STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 14, 2013

Yanga yaipigisha kwata KMKM uwanja wa Taifa












Kikosi cha Yanga kilichoisulubu KMKM jioni ya leo
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imeipigisha kwata maafande wa KMKM ya visiwani Zanzibar kwa kuicharaza mabao 3-2 katika pambano la kirafiki lililoichezwa jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Pambano hilo dhidi ya KMKM ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya Nani Mtani Jembe kati yao na Simba litakalochezwa kwenye uwanja huo wa Taifa Jumamosi ijayo.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts alimuanzisha langoni mlinda mlango Juma Kaseja katika mchezo huo ikiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu ajiunge na Yanga katika kipindi cha usajili dirisha dogo, huku msomi Reliants Lusajo akianza katika nafasi ya dimba kubwa.
Kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote kucheza taratibu huku zikisomana na Yanga ndo ilikuwa ya kwanza kufanya mashambulizi langoni mwa KMKM lakini kutokua makini kwa washambuliaji wake kulipelekea kupoteza nafasi hizo.
Dakika ya 43 mshambuliaji Jerson Tegete aliipatia Yanga bao la kwanza na kuifanya timu yake kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa bao moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga wakisaka mabao ya haraka haraka, Nahodha Nadir Haroub "Cannavaro" aliipatia Yanga bao la pili kwa kichwa akiunganisha mpira uliorushwa na mlinzi wa kati Mbuyu Twite.
Mabadiliko yaliyofanywa na Brandts ya kuwatoa Nadir Haroub, Reliants Lusajo, Oscar Joshua, Jerson Tegete, Didier Kavumbagu, Nizar Khalfan yaliwapelekea KMKM kupata mabao mawili ya haraka haraka kufuatia uzembe wa walinzi na kufanya matokeo kuwa 2-2.
Dakika ya 84 ya mchezo kiungo Hamis Thabit aliipatia Yanga bao la tatu na la ushindi kwa shuti kali nje ya eneo la hatari ambapo mlinda mlango wa KMKM aliruka bila mafanikio.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 3-2 KMKM.
Mara baada ya mechi ya leo kocha mkuu wa Yanga Ernie Brandts amesema vijana wake walipunguza umakini katika mchezo hasa kipindi cha pili hali iliyopelekea KMKM kupata mabao mawili lakini kikubwa nashukuru waliweza kupigana na kupata ushindi.
Mabingwa hao wa visiwani Zanzibar, KMKM kesho itashuka tena dimbani kupepetana na Simba katika mchezo mwingine wa kirafiki katika ziara yake ya jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment