STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 17, 2013


Bondia Fadili Majia akiwa na kombe la ubingwa wa kimataifa wa ngumi alililonyakua nchini Indonesia wiki iliyopita alipo mpiga bondia Heri Amol  hapa alipolakiwa baada ya kutua jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini, Rajabu Mhamila 'Super D', mabondia Japhet Kaseba, Kanda Kabongo na Pendo Njau.
Kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' kushoto akifurahia jambo na bondia Pendo Njau baada ya kumpokea Fadhili Majiha katikati aliyerudi na kombe la ubingwa aliouchukua Indonesia wiki iliyopita  baada ya kumtwanga bondia Heri Amol wa pili ni Japhet Kaseba mwingine ni Kanda Kabongo.

JKT Ruvu yaapa kupambana mpaka mwisho Ligi Kuu

Kikosi cha JKT Ruvu Stars

WACHEZAJI wa klabu ya JKT Ruvu wameapa kupigana kufa na kupona ili kuhakikisha timu yao haishuki daraja kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara, wakizitangazia vita na kuzitaka zikae chonjo timu nne watakazokutana  nazo kabla ya kumaliza mechi zao za msimu.
JKT Ruvu ambayo kwa msimu huu imeonekana kutetereka tofauti na msimu kadhaa ya nyuma ambayo ilipokuwa ikimaliza ligi katika Nne Bora, ni miongoni mwa timu zilizopo katika eneo la hatari la kushuka daraja ikiwa na pointi chache huku ligi ikielekea ukingoni.
Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wamesema pointi moja waliovuna Mkwakwani-Tanga mbele ya Coastal Union waliotoka nayo sare ya 0-0, wamepata nguvu ya kuhakikisha wanafanya vyema katika mechi zao zilizosalia ikiwamo dhidi ya Yanga Jumapili jijini Dar es Salaam.
Kessy Mapande mmoja wa wachezaji waandamizi wa timu hiyo, alisema mechi nne zilizosalia kwao
ni kama fainali kwa kuamini kuteleza kidogo tu kutairudisha JKT Ruvu Ligi Daraja la Kwanza kitu ambacho hawakati kukisikia hata kidogo.
Mapande walisema mechi zao nne zilizosalia ikiwamo ya Jumapili dhidi ya Yanga, African Lyon, Prisons ya Mbeya na ile ya mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar zote wanazichukulia kwa uzito mkubwa wakipania kushinda au kupata pointi za kutosha za kuwaepusha kushuka daraja.
"Tutapambana mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha tunapata ushindi na kuvuna pointi za
kutunusuru kushuka daraja, yaani mechi zilizosalia kwetu ni kama fainali tutashuka dimbani
kupigana kiume kuinusuru JKT isirudi daraja la kwanza," alisema Mapande.
JKT ambayo imepoteza aliyekuwa kocha wao, Charles Kilinda aliyetangaza kujiuzulu kutokana na
timu kufanya vibaya msimu huu, mpaka sasa ipo katika nafasi ya 11 baada ya juzi kupata suluhu
Tanga iliyoifanya ifikishe pointi 23 na kuishusha Toto katika nafasi hiyo.
Kikosi hjicho cha maafande kitashuka dimbani Jumapili kuwakabili Yanga kabla ya Jumatano ijayo
kuvaana na African Lyon uwanja wa Chamazi kisha kuumana na Prisons wiki ijayo kwenye uwanja
huo huo wiki ijayo na kwenda kumalizia Manungu dhidi ya Mtibwa Sugar Mei 18

