STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, March 18, 2013

Chove: Kipa ajiandaaye kutua As Vita baada ya kutemwa Coastal


Kipa Jackson Abraham Chove akiwa katika pozi

 IMEKUWA ni desturi kwa wachezaji wengi nchini wanapobahatika kupata nafasi ya kuzichezea timu kubwa za hapa Tanzania au kucheza soka la kulipwa nje ya nchi huridhika na kujiona wamefikia kilele cha mafanikio na kubweteka.
Kwa golikipa Jackson Abraham Chove aliyewahi kucheza soka la kulipwa katika klabu kadhaa za Afrika Mashariki na Kati na kuzidakia Yanga, JKT Ruvu, Prisons-Mbeya, Azam na Moro United, hali ni tofauti.
Kipa huyo aliyeidakia Coastal Union ya Tanga katika mechi za duru la kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kabla ya kutemwa, anasema bado hajaridhika licha ya kucheza soka la kulipwa mara kadhaa na kurejea nyumbani.

Oyaaa mambo gani sasa! Chove akimuonya Felix Sunzu wa Simba wakati wa mechi ya Coastal Union na Simba duru la kwanza iliyoisha kwa suluhu ya kutofungana.

Kwa sasa, nyota huyo anayefahamika kama 'Mandanda' akifananishwa na kipa wa Ufaransa mwenye asili ya Kongo, Steve Mandanda, anajiandaa kwenda nchini DR Congo kucheza soka la kulipwa katika klabu ya As Vita.
"Kila kitu kimekamilika kwa ajili ya safari hiyo ya Kinshasa ambayo nilikuwa niondoke wiki mbili zilizopita kabla ya kuibuka baadhi ya mambo ambayo yamenifanya nikawie kwenda huko," anasema.
Chove, shabiki mkubwa wa Mtibwa Sugar na Manchester United, anasema wakati wowote mambo yake yakikaa vizuri ataondoka nchini kwenda kujiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo.
Anasema anaamini ana uwezo wa kucheza soka katika klabu hiyo ya Vita na kwamba umahiri aliouonyesha wakati akicheza soka la kulipwa katika klabu ya As Dolpine ya huko ndiyo 'tiketi' iliyomfanya uongozi wa klabu hiyo kumsaka.
"Unajua nilishawahi kucheza nchini humo miaka ya mwanzoni ya 2000 katika klabu ya As Dolphine ndiyo maana As Vita wamenifuata," anasema.

MKALI
Chove aliyezaliwa miaka 30 iliyopita, akiwa shabiki mkubwa wa muziki wa Kicongo akiizimia bendi za Mapacha Watatu na Akudo Impact, ni mmoja wa makipa hodari nchini waliozichezea timu nyingi ndani na nje ya nchi.
Kitu cha ajabu ni kwamba kabla ya kuwa kipa alikuwa mmoja wa mabeki hodari na pia alipata kucheza kama mshambuliaji wa kati kabla ya kubadilisha namba na kuhamia kwenye nafasi anayoichezea kwa miaka kadhaa sasa.
Chove anayependa kuwa mfanyabiashara mkubwa mara atakapotundika glovu zake, alianza makeke yake tangu shuleni mjini Dodoma akiitaja klabu iliyokuza kipaji chake kuwa ni Job Lusinde chini ya kocha Shaaban Tall.
Baada ya kutoka Lusinde alihamia Vijana Airport aliyocheza na nyota kama Athuman Idd 'Chuji' na wengine na baadaye kutua Makore FC, Zulphat na Mji Mpwapwa na kukimbilia Singida United kabla ya kuichezea Milambo ya Tabora.
Milambo ilimuita akazibe nafasi ya kiungo Mohammed Banka aliyekuwa amehamia Moro United.
Mwaka 2003 alitua Tukuyu Stars na miaka miwili baadaye alitua Kahama United, kisha kwenda Twiga Sports aliyoitema na kuhamia CDA Dodoma kabla ya kutimkia Malawi kuidakia Mzuzu Medical.
Aliporejea nchini  mwaka 2007 aliidakia Friends Rangers ikicheza Ligi ya TFF Kinondoni na kuivutia Yanga iliyomnyakua msimu wa 2007-2008 kabla ya miamba hao kumtema msimu uliofuata ambapo alienda kujiunga na Prisons ya Mbeya.
Chove anayemmwagia sifa kocha Stewart Hall kama mmoja wa makocha bora kuwahi kukutana nao, alikaa na Prisons kwa muda mfupi kabla ya kutimkia Rwanda kukipiga katika klabu ya Marine na baadae AS Dolpine ya DR Congo.
Aliitwa SC Villa na kuichezea kidogo sambamba na akina Steve Bengo na Emmanuel Okwi, kabla ya kurudi Marine na kuisaidia kuinyima ubingwa timu ya Atraco iliyotaka kumsajili kabla ya kughairi.
Baada ya kutoswa na Atraco alihamia Kiyovu na mwishoni mwa msimu wa 2009-2010 alisajiliwa JKT Ruvu kwa mkataba mfupi na kabla ya kuisha alitua Azam iliyokuja kumtema baada ya msimu mmoja na kuhamia Moro Utd.
Msimu huu alisajiliwa Coastal Union na kucheza kwa nusu msimu kabla ya kutemwa pamoja na wachezaji wengine kwa pendekezo la kocha, Hemed Morocco.

