STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 10, 2014

Hapatoshi Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi leo

Kikisi cha Simba kitakachovaana na URA

Watetezi Azam watakaovaana na KCC

LEO ni kimbembe katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi wakati Azam itavaana na KCC ya Ungada wakati Simba ikishuka dimbani usiku kuivaa URA.
URA imekuwa ikiionea Simba kila wanapokutana nao kwa muda mrefu sasa iwe kwenye mashindano au mechi za kirafiki na kufanya mechi hiyo kuwa yenye mvuto zaidi kuliko ya KCC na watetezi Azam.
Hata hivyo mechi zote zinaonekana kusisimua kutokana na ukweli inazikutanisha timu za Tanzania na Uganda ambazo timu zao za taifa zimekuwa zina upinzani katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Simba ilitinga nusu fainali baada ya kuibamiza mabao 2-0 timu ngumu ya Chuoni FC ya Unguja katika mchezo wa robo fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan usiku wa kuamkia jana na URA URA ikifuzu baada ya kuifunga KMKM bao 1-0 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba juzi.
Azam ambayo haijapoteza mchezo wowote katika michuano hiyo mpaka sasa itataka kuitoa nishai KCC ili kuweza kutinga fainali na kusubiri kuona itaumana na nani Jumapili kutetea taji lake.
Simba wenyewe itawavaa URA ikimtegemea nyota wake Ramadhani Singano 'Messi' na wakati wengine walioipaisha timu hiyo kwenye michuano hiyo.
Messi alifunga mabao mawili katika mechi ya robo fainali na kuibuka mchezaji bora wa michuano hiyo, japo Mrundi Amissi Tambwe ameling'ang'ania moja ya mabao hayo akidai alifunga yeye.
Makocha wa timu zote nne zilizotinga nusu fainali wamenukuliwa visiwani humo wakitamba kuwa wapo tayari kwa vita ili kuona vikosi vyao vikitinga fainali na hatimaye kunyakua taji hilo.
Tangu michuano hiyo ilipoanzishwa, hakuna klabu kutoka nje ya Tanzania imefanikiwa kutwaa taji hilo na hivyo Simba na Azam kuwa na mtihani wa kuhakikisha zinakutana tena zenyewe kwa zenyewe kulinda rekodi.

Yaya Toure atwaa tena tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika


KIUNGO nyota wa klabu ya Manchester City na timu ya taifa ya Ivory Coast, Yaya Toure ametawazwa kwa mwaka wa tatu mfululizo kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika.
Yaya aliwashinda Mnigeria John Obi Mikel aliyeshika nafasi ya pili na Didier Drogba.
Toure, aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 2011 na 2012, alipata kura 373 dhidi ya 265 na 236 za Mikel na Drogba waliomfuatia.
Sherehe za utoaji tuzo hiyo na nyingine zilihudhuriwa na Maofisa mbalimbali wakiwemo Rais wa CAF, Issa Hayatou, Gavana wa Lagos, Babatunde Fashola Raji Fashola, Waziri wa Vijana na Michezo Nigeria, Alhaji Bolaji Abdullah, Wajumbe wa Kamati Kuu ya CAF na wengineo.
Kwa tuzo ya mchezaji bora anayecheza Afrika, ilienda kwa kiungo wa Misri, Mohamed Aboutrika aliwashinda  Ahmed Fathy  wa Misiri na Sunday Mba wa Nigeria.
Hiyo ilikuwa mara ya nne, Aboutrika, aliyetangaza   kustaafu soka hivi karibuni kushinda tuzo hiyo akifanya hivyo mwaka 2006, 2008 na 2012.

TUZO ZA CAF ZILIZOTOLEWA JANA:

Mchezaji Bora wa mwaka; Yaya Toure, Ivory Coast na Manchester City
Mchezaji bora wa mwaka anayecheza Afrika; Mohamed Aboutrika, Misri na Al-Ahly
Mwanasoka anayechipukia; Kelechi Iheanacho (Nigeria)
Timu bora ya mwaka; Nigeria
Timu bora ya vijana ya mwaka; Nigeria U-17 klabu bora ya mwaka; Al-Ahly (Misri)
Kocha bora wa mwaka; Stephen Keshi (Nigeria)
Refa bora wa mwaka; Haimoudi Djamel (Algeria)
Tuzo ya mchezo wa kiungwana; Mashabiki wa Nigeria
Magwiji wa CAF; Bruno Metsu, Mehdi Faria
Tuzo ya Platinum; Goodluck Jonathan (Rais wa Nigeria)
11 bora wa kuunda kombaini ya Afrika;
Kipa: Vincent Enyeama (Nigeria)
Mabeki: Ahmed Fathy (Misri), Mehdi Benatia (Morocco), Kevin Constant (Guinea)
Viungo: Jonathan Pitroipa (Burkina Faso), John Obi Mikel (Nigeria), Yaya Toure (Ivory Coast), Mohamed Aboutreika (Misri)
Washambuliaji: Emmanuel Emenike (Nigeria), Asamoah Gyan (Ghana) na Pierre-Emerick Aubameyang (Gabon).

Mara baada ya kupokea tuzo yake Yaya amewashuku kaka zake,Obi Mikel na Drogba.