STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, June 6, 2014

Lupita Nyong'oa anaswa na Paparazi katika kivazi cha ufukweni mcheki...!

MSHINDI wa tuzo ya OIscar, Lupita Nyong'o amefumaniwa akiwa mapumzikoni na Paparazi , ambaye bila ya ajizi aliamua kumfotoa mipicha kibao kama ainavyoonekana akiwa katika kivazi cha ufukweni. Kama kawa kwa mbali utunda unaonekana kuthibitisha kuwa yeye ni Muafrika Halisi!

Vyombo vyaikwamisha Bombastic Modern Taarab

KUNDI jipya la miondoko ya taarab lililokuwa limeanza kuwashika mashabiki, Bombastic Modern, limesitisha shughuli zake kutokana na ukosefu wa vyombo vya muziki.
Bombastic linalomilikiwa na nyota wa zamani wa kundi la Babloom Modern na Dar Modern Taarab, Mridu Ally 'Tx' lilikuwa likijipanga kuingia studio kurekodi nyimbo zake mpya baada ya kufanya maonyesho kadhaa na kuwavutia mashabiki wa muziki huo.
Hata hivyo akizungumza na MICHARAZO, Mridu alisema wamesitisha shughuli ili kujipanga kusaka vyombo vya muziki kwa vile gharama za kukodisha vyombo pamoja na zile za usafiri wamejikuta wakifanya kazi ya bure.
"Tumesitisha shughuli zote za muziki kutokana na tatizo la vyombo, tumekuwa tukikodi na kubeba gharama kubwa ambazo zikichanganyikana na usafiri na malipo kiduchu ya kutoa burudani nahisi wasanii wataona kama wanadhulumu hivyo nimeamua tutulie tujipange kusaka vyombo vyetu wenyewe," alisema.
Mridu alisema mara baada ya kufanikiwa kupata vyombo watarejea kwa kishindo kutoa burudani kwenye kumbi mbalimbali kabla ya kuingia studio kurekodi nyimbo zao mpya ambazo walikuwa wameanza kuzifanyia mazoezi.
Mtunzi, muimbaji na mcharaza gitaa huyo alisema hataki kuja kuona kundi likiyumba na kuwaacha wasanii wake katika hali mbaya ya kifedha ndiyo maana anaona bora watulie na kujipanga upya akidai ushindani kwenye soko la miondoko hiyo linataka mtu kuwa makini na siyo kukurupuka na kutaka kushindana bila kuwa na misingi imara.

TOT Band waingia studio kufyatua mpya

Redock Mauzo
BENDI ya TOT 'Vijana Fashion' wanatarajia kuingia studio wiki ijayo kurekodi nyimbo zao mbili wakianza na 'Akili ni Mali' kabla ya kumalizia 'Maisha Duni'.
Akizungumza na MICHARAZO kiongozi wa bendi hiyo Redock Bokassa 'Redock Mauzo' alisema wataingia studio za Amaroso, zilizopo jijini Dar es Salaam.
Redock alisema wataanza kazi hiyo wiki ijayo kwa kibao cha 'Akili ni Mali' alioutunga yeye na baada ya hapo watamalizia wimbo wao wa pili wa 'Maisha Duni' wa Frank Kabatano kabla ya kuendelea na nyimbo nyingine zinazoendelea kutungwa sasa kwa ajili ya kukamilisha albamu yao mpya.
"Vijana wa Fashion, tunatarajia kuingia studio za Prodyuza Amoroso kuanza kurekodi nyimbo zetu mpya, kazi hiyo itaanza wiki ijayo kwa wimbo wa 'Akili ni Mali'," alisema.
Rapa na muimbaji huyo aliyekuwa Extra Bongo kabla ya kurejea TOT Band, alisema wamepania kurejesha heshima ya bendi hiyo iliyowahi kutikisa anga la muziki wa dansi kwa vibao murua vilivyokuwa kwenye albamu zao kadhaa ikianzia 'Mtaji wa Maskini'.

