STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, May 29, 2016

Waganda kuziamua Taifa Stars v Harambee Stars

NA ALFRED LUCAS, NAIROBI
WAAMUZI watatu wa soka kutoka Uganda, ndio wakaochezesha mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Taifa Stars ya Tanzania na Harambee Stars ya Kenya utakaofanyika leo Jumapili kwenye  Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi, Kenya.
Waamuzi hao watakaochezesha mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni na kurushwa moja kwa moja na Kituo cha Televisheni cha Azam Tv kwa kushirikishi na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) ni Brian Nsubuga atakayepuliza kipenga na wasaidizi wake ni Bugembe Hussein upande wa kulia (line 1) na Katenya Ronald kwa upande wa kushoto (line 2).


Kamishna wa mchezo atakuwa Amir Hassan kutoka Somalia ambako Meneja wa Uwanja wa Moi Kasarani, Lilian Nzile amesema kwamba mazingira uwanja ni mazuri na mipango yote ya mchezo huo imekaa vema ikiwa ni pamoja na usalama uliothibitishwa pia na Kanali wa Jeshi la Polisi, Muchemi Kiruhi OCS wa Kasarani.

Kwa upande wa Kocha Mkuu Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanjaro inayozalishwa na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), Charles Boniface Mkwasa atawakosa washambuliaji wake watatu katika kikosi ambacho kitaivaa Harambee Stars.

Washambuliaji hao ni Mbwana Samatta kutoka Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu anayechezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na John Bocco ambaye ni majeruhi wa mguu aliumia wakati wa fainali za Kombe la FA kati ya Yanga na Azam Jumatano wiki hii.

“Madaktari wamempa Bocco saa 72 za mapumziko. Bila shaka kabla ya kucheza na Misri atakuwa amepona,” alisema Mkwasa leo Mei 28, 2016 asubuhi na kuongeza kuwa Samatta ametuma taarifa kukosa mchezo dhidi ya Kenya kwa kuwa ana ratiba ya kucheza mchezo muhimu Mei 30, mwaka huu na matarajio ni kujiunga na timu Juni 1, 2016 kabla ya kuivaa Misri Juni 4, mwaka huu.

Kwa upande wa Ulimwengu, uongozi wa TP Mazembe nao waliomba kumtumia Ulimwengu katika mchezo wa ushindani wa mpinzani wake AS Vita. TP Mazembe na AS Vita ni timu pinzani huko DRC Congo na uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ukaridhia na Mkwasa sasa amejipanga kukiandaa kikosi bila nyota hao mahiri.

“Katika mchezo huu sitakuwa na professionals (wachezaji wa kulipwa),” alisema Mkwasa ambaye jioni ya leo ameahidi kutoa kikosi cha nyota 11 watakaonza dhidi ya Kenya kesho.

Kwa sasa anaangalia namna ya kuipanga vema safu yake ya ulinzi baada ya kumkosa Kelvin Yondani anayetumikia adhabu ya kuonywa mara mbili kwa kadi ya njano hivyo kutojumuishwa kwenye mipango mchezo dhidi ya Misri. Mabeki anaotarajiwa kuanza nao ni Juma Abdul upande wa kulia na Mohammed Hussein upande wa kushoto.

Walinzi wakaoachukua nafasi ya Yondani na Nadir Haroub Cannavaro ambaye hakuongozana na timu katika safari ya Kenya ni Erasto Nyoni, Aggrey Morris na David Mwantika huku viungo wa kati wanaotarajiwa kupangwa ni Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude na pembeni ni Farid Mussa na Shiza Kichuya. Washambuliaji watakaotikisa Kenya katika mchezo wa kesho ni Elisu Maguli na Ibrahim Ajib.

“Kipa anaweza kuanza Dida (Deo Munishi) au Aishi Manula. Lakini hao niliokutajia ni proposed team (kikosi tarajiwa), lakini hasa nani anaaza kesho nitakutajia jioni ya leo mara baada ya mazoezi pale Moi Kasarani,” alisema Mkwasa aliyeonekana kujiamini na mipango yake kama lilivyo jina lake la umaarufu la Master.

“Nimeiandaa timu kucheza mifumo miwili ambayo ni 4-3-3 ambao ni mfumo wa kushambuliaji na pale tutakapokuwa tuna-defense (tunazuia) basi mfumo utakuwa ni 4-5-1,” alisema Mkwasa.

Katika mchezo wa kesho Mkwasa anayesaidia na Hemed Morocco na Manyika Peter anayewanoa makipa atapata nafasi ya kubadili wachezaji hadi sita ambao ni utaratibu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa mechi za kirafiki za kimataifa kadhalika makubaliano katika mkutano wa kabla ya mchezo wa kesho.

