STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 14, 2013

Yanga yaipigisha kwata KMKM uwanja wa Taifa
Kikosi cha Yanga kilichoisulubu KMKM jioni ya leo
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imeipigisha kwata maafande wa KMKM ya visiwani Zanzibar kwa kuicharaza mabao 3-2 katika pambano la kirafiki lililoichezwa jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo dhidi ya KMKM ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya Nani Mtani Jembe kati yao na Simba litakalochezwa kwenye uwanja huo wa Taifa Jumamosi ijayo.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts alimuanzisha langoni mlinda mlango Juma Kaseja katika mchezo huo ikiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu ajiunge na Yanga katika kipindi cha usajili dirisha dogo, huku msomi Reliants Lusajo akianza katika nafasi ya dimba kubwa.
Kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote kucheza taratibu huku zikisomana na Yanga ndo ilikuwa ya kwanza kufanya mashambulizi langoni mwa KMKM lakini kutokua makini kwa washambuliaji wake kulipelekea kupoteza nafasi hizo.
Dakika ya 43 mshambuliaji Jerson Tegete aliipatia Yanga bao la kwanza na kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa bao moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga wakisaka mabao ya haraka haraka, Nahodha Nadir Haroub "Cannavaro" aliipatia Yanga bao la pili kwa kichwa akiunganisha mpira uliorushwa na mlinzi wa kati Mbuyu Twite.
Mabadiliko yaliyofanywa na Brandts ya kuwatoa Nadir Haroub, Reliants Lusajo, Oscar Joshua, Jerson Tegete, Didier Kavumbagu, Nizar Khalfan yaliwapelekea KMKM kupata mabao mawili ya haraka haraka kufuatia uzembe wa walinzi na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Dakika ya 84 ya mchezo kiungo Hamis Thabit aliipatia Yanga bao la tatu na la ushindi kwa shuti kali nje ya eneo la hatari ambapo mlinda mlango wa KMKM aliruka bila mafanikio.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 3-2 KMKM.
Mara baada ya mechi ya leo kocha mkuu wa Yanga Ernie Brandts amesema vijana wake walipunguza umakini katika mchezo hasa kipindi cha pili hali iliyopelekea KMKM kupata mabao mawili lakini kikubwa nashukuru waliweza kupigana na kupata ushindi.
Mabingwa hao wa visiwani Zanzibar, KMKM kesho itashuka tena dimbani kupepetana na Simba katika mchezo mwingine wa kirafiki katika ziara yake ya jijini Dar es Salaam.

Andy Cole nyota wa zamani wa Man Utd atua Tanzania

Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Bw. Jackson Mbando (kulia) akimkaribisha Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United Andy Cole (kushoto) mara tu baada ya kuwasili nchini kwa mwaaliko wa kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania . Kati kati ni Afisa Uhusiano wa klabu ya Manchester James Turner.
Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United Andy Cole akikabidhiwa maua mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana usiku kwa mwaaliko wa kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania .
Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Bw. Jackson Mbando (kushoto) akimuongoza Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United Andy Cole (katikati) kuelekea sehemu ya VIP kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)mara tu baada ya kuwasili nchini jana usiku.
Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United Andy Cole (kushoto) pamoja na Afisa Uhusiano wa klabu ya Manchester James Turner (kulia) wakikamilisha taratibu zakupata hati ya kuingia nchini kwenye kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana usiku mara tu baada ya kuwasili kwa mwaaliko wa kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania .
Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Bw. Jackson Mbando (kulia) akimuelekeza jambo Afisa Uhusiano wa klabu ya Manchester James Turner (katika) mara tu baada ya kuwasili kwa mwaaliko wa kampuni ya Mawasiliano ya Airtel Tanzania . Kushoto ni Picha na Mpiga picha wetu. Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United Andy Cole.
Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Manchester United Andy Cole (mbele) akitoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwelekea hotelini alipofikia mara bada ya kuwasili nchini jana usiku. Nyuma yake ni mwenyeji waka ambaye ni Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Bw. Jackson Mbando . 
Picha kwa hisani ya AIRTEL TANZANIA

Chelsea yaipumulia Arsenal kileleni, Everton yaua

Fernando Torres and Willian
Torres akipongezwa baada ya kuifungia Chelsea
Leon Osman
Everton wakiwatungua Fulham