Benny Ngassa ataka wadau wa soka Ilala kuisaidia Ashanti United

Kikosi cha Ashanti kilichorejea Ligi Kuu

Benny Ngassa katika pozi
BAADA ya kuthibitishwa rasmi kuwa miongoni mwa timu tatu zilizopanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, baadhi ya wachezaji wa Ashanti United wamewaomba mapema wadau wa soka wa Ilala kuiunga mkono kwa hali na mali ili ifanye vyema katika ligi hiyo.
Wachezaji hao walisema juhudi walizofanya kuirejesha tena Ashanti katika ligi hiyo baada ya misimu kadhaa ya kusota Ligi Daraja la Kwanza ni lazima ziungwe mkono kwa wadau kuiwezesha timu hiyo kufanya usajili mzuri na kumudu gharama za ushiriki wa ligi kuu msimu ujao.
Mmoja wa wachezaji hao, Bennedict Ngassa, alisema bila wadau wa soka wa Ilala kuiunga mkono klabu yao katika ushiriki wa ligi kuu msimu ujao, timu inaweza kuyumba na kufanya vibaya kitu ambacho alisema wachezaji wa Ashanti wasingependa kuona baada ya kuipandisha timu daraja.
"Tunashukuru kwa kufanikiwa kuipandisha timu daraja na kuirejesha Ashanti Ligi Kuu, lakini kazi bado haijaisha kwa wale wote waliokuwa wakituunga mkono, tunahitaji sapoti zaidi katika maandalizi na ushiriki wa ligi hiyo ili tusirudi tena FDL (ligi daraja la kwanza)," alisema Ngassa.
Ngassa aliyetua Ashanti baada ya kushuka daraja na timu ya Moro United msimu uliopita na kuifungia mabao matatu, alisema nguvu ya pamoja na sapoti toka kwa mashabiki na wadau wote wa soka wa Ilala, ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na kutisha kwenye ligi hiyo.
Ashanti United iliyowahi kucheza na kutamba kwenye ligi kuu kabla ya kushuka msimu wa 2007-2008,
imerejea tena katika ligi hiyo ikiwa sambamba na timu za Mbeya City na Rhino Rangers ya Tabora baada ya kufanya vyema katika mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza iliyomalizika hivi nkaribuni

Bi Kidude kuzikwa kesho, wengi wamlilia

Bi Kidude enzi za uhai wake

MKONGWE wa muziki wa taarab nchini aloyejipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi, Fatuma Bint Baraka Bint Khamis 'Bi Kidude' aliyefariki asubuhi ya leo anatarajiwa kuzikwa kesho visiwani Zanzibar.
Bi Kidude anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya 100, alifariki Bububu Zanzibar kutokana na kuugua kwa muda mrefu maradhi ya Kisukari.
Taarifa kutoka kwa ndugu za marehemu zinasema kuwa Bi Kidude alizidiwa kwa siku nne mfululizo kabla ya kufariki leo na kwamba mwili wake utapelekwa kwake Rahaleo kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho. 
Bi Kidude aliyezaliwa katika kijiji cha Mfereji Maringo, akiwa mmoja wa watoto saba wa mchuuzi maarufu wa nazi wa eneo hilo na alianza kuimba akiwa mwaka 1920 kabla ya kutoka kwao baada ya kulazimishwa kuolewa.
Enzi za uhai wake alifanya kazi ya sanaa akiimba na makundi mbalimbali za muziki wa mwambao uliomtangaza vyema ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya makundi aliyoyafanyia kazi mwanamuziki huyo aliyewahi kwenda kuimba Misri ni pamoja na Egyptian Musical Club ya Dar es Salaam, Cultural na vingine.
Nyimbo zilizompa umaarufu ni pamoja na Muhogo wa Jang'ombe na alikuwa akishiriki maonyesho mbalimbali ya jukwaani ambapo hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya maisha katika Tamasha la Filamu za Nchi za Majahazi, ZIFF.
Pia alitapa tuzo za Womax na mwaka jana katika kusherehekea miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania alkitunukiwa nishati ya heshima na rais Jakaya Kikwete.
Pia alikuwa akishirikishwa nyimbo za wasanii mbalimbali wa kizazi kipya baadhi wakitumia pia nyimbo zake, huku akiwa mwingi wa utani.
Marehemu Bi Kidude hakubahatika kuzaa mtoto kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe alipohojiwa enzi za uhai wake.
Baadhi ya wasanii mbalimbali nchini kama akina Jacob Stephen 'JB', Lady Jay Dee, Fid Q na wakali wengine wameonyesha kusikitishwa na kifo cha mkongwe huyo kwa kudai Tanzania imepoteza lulu katika tasnia ya sanaa.
Huku wakimtaja kama 'kungwi' katika muziki na masuala ya 'Unyago' akiwafunda wanawake jinsi ya kuheshimu ndoa zao pamoja na kuwa na maadili mema ndani na nje ya ndoa zao sambamba na kwenye  jukwaa la sanaa ili wadumu kama ilivyokuwa kwake.
Pamoja na sauti tamu aliyokuwa nayo Bi Kidude mwenyewe aliwahi kukiri kuwa ni 'mlevi' wa kutupwa wa kuvuta sigara.
Mungu Amlaze Mahali Pema Peponi Bi Kidude Ameen!

