STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, June 24, 2014

Hatma ya Ivory Coast, Italia, Uruguay leo Brazili

Suarez ataendelea kuwatungua makipa leo Brazili?
Tembo wa Afrika watashangilia tena kama hivi kwa Ugiriki leo nchini Brazili?
HATMA ya Ivory Coast na Italia kuendelea kubaki kwenye Fainali za Kombe la Dunia inatarajiwa kufahamika leo wakati mechi za Kundi C na D zitakapochezwa usiku wa leo kukamilisha ratiba yao zitakapochezwa kwenye viwanja vinne tofauti.
Ivory Coast itavaana na Ugiriki ikihitaji ushindi ili kuungana na Colombia kucheza hatua ya 16 Bora, huku Italia itavaana na Uruguay inayochuana kuwania nafasi ya kuungana na Costa Rica kucheza hatua ya pili.
Italia ilitulizwa na Costa Rica katika mechi yao iliyopita na kuwafanya kuomba dua ishinde leo ili kufuzu hatua ya pili vinginevyo itaunga na England kutoka kwenye michuano hiyo.
England iliyopoteza mechi zake mbili zaawali itakamilisha ratiba kwa kuvaana na Costa Rica katika mechi nyingine ya kundi D ambapo matokoe yoyote hayawezi kubadilisha chochote kwa timu hizo mbili.
Katika mechi nyingine zinazochezwa usiku wa leo, Ivopry Coast wenye pointi tatu nyuma ya Colombia itakuwa na kibarua kigumu kuvaana na Ugiriki, wakati vinara wa kundi C, Colombia watavimbiana vifua na Japan.
Mpaka sasa katika kundi hilo ni Colombi tu iliyojihakikishia nafasi huku Japan, Ugiriki na Ivory Coast zote zikiwa na nafasi sawa kama watafanya vema katika mechi hizo za kufungia ratiba.
Japan ikipata ushindi kwa Colombia na Ugiriki ikailaza Ivory Coast moja ya timu hizo itafuzu kwa uwiano wa mabao au walivyoumana wenyewe kwa kwenyewe kuungana na Colombia.
Hata hivyo Ivory Coast wanaoshika nafasi ya pili wanapewa nafasi kubwa kufuzu hatua ya pili iwapo italazimisha sare dhidi ya Ugiriki, vinginevyo isubiri miujiza kama inayosubiri Italia kwa Uruguay.

Ratiba ya mechi za LEO:
Costa Rica  vs  England (Saa 1 Usiku)
Italia vs     Uruguay (Saa 1 Usiku)
Japan vs    Colombia (Saa 5 Usiku)
Ugiriki  vs Ivory Coast (Saa 5 Usiku)

Stars kuzivaa Botswana, Lesotho kirafiki ughaibuni

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya wenyeji Botswana na Lesotho kwa ajili ya kujiandaa kuivaa Msumbiji (Mambas) imeelezwa jana jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa, alisema kuwa tayari vyama vya soka vya nchi hizo mbili vimethibitisha kuwepo kwa michezo hiyo itakayofanyika jijini Gaborone.

Mwesigwa alisema kuwa Taifa Stars itaanza kuwakabili wenyeji Julai Mosi mwaka huu na baadaye Julai 5 itashuka kucheza mechi ya pili kwa kuivaa timu ya Taifa ya Lesotho.
Katibu huyo wa zamani wa Yanga alisema kuwa maandalizi ya safari yamekamilika na kikosi cha Stars kinatarajia kuondoka nchini leo saa 12:00 asubuhi kuelekea Gaborone.
Alisema kwamba nyota wote 26 waliotajwa wataondoka na wanaamini kambi hiyo itasaidia kukiimarisha kikosi hicho kinachohitaji ushindi ili kiweze kuingia hatua ya makundi.

Aliwataja wachezaji watakaosafiri leo wakiwa chini ya Mholanzi, Mart Nooij, ni pamoja na Deogratias Munishi 'Dida', Aishi Manula, Benedictor Tinoko, Kelvin Yondani, Said Moradi, Nadir Haroub 'Cannavaro', Joram Nason, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Edward Charles, Aggrey Morris na Pato Ngonyani.

Wachezaji wengine ni Frank Domayo, Amri Kiemba, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Said Juma, Haroun Chanongo, Himid Mao, John Bocco, Simon Msuva, Kelvin Friday, Ramadhan Singano 'Messi', Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Mwegane Yeya.