Maximo awakabikisha Mkwasa, POndamali Yanga


Kocha Maximo, enzi zkiinoa Stars
KOCHA Marcio Maximo kutoka Brazil, tayari ameupitia mkataba wa kuanza kufanya kazi Yanga na kusema: “Nitaanza kazi na (Charles) Mkwasa pamoja na (Juma) Pondamali.”
Awali kulikuwa na hofu huenda kocha huyo angetaka kutua nchini na msaidizi wake kutoka Brazil lakini sasa atalazimika kuwataja wazawa hao katika benchi lake la ufundi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinaeleza Maximo ametumiwa mkataba huo ambao awali ulipitiwa na mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji na ukatumwa nchini Brazil kupitia mwakilishi wake anayeishi jijini Dar es Salaam na amekubali kushirikiana na Mkwasa na Pondamali.
Suala la kocha msaidizi kutoka Brazil, Yanga na Maximo walikubaliana kuwa, atakapokaa mwaka mmoja na kufanya kazi kwa mafanikio, basi Yanga inaweza kuliangalia hilo kama wamuongeze kwenye benchi la ufundi.
Mwakilishi huyo wa Maximo ambaye amekuwa akisimamia zoezi hilo, ameutuma mkataba huo na Maximo ameupokea na kuupitia.
Habari za uhakika zinaeleza, inachotaka Yanga ni Maximo kupunguza dau lake ambalo alianzia dola 16,000 (zaidi ya shilingi milioni 25) kwa mwezi kabla ya kushuka hadi dola 15,000 (zaidi ya shilingi milioni 24), lakini Yanga imesisitiza inataka ashuke kidogo.
Ahadi nyingine ambazo amepewa Maximo ni nyumba na gari la kutumia pamoja na marupurupu mengine ambayo hayajajulikana.
Championi kama kawaida, ndiyo lilikuwa ni gazeti la kwanza kuandika kuhusiana na ujio wa Maximo, taarifa hiyo ilitoka wiki nne zilizopita.
Iwapo Maximo ataupitia mkataba huo na kuukubali, atatua nchini ndani ya siku nne zijazo na kusaini mkataba huo kabla ya kuanza kazi moja kwa moja.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji alisema mbele ya wanachama kwamba yuko katika hatua za mwisho kuhakikisha Maximo anatua nchini.
Maximo atafanya kazi na makocha wazalendo, Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali na huo ndiyo umekuwa msimamo wa Manji.
Pondamali aliwahi kufanya kazi na Maximo wakati akiwa katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Katika majadiliano yanayoendelea kati ya Yanga na Maximo ni pamoja na suala la kipa Juma Kaseja ambaye hakuwa na uhusiano mzuri na kocha huyo wakati akiinoa Stars.
Maximo akimalizana na Yanga na kuanza kazi, rasmi atakuwa amechukua nafasi ya Hans van der Pluijm anayekwenda kupiga kazi nchini Saudi Arabia ambaye pia alichukua nafasi ya Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts.
CHANZO NI CHAMPIONI IJUMAA

Nisha huyoo mtaani, Kajala ana laana bhana!

Salma Jabu 'Nisha' katika pozi. Msanii huyo anajiandaa kuiachia filamu yake mpya ya Zena na Betina siku ya Jumatano ijayo
Kajala Masanja anayejiandaa kuitoa Laana kupitia kampuni yake ya Kay Films Production

