STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 11, 2013

Chelsea yafa ugenini lakini yatinga nusu fainali UEFA ndogo


Wachezaji Chelsea wakimpongeza Torres kwa kufunga bao akuongoza
LICHA ya kupokea kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa wenyeji wao Rubin Kazan ya Russia, Chelsea ya Uingereza imekuwa timu ya kwanza muda mfupi uliuopita kufuzu hatua ya nusu fainali ya UEFA Ndogo.
Chelsea imefanikiwa kufuzu hatua hiyo kutokana na ushindi mnono wa mabao 3-1 iliyopata katika mechi yao ya wali iliyochezwa 'darajani' mjini London hivyo kupenya kwa jumla ya mabao 5-4.
Fernando Torres aliiandikia Chelsea bao la kuongoza dakika chache baada ya kuanza kwa pambano hilo kwa kumalizia kazi nzuri ya Frank Lampard, goli lililodumu hadi wakati wa mapumziko kabla ya wenyeji kusawazisha dakika ya 51  Marcano.
Victor Moses mmopja wa wafungaji wa mabao katika pambano la wiki iliyopita baina ya timu hizo aliiongezea Chelsea bao la pili dakika nne baadaye kabla ya wenyeji kusawazisha katika dakika ya 62 kupitia kwa Gokdeniz Karadeniz kabla ya Bibras Natcho kufunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penati dakika ya 75.
Michezo mingine ya ligi inatarajiwa kuchezwa muda mfupi ujao kwenye viwanja vingine vitatu tofauti kupata timu tatu za kuungana na Chelsea katika hatua hiyo ya nusu fainali.

Jahazi la African Lyon lazidi kuzama VPL


Kikosi cha African Lyon kilichozamishwa leo jioni
JAHAZI la timu ya African Lyon jioni ya leo limeendelea kuzama baada ya kubamizwa mabao 3-1 na Azam katika pambano pekee lililochezwa kwenye uwanja wa Chamazi, jijini Dar es Salaam.
Kipigo hicho kimezidi kuifanya Lyon kusalia nafasi nafasi ya 13 ikijiweka pabaya katika kuepuka kushuka daraja tofauti na tambo zilizokuwa zikitolewa awali kuwa ni vigumu kwao kushuka daraja, kwani wamesaliwa na pointi 19 tu
Mabao yalioinyong'onyesha Lyon yalitupiwa kimiani na nyota wa Azam, Mcha Khamis ‘Vialli’ katikam dakika ya 9 kabla ya mfungaji kinara wa mabao wa VPL, Kipre Tchetche kuongeza mengine mawili katika dakika ya 28 na 61.
Bao pekee la Lyon lilifungwa na Adam Kingwande katika kipindi cha kwanza na kufanya wakati wa mapumziko matokeo yawe mabao 2-1.


                                          P      W     D     L     F      A     GD     PTS
    1.  Young Africans         21     15     4     2    37     12    +25     49
    2. Azam                         22     14     4     4    39     17     +22     46   
    3. Kagera Sugar            22     10     7     5    25     18     +7      37    
    4. Simba                        21     9      8     4     30     19    +11     35
    5. Mtibwa Sugar            23     8      9     6     26     24     +2      33  
    6. Coastal Union            22     8     8      6     23     20     +3     32   
    7.  Ruvu Shooting           22     8     6     8     21     19     +2     30    
    8.  JKT Oljoro FC            22     7     7     8     22     24     -2     28    
    9. JKT Mgambo              22     7     3     12     14     22     -8     24
    10.Tanzania Prisons      23      5     8     10     12     21     -9     23   
    11.Ruvu Stars                21     6     4     11     19     34     -15     22
    12. Toto Africans           24     4     10     10    22     32     -10     22
    13.  African Lyon            23     5     4     14     16     35     -19     19
     14. Polisi Morogoro      23     3     10     10     11     21     -10     19   
 

