STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 12, 2014

Simba yalala kwa URA, kesho kuwafuata Ndanda FC

Amri Kiemba akijaribu kuwatoka wachezaji wa URA huku Emmanuel Okwi akiwa tayari kutoa msaada
KLABU ya soka ya Simba imeendeleza uteja wake mbele ya URA ya Uganda baada ya jioni ya leo kunyukwa bao 1-0 katika pambano la kirafiki la kimataifa lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa.
Simba iliyotoka kuionea Gor Mahia kwa kuilaza mabao 3-0 ilishindwa kupata dawa ya kugeuzwa mteja wa kudumu kwa Watoza Ushuru hao wa Uganda kwa kulazwa bao hilo ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Simba kupoteza chini ya kocha Patrick Phiri.
Bao pekee lililoizamisha vijana wa Msimbazi ambayo haijaifunga URA katika mchezo wowote wanaokutana nao iwe kwenye mashindano au mechi za kirafiki liliwekwa kimiani na Frank Kalanda katika dakika ya 42, akimalizia kazi nzuri ya Elkanda Nkungwa.
Kesho asubuhi Simba itapaa angani kuelekea Mtwara tayari kwa pambano lao jingine dhidi ya Ndanda Fc katika kunogesha Siku ya Ndanda (Ndanda Day) linalofanyika kesho kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini humo.

Wahitimu Shule ya Brian Trust, wengine watahadharishwa

Mgeni rasmi wa mahafali ya Shule ya Brain Trust, Richard Mngomo alitoa nasaha zake jioni ya leo
Wahitimu wakionyesha umahiri wao wa kuimba ngonjera
Wahitimu wakielekea eneo la shughuli ya kuagwa kwao kwa kuhitimu darasa la saba
Mkuu wa Shule ya Msingi, Nervin Marandu akitoa natoa nasaha zake
Wahitimu wakiingia uwanjani kuonyesha umahiri wao
Wakiimba
Samuel Robert akiwaongoza wahitimu wenzake kuonyesha umahiri wa kuimba ngonjera
Skauti wakionyesha umahiri wao mbele ya meza kuu
Mericiana Ronald akianza kuonyesha umahiri wake wa kucheza muziki
Acha kama Aisha Madinda! Mericiana akiendelea kuangusha rhumba
Mkuu wa Shule ya Msingi, Nervin Marandu akisoma wasifu wa shule hiyo katika mahafali hayo pembeni yake ni mmoja wa walimu wa shule ya Brain Trust
Immaculatha Justine Limonga akipokea cheti chake cha kuhitimu Darasa la Saba toka kwa mgeni rasmi
WAHITIMU wa darasa la saba wa Shule za Msingi nchini kote wamehimizwa kuwa makini wanaporudi mtaani kusubiri matokeo yao ya mitihani ili kuepuka kuharibikiwa na kutumbukia kwenye maovu.
Aidha wazazi wamesisitizwa kuhakikisha wanapambana na kusaidia kuwaendeleza watoto wao kwa masomo ya sekondari badala ya kuridhika na Elimu ya Msingi wanaomaliza watoto wao.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Shule ya Brain Trust, Irene Makinda wakati wa mahafari ya wahitimu wa darasa la saba wa shule hiyo yaliyofanyika jioni ya leo.
Makinda alisema wahitimu wa darasa la saba wanachangamoto kubwa katika kipindi chao cha kusubiri matokeo ya mitihani yao kwani wanakutana na na makundi ya watu tofauti, hivyo wawe makini.
Alisema ni vyema wazazi wakawaunganisha watoto wao na masomo maalum ya kujiandaa kujiunga sekondari (Pre form One) ili kuendeleza kuzifanya akili zao zichemke na kuepushiwa kuingia kwenye maovu.
"Hapa shuleni tunapokea wanafunzi kwa masomo hayo hivyo wazazi wasizembee wawalete watoto na pia shule yetu ina masomo ya sekondari hivyo wanafunzi wanaweza kuendelea hapa hapa," alisema.
Naye mgeni rasmi wa sherehe hizo zilizofanyika Yombo Vituka, Richard Mgomo wa Tanzania Printers, alisema wahitimu hao wa la saba wasidhani wameshamaliza kazi badala yake wajipange zaidi kimasomo.
"Kazi haijaisha, miaka saba mmepambana na kufanikiwa kufika mlipofikia, tunawapongeza, lakini kazi haijaisha kuna mtihani mkubwa zaidi mbeleni hivyo mjipange. Msiwangushe wazazi na walezi," alisema.
Mgomo, alisema ni wajibu wa wazazi na walezi kuwaendeleza watoto wao kwa masomo ya sekondari na nafasi hizo zikipatikana wanafunzi hao wasiwaangushe wazazi na walezi badala yake wajibidiishe zaidi.
Kabla ya mgeni rasmi huyo kuzungumza, Mkuu wa Shule ya Msingi Nervin Marandu alisoma historia fupi ya shule hiyo na kusema ilianzishwa Sept Mosi, 1998 ikiwa na wanafunzi 48 tu.
Hata hivyo alisema mpaka sasa shule hiyo ya msingi ina wanafunzi wapatao 850 na kusisitiza shule yao haibagui wanafunzi wa kuwapokea na kujivunia mafanikio inayopata kila mwaka tangu ianzishwe.
Katika mahafali hayo yaliyohudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwamo walimu wa shule za jirani na wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma shule hiyo kulipambwa na burudani toka kwa wanafunzi.
Miongoni mwa burudani hiyo ni mwanafunzi wa shule ya chekechea ya shule hiyo ya Brain Trush Mericiana Ronald aliyeonyesha kipaji cha kucheza muziki na kutuzwa maelfu ya fedha na waliokunwa naye.