WAKATI Salma Jabu 'Nisha' akijiandaa kuingiza sokoni filamu yake mpya ya 'Zena na Betina' keshokutwa kisura mwingine wa Bongo Movie, Kajala Masanja, yupo mguu sawa kutoa kazi yake ya kwanza binafsi iitwayo 'Laana'.
Muongozaji mkuu wa filamu hizo, Leah Richard 'Lamata' aliliambia MICHARAZO kuwa, filamu ya Nisha itatoka Juni 12 wakati ile ya Kajala itatoka mwishoni mwa mwezi huu.
Lamata alisema filamu ya Zena na Betina ambayo ni comedian serious ni moja ya filamu tamu kama kazi nyingine alizowahi kuziandikia miswada, kutungia hadithi zake au kuziongoza.
"Filamu ya 'Zena na Betina' na Nisha inatarajiwa kuingia sokoni Juni 12, ikishirikisha wasanii mbalimbali nyota akiwamo yeye Nisha na nimeiongoza mwenyewe, kadhalika tupo katika mipangpo ya mwisho ya kuja kuitoa hadharani filamu mpya ya Kajala Masanja, kazi yake inaitwa Laana na ni bonge la filamu, ambayo shabiki hapaswi kuikosa," alisema Lamata.
Lamata, mmoja wa waongozaji mahiri nchini kwa sasa anatamba mtaani na kazi kadhaa kama Elimu Mtaani aliyotunga na kuiangdikia muswada, Jicho Langu na nyingine akizidi kuwakimbiza waongozaji wa kiume waliokuwa wametawala soko la filamu Tanzania.
Katika fikamu za Zena na Betina, Nisha ameigiza pamoja na Ulimboka Mwakilasa 'Senga' na Hanifa Daud 'Jenifer' na wakali wengine. Siyo ya kukosa hii kitu

Cheka na Kitime kabla ya Agosti

MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, John Kitime aliyejitosa kwenye utunzi wa vitabu, amesema kitabu chake kipya cha 'Cheka na Kitime' kitatoka kabla ya Agosti mwaka huu.
Akizungumza na MICHARAZO, Kitime anayepiga muziki katika bendi ya Kilimanjaro Band 'Wana Njenje', alisema kitabu hicho kilikwama kutoka mapema kutokana na sababu zilizo juu ya uwezo wake.
Alisema awali alikuwa amepata mfadhili ambaye angempiga tafu kukiingiza sokoni, lakini wakati mambo yakielekea pazuri mfadhili huyo alipatwa dharura na hivyo mipango yote ikavurugika na kuamua kutulia na kujipanga upya.
Alisema tayari amekamilisha kila kitu kwa ajili ya kukiingiza sokoni kitabu hicho chenye vichekesho na kwamba kabla ya Agosti kitakuwa mtaani na kufuatiwa na mfululizo wa matoleo mengine ya Vol 1 na 2 ambavyo ameshaviandaa mapema.
"Ningependa kuwaambia mashabiki kuwa kile kitabu cha vunja mbavu cha 'Cheka na Kitime' kipo njiani kutokana awali kukwama kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu," alisema.
Kitime alisema pia anaendelea kuandika vitabu vingine viwili tofauti na vunja mbavu vya 'Kilimanjaro Band' ambavyo ni maalum kwa ajili ya kuzungumzia histoari ya bendi yao ilipotoka ilipo na inapoenda sambamba na wasifu wa wanamuziki wake.
"Kitabu kingine cha tatu ni cha 'Haki Miliki', nimeamua kuandika kwa nia ya kuwazindua wasanii kufahamu haki zao katika miliki ya kazi zao," alisema mkongwe huo.
Kitime anakuwa mwanamuziki wa pili mkongwe kujitosa kwenye fani ya uandishi vitabu, baada ya Tshimanga Kalala Assosa, aliyetunga kitabu cha 'Jifunze Lingala' ambacho kinaendelea kutamba sokoni kwa sasa huku akiandaa kingine cha wasifu wake.

