka huu, alisema pia sio kweli kama klabu yao imemteua Mwandishi Rachel Mwiligwa kuwa Msemaji wao, akisisitiza nafasi hiyo bado inashikiliwa na Idd Godigodi aliyetangaza kujiuzulu.
"Hatutateua msemaji mpya kwa kuwa nafasi hiyo na zile zinazotakiwa zitolewe kwa ajira rasmi, zitatangazwa baada ya kikao chetu, kwa maana hiyo Godigodi aliyetangaza kujiondoa baada ya kusoma taarifa za uteuzi wa Mwiligwa ataendelea na nafasi yake," alisema Uledi.
Mwenyekiti huyo aliongeza katika kikao chao watajadili suala la ushiriki wa timu yao katika msimu mpya wa ligi waliorejea baada ya kushuka msimu wa 2008-2009.
Villa Squad ni miongoni mwa timu nne 'mpya' zitakazocheza ligi ya msimu ujao iliyopangwa kuanza Agosti 20, zingine zikiwa ni JKT Oljoro, Coastal Union na Moro United.

Mwisho

Waumini Answar Sunna wacharuka, watulizwa na RITA

WAUMINI wa Jumuiya ya Answar Sunna Tanzania wanaoshinikiza uongozi wa juu ya jumuiya hiyo hung'oke madarakani kwa kukiuka katiba, wametulizwa wakitakiwa kuwa na subira wakati ofisi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini, RITA ukisubiri kutoa maamuzi juu ya mgogoro huo.
Wito huo umetolewa jana kwenye maazimio ya mkutano wa pamoja kati ya waumini hao na kamati yao maalum inayofuatilia mgogoro huo, uliofanyika kwenye msikiti uliopo makao makuu ya Answar Sunna, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kadhalika wito kama huo umetolewa na Meneja wa Ufilisi na Udhamini wa Rita, Linna Msanga Katema, alipozungumza na MICHARAZO akithibitisha ofisi yao imeomba ipewe muda wa mwezi mmoja kutoa majibu juu ya sakata linaloendelea kwenye jumuiya hiyo.
Meneja huyo alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kueleza tofauti na awali walipokuwa wakikosa ushirikiano toka kwa viongozi wanaolalamikiwa wakiwemo Baraza la Wadhamini na Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh Juma Poli, sasa mambo ni shwari.
"Tumeshawaandikia barua kuomba watupe muda wa mwezi mmoja toka Julai 26 tuliowaandikia barua ili RITA tutoe maamuzi juu ya kinachoendelea baina ya pande hizo mbili, hivyo tunaomba waumini watulie haki itatendeka," alisema Katema.
Katika mkutano wao wa jana, waumini hao walionyesha kuwa na hasira ya kutaka viongozi wang'oke kwa kukiuka katika na kushindwa kuipeleka mbele jumuiya yao, kabla ya Mwenyekiti wa Kamati yao, Hamis Buguza kuwasihi wavute subira.
"Vuteni subira tusubiri maamuzi ya RITA ili kuona nini kitaamuliwa, ila lolote litakalotolewa tunawaahidi kuyaleta kwenu mjue kitu cha kufanya, ila kwa sasa ni mapema mno na Uislam unatufundisha kuwa na subira," alisema mwenyekiti huyo.
Kutokana na kauli ya Mwenyekiti pamoja na Katibu wao, Abdulhafidh Nahoda, waumini hao katika kutoa maazimio waliafiki kuvuta subira hadi maamuzi ya RITA yanayotarajiwa kutolewa Agosti 26, ili wajue la kufanya.
Hata hivyo walitoa angalizo kwa kudai kama kutakuwa na aina fulani ya upendeleo basi, watakachoamua wasije wakaamuliwa kwa madai wamechoka kuvumilia.
Mzozo wa waumini wa jumuiya hiyo na uongozi wao umeanza tangu mwaka juzi kutokana na madai viongozi wamekiuka katiba kwa kutoitisha mikutano kwa muda wa miaka 10, huku wakifanya maamuzi bila kuwashirikisha kama wanavyoelekezwa kwenye katika mama ya mwaka 1992.

Mwisho