Ruvu Shooting yaitahadharisha TFF Kamati za Ushindi zinazoibuka sasa Ligi Kuu

IKIWA safarini mkoani Mbeya kwa ajili ya pambano lao lijalo dhidi ya wenyeji wao, Prisons ya Mbeya, uongozi wa timu ya Ruvu Shooting umeliomba Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuwa makini na Kamati ya Ushindi za klabu mbalimbali zilizoundwa wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikielekea ukingoni.
Uongozi huo wa Ruvu umedai kuwa, kamati hizo huenda zikatumika vibaya katika upangaji na hulazimishaji wa matokeo viwanjani kutokana na ukweli kamati hizo mara nyingi huusisha viongozi wa FA mkoa na hata ofisi za wakuu wa mikoa husika wanaoweza kutumia vibaya nafasi zao kuzibeba timu zao hasa zikiwa kwao.
Akizungumza na MICHARAZO hivi punde, Msemaji wa klabu hiyo, Masau Bwire alisema kamati ya kusaka ushindi kwa timu za ligi kuu, siyo tatizo ila hofu yao namna zinavyoundwa wakati huu ligi ikielekea ukingoni na baadhi yao ni zile timu ambazo zipo katika hali mbaya kwenye ligi hiyo.
Bwire alisema, ingekuw vyema wakafuatilia kwa ukaribu mechi za mwisho za ligi hiyo ili kuepusha hujuma kwa timu nyingine, ili ligi imalizike salama kama ilivyoanza.
"Hatupingi kuundwa kwa hizi kamati kwa baadhi ya timu, lakini zinatutia hofu kwa namna zinavyoundwa kila mara timu zikiwa katika nafasi mbaya na hasa ligi ikielekea ukingoni, mbaya zaidio hujumuisha watu wenye nyadhifa ambazo wanaweza kutumika kuwatisha au kuwalazimisha waamuzi kutengeneza matokeo ya kuzibeba timu hizo," alisema Bwire.
Alisema kwa vile vyama vya mikoa (FA) ni wanachama wa TFF na majukumu yao ni kuhakikisha utekelezwaji wa sheria 17 za soka zinatumika uwanjani, hadhani ni sahihi nao kuingizwa kwenye kamati hizo kwani wanaweza kulaumiwa inapotokea dosari kwenye mechi ndani ya mikoa yao.
Aliongeza kuwa ni vyema kamati hizo zingekuwa zikiundwa mapema na kufanya kazi kuzisaidia timu zao kuliko sasa ambako imekuwa kama fasheni na kuleta hisia mbaya hasa wakati huu watanzania wakiwa na hisia kali juu ya vitendoi vya rushwa michezoni.
Juu ya pambano lao lijalo Bwire alisema kikosi chao kipo safarini lakini wakiwa na morali wa kupata ushindi mjini Mbeya, cha muhimu akiiomba TFF kuhakikisha wanausimamia kwa ukamilifu mchzeo huo ili kusiwepo na matukio kama waliyokutana nao jana kwenye pambano lao na Polisi Moro lililoisha kwa suluhu ya 0-0.

Ecuador yaingia Top 10 ya FIFA, England yaporomoka, Tanzania yapaa



NCHI ya Ecuador imeweka hostoria kwa kufanikiwa kuingia kwa mara ya kwanza kwenye Top 10 ya orodha timu bora duniani kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA.
Kwa mujibu wa orodha iliyotangazwa na FIFA, Ecuador imeshika nafasi hiyo kutokana na ushindi wa mechi mbili mfululizo walizocheza ndani ya mwezi uliopita.
Mechi hizo ni pamoja na ile ya kirafiki ya kimataifa dhidio ya El Salvador waliposhinda mabao 5-0 na ile ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Paguguay waliowalaza mabao 4-1.
Wakati Ecuador wakitinga hatua hiyo, Russia wamejikuta wakiporomoka, huku Croatia wakitinga hadi nafasi ya nne katika msimamo wa orodha hiyo mpya ya FIFA baada ya kushinda mechi zake mbili dhidi ya Wales na Serbia.
Orodha hiyo mpya ya FIFA inaoonyesha timu ya Hispania imeendelea kuongoza msimamo ikifuatiwa na Ujerumani kisha Argentina na Ureno ikikamilisha orodha ya timu Tano Bora ikitoka nafasi ya saba.
Colombia imeendelea kusalia kwenye nafasi ya sita huku England ikifuatia ikiporomoka kwa nafasi tatu, Italia imeshika nafasi ya nane baada ya kushuka kwa nafasi tatu na Uholanzi walioshuka nafasi moja wameshika nafasi ya tisa mbele ya Ecuador.
Katika orodha ya nchi za Afrika, Ivory Coast imeendelea kuongoza ikiwa ipo nafasi ya 12 duniani, ikifuatiwa na majirani zao Ghana walipo nafasi ya 22 duniani ikishika nafasi ya pili Afrika.
Zilizopo kwenye Top 10 ni Mali, Nigeria, Algeria, Tunisia, Zambia, Burkina Faso, Guinea ya Ikweta na Cameroon. Kwa ukanda wa CECAFA, Uganda imeendelea kuwa kinara ikifuatiwa na Tanzania iliyopanda kwa nafasi tatu toka 119 duniani hadi ya 116 huku Afrika ikiwa nafasi ya 33.

