http://2.bp.blogspot.com/-GzA5wdVSnVg/UbiCcnJ1ARI/AAAAAAAAKkc/yJLidr__aXY/s1600/baraza+la+uuguzi1.JPG
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Lena Mfalila akizungumza leo jijini Dar (picha:Audiface Jackson Blog)
BARAZA la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) , limetangaza kuvisaka na kuvifungia vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya ngazi ya cheti na stashahada yasiyokidhi viwango vilivyowekwa na baraza hilo.
 
Aidha imeelezwa kuwa vyuo zaidi ya 200 nchini kote havina sifa ya kutoa mafunzo ya taaluma hiyo kwa kutokusajiliwa na TNMC.
 


Msajili wa vyuo vya uuguzi na ukunga nchini Lena Mfalila alisema hadi sasa Baraza linatambua uwepo wa vyuo 34 vinavyotoa mafunzo ya uuguzi nchini.
    
Mfalila alisema ili mafunzo ya chuo yaweze kutambulika ni lazima kiwe kimesajiliwa, kiwe na walimu wenye sifa pamoja kutumia mitaala inayotambuliwa na Baraza.
 
Aliwataka wazazi na wanafunzi wote wanaohitaji kupata elimu katika vyuo mbalimbali hapa nchini kuvichunguza kwanza kabla ya kujiunga navyo kwani wasipofanya hivyo watakuwa wanapoteza muda wao.
 
“Lazima wanaotaka kujiunga na chuo wanachotaka kusoma wahakikishe kama kimesajiliwa na baraza chini ya sheria ya ‘Nursing and Midwifery’ ya mwaka 2010 na kuangalia mitaala yao ya  kufundishia,” alisema Mfalila.
 
Kwa upande wa vyuo vinavyofundisha uuguzi, alisema Baraza limekumbana na changamoto nyingi ikiwa ya kuibuka kwa vyuo ambavyo havitambuliki kisheria lakini vinaendesha mafunzo kinyemela.
 
Aidha alisema kutoka na  malalamiko ya jamii kuhudumiwa huduma duni ya uuguzi na ukunga zinazotolewa na watumishi wa afya ambao wameajiriwa kutoka vyuo  visivyotambulika,baraza limetoa agizo kwa watumishi wa afya kutoa taarifa.