Chove (kati walio mbele) akiwa na kikosi cha Coastal Union


MAFANIKIO
Chove aliyeanza kucheza kama beki kabla ya kuhamia kwenye ushambuliaji na baadaye kuhamia kwenye ukipa hadi sasa, anajivunia soka kumpa mafanikio yakiwamo ya kumiliki maduka ya nguo na saluni za kiume.
"Siyo siri soka limenisaidia mengi kimaisha na kiuchumi. Mbali na kunipatia marafiki wengi na kusafiri nchi nyingi, limeniwezesha kumiliki miradi yangu ya kuniingizia pesa," anasema.

Chove akiwa ndani ya Pipa wakati akiichezea Taifa Stars
Kipa huyo mwenyewe mbwembwe anaitaja mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu msimu wa 2008-2009 kuwa ngumu kwake na asiyoisahau.
Anasema anaikumbuka mechi hiyo kwa vile ilikuwa pambano lake la kwanza kuidakia Yanga katia Ligi Kuu na kuisaidia kushinda bao 1-0.
"Naikumbuka kwa ugumu wake, lakini kubwa kuwa mechi yangu ya kwanza kuidakia Yanga kwenye ligi na tulishinda bao 1-0," anasema.

STARS
Chove anayependa kula wali kwa njegere na kunywa soda ya Fanta, anaitabiria timu ya taifa (Taifa Stars) kufika mbali ikiwa chini ya kocha Kim Poulsen lakini amewataka wachezaji wanaoichezea 'kukaza' ili kuipa mafanikio hayo.
"Stars chini ya Poulsen ni kama ilivyokuwa na Marcio Maximo, muhimu wachezaji wajitume ili kuzidi kuwapa raha Watanzania. Naamini wakikomaa tunaweza kufuzu fainali kubwa tunazoshiriki," anasema.

Jackson Chove (kulia) akiwa na Marcio Maximo
Stars inatarajiwa kushuka dimba wiki hii kucheza dhidi ya Morocco katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ikiwa inashika nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast katika Kundi C.
Chove ambaye aliwahi kuichezea Stars kwa nyakati tofauti chini ya makocha Maximo na Jan Poulsen, anasema kama wachezaji watajitoa mhanga uwanjani ni wazi wanaweza kupata pointi tatu muhimu zitakazowaweka pazuri zaidi.
Kipa huyo mwenye watoto wawili, Senior na Junior, wenye umri wa miaka sita, anasema soka la Tanzania limepiga hatua kubwa ila ni vema viongozi wa klabu wakaondoa ubabaishaji kuweza kuwasaidia wachezaji.
Anasema kama viongozi wakiwa watu wa 'longolongo' ni vigumu wachezaji kupata moyo wa kujituma uwanjani na akawataka waache tabia ya kubadilisha makocha ovyo akidai inachangia kuwachanganya wachezaji.
Juu ya wachezaji wenzake anawasihi wasibweteke na kucheza ndani badala yake wachangamkie fursa wanazozipata za kwenda kucheza soka la kulipwa nje kama anavyofanya yeye kila mara.