Pan Africans kwafukuta moto, IDFA yaamua kuingilia kati

Jengo la makao makuu ya klabu ya Pan African
WANACHAMA wa klabu ya Pan African wameushtaki uongozi wao kwa Chama cha Soka Wilaya ya Ilala (IDFA) kwa madai ya kukiuka katiba wakishindwa kuitisha mikutano tangu walipoingia madarakani mwaka 2009.
Kwa mujibu wa barua yao kwenda ya Machi 30, 2012 kwenda kwa Katibu Mkuu wa IDFA, wanachama hao wa Pan wanadai tangu uongozi wao ulipoingia madarakani Aprili 18, 2009 hawajaitisha mkutano wowote wala kushirikisha wanachama katika baadhi ya maamuzi waliyoamua kuyafanya.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na mmoja wa wanachama wa klabu hiyo kwa niaba ya wenzake, Abbas Ally (kadi namba 0075), imedai mbali kutoshirikishwa katika maamuzi yanayofanywa na uongozi huo, pia klabu imekuwa haina ofisi.
"Japo jingine linalotutisha ni klabu kutokuwa na ofisi wake tuna jengo letu ambalo uongozi umelipangisha lote kiasi sisi wanachama kukosa mahali pa kupata huduma za klabu au kupata taarifa na kulipia ada za uanachama," taarifa hiyo ilisema.
Iliongeza kwa kuiomba IDFA kama mlezi wa klabu za Ilala kuushinikiza uongozi kuitisha mkutano wa wanachama na wao (IDFA) wakiwepo kama shahidi juu ya uongozi lazima uwasilishe mambo manne kwao siku hiyo.
Moja na mambo hayo ni ripoti ya mapato na matumizi kwa kipindi chote walichokaa madarakani na ukaguzi juu ya mapato hayo, taarifa ya sababu zilizoufanya uongozi huo kupangisha jengo lote kiasi cha kukosa ofisi na  mengine.
MICHARAZO liliutafuta uongozi wa Pan kufafanua madai hayo, ambapo  Makamu Mwenyekiti, Ally Hemed alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo badala yake akataka atafutwe Katibu Mkuu wake Saad Mateo ambaye simu zake hazikupatikana hewani.
Hata hivyo Katibu Mkuu wa IDFA, Daud Kanuti ilithibitisha juu ya kupokea barua ya wanachama hao wa Pan na kudai kamati yao ya Utendaji ilishakutana na kuamua kuziita pande mbili zinazosigana kukaa meza moja kuzungumza.
Kanuti alisema kikao hicho kitafanyika Jumamosi ili kuzisikiliza pande zote mbili kwa kuipitia katiba ya klabu hiyo kisha kutoa maamuzi yatakayoleta suluhu ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Lyon kuendeleza maajabu leo mbele ya Azam?


Kikosi cha African Lyon

Azam Fc
TIMU ya soka ya Azam leo inatarajiwa kushuka dimbani kuvaana na African Lyon, inayopigana kuepuka kushuka daraja katika pambano pekee litakalochezwa kwenye uwanja wa Chamazi.
Lyon ambayo katika mechi yake iliyopita ilifanya maajabu kwa kuilaza Coastal Union na kuondoka mkiani, hali inayofanya mashabiki kutaka kuona kama itaendeleza ubabe huo au la.
Pambano na kwamba Lyon hiyo ni mechi yake muhimu, lakini pia kwa Azam ni muhimu zaidi katika mbio zake za kutaka kuwaengua Yanga kileleni na kuweka rekodi ya kuwa mabingwa wapya nchini.
Azam ipo nafasi ya pili nyuma ya Yanga ikiwa na pointi 43, sita zaidi ya vinara hao na iwapo itashinda itapunguza pengo hilo hadi kuwa tatu kabla ya kuvaana na Simba Jumapili uwanja wa Taifa.
Makocha wa timu hizo mbili zenye upinzani wa jadi kutoka wilaya ya Temeke, wametamba kuhakikisha wanaibuka na ushindi ili kutimiza malengo yao tofauti.
Kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall, alinukuliwa akisema wataingia uwanjani bila kuidharau Lyon licha ya kusaka ushindi ili kujiweka pazuri katika harakati zao za ubingwa.
Naye kocha wa Lyon, Charles Otieno, alitamba kwamba wamejipanga kushinda mchezo wa leo ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuepuka kurudi Ligi Daraja la Kwanza.
Kikosi cha Lyon mpaka sasa kimejikusanyia pointi 19 wakilingana na Polisi Moro wanaoshikilia mkia kwa tofauti ya uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Ili kujua nani atakayekuwa ametimiza malengo ni kusubiri mpaka baada ya dakika 90 za pambano hilo pekee kwa siku ya leo.

