STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 30, 2014

Miili ya waliokufa ajali ya Singida waanza kutambuliwa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj3HAzgI5ejXZIyNcqMJaTT85XjZvOu2bov0tWDiQnia54biJdpoDHHWW0xYFF75HuMykuls7TOCKVf843bs4_U_60SbULAnYrqhsrxDbBOguGfwBnOHWDTHZRWU8-CxwzgdZkBPuTnO7o/s1600/1.jpg
Baadhi ya miili ya watu waliokufa kwenye ajali iliyosababishwa na basi la Sumry
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEicj2zByf8m-xK1qel4ADrQklEgUEenqOL_dhOswXFx3_FS3FE-RfUGdKF6RvS0-8JPmbot7v-ZvJp6amixQ029lnaoZFqBmhCoDrQ-r7TxE-2l8fsPCRVsJd1DYmAUce3Lu2ffVOYf5Yg/s1600/2.jpg
Ndugu, jamaa na familia za marehemu wa ajali iliyosababishwa na basi la Sumry wakiwa nje ya hospitali kusubiri kutambua miili ya ndugu zao
MIILI ya watu waliofariki kwenye ajali iliyosababishwa na basi la Sumry, iliyoaua watu 19 wakiwamo trafiki wanne imeanza kutambuliwa.
Ajali hiyo ilitokea juzi kwa basi la Sumry lililokuwa linatokea Kigoma kwenda Dar baada ya kuwaparamia watu waliokuwa wakitoa msaada ya mwendesha baiskeli aliyekuwa amekufa kwa kugongwa katika kijiji cha kijiji cha Utaho, wilayani Ikungi, barabara kuu ya Singida- Dodoma.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Geofrey Kamwela, alisema siku ya tukio hilo wananchi wakiwa na askari polisi wa doria walikuwa wamekusanyika pembezoni mwa barabara kuupakia mwili wa mwendesha baiskeli, Gerald Zefania, aliyegongwa na lori na kufa papo hapo siku hiyo saa 1:30 jioni.
Alisema wakati wakiupakia mwili huo kwenye gari la polisi namba PT 1424 huku likiwa limeegeshwa pembeni mwa barabara, basi hilo lilitokea ghafla kwa kasi na kuwagonga watu 15 na kufariki dunia papo hapo, wengine wanne walikata roho wakati wakipelekwa hospitalini.
Kamanda Kamwela alisema dereva wa basi hilo, Paulo Njilo, mkazi wa jijini Dar es Salaam baada ya kukaribia eneo hilo aliliona gari la polisi likiwa limeegeshwa pembeni kushoto mwa barabara, lakini wakati akijaribu kulikwepa ndipo alipoliparamia kundi la watu waliokuwa na askari.
 Aidha, alisema dereva wa basi hilo baada ya ajali hiyo aliendelea na mwendo hadi aliposimama kilomita 25 katika makao makuu ya Wilaya ya Ikungi na kutokomea kusikojulikana, lakini juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Kamanda huyo aliwataja askari waliokufa kuwa ni F.849 D/CPL Boniface Magubika wa CID Wilaya ya Singida, F.6837 Pc Jumanne Mwakihaba wa FFU Singida, G.7993 Pc, Novatus Tarimo wa ofisi ya RCO na G.8948 Pc, Michael Mwakihaba wa FFU Singida.
Wengine ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha Utaho, Ramadhan Mjengi; Mwenyekiti wa Kijiji Utaho, Paul Hamis; Mwenyekiti wa Kitongoji cha Utaho, Ernest Salanga; Said Rajab, Usirika Itambu, Chima Mughenyi, Salim Juma, Abeid Ramadhan, Mwinyi Hamis na Issa Hussein, wote wakazi wa kijiji cha Utaho.
Kamanda Kamwela alisema miili ya marehemu wengine wanne bado haijatambuliwa na ndugu zao na imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Kamanda Kamwela alisema majeruhi wawili kati ya nane wa ajali hiyo  wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa Singida na wengine sita wapo hospitali ya Misheni Malikia wa Ulimwengu iliyopo Puma.
Aliongeza kuwa  miili ya askari polisi inatarajiwa kusafirishwa kwenda katika mikoa wanakotoka wakati wowote baada ya taratibu za kipolisi kukamilika ikiwamo kuwasiliana na ndugu zao walioko mikoa ya Kilimanjaro, Pwani, Mbeya na Iringa.