----------

TFF YAIPONGEZA AZAM KWA USHINDI

Kikosi cha Azam Fc ambao  jana waliitoa kimasomaso Tanzania kwa kushinda ugenini nchini Liberia

Na Boniface Wambura

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaipongeza klabu ya Azam kwa ushindi wa mabao 2-1 ilioupata timu yake katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
Mechi hiyo dhidi ya Barrack Young Controllers II ilichezwa jana jijini Monrovia, na timu hizo zitarudiana wikiendi ya Aprili 6 au 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo unaiweka Azam chini ya kocha wake Stewart John Hall katika mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya mechi ya marudiano. Bila shaka ushindi wa timu ya Azam pamoja na mambo mengine umechangiwa na klabu hiyo kujipanga vizuri.
Hata hivyo ushindi huo bado ni changamoto kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa Azam kuhakikisha unajipanga vizuri kwa mechi ya marudiano kwa vile mpira wa miguu una matokeo ya aina tatu; kushinda, kutoka sare au kufungwa.
Msafara wa timu ya Azam unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Blassy Kiondo unatarajiwa kurejea nchini kesho alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.

Hii ndiyo ratiba kamili ya Taifa Stars kuivaa Morocco

Kocha Kim Poulsen akiwaonoa wachezaji wa Stars walipokuwa wakijiandaa kucheza na Cameroon

Na Boniface Wambura 
TIMU ya taifa, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014 zitakazofanyika nchini Brazil dhidi ya Morocco. Mechi hiyo itachezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ratiba kamili ya timu hiyo kuelekea kwenye mchezo huo ni kama ifuatavyo; 

Jumamosi, Machi 16- Wachezaji kuanza kuripoti kambini

Jumapili, Machi 17- Mazoezi Uwanja wa Karume- Saa 2 asubuhi

Jumatatu, Machi 18- Mazoezi Uwanja wa Karume- Saa 9 alasiri

Jumanne, Machi 19- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri

Jumatano, Machi 20- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 2 asub na saa 9 alasiri

Alhamisi, Machi 21- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri

Ijumaa, Machi 22- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri

Jumamosi, Machi 23- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 10.30 jioni

Uongozi mpya TAFCA wapongezwa

Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Machi 16 mwaka huu) mjini Dodoma.

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAFCA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia taaluma ya ukocha nchini.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAFCA chini ya uenyekiti wa Oscar Don Koroso aliyeibuka mshindi kwa kura zote za ndiyo baada ya kukosa mpinzani.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya TAFCA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA chini ya Ramadhan Mambosasa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Safu nzima ya uongozi wa TAFCA iliyochaguliwa inaundwa na Dk. Oscar Dan Koroso (Mwenyekiti), Lister Manyara (Makamu Mwenyekiti), Michael Bundala (Katibu Mkuu), Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Dismas Haonga (Mhazini), Wilfred Kidao (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF).

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa ni Jemedari Saidi, George Komba na Magoma Rugora.

Wajanja wasiitumie 'Kanumba Day' kujinufaisha

Steven Kanumba enzi za uhai wake
 
MWEZI ujao mashabiki wa sanaa hasa wale wa filamu wataadhimisha mwaka mmoja tangu wampoteze kipenzi chao na nyota wa fani hiyo nchini, Steven Kanumba 'The Great' aliyefariki ghafla nyumbani kwake Aprili 6, mwaka uliopita.
Kanumba alifariki kwa kile kilichoelezwa alianguka na kubamiza kichwa wakati wa mzozo kati yake na aliyekuwa mpenzi wake ambaye ni muigizaji nyota, Elizabert Michael 'Lulu' na kuwaachia majonzi W`atanzania waliokuwa wakimfuatilia.
Hakuna ubishi kwamba msanii huyo alikuwa gwiji na mmoja wa wasanii wachache waliokuwa wakielekea kwenye mafanikio ya kimataifa kupitia kazi mbalimbali alizocheza enzi za uhai wake.
Kifo chake kilitokea wakati akijiandaa kwenda Ghana na Marekani kwa ajili ya kurekodi kazi kulingana na mkataba aliokuwa amepata wiki chache kabla ya kukumbwa na mauti.
Pia alifariki wakati Watanzania wakiendelea kumhitaji katika kuwapa burudani kupitia fani aliyokuwa akiifanya kwa nidhamu ya hali ya juu kiasi cha kuwaacha wenzake mbali kimafanikio.
Pengo la msanii huyo bado linaonekana halipata mtu wa kuliziba licha ya kuwepo kwa baadhi ya wasanii kufurukuta kutaka kuvaa 'viatu' vyake ndani ya faani hiyo ya filamu nchini ambayo imekuwa ikielezwa ilitetereka kisoko tangu alipofariki.
Kifupi ni kwamba Watanzania wanaendelea kukumbuka na kumlilia Kanumba kwa yale aliyoyafanya kama msanii mwenye weledi na anachojua alichokuwa akikifanya.