Tanzania yaongoza kwa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii

TANZANIA imetajwa kama kinara wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na hasa Instagram kutokana na wengi wao kutumia kuweka picha za utupu.
Taarifa hiyo imetolewa na Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungy alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Radio One ambapo alisema ni aibu kuona watanzania badala ya kuitumia vyema mitandao ya kijamii wenyewe wamejikita kwenye mambo ya upuuzi.
Mungy alisema Tanzania imetajwa kama kinara wa matumizi mabaya ya mtandao wa Instagram duniani kutokana na kukithiri kutweka picha ziisizo za maadili na kuwaomba watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini kuonyesha ustaarabu kwa kuitumia vizuri.
Alisea TCRA wanaendelea kuhimiza watanzania kuepuka kusambaza meseji za chuki na uchochezi pamoja na kutumia mitandao hiyo ya kijamii kudhalilisha watu wengine au kujidhalilisha wenyewe kwani hatua kali zitachjukuliwa dhidi ya wote.
Kauli ya Mungy imekuja siku chache baada ya mmiliki wa mtandao huo kutangaza kufuta picha zote za utupu kutokana na kukerwa na watumiaji wake kutaka kuuharibia mtandao huo.
Mmoja wa waasisi wa mtandao wa kijamii wa Instagram, ameambia BBC kuwa sheria zake kuhusu picha za uchi hazimbagui mtu yeyote.
Kampuni hiyo imekosolewa vikali kwa kwa kuondoa picha za wanawake walio nusu uchi kwenye mtandao huo.
Lakini Afisaa mkuu mtendaji wa mtandao huo wa kijamii, Kevin Systrom, amesema kuwa sheria hizo zinalenga kuhakikisha kuwa vijana na watu wazima wanaotumia mtandao huo wako salama.
Masharti ya matumizi ya mtandao wenyewe, yanasema: 'Mtu haruhusiwi kuweka picha za watu walio nusu uchi na picha zenye mada ya ngono. ''
Matamshi yake yanakuja baada ya mwanawe muigizaji maarufu, Bruce Willis, Scout Willis kuweka picha yake kwenye mtandao huo akiwa nusu uchi bila kitu kifuani.
Picha hiyo iliondolewa kwenye mtandao huo na wamiliki wa mtandao na hapo ndipo malalamiko yalianza kuibuka.
Muimbaji Rihanna, ambaye alikuwa na wafuasi milioni 1.3 aliunga mkono kampeini hiyo kabla ya kufunga akaunti yake.
Wamiliki wa mtandao huo wanasema sheria zinapaswa kufuatwa na kila mtu awe mtu mashuhuri au vinginevyo.
"lengo letu ni kuhakikisha kuwa Instagram, ni mahala salama kwa kila mtu , awe maarufu au la. ''
"tunapaswa kuwa na sheria na kuhakikisha kuwa kila mtu anafuata sheria hizo. Bila shaka tunapata changamoto nyingi lakini tutnaedneklea kusisitiza umuhimu wa sheria kufuatwa, '' alisema Systrom
Huku umaarufu wa mtandao huo ukiendelea kuimarika, mtandao huo umekosolewa kuhusiana na baadhi ya picha zinazochapishwa humo . Pia mtandao wenye umebana baadhi ya maneno yanayohusiana na madawa ya kulevya.
Instagram ilinunuliwa na Facebook mwaka 2012.

