Wazee kama hawa wanahitaji kusaidiwa
Na Suleiman Msuya
KATIKA kuhakikisha kuwa usawa unakuwepo katika jamii yote kwa pamoja Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ipo kwenye mapitio ya mfumo wa sheria ya huduma ya jamii kwa wazee (elderly social care).
Hayo yalisemwa na Afisa Habari wa tume hiyo Munir Shemweta wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam.
Alisema mapitio hayo yana lengo la kubaini mapungufu yaliyoko kwenye mfumo huo na kutoa mapendekezo stahiki ili kuweza kuwa na mfumo mzuri wa sheria  utakaolenga ustawi na hifadhi kwa wazee wote wenye miaka zaidi ya 60 wa mjini na vijini.
Shemweta alisema utafiti unaonyesha kuwa wazee wakishafikisha miaka 60 na kuendelea uwezo wao wa kufanya kazi unakuwa mdogo hali ambayo inawafanya wakose mahitaji muhimu kama chakula, mavazi,malazi pamoja na kupungua nguvu kazi kwa Taifa.
“Tume ipo katika mchakato wa kufanyia mapitio ya mfumo wa sheria ya huduma ya jamii kwa wazee kwani kuna dalili za kufanya wazee wawe katika maisha magumu,” alisema.
Afisa Habari huyo alisema pamoja na kuwa na sera ya Taifa ya Wazee (National Ageing Policy 2003) Tanzania haina sheria maalumu katika eneo hilo, hali ambayo inachangia mgawanyiko baina ya kundi hilo.
Alisema sheria mbalimbali za mafao zinawagusa wazee wanaostaafu kazi Serikalini na sekta binafsi ambao ni sehemu ndogo ya kundi la wazee wengi wanaokosa huduma muhimu za maisha.
“Ikumbukwe kuwa wazee hawa ni wale waliotumikia Taifa kwa nguvu na moyo wote kwenye ngazi mbalimbali wakati wakiwa na nguvu zao hivyo wanapokuwa wamezeeka ni muhimu wakawekewa mfumo bora wa kisheria ili kuhakikisha wanaishi maisha mazuri bila kujali kupungua kwa uwezo wao wa kujishughulisha katika kazi,” alisema.
Shemweta alisema Tume inaendelea na rasimu ya awali ya kuangalia hali halisi ya Tanzania kuhusiana na suala zima la wazee ikiwemo mikataba ya kimataifa, mifumo ya kisheria na jamii pamoja na sera.
Alisema matarajio ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania  ni kuwa baada ya kukamilika kwa mapito ya mfumo huo wa kisheria kuhusiana na huduma za jamii kwa wazee, Tume itakuja na mapendekezo ya kisheria na yasiyo ya kisheria ambayo yataleta tija kwa Taifa kwa ujumla.