STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, October 14, 2013

Mashauzi kutambulisha mpya Da West Tabata

 
Isha Mashauzi
KUNDI la muziki wa taarab ya Mashauzi Classic inatarajiwa kutambulisha nyimbo zao mpya kwenye onyesho maalum ya kusherehekea sikukuu ya Idd el Hajj katika ukumbi wa Dar West Park, Tabata.
Onyesho hilo ambalo linajulikana kama ‘Usiku wa Isha Mashauzi’, imeandaliwa na Keen Arts na  Bob Entertainment chini ya udhamini wa kinywaji cha Konyagi, Straika, Kwetu Mbambabay  na Saluti5.
Mratibu wa onyesho hilo, Joseph Kapinga amesema kuwa onyesho litakuwa la kipekee na maalum kwa kusherehekea sikukuu ya Idd El Hajj.
Amesema katika onyesho hilo, Mashauzi atatambulisha albamu yake mpya ijulikanayo kama “Asiyekujua Hakuthamini” ambayo ina nyimbo kama “Mimi Bonge la Bwana,” utunzi wake Hashim Said, “Ropokeni Yanayoyahusu” ( Saida Ramadhani) na “Haya ni Mapenzi Tu” (Zubeda Malik).
Zawadi mbalimabli zitatolewa kwa mashabiki wa bendi hiyo inayojulikana kama Wakali wa Kujiachia.
“Tumeandaa zawadi mbalimbali kwa mashabiki wetu. Pia bendi ya Mashauzi Classic watatumia onyesho hilo kutambulisha nyimbo zao mpya,” Kapinga alisema.
“Mashauzi Classic watapiga albamu zao zote. Matumaini yetu ni kuwa watu watapata burudani ya kutosha kuliko siku zingine zote,” alisema Kapinga.
Nyimbo zingine zitakazopigwa ni  “Viwavijeshi” (Issa Ramadhani), “Sitasahau Yaliyonikuta” (Abdul Malik), “La Mungu Halima Mwamuzi” (Zubeda Malik) na “Sijamuona Kati Yenu” (Rukia Juma).
Naye mkurugenzi wa bendi hiyo, Isha Mashauzi, alisema kuwa onyesho la Da West litakuwa la kihistoria na kutaka watu wajitokeze kwa wingi ili historia isiwapite.
“Kwa kweli bendi iko fiti,” alisema Mashauzi.

Linnah Kessy kusimamia Kombe la Dunia

Linna Kessy
 SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Mtanzania Lina Kessy kuwa kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya umri wa miaka 20 kati ya Botswana na Afrika Kusini.

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itachezwa nchini Botswana kati ya Oktoba 25 na 27 mwaka huu. Waamuzi kutoka Zimbabwe ndiyo watakaochezesha mechi hiyo namba tisa.

Waamuzi hao wataongozwa na Pamela Majo atakayepuliza filimbi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Rudo Nhananga, namba mbili ni Stellah Ruvinga na mezani atakuwepo Tambudzi Tavengwa.

Kituo cha IDYDCC chafunguliwa Iringa



Na Boniface Wambura
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Ali Amir amefungua kituo cha kwanza cha Football for Hope kilicho mkoani Iringa kwa kuwataka wananchi kukituia vizuri ili wanufaike na huruma za kijamii zinazotolewa na taasisi ya IDYDC pamoja na kuendeleza mpira wa miguu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo hicho jana (Oktoba 13 mwaka huu), kiongozi huyo amesema taasisi ya IDYDC (Iringa Development of Youth, Disabled and Child Care) wamefanya vizuri kuamua kutumia mpira wa miguu kusaidia jamii kwa kuelimisha juu ya mambo mbalimbali kama ugonjwa wa ukimwi, kusaidia walemavu, haki za watoto na afya ya jamii.
Naye Mwakilishi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Patrick Onyango amesema amefurahishwa na kukamilika kwa kituo ambacho kitasaidia jamii.
Amesema idadi kubwa ya watu waliofika kwenye uzinduzi huo inadhihirisha ni kiasi gani kituo hicho kitakuwa na matokeo mazuri kwa jamii.
Onyango alisema hicho ni kituo cha 14 kukamilika kati ya 20 vinavyojengwa barani Afrika ikiwa ni mpango wa FIFA kurudisha kwa jamii mafanikio iliyopata kwenye fainali za kwanza za Kombe la Dunia barani Afrika.

Kituo hicho kina uwanja mdogo wa mita 20 kwa 40 uliowekwa nyasi bandia, jengo lenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya semina, chumba cha kupimia ukimwi, chumba cha ushauri nasaha, maktaba na ofisi.
Zaidi ya dola 270,000 za Marekani zimetumika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kilicho eneo la Mtwivila, Iringa mjini.

Kamati ya Rufaa ya Maadili yafanya mapitio

Na Boniface Wambura
KAMATI ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana jana (Oktoba 13 mwaka huu) kusikiliza maombi ya mapitio (revision) na mwongozo ya uamuzi wa Kamati ya Maadili.

Sekretarieti ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati hiyo ya juu kabisa ya masuala ya maadili kutokana na ugumu wa utekelezaji wa uamuzi wa Kamati ya Maadili juu ya mashauri nane yaliyowasilishwa mbele yake.

Kamati ya Rufani ya Maadili itaendelea na kikao chake kesho (Oktoba 15 mwaka huu), na baadaye itakutana na waandishi wa habari (saa 10 jioni) kwa ajili ya kutangaza uamuzi wake juu ya mwongozo ulioombwa na Sekretarieti ya TFF.