Yanga yabanwa, Mtibwa yainyuka Oljoro, Toto ikizama Kaitaba


WAKATI vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ikicheleweshewa sherehe zake za ubingwa Mkwakwani, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar zimetaka nyumbani kwa kuzizamisha JKT Oljoro na Toto African.
Yanga ilisimamishwa kwa kusubiri dakika za jioni kupata bao la kusawazisha la kusawazisha mbele ya Mgambo JKT iliyoongoza kwa bao 1-0 wakati wa mapumziko.
Bao lililoinusuru Yanga na kipigo cha kwanza tangu duru la pili kuanza lilifungwa na Simon Msuva na kuifanya Yanga kuongeza pointi moja kileleni ikifikisha 53 na sasa kusubiri mechi ijayo dhidi ya Ruvu Shooting kujiweka tayari kushangilia ubingwa.
Mgambo kwa sare hiyo imefikisha pointi 25 na kupata matumaini ya kusalia Ligi Kuu, kutokana na ukweli bado ina mechi tatu mkononi na inahitaji pointi moja tu kujihakikishia usalama wa kusalia katika ligi hiyo.
Mtibwa ikiwa nyumbani uwanja wa Manungu imeilaza Oljoro JKT kwa bao 1-0 lililofungwa katika dakika ya 37 na Twaha Ally, na kuwafanya mabingwa hao wa zamani kufikisha pointi 36 sawa na Simba na kurejea kwenye nafasi yake ya tano iliyoshikiliwa kwa muda na Coastal ambayo jana iliiengua baada ya kupata sare kwa JKT Ruvu.
Nako mjini Bukoba, Kagera Sugar ilipigilia msumari wa mwisho katika jeneza la Toto Africans baada ya kuilaza kwa bao moja lililofungwa dakika za mapema na Themi Felix na kuzidi kuiweka pabaya wageni wao kusalia kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Toto kwa kipigo hicho imendeelea kusalia na pointi 22 ikisaliwa na mechi moja tu, na kusalimika kwake kubaki ligi kwa msimu ujao itategemea na matokeo ya mechi yake ya mwisho na kuziombea Mgambo JKT na JKT Ruvu ziteleze katika mechi zao kitu ambacho ni miujiza mitupu.
Kabla ya kwenda Kagera, Toto ilitishia isingeenda kwa madai wanakaribia kumaliza mechi zao wakati timu nyingine zikiwa na mechi chache kitu ambacho kinaweza kuwaathiri kimatokeo na kiushuka daraja kionevu.
Hata hivyto kwa mkwara waliochimbwa na TFF walilazimika kwenda na kukumbana na maafa hayo ambayo yanaifanya timu hiyo kuelekea kurudi ligi ya FDL baada ya kuwa na misimu mibaya katika ligi hiyo.