VIJANA Jose Morinho, Chelsea muda mfupi uliopita imepata ushindi muhimu wa mabao 2-1 ikiwa uwanja wa Stanford Bridge kwa kuicharaza Crystal Palace.
Bao la kwanza la Chelsea kutumbukiwa wavuni na Fernando Torres katika dakika ya 16 kabla ya Marouane Chamakh kuisawazishia wageni dakika ya 29.
Katika dakika ya 35 Ramires aliiongezea Chelsea bao la pili na kudumu hadi wakati wa mapumziko na hata kipindi cha pili kilipoanza matokeo yalibaki hivyo na wenyeji kuvuna pointi tatu na kukamata nafasi ya pili nyuma ya Arsenal waliopigwa mchana wa leo.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo Everton walikwea hadi nafasi ya nne baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-1 wakiwa nyumbani dhidi ya Fulham,  huku Newcastle United ilibanwa nyumbani na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na timu ya Southampton.
West Ham United nayo ikiwa nyumbani ililazimishwa suhulu ya bila kufungana dhidi ya Sunderland, ilihali Cardiff City ilipata ushindi wa kushtukiza wakiwa nyumbani kwa kuilaza West Brom kwa bao 1-0.
Hull City muda mchache uliopita imeanza pambano lake dhidi ya wageni wao Stoke City katika pambano jingine la kufungia dimba siku la leo kabla ya kesho kushuhudiwa kivumbi cha mechi nyingine tatu.

Arsenal nyang'anyang'a kwa Manchester City

Yaya Toure akiwajibika uwanjani kuisaidia City kuiua Arsenal mabao 6-3

Kun Aguero akishangilia bao lake lililofungua kapu la mabao kwa Arsenal leo
MASHABIKI wa klabu ya Arsenal, vinara wa Ligi Kuu ya England leo watalala wakiota njozi mbaya baada ya timu yao kupokea kipigo cha aibu cha mabao 6-3 toka kwa Mancherster City katika mfululizo wa Ligi hiyo.
Wakicheza ugenini huku wakiwa wanaugulia kipigo cha mabao 2-0 walichopewa na Napoli ya Italia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya,  vijana wa kocha Arsenal Wenger walishindwa kufurukuta kwa City waliokuwa uwanja wao wa Itihad.
Goli la mapema la Sergio 'kun' Aguero katika dakika ya 14 lilionyesha dalili mbaya kwa wageni japo winga aliyerejea tena dimbani, Tim Walcot alisawazisha bao hilo dakika ya 31 kwa pasi ya Mesut Ozil kabla ya Negredo kuongeza bao la pili dakika nane baadaye na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 2-1.
Fernandinho aliiongezea City bao la tatu dakika tano baada ya kipindi cha pili  kabla ya Walcot kurejea tena nyavuni kwa kuifunga Arsenal bao la pili dakika ya 63 akimalizia kazi ya Aaron Ramsey.
Hata hivyo jahazi la Gunners liliendelea kuzama ugenini kwa mara ya pili mfululizo baada ya David Silva kufunga bao la nne dakika tatu baadaye kwa pasi ya Juses Navas na Fernandinho kuongeza bao jingine dakika mbili kabla ya mchezo huo kuisha akimalizia pasi ya Samir Nasir.
Beki Pet M Mertesacker aliifungia Arsenal bao dakika ya nne ya nyongeza ya pambano hilo kabla ya Yaya Toure kupigilia msumari wa mwisho kwa kufunga bao kwa mkwaju wa penati dakika mbili baadaye katika muda huo wa nyongeza na kufanya mechi kuisha kwa mabao 6-3, Arsena ikiwa hoi.
Mechi nyingine zinaendelea hivi sasa katika ligi hiyo na MICHARAZO itaendelea kuwaleta.

Hatari! Ajali nyingine tena yaua wawili

http://2.bp.blogspot.com/-zi0IyhiWMxc/UPLg_aV_I9I/AAAAAAAAAnI/ErisIjIpVeQ/s1600/bunda+express+accident-kuninews+blog.jpg
Hii kati ya ajali ambazo zimekuwa zikitokea kila mara Tanzania
WATU wawili wamekufa na wengine 14 kujeruhiwa baada ya basi 
waliolokuwa wakisafiria la Simiyu Express kupinduka katika eneo la 
Ihumwa nje kidogo ya manispaa ya Dodoma.

Basi hilo lenye namba za usajili T 717 ANL aina ya scania basi lilikuwa
likiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina la Mramba Issa (31).