Rodgers awaka majeruhi ya Sturridge

http://i.telegraph.co.uk/multimedia/archive/02579/daniel-sturridge_2579270b.jpgMENEJA wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers amesema kuwa majeruhi ya Daniel Sturridge yangeweza kuepukika na Chama cha Soka cha Uingereza kinapaswa kuwaepusha wachezaji na majeruhi pindi wawapo katika majukumu ya kimataifa. 
Mshambuliaji huyo alicheza kwa dakika 89 wakati Uingereza ikishinda bao 1-0 dhidi ya Norway katika Uwanja wa Wembley Jumatano iliyopita kabla ya kurejea tena mazoezini saa 36 baadae na kupata majeruhi akiwa mazoezini. 
Sturridge, 25 alikosa mchezo ambao Uingereza iliibugiza mabao 2-0 Uswisi katika mchezo wa kufuzu michuano ya Ulaya Jumatatu kutokana na majeruhi hayo na sasa anatarajiwa kukaa nje kwa wiki mbili zaidi. 
Rodgers amesema wamesikitishwa sana kutokana kazi kubwa aliyofanya wakati wa maandalizi ya msimu kwani wanadhani majeruhi aliyopata yalikuwa yanaepukika kama wahusika wangekuwa makini. 
Liverpool itajitupa uwanjani Jumamosi hii kukwaana na Aston Villa katika mchezo wa Ligi Kuu.

Pele asema Messi ananafasi ya kutwaa Kombe la Dunia

http://i.lidovky.cz/10/042/lnc460/ANT326be7_pele_messi.jpg
GWIJI wa soka wa Brazil, Pele amesema kwamba Lionel Messi bado anayo nafasi ya kutwaa Kombe la Dunia na kuongeza kwamba nyota huyo wa Barcelona tayari ni mmoja wa magwiji wa soka hata kama atashindwa kuiongoza Argentina kutwaa taji hilo.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alikaribia kubeba Kombe la Dunia wakati alipoiongoza Argentina kufika fainali nchini Brazili, lakini likatua kwa Ujerumani walioshinda katika muda za ziada.
Licha ya hivyo, Pele ameweka wazi kwamba Messi bado anayo nafasi na anaamini kwamba atapata fursa nyingine ya kutwaa tajihilo 2018.
"Hakika, Messi bado anaweza kutwaa Kombe la Dunia," Pele aliiambia DPA.
"Messi ni mchezaji aliyekamilika na yuko katika hali nzuri sana kimwili. Sina shaka kwamba bado atatamba kwenye Kombe la Dunia.
"Kufungwa katika fainali Brazil hakumuondolei ukweli kwamba Messi ni mchezaji mkubwa sana. Atapata fursa nyingine ya kutamba nchini Russia.
"Hakuna shaka kwamba Messi ni bonge la mchezaji. Hatuwezi kuhoji uwezo wake kwa sababu tu hajatwaa Kombe la Dunia bado."
Messi amecheza mechi 93 za timu yake ya taifa na ameifungia magoli 42.

