STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, June 28, 2014

Kimbembe cha 16 Bora leo, nani kufuzu Robo Fainali?!


Colombia
Uruguay
KIVUMBI cha hatua ya mtoano cha 16 Bora cha Fainali za Kombe la Dunia 2014  kinatarajia kuanza kutimka rasmi leo wakati wenyeji Brazil na nchi nyingine tatu za Amerika Kusini zitakapochuana kuwania nafasi ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo inayoendelea nchini Brazil.
Brazil chini ya nyota wake wakiongozwa na Neymar watakawakabili majirani zao Chile, huku Colombia itapepetana na Uruguay itakayomkosa nyota wake Luis Suarez aliyefungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa kitendoi cha kumuuma mchezaji Giorgio Chiellini wa Italia.
Wenyeji waliongoza msimamo wa kundi A mbele ya Mexico watashuka dimbani mapema saa 1 usiku kwenye uwanja wa Governador Magalhães Pinto, kuwakabili Chile watakaomtegemea Alexis Sanchez katika mechi inayosubiriwa kwa hamu kuona kama Brazil watatoka salama kwa wapinzani wao.
Ingawa rekodi zinaonyesha kuwa, timu hizo zimeshakutana mara 68 na Brazil ikiwatambia wapinzani wao mara 48 na kufungwa mara 7 na kutoka sare michezo 13, huku wenyeji hao wakifunga jumla ya mabao 159-58 katika michezo waliyokutana, bado Chile siyo timu ya kubezwa.
Katika fainali za mwaka huu wakiwa kundi B waliweza kumaliza katika nafasi ya pili bila kutarajiwa mbele ya waliokuwa mabingwa watetezi Hispania na Australia walizozipatia katika mechi za makundi.
Katika michuano ya  Kombe la Dunia hatua ya Mtoano, Brazil na Chile zimekutana mara 3 na zote Brazil kushinda. Mwaka 1962, kwenye Nusu Fainali, Brazil ilishinda 4-2. Mwaka 1998, Raundi ya Mtoano ya Timu 16, Brazil walishinda 4-1 na huko Afrika Kusini, Mwaka 2010 pia Raundi ya Mtoano ya Timu 16, Brazil ilishinda 3-0.
Hata hivyo tayari kocha wa Chile, Jorge Luis Sampaoli Moya kutoka Argentina amesema watashuka dimbani leo kuhakikisha wanapata matokeo bora ili kuona kikosi chake kinavuka hatua hivyo, licha ya kukiri ni mtihani mgumu mbele ya Brazil yenye nyota kama Neymar.
Cha kuvutia katika mechi hiyo ni kwamba itachezeshwa na refa Howard Webb kutoka England ambaye hii itakuwa ni mara yake ya pili kuzipambanisha timu hizo katika hatua kama hiyo.
Ndiye aliyezihukumu katika Fainali zilizopita nchini Afrika Kusini ambapo Brazil waling'ara kwa kushinda kwa mabao 3-0 kabla ya kwenda kung';oka mbele na kuziacha Hispania na Uholanzi zikicheza fainali.
Pambano jingine litakalochezwa leo litazikutanisha timu za Colombia na Uruguay pambano litakalochezwa usiku wa saa 5 kwenye uwanja wa mkubwa wa Maracana.
Uguruay itashuka dimbani bila huduma za Suarez aliyerudishwa nyumbani kutokana na kitendo cha kufungiwa na FIFA kwa kosa la kumng'ata mchezaji wa Italia Giorgio Chiellini wakati wa mechi ya kufungia pazia la hatua ya makundi na Uguguay kushinda kwa bao 1-0 na kutinga bila kutrarajiwa nyuma ya Costa Rica.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa tamu pengine kuliko lile la Brazil na Chile kutokana na Colombia kuwa miongoni mwa timu zisizotabirika na kati ya chache zilizoshinda kwa asilimia 100 michezo yao ya makundi.
Ikiongozwa na James Rodriguez aliyeziba kwa mafanikio pengo la Radamel Falcao ambaye aliondolewa kwenye kikosi hicho kutokana na majeraha, Colombia inatarajiwa kutoa upinzani mkali.
James Rodriguez ana mabao matatu mpaka sasa kwenye michuano hiyo akishika nafasi ya pili pamoja na nyota wengine wa timu zilizoshiriki michuano hiyo na atakuwa akisaidiana kusaka ushindi kuvuka hatua hiyo na wachezaji wenzake kama Jackson Martínez,Armero, Cuadrado na Gutierrez.
Hata hivyo Uruguay pamoja na kumkosa Suarez, bado ina silaha kali kama Edinson Cavani, Diego Godin, Arevalo na wengine kuhakikisha wanafanya kweli katika mechi hiyo ambayo itakuwa ni ya 15 kwa timu hizo kukutana katika michezo mbalimbali tangu mwaka 2005.
Rekodi zinaonyesha katika kukutana huko, Uruguay imeitambia Colombia mara 8 na kupoteza mechi nne na mbili zilizosalia walitoshana nguvu kwa kutoka sare.
Je, ni Brazil au Chile itakayokuwa ya kwanza kufuzu robo fainali na Colombia itaendelea kuwa mnyonge kwa Uruguay na kupigwa kumbo kutinga hatua inayofuata au watajitutumua na kuinyuka Uruguay bila ya Suarez? Tusibiri tuone baada ya kumalizika kwa mechi hizo kabla ya kesho kushuhudia kitupe kingine.

