STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 5, 2013

Yanga kwenda Kanda ya Ziwa bila nyota wake saba

Wachezaji wa Yanga inayoondoka jijini Dar kwenda Kanda ya Ziwa
MABINGWA wa Soka wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga leo wanatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam na kuelekea Mwanza kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda, KCC mchezo utakaofanyika kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini humo.
Hata hivyo Yanga itaondoka bila ya nyota wake saba walioko katika kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) ambacho kimeshaingia kambini  kwa ajili ya kujiandaa kuikabili timu ya taifa ya Uganda (Cranes) katika mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Wachezaji wa Yanga walioko kwenye kikosi cha Taifa Stars ni pamoja na Athumani Iddi (Chuji), Ally Mustapha 'Barthez', Frank Domayo, Simon Msuva, David Luhende, Kelvin Yondani na Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema kuwa kikosi hicho kitaondoka kwa ndege leo mchana.
Kizuguto alisema kuwa wakiwa huko watacheza mechi mbili, ya pili ikichzwa Jumapili kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga dhidi ya Waganda hao.
Kizuguto alimtaja kiungo wa kimataifa wa timu hiyo, Haruna Niyonzima kuwa vilevile hatakuwapo kwenye ziara hiyo kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia nchini kwao  Rwanda.

No comments:

Post a Comment