Kaole Kwanza waanza mazoezi ya Kipusa

http://4.bp.blogspot.com/-YOSn_Am3rdg/U8yolhUqOTI/AAAAAAAAMlU/62UARys1Ok8/s1600/Kaole1.jpg
Kundi la Kaole Kwanza katika picha ya pamoja siku walipozindua Kipusa chao
KUNDI la Kaole Kwanza ambalo linaoundwa na wasanii waliowahi kutamba na Kaole Sanaa, limeanza tena mazoezi kwa ajili ya kuendelea kurekodi tamthilia yao iitwayo 'Kipusa' ambayo inatarajiwa kuanza kurushwa hewani kupitia runinga.
Akizungumza na MICHARAZO mmoja wa viongozi wa Kaole Kwanza, Issa Kipemba alisema baada ya kusitishwa kwa kambi ya mazoezi ili kurekebisha mchakato wa kusaka kituo cha kurushia mchezo wao, hatimaye mazoezi hayo yameanza tena.
Kipemba alisema wanafanya mazoezi hayo kabla ya kuendelea kurekodi kazi hiyo tayari kwa kuanza kurushwa na moja ya vituo vya televisheni nchini ambacho hata hivyo hakupenda kukitaja jina kwa sasa kwa madai ni mapema mno.
"Muda ukifika wa kuanika jina la kituo hicho tutaweka bayana, ila tumeshaanza mazoezi ili kuendelea na kurekodi tamthilia yetu ya 'Kipusa' tuliyoizindua kwa mashabiki mapema mwaka huu," alisema Kipemba.
Kundi hilo linaloongozwa na Ndimbagwe Misayo Thea, linaundwa na wakali kama Muhogo Mchungu, Bi Hindu, Swebe Santana, Bi Staa, Bi Terry, Kingwendu, Davina na wengine.

Anti Fifii atengeneza Documentary ya maisha yake, kurusha hewani


NYOTA wa filamu nchini, Tumaini Biligimana maarufu kama Anti Fifii yupo hatua ya mwisho kutengeneza filamu inayohusu maisha yake (documentary) ya kisanii tangu alipoanzia sanaa hiyo mkoani kwa Kigoma hadi alipofikia sasa akiwa ni mtunzi, mwandishi, muongozaji na mtayarishaji.
Akizungumza MICHARAZO, Anti Fifii alisema kuwa kazi hiyo anayoitengeneza kupitia kampuni yake ya See Breeze Art ipo mwishoni kukamilika kabla ya kuanza mchakato wa kusaka mdhamini ili kurushwa hewani katika kituo chochote cha runinga watakachokubaliana nacho.
"Namalizia kutengeneza 'documentary' ya maisha yangu kuanzia nilipotokea kwetu Kigoma hadi kufika nilipo sasa na itarushwa kwenye runinga yoyote baada ya kukamilisha mchakato wa kupata wadhamini," alisema Fifii.
Nyota huyo wa filamu za 'Copy', 'Sound of Death', 'Senior Bachelor', 'I Deserve It', 'Kaburi la Mapenzi', 'Kizungumkuti', 'Fake Smile' na 'Daddy' alisema makala hiyo ya filamu itaenda kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Aidha aliongeza kuwa, anafanya mchakato wa kuweka kwenye makala ya filamu, kitabu chake kilichopo mtaani kinachoitwa 'Migogoro ya Ndoa na Suluhisho Lake'.
"Baada ya kukamilisha jambo hili, nitaanza mpango wa kutengenezea makala ya kitabu changu ili irushwe pia kwenye runinga kwa lengo la kuisaidia jamii," alisema.
Anti Fifii alisema anashukuru namna Watanzania walivyokipokea kitabu chake hicho cha kwanza kutunga nje na sanaa yake ya uigizaji aliyoianza miaka 20 Kigoma.

Yanga majanga tena, Fc Lupopo yaikoromea usajili wa Twite

WAKATI sakata la Emmanuel Okwi hata halijapoa, uongozi wa Yanga upo kwenye msukosuko mwingine baada ya viongozi wa klabu ya FC Lupopo ya DR Congo kutua jijini na kudai kudhulumiwa fedha na klabu hiyo kupitia usajili wa Muyu Twite. Mmoja wa viongozi wa FC Lupopo, amesema Yanga walitakiwa kulipa dola 15,000 kama wamemuongezea mkataba Twite. "Lakini hawajafanya hivyo na nimekuja hapa viongozi wao Seif (Magari) na Abdallah (Bin Kleb) hawataki kulimaliza hili suala. "Mwanzo walisema hawataki maneno na sisi lakini mkataba unaonyesha mchezaji ni wetu na anacheza kwao kwa mkopo tu. "Kama waliona wanataka kuongeza mkataba lazima watulipe, tumewasiliana na chama chetu cha soka, ndiyo maana nimekuja hapa. "Lakini naona wanatuzungusha, tutasonga mbele hadi Fifa," alisema akisisitiza amefika hadi TFF lakini mambo yanaonekana ni magumu.
Bin Kleb alinukuliwa na kituo kimoja cha redio kuwa atatoa ufafanuzi mara baada ya kutua Dar kwani alikuwa safarini.