Liverpool sasa kumuua Suarez kuwabeba Lallana na Markovic

Suarez akiwajibika siku ya mechi dhidi ya England kabla ya kuja kuharibu wakiumana na Italia
KLABU ya soka ya Liverpool ipo kwenye mpango wa kumuuza nyota wake Luis Suarez katika klabu ya Barcelona, ili kupata fedha za kuwanyakua Adam Lallana na Lazar Markovic.
Barcelona imetajwa kuoingoza mbio za kumnyakua mchezaji huyo aliyefungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) baada ya kumng'ata beki wa Italia Giorgio Chiellini .
Klabu hiyo ya Hispania imeweka wazi kuwa hata kama Suarez amefungiwa miezi minne kucheza soka, hiyo haizuii nia yao ya kumsajili na mpaka sasa Liverpool hawajahangaika kutafuta mbadala wa mshambuliaji huyo hatari.
Ingawa Liverpool walikuwa wanaweka ngumu kwa dau hilo, lakini baada ya kupokea taarifa za FIFA kuhusu kumfungia Suarez wamelazimika kukubali na kumruhusu Muurguay huyo kuondoka klabuni hapo.
Licha ya kufungiwa, Liverool wanaamini Barcelona inaweza kulipa paundi milioni 80 na tayari mmiliki mkuu wa klabu hiyo John W Henry anaonekana kutokuwa tayari kumuuza kwa bei rahisi.
Mwanasheria wa Suarez Alejandro Balbi alikuwa Barcelona kujadili hatima ya mteja wake, wakati kocha mpya wa Barca Luis Enrique alisema hakuna tatizo lolote juu ya kumsajili nyota huyo mwenye miaka 27.
Alimfananisha Suarez na mshambuliaji gwiji wa Barca Hristo Stoichkov na alisema : ‘Stoichkov kiukweli aliwahi kufanya madhambi makubwa dhidi ya mwamuzi, lakini aliendelea kufirika kuwa mcheza mkubwa".
Kama Liverpool watamuuza Suarez kwa paundi milioni 80, hiyo itakuwa biashara nzuri kwa Brendan Rodgers ambapo atatumia mkwanja huo kuimarisha kikosi chake.
Wachezaji ambao Liverpool inawapigia jaramba kuwanasa ni Adam Lallana kutoka Southampton anayetajwa atakuwa mali ya Vijogoo hao wekundu  saa 24 zijazo baada ya Southampton kukubali ofa ya paundi milion 25 kwa mshambuliaji huyo wa England, na hii ni baada ya kupita wiki nne tangu apokee simu kutoka kwa maofisa wa Anfield ambao pia wameanza mbio za kumuwania mchezaji wa Benfica, Lazar Markovic.
Mserbia, Markovic ni moja ya wachezaji bora wenye umri mdogo katika soka la Ulaya na bei yake ni paundi milioni 20.