Mechi ya kwanza kati ya Taifa Stars dhidi ya Mambas itakuwa kati ya Julai 19 na 20 na marudiano yatafanyika mjini Maputo baada ya wiki mbili.

Stars ilifanikiwa kusonga mbele katika mashindano hayo ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za mwakani za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuifunga Zimbabwe jumla ya magoli 3-2.

Chuji, Luhende watupiwa virago Yanga, Barthez, Tegete wabakishwa

Chuji ametemwa
Barthez kabakishwa Jangwani

Tegete (kulia) aliyebakishwa akiwa na baba yake John Tegete
KLABU ya soka ya Yanga imetangaza kuwatema kundini nyota wake kama Athuman Idd 'Chuji', beki David Luhembe na Ibrahim Job, huku ikiwasainisha mikataba mipya wakali kama Ally Mustafa 'Barthez', Jerry Tegete na Oscar Joshua.
Kupitia tovuti ya klabu hiyo, ambayo msimu uliopita ilikua na kikosi bora kabisa ambacho kiliweza kuwatoa jasho Mabingwa wa Kihistoria Barani Afrika timu ya Natioal Al Ahly katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, ambapo Mabingwa hao wa kutoka nchini Misri waliweza kusonga mbele kwa mikwaju ya penati imewatema jumla ya wachezaji 11.
Msimu uliopita Young Africans ilikuwa na kikosi cha wachezaji 30 kutoka timu ya Wakubwa na wachezaji watano (5) kutoka timu ya vijana (U20) waliokuwa wamepandishwa kwa ajili kupata uzoefu na kuingozea nguvu timu ya wakubwa katika michezo mbalimbali.
Kutokana na ripoti ya Benchi la Ufundi iliyowasilishwa mara baada ya kumalizika kwa Msimu wa Ligi Kuu 2013/2014 baadhi ya wachezaji hawataitumikia tena Yanga SC kwenye msimu ujao, wachezaji 11 wamemaliza muda wao na kumalizana na uongozi hivyo wapo huru kujiunga vilabu mbalimbali:
Wachezaji hao waliotemwa ni:
1. David Luhende
2. Athuman Idd “Chuji”
3. Geroge Banda -U20
4. Yusuph Abdul -U20
5. Rehani Kibingu -U20
6. Hamisi Thabiti
7. Reliants Lusajo
8. Bakari Masoud – U20
9. Shaban Kondo
10. Abdalllah Mguhi “Messi” U-20
11. Ibrahim Job

Neymar aiua Cameroon, Spain yaondoa gundu, Mexico we acha

WAWAKILISHI wa Afrika Cameroon 'Wazee wa Posho' wameaga kwa aibu michuano ya Kombe la Dunia baada ya usiku wa kuamkia leo kukandikwa mabao 4-1 na wenyeji Brazil na kumaliza mechi zake bila kuambulia pointi hata moja, tofauti na waliokuwa watetezi Hispania walioondoa gundu kwa kuilaza Australia kwa mabao 3-0 katika mechi za kukamilisha michezo ya makundi.
Nyota wa Brazil anayekipiga Barcelona, Neymar ndiye aliyekuwa mwiba wa Cameroon baada ya kufunga mabao mawili na kukwea hadi kileleni kwenye orodha ya wafungaji wa fainali hizo za 20 za Kombe la Dunia akifikisha jumla ya mabao manne.
Neymar alifunga mabao yake katika dakika za 17 na 34, wakati mabao mengine yalifungwa na Fred dakika ya 49 na Fernandinho dakika ya 84, huku bao pekee la Cameroon likitumbukizwa kimiani na Matip dakika ya 26
Katika mechi nyingine ya kundi hilo la A, Mexico nayo ilimaliza na ushindi wa 3-1 dhidi ya Croatia, mabao yake yakifungwa na Rafael Marquez, Andres Guardado na Javier Hernandez. Bao la kufutia machozi la Croatia iliyompoteza mchezaji wake Ante Rebic aliyetolewa kwa kadi nyekundu mwishoni mwa mchezo, lilifungwa na Ivan Perisic.
Brazil inamaliza na pointi saba sawa na Mexico, lakini inakaa kileleni kwa wastani mzuri zaidi wa mabao na sasa wenyeji hao watavaana na Chile katika mechi ya 16 Bora huku Mexico wakivaana na Uhalanzi waliopata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Chile usiku wa jana.
Watetezi Hispania waliotemeshwa tajhi mapema waliaga michuano hiyo kwa heshima kwa kuicharaza Australia mabao 3-0, magoli yaliyowekwa kimiani na David Villa katika dakika ya 36, Fernando Torres dak.69 na Juan Mata dk. 82.
Katika mechi ya Uholanzi na Chile, mabaio ya washindi yaliwekwa kimiani na Fer katika dakika ya 77 na Depay na kumaliza kwenye kundi B ikiwa kinara kwa kushinda mechi zote na kufikisha pointi 9.