Yazidu, Mualgeria kuzipiga leo Kilimanjaro

http://2.bp.blogspot.com/-eY8HFEehT2A/VBHMHGVeWII/AAAAAAAAGPI/yiWoQtipENI/s1600/IMG_1831.JPG
Said Yazidu (kushoto) ma Dahou wakiinuliwa mikono jana walipomaliza kupima uzito
BONDIA mkongwe nchini Said Yazidu wa Tanzania na Djamel Dahou kutoka Algeria wanatarajia kuonyeshana kazi leo kwenye pambano la kuwania Ubingwa wa Dunia wa UBO katika pigano litakalofanyika mjini Moshi, Kilimanjaro.
Tayari Dahou ameshatua nchini tangu juzi tayari kwa pambano hilo la raundi 12 ambalo litafanyikia kwenye ukumbi wa YMCA, mjini Moshi na kusindikizwa na michezo mingine kadhaa ya utangulizi likiwemo la kuwania ubingwa wa UBO Afrika.
Mabondia wote wanaopanda ulingoni leo wamepimwa afya na uzito jana na wameonekana fiti tayari kurushiana makonde.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST), Anthony Rutta, pambano hilo la ubingwa wa Afrika litahusisha mabondia  Mtanzania Ali Ramadhan 'Alibaba' dhidi ya Mmalawi, Alick  Mwenda.
Ruta alisema mapambano yote hayo yameandaliwa na kampuni ya Green Hill Promotion na ni fursa nzuri ya kufufua ngumi za kulipwa katika mkoa wa Kiliamanjaro.
"Mpinzani wa Said Yazidu, Djamel Dahou ameshatua na anaelekea Kilimanjaro kwa ajili ya pambano lao la Septemba 12 kwenye ukumbi wa YMCA," alisema.
Rutta alisema pambano hilo litatanguliwa na michezo kadhaa ya utangulizi likiwamo la UBO Afrika la raundi 10 kati ya Alibaba na Mwenda wa Malawi.
Mengine ni kati ya Fatuma Yazidu dhidi ya Joyce Adam, Emmanuel Alex dhidi ya Ali Bugingo huku Pascal Bruno atazipiga na Cosmas Kibuga, George Allen atazipiga na Ssebo Husseni na Raymond Bwango dhidi ya Fadhil Mkinda.

Kivumbi la michuano ya Pool Taifa kuanza kutimka leo

http://3.bp.blogspot.com/-pOKKaQOaLGk/UXZdzG-D3LI/AAAAAAAAHHg/xHbyBbqikAk/s640/DSC_0052.JPGFAINALI za Taifa za mashindano ya mchezo wa pool ya 'Safari Lager National Pool Championship 2014' zinazinduliwa leo mjini Kilimanjaro huku wachezaji wa timu zote 17 na viongozi wao wamewasili jana salama kwa ajili ya fainali hizo.
Katibu mkuu wa chama cha mchezo huo taifa (TAPA), Amosi Kafwinga aliliambia gazeti hili mkoani hapa kuwa taratibu zote zinazohusiana na fainali za mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager zimekamilika.
Kafwinga alisema wachezaji wa timu zote zitakazoshiriki fainali hizo tayari wamewasili huku kila timu ikitamba kutwaa ubingwa huo.
"Tunawashukuru wadhamini wetu bia ya Safari Lager kwa kufanikisha timu zote kuwasili kwa muda mwafaka huku kila kitu kinachohusiana na fainali hizo ikiwamo zawadi za washindi kikiwa kimekamilika," alisema Kafwinga.
Kafwinga alizitaja timu ambazo zitashiriki fainali hizo na mikoa yao ikiwa kwenye mabano kuwa ni Blue Leaf (Lindi), Yakwetu (Pwani), Billiard (Mwanza), New Stend (Shinyanga), Topland (Kinondoni), Absome (Tanga) na Corner Kasarani (Manyara).
Nyingine ni Mashujaa (Ilala), Tiptop (Tabora), Bilele (Kagera), Mboya (Kilimanjaro), Mpo Afrika (Temeke), Anatory (Morogoro), Delux (Dodoma), Ngija Point (Iringa) na Break Point (Mbeya).
Kafwinga alisema bingwa wa fainali kwa upande wa timu atajinyakulia fedha taslim Sh. milioni 5, kikombe na medali 10 za dhahabu, wakati kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume) bingwa atazawadiwa Sh.500,000 na bingwa kwa upande wa wanawake ataondoka na Sh.350,000.
Naye nahodha wa mabingwa watetezi wa fainali hizo, Topland ya Kinondoni, Patrick Nyangusi akizungumza baada ya kuwasili mkoani hapa alisema lengo lao ni kutetea ubingwa wao na kurejea nao tena Dar es Salaam.
Nyangusi ambaye pia ni bingwa wa Afrika kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume), alisema hakuna timu ya kuwazuia kuchukua tena ubingwa huo kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
"Tumekuja  kutetea ubingwa wetu na tuna imani ya kurudi nao tena Kinondoni. Hakuna timu ya kutuzuia tumejiandaa vizuri, hivyo wadau wetu wa Kinondoni waondoe shaka tutawawakilisha vizuri na kurejea tena na ubingwa wetu," alisema Nyangusi.