MTANZANIA KUONGOZA UJUMBE MKUTANO WA NGUMI MAREKANI


MTANZANIA  Onesmo Ngowi ambaye ndiye ni Rais wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati, ataongoza ujumbe mzito kutoka bara la Afrika na Ghuba ya Uajemi kwenye mkutano wa 30 wa Shirikisho la Ngumi la Kimataifa na Chama Cha Ngumi Cha Marekani (IBF/USBA).
Mkutano huo utafanyika katika hotel ya nyota tano ya Concorde Berlin iliyo karibu na Kanisa la kumbukumbu la Kaiser Wilhelm pamoja na taasisi ya Helmut Newton na Jumba la ukumbusho wa Picha jinini Berlin, Ujerumani.
 
Ujumbe atakaoongoza Ngowi utajumuisha wajumbe kutoka katika nchi za Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati na mpaka sasa ni nchi 31 zitakazo jumuika katika ujumbe huo ambao utajumuisha viongozi wa mashirika mbalimbali ya kusimamia utalii, biashara na michezo.
 
Mbali na kuhudhuria mkutano huo utakaofanyika kwa siku sita kuanzia Mei 21 mpaka Mei 26, ujumbe wa Ngowi utafanya pia mazungumzo na viongozi pamoja na taasisi mbalimbali zinazosimamia Utalii, Uwekezaji pamoja na Utalii wa Michezo katika nchi ya Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya ambazo zitatembelewa na ujumbe huo.
 
Katika msafara huo ambao utajumuisha pia viongozi wa bodi za Utalii na Michezo kutoka katika nchi za Botswana, Afrika ya Kusini, Ghana, Misri na Falme za nchi za Kiarabu (UAE),ujumbe huo utatembelea pia nchi za Ufaransa, Ubeljiji, Uhispania pamoja na Uholanzi!
 
Ngowi amewahimiza watanzania juu kuchangamkia fursa za kujitangaza kibiashara nje ya nchi na kuwataka kujituma. “Ni muhimu Watanzania wakafungua macho na wajue kuwa dunia sasa ni kijiji na wasipoangalia watajikuta wanabaki nyuma kila mara” aliema Ngowi ambaye kwa ujumla alionyeha kusikitishwa na muitikio mdogo wa watanzania kwenye masuala ya kujitangaza kibishara nje ya nchi.
 
Ujumbe wa Ngowi utaondoka barani Afrika tarehe 17 Mwezi Mei na kuelekea Dubai ambako ndipo wajumbe wote watakapokutana tayari kwa msafara wa kuelekea jijini Berlin, Ujerumani!

Yanga kuvuna nini kwa Mgambo, Toto kujishusha daraja?