Aliyembunia Rihanna gauni lililozua gumzo alonga

TANGU Rihanna alipotinga katika zulia jekundu la tuzo za mitindo ya mavazi za CFDA na kupozi kwa picha Jumatatu, mitandao ya internet imetawaliwa na mijadala kuhusu chaguo lake la kivazi alichoibuka nacho siku hiyo ambacho ni cha nyavu nyavu na kilichokuwa kikianika kila kilicho ndani.
Ipo sababu iliyomfanya kimwana huyo akapewa tuzo ya Fashion Icon Award 2014, na Adam Selman ambaye alimbunia gauni hilo ndiye pekee anayeweza kufafanua ni kwanini.
Selman amefanya mahojiano na jarida la ELLE na kueleza kwanini alimtengenezea gauni la aina ile.
Katika mahojiano hayo, Selman alibainisha kwamba gauni lile lilitumia siku saba kukamilika huku watu 20 wakihusika kulitengeneza. Licha ya kwamba gauni hilo limetumia siku saba kukamilika, Selman amesema wazo hilo lilikuja mwezi mzima uliopita.
"Tulikuwa mjini Los Angeles na Rihanna kwenye tuzo ya MTV Movie Awards kama mwezi uliopita na sote tukaanza kujadili kuhusu tuzo za CFDA," alisema. "Tukaafikiana wazo la kutengeneza gauni kama lile. Kisha jambo lililofuata nikachora mchoro wa gauni lenyewe. Rihanna akaliidhinisha na kazi ikaanza!"
Aliongeza kwamba Rihanna alifahamu fika kitu alichohitaji. Mbunifu huyo alisema alitokwa na machozi alipomuona kwa mara ya kwanza Rihanna akiwa ametinga gauni hilo.
Selman akatetea chaguo hilo linaloshambuliwa vikali katika mitandao akisema  "...linawatuliza watu. Alionekana amependeza kwa kila mlima wa mwili aliojaaliwa."

Uholanzi yapata pigo, Van Persie naye aumia

MSHAMBULIAJI wa Uholanzi, Robin Van Persie sasa atatakiwa kumuona daktari baada ya kuumia nyonga akiichezea timu yake hiyo juzi  katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Wales mjini Amsterdam.
Wazi kocha Louis Van Gaal atakuwa anaumia sana kichwa kwa maumivu ya mshambuliaji huyo wa Manchester United, zikiwa zimebaki siku zisizozidi 10 kabla ya kucheza na Hispania katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia.
Kabla ya kuumia na kutoka, Van Persie alitengeneza bao la kwanza lililofungwa na Arjen Robben wakati bao la pili lilifungwa na Jeremain Lens.

Stars kuingia kambini J'5 kuisubiri Mamba

KIKOSI  cha Taifa Stars kinaingia tena kambini Jumatano (Juni 11 mwaka huu) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji itakayochezwa Julai 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa na kambi ya siku tatu jijini Dar es Salaam ikijumuisha wachezaji 28. Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mart Nooij, Stars itaingia tena kambini Juni 24 mwaka huu.
 Wachezaji wanaotakiwa kuripoti kambini ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Benedictor Tinoko, Kelvin Yondani, Said Moradi, Nadir Haroub, Joram Nason, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Edward Charles, Aggrey Morris na Pato Ngonyani.
 Wengine ni Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Said Juma, Haruna Chanongo, Himid Mao, Said Ndemla, John Bocco, Simon Msuva, Kelvin Friday, Ramadhan Singano, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Mwegane Yeya

Njemba afariki ndani ya gari

Na Dixon Busagaga, Moshi 
WATU wawili wamefariki dunia mkoani Kilimanjaro katika matukio tofauti, likiwemo la mmoja aliyekutwa amekufa akiwa katika basi la Kampuni ya Kilenga akiwa safarini kuelekea mkoani Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Moita Koka, alisema kuwa mtu huyo ametambuliwa kwa jina la Sayuni Joel (53), mfanyabiashara, mkazi wa Mwembe, wilayani Same, Kilimanjaro.

Akizungumzia mazingira ya tukio hilo, Kamanda Koka alisema Joel alipanda basi hilo T 398 BAT na kwamba kabla ya kufikwa na mauti, alikuwa akisumbuliwa na tumbo na alikuwa akielekea hospitali kupata matibabu.

Alisema Joel aligundulika kuwa amepoteza maisha baada ya gari hilo kuingia katika stendi kuu ya mabasi Moshi.

Maiti yake imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC huku uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho ukiendelea.

Katika tukio jingine, mkazi wa Kijiji cha Kilema – Kiyou, Kata ya Kilema, wilayani Moshi, Martin Michael (45), amekufa baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya chandarua.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema lilitokea juzi, saa 8 mchana na kudai kwamba amefikia uamuzi huo kutokana na kuchoshwa na hali yake kiafya ambayo imemfanya kutumia dawa kila mara na kwamba kabla ya tukio hilo aliwahi kusikika akilalamikia hali hiyo.