Bayern Munich yapumua, Ribery arejea uwanjani

http://multimedia.pol.dk/archive/00430/Germany_Soccer_Bund_430303a.jpg
Franck Ribery
KLABU ya Beyern Munich imepumua baada ya wingawao Franck Ribery kuwa fiti baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu sasa.
Winga huyo anatarajiwa kuwa fiti kwa ajili ya mchezo wake wa msimu huu wakati timu yake itakapokwaana na VfB Stuttgart kesho Jumamosi.
Ribery amekuwa nje ya uwanja kwa muda kutokana na majeruhi yaliyokuwa yakimsumbua lakini sasa anaonekana kuwa fiti. 
Mabingwa hao watetezi wameanza kwa kusuasua msimu huu kuliko ilivyokuwa kwa msimu uliopita kufuatia sare ya bao 1-1 dhidi ya Schalke katika mchezo wao wa pili. 
Kwa sasa wasiwasi upo kwa kiungo mpya aliyesajiliwa kiangazi hiki Xabi Alonso ambaye alikosa mazoezi wiki hii kutokana na kuumia mguu na ndio kwanza maenaza kukimbia tena. 
Winga mahiri wa kimataifa wa Uholanzi, Arjen Robben naye pia amefanya mazoezi peke yake kutokana na majeruhi ya kifundo cha mguu wakati beki Rafinha naye akiwa bado nje kutokana na majeruhi ya goti.
Kurejea kwa Ribery ambaye mapema mwezi huu alitangaza kustaafu soka la kimataifa kunakuwa ahueni kubwa kwa Bayern kabla ya mechi yake ya kesho.

Ajabu! Wanne wakamatwa wakilima shamba uchi wa nyama

http://www.fullshangweblog.com/wp-content/uploads/2014/05/22a.jpg
Picha Haiuhusiani na habari hiyo
Na Faustine Fabian-Simiyu
JESHI  la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia watu wanne wa familia moja kwa tuhuma ya kukutwa wakilima uchi wa mnyama shambani kwa kile kinachodaiwa  kuwa ni imani za kishirikina.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Simiyu, Venansi Kimario alisema tukio hilo limetokea Sept. 2 majira ya saa 12 asubuhi katika kijiji cha Bushikwamala kata ya Kalemela wilayani Busega Mkoani Simiyu
Kimario alisema kuwa watu hao walikamatwa na jeshi la polisi alfajiri huko Bushigwamhala wakiwa wanalima kwenye shamba lao na walipohojiwa walidai kuwa walielekezwa na babu yao kipindi cha uhai wake kuwa wakilima uchi watapata mavuno  mengi.
Kamanda Kimario aliwataja waliokamatwa kuwa ni Makoye Kagoje (42), na mke wake Neema Kigwela (31) pamoja na watoto wao, mmoja wa kiume (15) na wa kike (12) majina yamehifadhiwa.
Aidha Kimario alisema watu hao pamoja na watoto wao wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kukutwa wakifanya vitendo vya ushirikina.
Babu yao alishafariki mwaka jana na aliwaambia kuwa wakilima wapo uchi watapata mavuno mengi, hivyo waliamua kufanya hivyo kutokana na wosia wa babu yao.
Alisema baada ya jeshi la polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema liliweza kufika katika eneo hilo na kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa wanaendelea kulima bila nguo.
Hata hivyo Kimario amewataka watu wasijishirikishe kwenye vitendo vya ushirikina na siyo kwamba ukilima uchi utapata mazao mengi tofauti na kufuata kanuni za kilimo bora, viongozi wa madhehebu ya dini na viongozi wa serikali tuwaelimishe watu waachane na imani za kishikina .