Neymar, Muiller, Messi wabanana kuwania kiatu cha Dhahabu

Neymar wa Brazil
Lionel Messi wa Argentina
Thomas Muiller wa Ujerumani  
WAKATI  kinyang'anyiro cha hatua ya mtoano ya 16 Bora ikianza rasmi leo kwa michezo miwili itakayozikutanisha timu za Amerika Kusini, hatua ya makundi ya Fainali za Kombe laDunia 2014 imevunja rekodi.
Jumla ya mabao 136 yamefungwa katika hatua hiyo, sita zaidi ya yale yaliyofungwa katika fainali za 2002.
Wachezaji watatu, Lionel Messi wa Argentina, Neymar wa Brazil na Thomas Muiller wa Ujerumani wanachuana kileleni katika orodha ya wafungaji bora.
Kila moja kati ya wachezaji hao amefunga mabao manne wakifuatiwa na wachezaji sita wenye mabao matatu kila mmoja.
Neymar ana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao yake kama leo ataendelea kucheka kwenye mechi yao na Chile kuwania kufuzu Robo Fainali.
Messi atakuwa na nafasi ya kuendelea kunguruma wakati atakapoiongoza Argentina kuvaana na Uswisi siku ya Jumatatu katika mechi nyingine ya 16 Bora.
Ukiondoa wakati hao wenye mabao manne, wachezaji wenye magoli matatu kila mmoja ni pamoja na Robin van Persie, Arjen Robben wote wa Uholanzi, Karim Benzema wa Ufaransa, Enner Valencia wa Ecuador, James Rodriguez wa Colombia na Xherdan Shaqiri wa Uswisi.
Kati ya hapo ni Valencia tu ndiye hana nafasi ya kuongeza idadi yake ya mabao kwa vile timu yake imeshaaga michuano hiyo nchini Brazili.
Katika orodha ya wafumania nyavu hiyo pia wapo wachezaji wenye mabao mawili mawili ambao ni;Tim Cahill wa Australia, Mario Mandzukic wa Croatia, Martinez wa Colombia, Dempsey wa Marekani, Wilfried Bony wa Ivory Coast, Andre Ayew wa Ghana, Asamoah Gyan wa Ghana, Ahmad Mussa wa Nigeria na Slimani wa Algeria.
Ukimuondoa Dempey wa Marekani, Mussa wa Nigeria na Slimani wa Algeria waliosalia timu zaoi zimeshaaga michuano na hivyo hawana nafasi ya kuongeza idadi.

Mashetani Wekundiu wazidi kujiimarisha England

Jembe Jipya! Luke Shaw akiwa na jezi mpya ya klabu yake ya Manchester United
Ander Herrera alipotangazwa ramsi kujiunga kwa Mashetani Wekundu
MABINGWA wa zamani wa England, Manchester United imezidi kuimarisha kikosi chake baada ya kufanikiwa kumsainisha beki wa kushoto wa Southamptom na timu ya taifa ya nchi hiyo iliyotolewa kwenye Kombe la Dunia, Luke Shaw.
Kwa mujibu wa duru za kandanda za England zinasema kuwa, Mashetani Wekundu hao wamekamilisha uhamisho wa Shaw kwa gharama za Pauni Milioni 31.5 kwa mkataba wa miaka minne.rd.
Mchezaji huyo amekamilisha vizuri vipimo afya katika Uwanja wa mazoezi wa United, Carrington na ameambiwa atakuwa beki wa kushoto chaguo la kwanza la kocha Louis van Gaal.
Inafahamika amehakikishiwa namba na beki mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Patrice Evra, ambaye atabakia United, anatarajiwa kupunguziwa majukumu klabuni hapo. 
Usajili wa Shaw umekuja siku moja baada ya klabu hiyo kufanikiwa kunyakua Ander Herrera kutoka Athletic Bilbao kwa ofa ya pauni milioni 29.
Man United ilikuwa na msimu mbaya ligi iliyopita chini ya kocha David Moyes ambaye alitimuliwa na nafasi yake kushikiliwa kwa muda Ryan Giggs kabla ya Luis van Gaal kupewa kibarua cha kuwa kocha mkuu sasa.

Soma orodha ya waliochaguliwa Kidato cha Tano 2014

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini, imetoa  majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na shule mbalimbali kwa ajili ya kuendelea na elimu ya sekondari kidato cha tano, sanjari na vyuo mwaka 2014.

Orodha hiyo imetangazwa jijini Dar es salaam tangu Juni 17, ambapo idadi ya wasichana waliochaguliwa kwa nafasi hizo ni 9,378, waliochaguliwa katika machaguo 13 ya masomo mbalimbali ya kidato cha tano na masomo 11 ya vyuo vya ufundi.

Shule zilizopangiwa wanafunzi ni 201, ambapo shule za wasichana pekee ni 61, huku shule 34 zikiwa za jinsia zote mbili, wasichana na wavulana.

Idadi ya wanafunzi wavulana waliochaguliwa katika machaguo 13 ya masomo mbalimbali ya ngazi hiyo, ni 22,138.
Kupata Majina Hayo tafadhali bonyeza Links Hizi Hapa chini