Dokii, Anita wa Mwanza waja na mpya


MUIGIZAJI nyota wa filamu nchini, Ummy Wenceslaus 'Dokii' anajiandaa kuingiza sokoni filamu mpya iitwayo 'I Love Mwanza' aliyoizalisha akishirikiana na 'shoga' yake ambaye ni Rais wa Wasanii jijini Mwanza afahamikaye zaidi kama Anita.
Akizungumza na MICHARAZO Dokii alisema filamu hiyo imekamilika kitambo kirefu na kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kuachiwa mtaani ikiwashirikisha wasanii mchanganyiko wakiwamo wakongwe na chipukizi wa mikoa ya Dar na Mwanza.
Dokii aliwataja baadhi ya wasanii walioshiriki filamu hiyo inayokuwa kazi yake mpya baada ya kuuza sura kwenye filamu ya 'Mdundiko' ni pamoja na yeye Dokii, Anita ambaye ni prodyuza anayekuja juu nchini kwa sasa kutokea Mwanza, Kulwa Kikubwa 'Dude', Sabrina Rupia 'Cathy', Kiwi, Fred na chipukizi wa jijini Mwanza.
"Ni moja ya filamu ya kusisimua yenye makali kama 'Mdundiko' iliyotwaa tuzo ya kimataifa nchini Marekani, kazi hii nimezalisha mimi na rafiki yangu Anita na imeshirikisha wasanii kadhaa nyota na chipukizi nchini," alisema.
Dokii, alisema anawaomba mashabiki wa filamu nchini kukaa mkao wa kula kupata burudani kupitia kazi hiyo ambayo ina ujumbe na mafunzo makubwa kwa jamii.

Msiba tena! Nyota wa zamani Simba, Gebo Peter afariki dunia

Gebo Peter (wa kwanza kushoto mstari wa kati) akiwa na wachezaji wenzake wa Simba enzi za uhai wake
Gebo Peter (wa kwanza kulia) akiwa na baadhi ya wadfau wa soka wakati wa mazishi ya kocha James Kisaka
MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu za Simba, Sigara na Taifa Stars, Gabriel Peter 'Gebo Peter' amefariki dunia usiku wa kuamkia leo.
Habari ambazo MICHARAZO ilizipata mapema asubuhi ya hii zilisema kuwa, Gebo alikumbwa na mauti akiwa amelezwa katika Hospitali ya Taifa ya  Muhimbili alipokuwa amehamishiwa kutoka Hospitali ya Mwananyamala alikokuwa amelazwa kutokana na kuzidiwa na maradhi yhaliyokuwa yakimsumbua.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Ilala (IDFA) Daud Kanuti, Gebo alikuwa amelazwa Mwananyamala kwa tatizo la tumbo na hali ilinadilika kuwa mbaya ndipo alipohamishiwa Muhimbili jana na kuwa chini ya uangalizi akipumulia mashine.
Enzi za uhai wake Gebo alisifika kwa kufumania nyavu kwa kutumia miguu yake yote miwili pamoja na vichwa, huku akiwa ni mmoja ya washambuliaji waliokuwa wakiiliza sana Yanga kila ilipokutana na timu alizokuwa akizichezea kuanzia Sigara mpaka Simba.
Mpaka mauti yanamkumba nyota huyo wa zamani ambaye ni mdogo wa nyota mwingine na shujaa wa Tanzania wa mwaka 1980, Peter Tino alikuwa mmoja wa viiongozi wa timu ya Manyema Rangers na kisoka aliwahi kuzichezea timu za Bora, Safari Contractors, Pan Africans, Sigara, Yanga na Kajumulo World Soccer
Taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na msiba unaelezwa upo nyumbani kwa Vingunguti.
MICHARAZO inatoa pole kwa ndugu, jamaa na familia nzima ya marehemu kwa msiba huo mzito na inawatakia kuwa na Subira katika kipindi hiki kigumu kwa kukumbuka kuwa kila nafsi ni lazima ionje mauti na BWANA Ametwaa na Yeye Ndiye Aliyetwaa Jina lake Lihimidiwe.