Messi aivusha Barca nusu fainali, Juve wakiona cha moto nyumbani

 
Pedro akishangilia bao lake la kusawazisha dhidi ya PSG jana usiku

NYOTA wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi usiku wa kuamkia leo alionyesha ni namna gani alivyo chachu ya mafanikio ya timu yake baada ya kuiwezesha Barcelona kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Messi aliyeingia kipindi cha pili wakati wenyeji Barca wakiwa nyuma kwa bao 1-0, alibadilisha taswira nzima ya mchezo huo uliochezwa uwanja wa Camp Nou na kuipa timu yake sare ya bao 1-1 dhidi ya wageni PSG ya Ufaransa.

PSG walitangulia kupata bao kupitia Javier Pastore na kuwapa wakati mgumu wenyeji waliokuwa wameelemewa licha ya  Xavi Hernendez kuweka rekodi ya kupiga pasi sahihi kwa asilimia 100 katika pambano hilo.

Mara baada ya kuingia uwanjani Messi aliifanya PSG kupoteza mwelekeo na yeye kutumia nafasi hiyo kutoa pasi murua kwa David Villa ambaye alimpasia Pedro aliyefunga bao la kusawazisha dakika ya 71.

Hata hivyo Barca wamefanikiwa kufuzu kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kupata sare ya mabao 2-2 ugenini wiki iliyopita na hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 3-3 na kuiondosha PSG kwenye michuano hiyo.

Katika pambano jingine ambalo lilichezwa mjini Turin, Italia wenyeji na vinara wa ligi kuu ya Seria A, Juventus walishindwa kutamba nyumbani baada ya kunyukwa mabao 2-0 na Bayern Munich ya Ujerumani.

Ushindi huo wa Munich umeifanya timu hiyo kufuzu nusu fainali ikiungana na timu za Real Madrid, Borussia Dortmund na Barcelona kwa jumla ya mabao 4-0.

Katika mechi yao iliyopita iliyochezwa nchini Ujerumani, Juve walilala kwa mabao 2-0.

Bayern ilipata ushindi huo ugenini kupitia mabao yaMario Mandzukic aliyefunga katika dakika ya 64 akimalizia mpira wa faulo uliopigwa na kiungo Bastian Schweinsteiger kabla ya Claudio Pizarro kufuinga bao la pili dakika ya 90.

Hatma ya timu zipi zitakazokutana katika hatua hiyo inatarajiwa kufahamika kesho Ijumaa itakapotangazwa droo ndogo huku kukiwa na hofu Wahispania na Wajerumani waliofuzu hatua hiyo kukutana wenyewe kwa wenyewe.


Golden Bush Fc haikamatiki Ligi ya TFF-Kinondoni

TIMU ya soka ya Golden Bush imezidi kuchanja mbuga kwenye Ligi Daraja la Nne wilaya ya Kinondoni, baada ya juzi kupata ushindi wa nne mfululizo  kwa kuwalaza TP Afrika kwa mabao 3-1 katika mfululizo wa ligi hiyo.
Ushindi huo wa juzi katika pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Itihad, Mwananyamala jijini Dar es Salaam limeifanya Golden Bush kuongoza msimamo wa kundi lake na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya pili ya michuano hiyo ninayochezwa kwenye viwanja mbaliumbali wilayani humo.
Golden Bush inayonolewa na nyota wa zamani wa soka nchini, Shija Katina na Madaraka Seleman, ilipata ushindi huo wa nne kupitia mabao yaliyofungwa na wachezaji wake nyota, Kenan Mwashinde aliyefunga mawili na Mrisho aliyefunga bao jingine.
Kabla ya ushindi huo wa juzi, Golden Bush ilianza ligi hiyo kwa kishindo kwa kuipa kipigo kitakatifu timu za Victoria ya Kijitonyama kwa kuwatandika mabao 6-1 kabla ya kuilazaa Makumbusho Talents kwa magoli 3-1 na kuizima Katabazi  na kufanya waongoze msimamo wa kundi lao wakiwa na pointi 12.