Stars iliwasili Nairobi, Kenya jana asubuhi na kupokewa na wenyeji Shirikisho la Soka Kenya iliyowapeleka hoteli ya Nairobi Safari Club iliyoko mtaa wa Koinange, katikati ya jiji la Nairobi ambako mchana kabla ya kwenda mazoezi ilitembelewa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. John Haule aliyewahakikishia usalama  timu hiyo licha ya kuwako kwa taarifa za kuvamiwa.

“Msaada wowote mnaotaka na chochote mnachohitaji tunaomba mtutaarifu tujue namna ya kuwasaidia. Msiwe na wasiwasi kabisa. Hata kama hamjaipenda hoteli, semeni,” alisema Dk. Haule ambaye aliitakia timu mafanikio mazuri katika mchezo wa dhidi ya Harambee na ule wa Mafarao wa Misri.

Viongozi wa msafara wa Taifa Stars, Ahmed Mgoyi na Omar Walii walimweleza Balozi DK. Haule kuridhika na kambi na kwamba hawakupata tatizo lolote hali ilivyo hadi sasa.

Real Madrid vidume Ulaya, yaikandamiza tena Atletico

http://theblogfc.com.au/wp-content/uploads/2014/08/real-madrid-champions-league.jpg KLABU ya Real Madrid usiku wa kuamkia leo Jumapili, imefanikiwa kutwaa taji lake la 11 la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuilaza kwa mikwaju ya penalti 5-3  mahasimu wao, Atletico Madrid.
Real na Atletico zilimaliza muda wa dakika 120 zikiwa nguvu sawa ya kufungana bao 1-1 katika mchezo mkali wa fainali uliochezwa Uwanja wa San Siro, Milan, Italia.
Kipa Keilor Navas Gamboa alijitanua vizuri langoni na Juan Francisco Torres Belen ‘Juanfarn’ akaona lango dogo na kugongesha nguzo ya pembeni penalti ya nne ya Atletico.
Cristiano Ronaldo akaenda kwa kujiamini kupiga penalti ya mwisho ya Real Madrid na kumtungua kipa Jan Oblak wa Atletico kuwapa Magalactiico taji la 11 la Ligi ya Mabingwa.
Wengine waliofungaa penalti za Real Madrid ni Lucas Vazquez, Marcelo, Gareth Bale na Sergio Ramos, wakati Atletico zimefungwa na  Antonio. Griezmann, Gabi na Saul.
Nahodha wa Reald Madrid, Sergio Ramos akiinua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuifunga Atletico Madrid kwa penalti 5-3 usiku huu Uwanja wa San Siro PICHA ZAIDI GONGA HAPA   

Mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa England, Mark Clattenburg aliyesaidiwa na Simon Beck na Jake Collin, Real Madrid walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa beki wake na Nahodha, Sergio Ramos dakika ya 15 aliyemalizia mpira wa kichwa wa winga Gareth Bale.
Baada ya bao hilo, Real waliuteka mchezo na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Atletico, lakini bahati haikuwa yao.
Kipindi cha pili, kocha Diego Simeone wa Atletico alianza na mabadiliko, akimpumzisha kiungo Muargentina mwenzake Augusto Matias Fernandez na kumuingiza kiungo Mbelgiji Yannick Ferreira Carrasco.
Mabadiliko hayo yalikuwa msaada kwa kikosi cha Simeone, kwani ni Carrasco aliyekwenda kuisawazishia Atletico dakika ya 79, akimalizia pasi ya Juan Francisco Torres Belen, maarufu kama Juanfran.
Bao hilo ‘likauamsha’ upya mchezo huo, timu zote zikicheza ka nguvu na kasi kusaka bao la ushindi, lakini dakika 90 zikamalizika kwa sare ya 1-1.
Awali ya hapo, mshambuliaji hatari wa Atletico Madrid, Antonio Griezmann alipaisha mkwaju wa penalti dakika ya 48 baada ya Fernando Torres kuangushwa na Pepe kwenye boksi.
Kocha Mfaransa, Zinadine Zidane aliwapumzisha Karim Benzema, Daniel Carvajal na Toni Kroos kipindi cha pili na kuwaingiza Isco, Danilo na Lucas Vazquez.
Katika dakika 30 za nyongeza timu zote zilicheza kwa tahadhari mno na mwishoni mwa mchezo, Simeone akawatoa Filipe Luis na Koke na kuwaingiza Lucas Hernandez na Thomas Teye Partey.
  Kwa ushindi huo Real inafikisha mataji 11 ya Ligi ya Mabingwa, mengine ikitwaa misimu ya 1955–1956, 1956–1957, 1957–1958, 1958–1959, 1959–1960, 1965–1966, 1997–1998, 1999–2000, 2001–2002 na 2013–2014.