Shilole kuendelea kuchuna buzi tu kwa sasa


NYOTA wa filamu na muziki nchini, Zuwena Mohammed 'Shilole' amesema hataharakisha kutoa wimbo mpya kwa sasa kwa vile 'Chuna Buzi' inaendelea kusumbua nchini.
Akizungumza na MICHARAZO, Shilole anayefahamika pia kama 'Shishi', alisema licha ya kuwa tayari ameshaandaa wimbo mpya, hatautoa mapema kwa sababu wimbo wake wa sasa 'Chuna Buzi' upo juu.
Shilole alisema wimbo huo ambao hivi karibuni aliiachia video yake bado unaendelea kutamba na asingependa kuwachanganya mashabiki kwa kutoa kazi mpya kwa sasa.
"Kwa kuwa wimbo wa Chuna Buzi upo juu ukisumbua kwenye vituo vya redio na televisheni, nimeamua 'kuuchuna' kwa kuachia kazi mpya licha ya kwamba tayari nimeshakamilika," alisema.
Shilole alisema wimbo huo mpya atauachia baadaye sana, huku akigoma kutaja jina lake kwa madai ni mapema mno, ila aliwataka mashabiki waendelee kupata burudani ya 'Chuna Buzi' kabla ya kupata ladha nyingine ambaye anaamini itawachengua zaidi.
Mwanadada huyo anayetamba na nyimbo kama 'Paka la Baa', 'Lawama', 'Dude Dada' na 'Nakomaa na Jiji', alisema kila uchao hufikiria namna ya kusuuza nyoyo za mashabiki wake.

Chamberlain aitia hofu England kuelekea Fainali za Kombe la Dunia

KIUNGO wa kimataifa wa Uingereza, Alex Oxlade-Chamberlain anatarajiwa kufanyiwa vipimo katika goti lake kufuatia kuzuka hofu kuwa alipata majeraha katika msuli wa ndani ya goti. 
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 20 alitolewa nje kufuatia kukwatuliwa na Carlos Gruezo wakati wa mchezo wa kujipima nguvu kati ya Uingereza na Ecuador ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Kocha wa timu ya taifa ya Uingereza, Roy Hodgson amesema itakuwa pigo kubwa kama wakimpoteza kinda huyo kwenye michuano ya Kombe la Dunia iliyo mbele yao kwani ni mmoja kati ya wachezaji anaowategemea katika kikosi chake. 
Uingereza inatarajiwa kucheza mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Italia Juni 14 mwaka huu huko Manaus. 
Timu hiyo imeshampoteza winga wake Tim Walcot ambaye aliumia naye goti na hivyo kumkosesha michuano hiyo ya Kombe la Dunia inayoanza Alhamisi ijayo.
T

Vijana Simba, Yanga kuchuana Rolling Stone

Simba
JUMLA ya timu 27 zinatarajiwa kushiriki katika michuano ya soka ya vijana ya Rolling Stone itakayoanza Julai 4, mwaka huu jijini Dar es Salaam ikishirikisha timu za Ukanda wa Maziwa Makuu.

Mratibu wa mashindano hayo, Willbroad Alphonce, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa michuano hiyo itafanyika kwa siku 10 na mechi zitakuwa zikichezwa kwenye viwanja vitatu.

"Tunawaandikia barua TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kuomba Uwanja wa Karume, Azam na wamiliki wa Uwanja wa TCC Sigara. Tunaamini watatukubalia kwa ajili ya kuendeshea michuano hiyo," alisema mratibu huyo.