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo watakuwa Mkwakwani Tanga kukabiliana na wenyeji wao Mgambo JKT, akili zao zikiwa kwenye taji la ubingwa ambalo kwa sasa halina mwenyewe baada ya Simba kulitema wiki iliyopita.
Yanga inahitaji pointi tano tu katika mechi zake nne zilizosalia kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2012-2013 kutangazwa kuwa bingwa, na tayari wameapa kwamba leo ni lazima Mgambo walegee kwao kabla ya kuwakabili JKT Ruvu Jumapili kwenye uwanja wa Taifa.
Ingawa leo kuna mechi nyingine mbili, ikiwamo iliyo katika hatia hati ya kuchezwa kati ya Kagera Sugar dhidi ya Toto African, macho na masikio ya mashabiki wa soka yapo Mkwakwani kutaka kusikia na kuona kama Yanga itaendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi yoyote ndani ya mwaka 2013.
Yanga imeapa kuvuna pointi tatu katika pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Athuman Lazi kutoka Morogoro atakayesaidiwa na Michael Mkongwa wa Iringa na Godfrey Kihwili kutoka Arusha na kamishna wa mchezo huo anatarajiwa kuwa Godbless Kimaro kutoka Moshi, ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa bingwa mpya wa Tanzania na kutwaa taji la 23 katika ligi hiyo tangu mwaka 1965.
Kocha wa  Ernie Brandts, alinukuliwa jana kuwa mchezo huo wa leo, utamwongezea asilimia 10 kati ya 90 alizokuwa nazo za kutwaa ubingwa na kudai kuwa awali alitishwa na kasi ya wapinzani wao Azam ambao Jumapili iliyopita walisimamishwa na Simba kwa kutoka sare ya mabao 2-2.
Licha ya kujipa asilimia hizo endapo watashinda mchezo huu, amewataka vijana wake kutokuwa na papara ili kuhakikisha wanashinda na kutimiza malengo yao kabla ya ligi kuisha.
Hata hivyo Yanga itawakabili Mgambo bila baadhi ya nyota wake ambao ni majeruhi na wengine wagonjwa akiwamo kiungo mahiri, Haruna Niyonzima, beki Juma Abdul na mshambuliaji Didier Kavumbagu.
Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizunguto alitamba kuwa licha ya kuwakosa nyota hao bado Yanga wapo imara kuweza kuvuna pointi tatu ili kuwaweka karibu na ubingwa na kuikimbia Azam waliopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo ambao watakuwa 'likizo' kujiandaa na pambano la kimataifa dhidi ya FAR Rabat ya Morocco katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ukiondoa pambano la Mkwakwani, jioni ya leo pia kutakuwa na mechi nyingine zinazohusisha timu ndugu za Mtibwa Sugar na Kagera Sugar ambazo zitakuwa viwanja vyao vya nyumbani kuzikaribisha JKT Oljoro na Toto African, japo Toto imesisitiza kuwa haitakwenda Kagera kuumana na Kagera Sugar leo.
Katika pambano la Manungu, Mtibwa na Oljoro zitahukumiwa na mwamuzi Israel Mkongo, ambapo wenyeji watakuwa wakisaka ushindi utakaowawezesha kuchupa hadi nafasi ya tano baada ya jana kuenguliwa na Coastal baada ya kuambulia sare ya 0-0 mbele ya maafande wa JKT Ruvu.
Yanga ina pointi 52, ikifuatiwa na Azam pointi 47, Kagera Sugar pointi 37, kisha kufuatiwa Simba yenye pointi 35 na kufuatiwa na Coastal na Mtibwa zenye pointi 33 kila mmoja na kutofautiana kwenye uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Washelisheli kuzihukumu Azam na FAR Rabat J'Mosi


Na Boniface Wambura
TIMU ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayoikabili Azam kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho inatua nchini leo (Aprili 17 mwaka huu) saa 7.30 mchana kwa ndege ya Qatar Airways.

Msafara wa timu hiyo wenye watu 28 kwa ajili ya mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utafikia hoteli ya Sapphire iliyoko maeneo ya Kariakoo.

Wakati Azam imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa timu ya Barrack Young Controllers II ya Liberia kwa jumla ya mabao 2-1, AS FAR Rabat imeingia raundi hiyo moja kwa moja kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri kwenye michuano ya klabu Afrika.

Timu nyingine ambazo zimeingia raundi hiyo moja kwa moja katika Kombe la Shirikisho kama ilivyo AS FAR Rabat ni Asec Mimosas ya Ivory Coast, Atletico Petroleos (Angola), C.S.S. (Tunisia), DC Motema Pembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), El Ahly Shandy (Sudan), Enppi (Misri), Heartland (Nigeria), Ismaily (Misri), Lobi Stars (Nigeria), U.S.M. Alger ya Algeria na Wydad Casablanca (Morocco).

Mwamuzi Emile Fred atakayesaidiwa na Steve Maire, Jean Ernesta na Jean Claude Labrossa wote kutoka Shelisheli ndiye atakayechezesha mechi hiyo. Kamishna ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda. Waamuzi watawasili nchini kesho (Aprili 18 mwaka huu) jioni.