STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 5, 2013

Zahoro Pazi aahidi Simba, akiri utoto ulimfanya aikache

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Zahoro.jpg
Zahoro Pazi katika uzi wa JKT Ruvu
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Zahoro Pazi ameahidi kuifanyia makubwa klabu hiyo iliyoingia naye mkataba wa miaka mitatu, huku akisema utoto aliokuwa nayo uliomfanya asijiunge na timu hiyo miaka mitatu iliyopita umeisha.
Pazi aliyesajiliwa na Simba akitokea JKT Ruvu aliyokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka Azam, aliwahi kusainishwa mkataba wa miaka minne msimu wa mwaka 2010 ili kujiunga na timu hiyo, lakini akakataa kujiunga nayo baada ya kutishwa na familia.
Anasema watu wa familia yake walimtishia kwamba angejiunga na Simba angeenda kuua kipaji chake kwani 'angepigwa misumari' na hivyo kuamua kubaki Mtibwa Sugar, jambo alililodai lilitokana na akili za kitoto na kutegemea ushauri wa watu wengine.
Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyetamba na timu mbalimbali ndani na nje ya nchi, Idd Pazi 'Father' alisema kwa sasa amekuwa na maamuzi binafsi ndiyo maana amesaini kuichezea Simba kwa miaka mitatu.
Alisema kutua kwake Simba kuna changamoto kubwa zinazomfanya apigane ili apate namba na pia kuifanyia makubwa kama alivyofanya baba yake wakati akiidakia timu hiyo.
"Sina miujiza kwa kutua kwangu Simba, lakini naahidi nitajituma na kucheza kwa moyo wangu wote ili kuipa mafanikio timu hiyo na kutouangusha uongozi na benchi zima la timu hiyo walioniamini na kunisajili," alisema Pazi.
Mshambuliaji huyo anayecheza pia kama winga, alisema anaamini Simba ya msimu ujao itakuwa moto wa kuotea mbali chini ya King Abdallah Kibadeni mmoja wa makocha waliochangia kukuza na kuendelea kipaji chake alipokuwa Mtibwa Sugar.
"Chini ya Kibadeni, Simba itarajie makubwa ni bonge la kocha na mtu ambaye siwezi kumsahau kwa jinsi alivyosaidia kukiendeleza kipaji changu nilipotua timu ya vijana Mtibwa," alisema.
Pazi aliyewafanyiwa majaribio ya kucheza soka la kulipwa na klabu ya Bloemfontein Celtic mapema mwaka huu na kufaulu japo alichwa baada ya Mzimbabwe Roderick Mutuma kupewa nafasi yake kwa vile nafasi iliyokuwa ikiwania ni moja, alisema anajisikia fahari kucheza timu aliyoichezea baba yake.

Yanga kwenda Kanda ya Ziwa bila nyota wake saba

Wachezaji wa Yanga inayoondoka jijini Dar kwenda Kanda ya Ziwa
MABINGWA wa Soka wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga leo wanatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam na kuelekea Mwanza kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda, KCC mchezo utakaofanyika kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini humo.
Hata hivyo Yanga itaondoka bila ya nyota wake saba walioko katika kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) ambacho kimeshaingia kambini  kwa ajili ya kujiandaa kuikabili timu ya taifa ya Uganda (Cranes) katika mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Wachezaji wa Yanga walioko kwenye kikosi cha Taifa Stars ni pamoja na Athumani Iddi (Chuji), Ally Mustapha 'Barthez', Frank Domayo, Simon Msuva, David Luhende, Kelvin Yondani na Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa kikosi hicho kitaondoka kwa ndege leo mchana.
Kizuguto alisema kuwa wakiwa huko watacheza mechi mbili, ya pili ikichzwa Jumapili kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga dhidi ya Waganda hao.
Kizuguto alimtaja kiungo wa kimataifa wa timu hiyo, Haruna Niyonzima kuwa vilevile hatakuwapo kwenye ziara hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia nchini kwao  Rwanda.

Tamasha la Matumaini kurindima Jumapili

 http://api.ning.com/files/X378Xfy1meuzEX8xHlBh-qQB8hV-1a9IRTU-sWUlJ2vVfLOTpjokDf51r7zq*IPOR8Llw33BkDDIl5dVaYmxQm*gckOwOa6v/ngumi.jpg
WANAMICHEZO, wanamuziki, wasanii wa filamu na wabunge wamezidi kutambiana kuelekea Tamasha la Usiku wa Matumaini litakalofanyika keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuchangia mfuko wa elimu nchini.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya washiriki wa tamasha hilo walisema wamejiandaa vyema huku kila upande ukitamba kufanya vizuri.
Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, ambaye pia ni kipa wa timu ya wabunge alisema kikosi chao kinachoendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam kiko vizuri na wana ukakika wa kuendelea kuifunga Yanga kama walivyoifunga mwaka jana.
Mratibu wa tamasha hilo, Abdallah Mrisho alisema kutakuwa pia na burudani kutoka kwa bendi za DDC Mlimani Park na Msondo, taarab ya Mzee Yusuf na muziki wa kizazi kipya kutoka kwa Diamond Platinumz, Chege, H.Baba na Mkenya Prezzo.
"Pia kutakuwa na muziki wa injili kutoka kwa wasanii Upendo Nkone, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Flora Mbasha na Asha Mwaipaja wa Mbeya," alisema Mrisho.
Mbali na wabunge wa Simba na Yanga kuvaana katika soka, pia kutakuwa na mechi nyingine kati ya wasanii wa Bongo Movie dhidi ya Bongo Fleva na mapambano ya ngumi kati ya mbunge Zitto Kabwe na Vicent Kigosi (Ray), Jacqueline Wolper dhidi ya mbunge Halima Mdee na Aunt Ezekiel dhidi ya mbunge Ester Bulaya.