Alisema tayari wameshapata kibali kutoka TFF kuendeshea michuano hiyo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana na timu nyingi zinaweza kupata wachezaji kupitia mashindano hayo.

Alisema michuano hiyo imewaibua wachezaji wengi wakiwamo Amir Maftaha, Salvatory Ntebe na wengine wengi ambao waliitwa kwenye timu za taifa za vijana, hivyo ni wakati wa viongozi wa timu za ligi kuu, daraja la kwanza na timu za Taifa kutumia michuano hiyo kwa ajili ya kupata wachezaji.

Alizitaja timu ambazo zitashiriki kuwa ni Burundi ambao watatoa timu mbili, Kongo (1), Rwanda (1), Uganda (2), Kenya (2), Zanzibar (2) na Tanzania timu zitakazoshiriki ni timu B za Simba, Yanga, Azam FC, Coastal Union, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting.

Nyingine kwa Tanzania ni mabingwa watetezi Eagle Rangers ya Tanga, Mbasco ya Mbeya, Moro, Alliance ya Mwanza na TSC, na kwa mkoa wa Arusha ni Rolling Stone, Vishop Dan, Youth Talent na Bom Bom ya Dar es Salaam.

Alphonce alisema timu zote zipo katika maandalizi shadidi kuhakikisha michuano hiyo inakuwa na upinzani mkali.

Pia aliwaomba wadhamini mbalimbali wajitokeze kudhamini michuano hiyo, kwani bado waandaaji michuano hiyo wanahangaika kutafuta udhamini ili kuyafanikisha.

Tanzania yapaa viwango vya FIFA, Algeria yaiengua Ivory Coast

Kikosi cha Taifa Stars kilichoiwzesha Tanzania kupaa kwenye viwango vya FIFA kwa kuzitoa nishai Zimbabwe na Malawi
TANZANIA imepaa katika viwango vya Soka vya Fifa kwa nafasi tisa huku ikiishusha Zimbabwe kwa nafasi moja baada ya kuitoa katika michuano ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Morocco 2015.
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), iliifunga Zimbambwe bao 1-0 Uwanja wa Taifa kabla ya kurudiana nchini Zimbabwe na kulazimisha sare ya 2-2, hivyo kuitoa kwa jumla ya mabao 3-2.
Katika viwango vilivyotangazwa jana na Fifa, Tanzania ambayo ilikuwa ikishika nafasi ya 122, imepanda hadi nafasi ya 113 wakati Zimbabwe ikishuka kutoka nafasi ya 98 hadi 99.
Msumbiji ambayo itakutana na Tanzania Julai 20, mwaka huu katika mechi ya kuwania kufuzu Afcon, imeporomoka kwa nafasi nne kutoka 114 hadi 118.
 Kwa upande wa Afrika Mashariki, Uganda ndiyo inayoongoza ikibaki nafasi ya 86 iliyokuwa mwezi uliopita huku Kenya licha ya kushuka kwa nafasi mbili kutoka 106 hadi 108 ikishika nafasi ya pili.
Rwanda imepaa kwa nafasi 15 na sasa inashika nafasi ya 116 huku Burundi ikiporomoka kwa nafasi tatu hivyo kushika nafasi ya 128.
Miamba itakayoliwakilisha Bara la Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia, Algeria ndiyo kinara ikipanda kwa nafasi tatu hivyo kushika nafasi ya 22 duniani ikifuatiwa na Ivory Coast ambayo ni ya 23 baada ya kushuka kwa nafasi mbili.
Ghana imepanda nafasi moja na sasa ni ya 37, Nigeria imebaki nafasi yake ya 44 ya mwezi uliopita huku Cameroon ikiwa ni 56 baada ya kushuka kwa nafasi sita.
Kumi bora ya viwango hivyo, Hispania ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Ujerumani, Brazil, Ureno, Argentina, Uswis, Uruguay, Colombia, Italia na England ikifunga orodha hiyo.