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kaimu Kamanda wa Polisi
mkoani hapa Susan Kaganda, alisema kuwa basi hilo lilikuwa linatokea
Bariadi kwenda Dar es salaam likiwa na abiria 60 liliacha njia na 
kupinduka kutokana na mwendo kasi .
Kamanda alisema kwamba ajali hiyo ilitokea leo alfajiri majira ya saa tisa
usiku katika barabara ya Dodoma-Dar es salaam  eneo la Elshadai .
Kamanda Kaganda aliwataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni 
pamoja na dereva wa basi hilo Mramba Issa mkazi wa Magomeni 
Dar es salaam na Frola Erenest(21) Mwali wa shule ya msingi Mwamoto 
kolokolo, Bariadi.
Aidha kamanda akizungumzia zaidi ajali hiyo alisema kwamba basi hilo
lilikuwa likiwakwepa askari wa barabarani kwa kupita njia za panya.
Alifafanua kuwa kwa basi hilo kusafiri usiku huo ni kukwepa askari .
Aliwataka pia wamiliki wa magari kuweka madereva wawili kwa 
magari ya masafa marefu na pia wazingatie sheria za barabarani. 
HABARI LEO 

Mabinti wengine wanaswa na 'unga' uwanja wa JKN

 http://api.ning.com/files/NWvFMlVPFcx5SxCYa4RDXr0NMMnq6gRcpSfjyInB*mxa*WWMz0x1MendQbi7EkT588mJKfgz3DjGsbaCvcR6Q0AgTJ03rTXA/Pipi.jpg Biashara ya dawa za kuelvya ni hatari, lakini hivi sasa imevamiwa hata na wanawake.

 POLISI imewakamata wasichana wawili wa Kitanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam, wakiwa na zaidi ya pipi 187 walizokuwa wamezimeza za madawa ya kulevya kwa ajili ya kusafirisha nchini China.
Aidha, polisi imemtia mbaroni, raia wa China Guoyn Shen (44), kwa kukutwa na madini aina ya quates kilo 19 aliyokuwa akiyasafirisha kwa njia ya ndege kuelekea China.
Wasichana waliokamatwa Jumatano ya wiki hii saa 11:00 jioni. uwanjani hapo walikuwa kwenye harakati za kupanda ndege ya kampuni ya ndege ya Qatar kuelekea China kupitia Hong Kong.
Kwa mujibu wa Mkuu wa kitengo cha kupambana na dawa za kulevya, nchini Kamanda Godfrey Nzoa, wasichana hao ni Mariam Makuhani (29) mkazi wa Tabata Kimanga  na Khadija Shomari (30), mkazi wa Magomeni Mapipa ambao hadi jana asubuhi walikuwa wanaendelea kuzitoa pipi hizo kwa njia ya haja kubwa.
Alisema Mariam kwa wakati huo (saa 5:00) alikuwa ametoa pipi 65  wakati Khadija alifanikiwa kutoa pipi 122 ambazo zitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kubaini ni za aina gani na thamani yake.
Alisema wasichana hao bado wapo chini ya uangalizi ambapo baada ya kumaliza zoezi hilo wataandaliwa mashitaka yao na kufikishwa mahakamani kujibu makosa yanayowakabili.
Kaimu wa Viwanja vya Ndege nchini, Mratibu wa polisi, Renatus Chalya, alisema awali baada ya wasichana hao kukamatwa, Mariam alikiri kumeza pipi 72 huku Khadija akidai alimsindikiza Mariam.
Akizungumzia changamoto za kupambana na madawa ya kulevya, Kamanda Nzoa alisema wasafirishaji wamekuwa wakiibuka na mbinu tofauti na wengine wakisafirisha viatilifu vya kutengenezea dawa hizo badala ya dawa zenyewe.
Alisema mbinu hizo zimekuwa zikifanywa kwa msimu na kutaja njia ambazo hutumiwa kuwa ni majini, viwanja vya ndege na nchi kavu.
Kufuatia changamoto hiyo, Tanzania na nchi nyingine duniani zilishiriki mikutano mbalimbali ambapo wa mwisho ulifanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini Afrika Kusini.
Alisema katika mkutano huo washiriki pamoja na mambo mengine walipata fursa ya kueleza changamoto wanazokabiliana nazo kwenye mapambano dhidi ya dawa hizo ambapo lililojitokeza ni usafirishaji wa viatilifu.
"Tuliliongelea kwa upana wake suala hili na kuafikiana kuwepo kwa sheria kali kwa kuwa tunayoitumia kwa mfano Tanzania haiwabani sana," alisema na kuongeza:
Alisema nchi zilizoshiriki mkutano huo zilibaini hiyo ni moja ya changamoto hivyo wakakubaliana kutungwe sheria itakayokuwa na makali zaidi.
Kamanda Nzoa aliwataja Watanzania wawili waliokamatwa kwa nyakati tofauti na viatilifu Agnes Masogange, Afrika Kusini na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Sada  aliyekamatwa Tanzania ambao kutokana na sheria hiyo walilipa faini ndogo na kuachiwa huru.
Alisema sheria iliyopo inatoa nguvu kwa mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambapo mtu akikamatwa na viatilifu hivyo bila kibali atachukuliwa hatua za kisheria.
Kamanda Nzoa alisema kuanzia mwezi Machi hadi Julai mwaka huu, wamefanikiwa kukamata kilo 1482 ambazo tayari zilishaharibiwa.
Alisema dawa hizo zilikamatwa kwa nyakati tofauti kwenye meli ambapo moja ilikutwa na kilo 500, nyingine kilo 300.
"Ipo iliyokutwa na kilo 200 meli nyingine ilikutwa na kilo 182 ambapo hata hivyo kutokana na eneo walilokutwa walishindwa kuwafikisha mahakamani badala yake waliharibu mzigo huo," alisema.
Kwa upande wa njia ya anga, alisema kwa mwaka huu wamefanikiwa kukamata kilo 50 bila kuzijumlisha zinazoendelea kutolewa na wasichana hao wawili waliokamatwa Jumatano.
"Ipo kesi ambayo ukija hapa ofisi kwangu nitakuonyesha mlolongo mzima, huwezi amini tulikamata watu tena wakazitoa dawa hizo kwa njia ya haja kubwa lakini mahakama iliwaachilia, kama nilivyosema tunapoenda mahakamani tunatakiwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka," alisema.
Kamanda Nzoa alisema kutokana na changamoto hizo, tayari wameshawapeleka vijana wao nchi mbalimbali na kutaja baadhi kuwa ni Afrika Kusini, Ghana, India, Iran, Ivory Cost  kwa ajili ya mafunzo maalum.
Kuhusu Mchina aliyekamatwana madini alisema kuwa Shen alikamatwa Jumatano wiki hii uwanjani hapo akiwa kwenye harakati za kusafirisha mzigo huo kuelekea nchini humo.
Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akisafiri na ndege ya kampuni ya ndege ya Ethiopia iliyokuwa iondoke jioni ya siku hiyo.
Alisema mtuhumiwa huyo alipokamatwa alipotakiwa kutoa kibali cha kusafirisha mzigo huo hakuwa nacho na alipoulizwa ameyapata wapi alidai ameyanunua kwa wananchi.
Alitaja namba za hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo kuwa ni 00609687.
Alisema upelelezi wa tukio hilo unaendelea ikiwa ni pamoja na kubaini thamani ya madini hayo.