Chelsea wapata afueni, Terry, Cech warejea dimbani

http://www2.pictures.zimbio.com/gi/Petr+Cech+John+Terry+Blackburn+Rovers+v+Chelsea+jBW-c2W_Ow3l.jpg
Terry na Cech wakipongezana katika moja ya michezo yao
KIPA tegemeo wa Chelsea Petr Cech na nahodha John Terry wanatarajiwa kucheza mechi ya leo na nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya kati yao na Atletico Madrid baada ya wachezaji hao kufanya mazoezi ya timu hiyo tangu juzi.
Ilisemekana Cech asingeweza kucheza tena msimu huu baada ya kuteua bega lake katika mchezo wa kwanza wakati Terry alitolewa nje kutokana na kuumia kifundo cha mguu katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 0-0. 
Eden Hazard na Samuel Eto’o ambao walikuwa majeruhi wao pia walionekana kuwa fiti kwa kufanya mazoezi  jana, huku viungo John Mikel Obi na Frank Lampard wote hawatakuwepo katika mchezo huo wa marudiano utakaofanyika katika Uwanja wa Stamford Bridge kutokana na kutumikia adhabu ya mechi moja.
Kwa sasa imebaki maamuzi ya kocha Jose Mourinho kuona kama anaweza kuwatumia wachezaji waliorejea toka kwenye majareha kwa ajili ya mechi hiyo kuwania nafasi ya kutinga fainali kuifuata Real Madrid iliyotangulia usiku wa jana kwa kuizabua waliokuwa watetezi, Bayern Munich kwa kwa mabao 4-0.

Malawi yatua kuifuata Stars Mbeya

http://www.malawidemocrat.com/wp-content/uploads/2012/06/Flames-e1339493490888.jpg
Malawi the Flames wanaotua leo kuivaa Taifa Stars
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhXy4DjvygUby0tzSChTVErun58_E3LDqa5xJ_i2zWfMLszWFaSyC9gFEfrYDK13Z3ay7OtaoFftdVKgyeW0ng6kOwB9SLKwda42hmSDnjKljVaRMR3dk2Wg9ugd3lFENkSbBF8-a-GegEK/s1600/FKB_1718.JPG
Taifa Stars itakayoikaribisha Malawi ikiwa na kocha mpya Mart Nooij
TIMU ya soka ya taifa ya Malawi (Flames) inatarajiwa kuwasili nchini kesho kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya.
Boniface Wambura, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), alisema jijini Dar es Salaam  kuwa Flames yenye msafara wa watu 31 utakaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka cha Malawi (FAM) itaingia Mbeya kwa usafiri wa barabara. Wachezaji katika msafara huo watakuwa 20.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha mpya, Mart Nooij tayari ipo jijini Mbeya tangu juzi kujiwinda kwa mechi hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano ya kuwania kufuzu fainali zijazo za Afrika (AFCON) dhidi ya Zimbabwe itakayochezwa jijini Dar es Salaam kati ya Mei 16 na 18 mwaka huu.
Mwishoni mwa wiki Taifa Stars iliyofinyangwa na TFF, ilitia doa sherehe za miaka 50 ya uwapo wa Tanzania baada ya kuchapwa  magoli 3-0 dhidi ya timu ya taifa ya Burundi (Intamba Murugamba) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

As Vita, Mazembe wapangwa kundi moja Afrika

http://www.adunagow.net/main/wp-content/uploads/Mazembe.jpg
Tp Mazembe

Al Ahly
KLABU za TP Mazembe na AS Vita za DR Congo zimepangwa kundi moja la  A katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa pamoja Al Hilal ya Sudan na Zamalek ya Misri.
Kundi B la michuano hiyo limezikutanisha timu za waarabu watupu, Esperance na C.S Sfaxien za Tunisia  E.S Setif ya Algeria na Ahly Benghazi ya Libya.
Katika droo iliyotolewa inaonyesha michezo za makundi hayo zitaanza kuchezwa kati ya Mei 16 na 18 na 23 na 25, Juni 6 na 8, Julai 25 na 27, Agosti 8 na 10 na  22 na 24 huku timu zitakazoshika nafasi mbili za juu kwenye makundi zikisonga Nusu Fainali.