Christian Bella jukwaani tena na Diamond Musica

Christian Bella
BAADA ya kufanya onyesho lao kwa kishindo, mwimbaji Christian Bella atashiriki tena onyesho la pili leo na bendi ya Diamond Musica Original ikiwa ni mwendelezo wa mikakati ya kujiandaa kumchukua ili ajiunge na bendi hiyo inayokuja kwa kasi.
Onyesho la kwanza kati na mwimbaji huyo na bendi ya Diamond Musica Original lilifanyika Ijumaa iliyopita na kupata mashabiki wengi waliojitokeza kulishuhudia na sasa limeandaliwa jingine litakalofanyika leo na huenda likamshirikisha pia Ndanda Kosovo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa bendi hiyo, Ally Ocs, maonyesho hayo yanalenga kumkaribisha Bella na kisha uongozi wa bendi utafanya naye mazungumzo ili kuona uwezekano wa kumchukua jumla mwimbaji huyo.
"Kama nilivyowahi kusema siku za nyuma Ndanda Kosovo tulishamchukua na huenda akawapo kwenye onyesho letu kwani wakati wowote anatarajia kurejea kutoka kwao Kongo alikokwenda kusalimia kabla ya kuanza kazi rasmi katika bendi yetu," alisema Ocs.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa katika onyesho atatambulishwa pia mnenguaji Mariam Bessie aliyechukuliwa kutoka bendi ya Mapacha Watatu inayoongzwa na Khalid Chokoraa na Jose Mara.
"Tumedhamiria kuingia kwenye muziki wa ushindani, hivyo hatuna budi kujipanga kisawasawa na hilo litawezekana kwani hadi sasa mambo yetu yanakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kuwachukua wanamuziki wenye majina makubwa," alisema.
Diamond Musica Original iko kwenye maandalizi ya albamu ya kwanza ikiwa imekamilisha baadhi ya nyimbo kama: 'Hatua',  'Shilingi', 'Upole wa Mapenzi', 'Fimbo la Mwaka', 'Kibali cha Mapenzi' na 'Deceiption'.

Kichanga chashangaza madaktari China kwa kubeba mimba

Madaktari wa nchini China walishangazwa kuona mtoto wa mwaka mmoja ana ujauzito.
Mtoto Kang Mengru wa nchini China alipelekwa hospitali baada ya wazazi wake kushtushwa na hali ya tumbo lake kuzidi kuwa kubwa siku hadi siku.
Baada ya mtoto huyo kufanyiwa kipimo cha ultrasound, madaktari waligundua kuwa mtoto huyo wa kike alikuwa amebeba kitoto kichanga kwenye tumbo lake ambacho kilikuwa kikiendelea kukua.
Madaktari wanaamini kuwa mama wa mtoto huyo alikuwa na mimba ya watoto wawili mapacha na pacha mmoja alijitokeza ndani ya tumbo la pacha mwenzake.
Hali kama hiyo ya kichanga kuzaliwa ndani ya kichanga kingine ni nadra sana kutokea na humtokea mwanamke mmoja katika wanawake 500,000.
Mtoto Kang atafanyiwa upasuaji kukiondoa kichanga hicho tumboni

Saida Karoli kutambulisha mpya Igunga, Nzega

Saida Karoli
MSANII nyota wa muziki wa asili, Saida Karoli ambaye alivumishiwa kifo hivi karibuni anatarajiwa kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza kufanya maonyesho maalum ya kudumisha amani yatakayofanyika mkoani Tabora.
Karoli aliyewahi kutamba na nyimbo mbalimbali kama 'Chambua kama Karanga' na nyingine atafanya onyesho la kwanza siku ya Jumapili katika shamrashamra za kusherehekea sikukuu ya Sabasaba mjini Igunga na kutambulisha nyimbo zake mpya kwa mashabiki wa mji huo.
Kwa mujibu wa mratibu wa maonyesho hayo, Livenus Madaraka, onyesho la pili la mwanadada huyo litafanyika Julai 9 katika mji wa Nzega, akiwadhihirishia mashabiki wake kwamba yu hai na anaendeleza 'makamuzi' kama kawaida.
Mratibu huyo alisema amewataka wale ambao bado hawajaamini kama Saida Karoli anadunda wajitokeze katika maonyesho hayo ambapo msanii huyo ameahidi kufanya makubwa katika kuwapa burudani mwanzo mwisho.
"Mwenyewe ameahidi kukata kiu ya mashabiki wake kwa kuwapa burudani kabambe na kuzitambulisha nyimbo zake mpya na zile za zamani zilizompatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania," alisema Madaraka.