STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, June 28, 2014

Kimbembe cha 16 Bora leo, nani kufuzu Robo Fainali?!


Colombia
Uruguay
KIVUMBI cha hatua ya mtoano cha 16 Bora cha Fainali za Kombe la Dunia 2014  kinatarajia kuanza kutimka rasmi leo wakati wenyeji Brazil na nchi nyingine tatu za Amerika Kusini zitakapochuana kuwania nafasi ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo inayoendelea nchini Brazil.
Brazil chini ya nyota wake wakiongozwa na Neymar watakawakabili majirani zao Chile, huku Colombia itapepetana na Uruguay itakayomkosa nyota wake Luis Suarez aliyefungiwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa kitendoi cha kumuuma mchezaji Giorgio Chiellini wa Italia.
Wenyeji waliongoza msimamo wa kundi A mbele ya Mexico watashuka dimbani mapema saa 1 usiku kwenye uwanja wa Governador Magalhães Pinto, kuwakabili Chile watakaomtegemea Alexis Sanchez katika mechi inayosubiriwa kwa hamu kuona kama Brazil watatoka salama kwa wapinzani wao.
Ingawa rekodi zinaonyesha kuwa, timu hizo zimeshakutana mara 68 na Brazil ikiwatambia wapinzani wao mara 48 na kufungwa mara 7 na kutoka sare michezo 13, huku wenyeji hao wakifunga jumla ya mabao 159-58 katika michezo waliyokutana, bado Chile siyo timu ya kubezwa.
Katika fainali za mwaka huu wakiwa kundi B waliweza kumaliza katika nafasi ya pili bila kutarajiwa mbele ya waliokuwa mabingwa watetezi Hispania na Australia walizozipatia katika mechi za makundi.
Katika michuano ya  Kombe la Dunia hatua ya Mtoano, Brazil na Chile zimekutana mara 3 na zote Brazil kushinda. Mwaka 1962, kwenye Nusu Fainali, Brazil ilishinda 4-2. Mwaka 1998, Raundi ya Mtoano ya Timu 16, Brazil walishinda 4-1 na huko Afrika Kusini, Mwaka 2010 pia Raundi ya Mtoano ya Timu 16, Brazil ilishinda 3-0.
Hata hivyo tayari kocha wa Chile, Jorge Luis Sampaoli Moya kutoka Argentina amesema watashuka dimbani leo kuhakikisha wanapata matokeo bora ili kuona kikosi chake kinavuka hatua hivyo, licha ya kukiri ni mtihani mgumu mbele ya Brazil yenye nyota kama Neymar.
Cha kuvutia katika mechi hiyo ni kwamba itachezeshwa na refa Howard Webb kutoka England ambaye hii itakuwa ni mara yake ya pili kuzipambanisha timu hizo katika hatua kama hiyo.
Ndiye aliyezihukumu katika Fainali zilizopita nchini Afrika Kusini ambapo Brazil waling'ara kwa kushinda kwa mabao 3-0 kabla ya kwenda kung';oka mbele na kuziacha Hispania na Uholanzi zikicheza fainali.
Pambano jingine litakalochezwa leo litazikutanisha timu za Colombia na Uruguay pambano litakalochezwa usiku wa saa 5 kwenye uwanja wa mkubwa wa Maracana.
Uguruay itashuka dimbani bila huduma za Suarez aliyerudishwa nyumbani kutokana na kitendo cha kufungiwa na FIFA kwa kosa la kumng'ata mchezaji wa Italia Giorgio Chiellini wakati wa mechi ya kufungia pazia la hatua ya makundi na Uguguay kushinda kwa bao 1-0 na kutinga bila kutrarajiwa nyuma ya Costa Rica.
Pambano hilo linatarajiwa kuwa tamu pengine kuliko lile la Brazil na Chile kutokana na Colombia kuwa miongoni mwa timu zisizotabirika na kati ya chache zilizoshinda kwa asilimia 100 michezo yao ya makundi.
Ikiongozwa na James Rodriguez aliyeziba kwa mafanikio pengo la Radamel Falcao ambaye aliondolewa kwenye kikosi hicho kutokana na majeraha, Colombia inatarajiwa kutoa upinzani mkali.
James Rodriguez ana mabao matatu mpaka sasa kwenye michuano hiyo akishika nafasi ya pili pamoja na nyota wengine wa timu zilizoshiriki michuano hiyo na atakuwa akisaidiana kusaka ushindi kuvuka hatua hiyo na wachezaji wenzake kama Jackson Martínez,Armero, Cuadrado na Gutierrez.
Hata hivyo Uruguay pamoja na kumkosa Suarez, bado ina silaha kali kama Edinson Cavani, Diego Godin, Arevalo na wengine kuhakikisha wanafanya kweli katika mechi hiyo ambayo itakuwa ni ya 15 kwa timu hizo kukutana katika michezo mbalimbali tangu mwaka 2005.
Rekodi zinaonyesha katika kukutana huko, Uruguay imeitambia Colombia mara 8 na kupoteza mechi nne na mbili zilizosalia walitoshana nguvu kwa kutoka sare.
Je, ni Brazil au Chile itakayokuwa ya kwanza kufuzu robo fainali na Colombia itaendelea kuwa mnyonge kwa Uruguay na kupigwa kumbo kutinga hatua inayofuata au watajitutumua na kuinyuka Uruguay bila ya Suarez? Tusibiri tuone baada ya kumalizika kwa mechi hizo kabla ya kesho kushuhudia kitupe kingine.

No comments:

Post a Comment