Bango kutoka TFF

FA MIKOA YAPATA MIPIRA TFF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa mipira kumi kwa kila chama cha mpira wa miguu cha mkoa ili isaidie kuendesha ligi za mikoa husika.

Mipira hiyo 250 yenye thamani ya sh. 16,250,000 tayari imeanza kutumwa kwa makatibu wa vyama vya mikoa husika. Mpira mmoja una thamani y ash. 65,000.

Ni maratajio ya TFF kuwa mipira hiyo itakuwa chachu kwa vyama vya mikoa katika uendeshaji wa ligi hizo.

MITIHANI YA WAAMUZI KUFANYIKA JUMAPILI
Robo ya mwisho ya mitihani ya waamuzi (Cooper Test) na utimamu wa mwili (physical fitness test) kwa mwaka 2013 kwa waamuzi inafanyika Jumapili (Desemba 15 mwaka huu).

Mitihani hiyo inayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam inashirikisha waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (TFF) na wale wa kundi la waamuzi (elite) ambao wanaweza kupendekezwa kupewa beji za FIFA.

Wakufunzi wa mitihani hiyo ya waamuzi ni Leslie Liunda, Soud Abdi na Riziki Majala.

Waamuzi wa FIFA watakaofanya mitihani hiyo ni Ferdinand Chacha, Hamis Chang’walu, Israel Mujuni, Jesse Erasmus, John Kanyenye, Josephat Bulali, Mgaza Kinduli, Oden Mbaga, Ramadhan Ibada, Samwel Mpenzu na Waziri Sheha.

Washiriki kutoka kundi la elite ni Charles Simon, Dalali Jaffari, Hellen Mduma, Issa Bulali, Issa Vuai, Janeth Balama, Jonesia Rukyaa, Judith Gamba, Lulu Mushi, Martin Saanya, Mfaume Nassoro na Mohamed Mkono.

KILIMANJARO STARS YAREJEA DAR
Timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) iliyoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika jana jijini Nairobi, Kenya inarejea jijini Dar es Salaam leo.

Kilimanjaro Stars iliyomaliza michuano hiyo katika nafasi ya nne inatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 12 kamili jilioni kwa ndege ya RwandAir.

Wenyeji Kenya (Harambee Stars) ndiyo walioibuka mabingwa wa michuano hiyo baada ya kuifunga Sudan mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa jana Uwanja wa Nyayo.

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)