Hata hivyo, wakati watanzania wakielekea kwenye kuadhimisha mwaka mmoja tangu mkali huyo kufariki, tayari kumekuwa na taarifa za maandalizi ya maadhimisho hayo ya kumuenzi Kanumba yatakayofanyika mwezi ujao hususani siku aliyofariki ya Aprili 6, nilikuwa natoa tahadhari juu ya wanaotaka kutumia siku hiyo kutaka kujinufaisha.
Kwa uzoefu nilionao kama mdau wa sanaa, wapo baadhi ya watu hutumia mwanya wa kuwepo kwa shughuli fulani kujinufaisha kimasilahi huku ndugu, jamaa na wanafamilia husika wakiachwa solemba, ndiyo maana natoa angalizo hilo mapema.
Ni vema maadhimisho ya kumuenzi Kanumba yatumiwe kwa nia ya dhati ya kuenzi yote aliyokuwa akiyafanya marehemu Kanumba ikiwemo kupenda haki, usawa na uaminifu.
Wanaoratibu shughuli zozote za maadhimisho hayo ya mwaka mmoja wa Kanumba maarufu kama Kanumba Day iwe jijini au kwingineko nchini, wafanye kwa lengo la kuenzi juhudi za msanii huyo na kuwashirikisha wanafamilia ili kuepuka manung'uniko.
Inakumbukwa mara alipofariki msanii huyo, wajanja walitengeneza fulana, kofia na hata vitabu bila kuwashirikisha wanandugu mpaka familia ilipokuja kushtuka na kupiga marufuku, hivyo hata katika kuelekea huko hilo lazima lizingatiwe.
Naamini haya yakifanyika Kanumba Day itakuwa na maana halisi kinyume cha hapo itakuwa ni sawa na wizi, utapeli na kutoitendea haki familia ya msanii huyo na hata Kanumba mwenyewe japo hayupo nasi kimwili, lakini kiroho tu pamoja nasi.

Malindi yaifumua Mundu mabao 2-1 Ligi Kuu ya Grand Malt

 Wachezaji wa Malindi, Abdala Said (no.5) na Amour Suleiman (katikati) wakimdhibiti Thabit Khamis wa Mundu, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Grandmalt Zanzibar uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung mjini Zanzibar. Katika mchezo huo Timu ya Malindi ya Zanzibar huku ikiwa pungufu kutokana na mchezaji wake mmoja kulimwa kadi nyekundu, iliweza kupata ushindi wa mabao 2-1 katika dakika za mwanzo wa mchezo.
Abdalla said wa Malindi (kushoto) na Thabit Khamis wa Mundu wakichuana kuwania mpira Picha:Martin Kabemba.

Baby Madaha aja na Wither Way, aitabiria makubwa


Baby Madaha akiwa na tuzo ya AMMA

BAADA ya filamu ya 'Ray of Hope' aliyocheza kama kinara mkuu na kunyakua tuzo ya kimataifa ya AMMA, msanii Baby Madaha anatarajia kuja na filamu iitwayo 'Wither Way', ambayo ametamba itakuwa "funika bovu" kwa jinsi simulizi lake lilivyo.
Baby alisema huenda ikatikisa kuliko filamu zake nyingine alizotoa chini ya kampuni ya Pilipili kutokana na kuandaliwa katika lugha mbili tofauti, moja ikiigizwa Kiswahili na nyingine Kiingereza.
Msanii huyo alisema tayari filamu hiyo itakayoshirikisha nyota kadhaa wa fani hiyo, imeshaanza kurekodiwa na kuwataka mashabiki wake kukaa mkao wa kupata burudani.
"Nipo katika harakati za mwisho za kuibuka na filamu nyingine mpya itakayofahamika kama 'Wither Way' ambayo naamini itanipa tuzo kama nyingine nilizozicheza na kunifanya nivune tuzo nne mfululizo," alisema Baby.
Filamu za nyuma zilizompa tuzo msanii huyo ambaye pia ni mahiri katika fani ya muziki ni 'Nani' mwaka 2010, Desperado (2011) na Ray of Hope (2012) zote kupitia Tamasha la Filamu la ZIFF zikiwa kama Filamu za Mwaka kabla ya kutwaa tuzo hiyo ya AMMA nchini Nigeria.
Alisema kwa namna filamu anayokuja nayo safari hii analenga tuzo ya tamasha la maarufu la kimataifa la filamu la The Cannes.
"Sitakia kuwa mtabiri, ila lazima niseme ukweli huenda filamu ya 'Wither Way' ikabeba tuzo ya Cannes, ngoja tuone itakapotoka," alisema Baby.