Wakati huo huo ratiba ya makundi kwa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika nayo imepangwa ambapo wababe wa Yanga, Al Ahly ya Misri imepangwa kundi B linalotajwa kama la kifo.
Kundi hilo linajumuisha timu za  Sewe Sport ya Ivory Coast, Etoile du Sahel ya Tunisia na Nkana Red Devils ya Zambia.
Kundi A lenyewe lina timu za Coton Sport ya Cameroon, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, AS Real ya Mali na AC Leopards ya Kongo Brazzaville.
Mechi za michuano hiyo zinatarajiwa kuchezwa kuanzia kati ya Mei 16 na 18 na Juni 23 na 25, Juni 6 na 8, Julai 25 na 27, Agosti 8 na 10 na 22-24 na washindi wawili wa kila kundi watasonga Nusu Fainali.
Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika
Kundi A: TP Mazembe (DRC), Al-Hilal (Sudan), Zamalek (Misri) na AS Vita (DRC)
Kundi B: Esperance (Tunisia), CS Sfaxien (Tunisia), Entente Setif (Algeria) na Al-Ahly Benghazi (Libya).
Makundi Kombe la Shirikisho Afrika:
Kundi A: Coton Sport (Cameroon), ASEC Mimosa (Ivory Coast), AS Real Bamako (Mali) na AC Leopards (Congo)
Kundi B: Al Ahly (Misri), Sewe Sport (Ivory Coast) Etoile du Sahel (Tunisia) na Nkana Red Devils (Zambia)

Bayern chali yapigwa 4-0 kwao na kuvuliwa taji

* Leo zamu ya Chelsea na Atletico Madrid

UNAWEZA usiamini ila ndivyo ilivyo, mabingwa watetezi wa Ligi ya Ulaya Bayern Munich wamevuliwa taji hilo baada ya kukandikwa mabao 4-0 na Real Madrid na kuwafanya wababe hao wa Hispania kutinga fainali.
Mpango wa kocha Carlo Ancelotti wa kuwapanga washambuliaji wake watatu Karim Benzema, Gareth Bale na Cristiano Ronaldo ulizaa mpango baada ya Real kuisambaratisha Bavarians nyumbani kwao bila kutarajiwa na kuzima ndoto za Pep Guardiola kubadilisha matokeo ya kipigo cha bao 1-0 ilichopewa timu yake katika  mechi ya kwanza.
Mabao mawili ya Sergio Ramos na mengine ya Cristiano Ronaldo yalitosha kukwamisha safari ya wababe hao wa Ujerumani kwenye uwanja wao wa Allianz Arena na kukubali kulitema taji hilo.
Ramos alianza kufunga bao la kwanza dakika ya 16 kwa pasi ya Luka Modric kabla ya kuongeza jingine dakika nne baadaye akimalizia pasi ya Pepe na Ronaldo alikuja kupigilia msumari katika dakika ya 34 kwa pasi ya Bale na kumalizia udhia dakika ya 90 kufunga bao la nne.
Real Madrid sasa inasubiri mshindi kati ya Chelsea ya England na Atletico Madrid wanaoumana leo katika mechi ya marudiano nyingine ya nusu fainali, mechi itakayochezwa mjini London.
Katika mechi ya kwanza timu hizo ziliotoka suluhu ya kutofungana na yeyeote eatakayetumia vyema karata yake ataifuata Real kwenye fainali ya Mei 24 mjini Lisbon Ureno.