STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, June 12, 2013

Jaji Mark Bomani aipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba


Jaji Mark Boman akizungumza mchana wa leo jijini Dar es Salaam
Na Suleima Msuya.
WAKATI Taifa  likiwa katika mjadala juu ya rasimu ya katiba ijayo Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali, Jaji Mark Boman ameipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba kwa kuja na rasimu nzuri na kuitaka kutoharakisha uwepo wa katiba husika ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi.
Jaji Boman amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari maelezo Jijini hapa.
Alisema mchakato mzima wa kuandaa rasimu unahitaji umakini, uadilifu na kuhakikisha kuwa hakuna misukumo yoyote ya kufanikisha suala hilo hivyo ni vyema wakahakikisha kuwa mambo ya msingi yanayohusu jamii yanahusika.
Mwanasheria Mkuu huyo Mstaafu alisema jambo ambalo linaonekana kugusa jamii kwa asilimia kubwa ni kuhusu muungano, hivyo ni vyema tume ikafanya tathmini sahihi juu ya utekelezaji wake ili kuhakikisha kuwa inakidhi kiu ya Watanzania.
Alisema kutokana na rasimu hiyo ilivyochambuliwa na tume imejikita hasa kuhusu jinsi ya kuwa na muungano wa nchi lakini ikajisahau kuwa ilikuwa ni fursa muhimu kwa wananchi kuhusika moja kwa moja juu ya aina ya muungano wanaotaka na isiwe na maoni ya wajumbe wa tume.
"Mimi kama Mtanzania na pia mwanasheria mkongwe ambaye najua masuala ya nchi hii kwa upana naamini tume imejitahidi kwa kiwango chake ila naona haipo sababu ya kukimbilia kuwepo kwa katiba bila kuhakikisha kuwa mahitaji ya msingi hajatekelezwa hasa ambayo yanagusa jamii," alisema.
Jaji Boman alisema suala la muungano linahitaji mchango wa wadau hasa wananchi kwani ni jambo ambalo linaweza kuweka muafaka wa hatma ya nchi kwa miaka ijayo.
Alisema ni vema Tume ikatambua kuwa suala la muungano halihitaji maoni ya watu wachache kwani ni wazi kuwa suala hilo limekuwa likiibua migogoro mingi kwa muda mrefu hasa katika upande wa Zanzibar.
Alisisitiza kuwa katika harakati za kutafua ufumbuzi juu ya sauala hilo la muungano ni vema tume ikachukua maoni ya waliowengi ili kuhakikisha kuwa haja yao inatimia hata kama wachache wenye uelewa watakuwa wanapinga.
Boman alisema dhana kuhusu serikali tatu kuwa zitaongeza gharama za undeshaji wa Serikali ni mtazamo finyu kwani kuna mifano ya nchi nyingi ambazo zimeungana na kuendeshwa kwa mfumo huo na hakuna athari ya moja kwa moja ambayo imeonekana.
Alisema ni vyema tume ikajikita kwa wananchi na kuachana na mitazamo ya baadhi ya viongozi wa kisiasa ambao wengine wanaonekana kuwa yapo mambo ambayo wanataka yawepo kwa maslahi yao na sio ya Taifa
Kwa upande mwingine Jaji Boman ameiomba tume kuhakikisha kuwa rasimu hiyo ya katiba ya nchi inakuwa na muongozo juu ya dira ya nchi, maslahi ya kijamii kwa jamii na mahitaji muhimu yatajwe ili iwe ni muongozo sahihi kwa kiongozi yoyote ambaye atapata kuongoza nchi.
Pia alisema ni vyema rasimu hiyo ya katiba ianishe uwepo na uatambuzi wa rasilimali za nchi ambazo kwa kiasi fulani zimeonekana kutumiwa kinyume na taratibu hivyo kutowafaidisha wananchi kwa ujumla.
Alitolea mfano suala la mikataba mibovu ambayo imekuwa ikiingiwa na Serikali iwapo kutakuwepo na muungozo wa kikatiba juu ya suala la mikataba inaweza kuwa njia sahihi ya kuwabana wahusika.
Alisema iwapo mambo hayo ya msingi yakikosekana ni dhahiri kuwa kila kiongozi anaweza kufanya anachotaka kutokana na mahitaji yake jambo ambalo ni kinyume na utawala unavyotaka hasa katika ngazi ya nchi.

No comments:

Post a Comment