Mkubwa na Wanawe sasa wabeba Bendera


KUNDI la muziki wa kizazi kipya lililopo chini ya kituo cha Mkubwa na Wanawe, kinachoongozwa na Said Fella, limefyatua wimbo mpya uitwao 'Bendera' likipigwa tafu na mwalimu wao, rapa Mheshimiwa Temba.
Wimbo huo umerekodiwa katika studio za kituo hicho za Poteza Records chini ya mtayarishaji Shirko na utaanza kusambazwa kwenye vituo vya redio wiki hii.
Akizungumza na MICHARAZO, 'bosi' wa kundi hilo, Said Fella alisema wimbo huo umeimbwa na baadhi ya wasanii wa kituo hicho cha Mkubwa na Wanawe pamoja na Mheshimiwa Temba.
Aliwataja wasanii walioshiriki katika wimbo huo ambao utakuwa wa kwanza kwa kituo hicho kuimbwa na wasanii zaidi ya wawili kuwa ni Dogo Aslay, Dogo Muu, H-Kumbi, Mugogo, DY, Maromboso na Beka.
Fella alisema wakati wimbo huo ukitarajiwa kuanza kurushwa hewani, wanafanya mipango ya kutoa video yake ili mashabiki wao wapate uhondo zaidi.
"Tumeanza na audio, video ipo njiani tukiwa tumedhamiria mwaka 2013 uwe wa Mkubwa na Wanawe," alisema Fella.

Asha Boko: Mwanadada mvunja mbavu shabiki la Yanga


Asha Boko katika sura ya kiusanii
 
WENGI wa mashabiki wa fani ya maigizo wanamfahamu kama Asha Boko, mmoja wa waigizaji wa kike wenye kuvunja mabavu akiringia umbile lake kubwa na kipaji halisi cha sanaa alichonacho.
Hata hivyo majina kamili ya msanii huyo aliyedumu ndani ya fani hiyo zaidi ya miaka 10 iliyopita akiwahi kutamba na kundi la Kaole Sanaa ni Tatu Yusuf mwenyeji wa mkoa wa Pwani.

Asha Boko akiwa katika pozi
Asha Boko, alisema japo alianza sanaa tangu akiwa kinda akionyesha kipaji shuleni, lakini alivutiwa kisanii na wakali ambao baadhi yao amefanya nao kazi kitu kinachomsisimua zaidi.
Aliwataja wasanii waliomvutia enzi akichipukia ni Bi Mwenda, Mzee Kipara, Steven Kanumba, King Majuto na Thea anaodai hadi leo bado anaendelea kuwazimia kwa umahiri wao.
Mkali huyo alisema katika safari yake ya sanaa amekutana na changamoto na mafanikio mbalimbali anayojivunia huku akiwa na ndoto za kufika mbali kisanii na kimaisha.
"Nashukuru sanaa imenipa ajira Al Riyamy na pia nimejenga nyumba na kuendesha shughuli zangu binafsi za biashara kwa fedha za sanaa, japo sijaridhika kwa vile nina kiu ya kufika mbali zaidi," alisema.
Asha Boko anayetamba kwenye kipindi cha kuchekesha cha Vituko Show na katika filamu lukuki za komedi akiwa na wakali wenzake kama King Majuto, Ringo, Masai Nyota Mbovu, Kiduku, Bizzo Man, Bessa na wengine alizaliwa miaka 37 iliyopita , Tumbi Kibaha mkoani Pwani.
Mwanadada huyo ni mtoto wa tano kati ya sita wa familia yao ni mmoja wa ndugu zake ni muimbaji mahiri wa Jahazi Modern Mariam Amour.
Elimu ya Msingi aliisoma Shule ya Kongowe na sekondari mkoani Dar es Salaam kabla ya kujikita katika sanaa akishiriki tamthilia kadhaa kama Taswira, Zizimo na nyingine kabla ya kuhamia kwenye filamu.
Baadhi ya filamu alizocheza mwanadada huyo anayependa kula chakula chochote kizuri na chenye kujenga afya yake na kunywa juisi, ni pamoja na Back From New York, Teja, Jazba, Kuku wa Kichina, Hekaheka, Kitimtim na nyinginezo kibao.
Asha Boko pia ni shabiki mkubwa wa soka akizishabikia timu za Yanga na Taifa Stars na anachizishwa na nguo ya rangi ya pinki na hupenda kutumia muda wake wa zaida kujifunza kuimba na anatoa wito kwa wasanii wenzake kupenda na kuipeleka mbele fani yao.
Juu ya serikali licha ya kuishukuru kwa kuitupia macho sanaa katika uongozi wa awamu ya nne, lakini aliitaka kuongeza juhudi ili wasanii wanufaike na jasho na kupewa thamani kama watu wengine mbele ya jamii, huku akiwaomba mashabiki wao kuwaunga mkono kwa hali na mali.