Onesmo Waziri Ticotico kuzikwa kesho Mafinga, wadau wamlilia

Herry Morris akimfariji dada wa marehemu Ticotico (Picha Zote kwahisani ya Geofrey Chambua)

Hili ndilo gari lililochukua uhai wa Ticotico, baadahi ya watu wakilishangaa
Inauma sana!
 


Ticotico (jezi no 11 akiwa na wachezaji wenzake wa Golden Bush katika pambano lililochezwa mjini Morogoro
MWILI wa marehemu Onesmo Waziri 'Ticotico' mmoja wa wadau wakubwa wa soka nchini unatarajiwa kuzikwa kijijini kwao Rugemba mjini Mafinga siku ya kesho.
Ticotico alikumbwa na mauti baada ya kupatwa na ajali usiku wa kuamkia Jumapili walipoenda mjini humo na klabu yake ya Golden Bush Veterani kwa ajili ya mechi za kirafiki za bonanza zilizokuwa zichezwe asubuhi ya Jumapili ambayo ingehusisha timu za Mafinga, Njombe na Makambako pamoja na Golden Bush ya jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa toka mjini humo zinasema kuwa mwili wa marehemu ambao uliharibika vibaya kutokana na ukubwa wa ajali hiyo utahifadhiwa kesho Jumatano baada ya taratibu zote za Ibada.
Inaelezwa kuwa marehemu alikumbwa na ajali hiyo karibu na kijiji chao baada ya kulivamia lori lililokuwa limeegeshwa pembeni na kuumia vibaya maeneo ya kichwani na kifuani, ikiwa ni muda mchache baada ya kuagana na wachezaji wenzake kwa ajili ya kujiandaa na bonanza hilo la siku ya Jumapili.
Kwa mujibu wa mmoja wa viongozi waandamizi wa Golden Bush, Geofrey Chambua ni kwamba Majira ya usiku akiwaaga wachezaji ambao aliambatana nao kwenye gari yake; Salum Sued 'Kussi', Mwarami Mohamed 'Shilton' Herry Morris na Sadiq Muhimbo kwamba anakwenda kulala.
"liwachukulia kabisa vyumba Mafinga ili waje naye asubuhi hapa Makambako kwa ajili ya Bonanza ambalo ilikua likutanishe timu toka Mafinga, Njombe na Makambako. Baadaye wakiwa wana mtrace (mpigia) kwenye simu akawa hapatikani hadi asubuhi zilipokuja taarifa kwamba amepata ajali na kufariki instantly. Mashushuda walioona gari wanasema inaonekana ilipasuka tairi na kubiringita na hapo ilipo ipo upside down ikiwa imebondeka sana," Chambua alidokeza kwenye ujumbe wa barua pepe.
Alidokeza kuwa 'Mchana wa Jumamosi baada ya kufika salama Mafinga, aliitambulisha Golden Bush Kijijini kwao Rungemba na kuwatambulisha nduguze kisha kusihi wapige picha ya ukumbusho.......Pia alikuwa na alikuwa mwenye furaha sana na alishikana mikono na karibu kila mchezaji  kana kwamba anawaaga (Goodbye!)
Kocha wa timu ya vijana ya Golden Bush, Shija Katina aliyekuwa Arusha wakati Ticotico anakumbwa na mauti, alisema mpaka sasa aamini kama kweli Mr Football ametangulia mbele ya haki.
"Inauma na kuhuzunisha mno, nilipata taarifa nikiwa safarini Arusha na ninageuza kuwahi kumzika rafiki yangu, siamini kama kweli Ticotico hatunaye tena, " alisema Shija kwa masikitiko na kusimulia alivyolia njia nzima baada ya kupewa taarifa hiyo.
Wadau wengine wa soka wamekielezea kifo cha Ticotico kama pigo kubwa kwa familia ya marehemu, jamaa ndugu na wadau wa soka kutokana na ukweli Ticotico alikuwa mtu wa watu na aliyependa mpira pengine kuliko hata kula....
Mungu Aiweke Mahali Pema Roho ya Marehemu Onesmo Waziri 'Ticotico'