Asha Boko katika pozi
Msanii huyo mwenye watoto wawili wa kike kwa sasa amegeukia muziki akiwa mbioni kutoka na wimbo wake aliowashirikisha wachekeshaji wenzake kama Kitale, Stan Bakora na Maiko.
Alisema pamoja na wimbo huo kuchezwa kwenye mitandao ya kijamii bado hajausambaza kwenye vituo vya redio, kazi anayopanga kuifanya mara baada ya kurejea toka Tanga kambini.

Azam bwana yaani mpaka rahaaaaaa


Kikosi cha Azam

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania, Azam imeendelea kuwapa raha watanzania baada ya jana kuwanyoa, Barracks YC  II ya Liberia kwa mabao 2-1 na kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Antonette Tubman mjini Monrovia, Liberia, Azam walienda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0.
Bao hilo lililowashtua Azam lilifungwa dakika moja kabla ya mapumziko na Junior Barshall kabla ya Azam kuzinduka kipindi cha pili kwa kusawazisha kupitia Mkenya, Humphrey Mieno.
KInda lililosajiliwa Azam kutoka Ruvu Shooting ndiye aliyeitoa kimasomaso Azam kwa kuifungia bao la ushindi lililoifanya Azam kuwa na kazi nyepesi kwa mechi ya marudiano wiki mbili zijazo ikihitaji sare yoyote tu.
Msafara wa wawakilishi hao wa Tanzania unatarajiwa kuondoka jioni ya leo kurejea nyumbani kwa mujibu wa msemaji wa klabu hiyo, Jaffar Idd watawasilia kesho Jumanne kabla ya kuingia kambini kujiandaa na mechi zao za Ligi Kuu pamoja na pambano lake la marudiano dhidi ya Waliberia.

Samatta, Ulimwengu kutua Stars leo

Mbwana Samatta (kushoto waliosmama) akiwa na kikosi cha Stars
WASHAMBULIAJI Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo wanatarajiwa kutua nchini leo usiku kujiunga na kambi ya timu ya Taifa Stars inayojiandaa kuikabili Morocco katika mechi ya Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili.
Kwa mujibu wa afisa habari wa shirikisho la soka nchini (TFF), Boniface Wambura, kikosi cha Stars kitakamilika kesho Jumanne asubuhi baada ya wachezaji walio katika kikosi cha Azam nchini Liberia kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho kurejea.
Taifa Stars ilianza kambi juzi jioni ambapo wachezaji 14 kati ya 23 walioitwa waliripoti na kufanya mazoezi jana asubuhi chini ya kocha Kim Poulsen.
Wachezaji walioripoti ni nahodha Juma Kaseja kutoka Simba na msaidizi wake Aggrey Morris wa Azam, Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud 'Cholo' (Simba), Shomari Kapombe (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Wengine ni Athuman Idd 'Chuji' (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mrisho Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).
Wachezaji Hussein Shariff, Issa Rashid na Shabani Nditi ambao timu yao ya Mtibwa Sugar juzi ilicheza mechi ya Ligi Kuu ya Bara mjini Turiani waliripoti kambini jana jioni.
Wakati huo huo, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua waamuzi kutoka Angola kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas).
Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne na kufuatiwa na Taifa Stars yenye pointi tatu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF jana, mwamuzi wa mechi hiyo ni Helder Martins de Carvalho wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Inacio Manuel Candido huku Ricardo Daniel Cachicumi akiwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Antonio Muachihuissa Caxala.
Waamuzi hao watawasili nchini saa 1.20 usiku Machi 22 mwaka huu kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Luanda, Angola kupitia Nairobi, Kenya.
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa David Fani kutoka Botswana anatarajiwa kuwasili Ijumaa Machi 22 saa 1:45 usiku kwa ndege ya South African Airways.
Naye mtathmini wa waamuzi (referee assessor) Neermal Boodhoo kutoka Afrika Kusini atawasili nchini Ijumaa pia saa 1:45 usiku kwa ndege ya South African Airways.