FAINALI za Taifa za mashindano ya mchezo wa pool ya 'Safari Lager National Pool Championship 2014' zinazinduliwa leo mjini Kilimanjaro huku wachezaji wa timu zote 17 na viongozi wao wamewasili jana salama kwa ajili ya fainali hizo.
Katibu mkuu wa chama cha mchezo huo taifa (TAPA), Amosi Kafwinga aliliambia gazeti hili mkoani hapa kuwa taratibu zote zinazohusiana na fainali za mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager zimekamilika.
Kafwinga alisema wachezaji wa timu zote zitakazoshiriki fainali hizo tayari wamewasili huku kila timu ikitamba kutwaa ubingwa huo.
"Tunawashukuru wadhamini wetu bia ya Safari Lager kwa kufanikisha timu zote kuwasili kwa muda mwafaka huku kila kitu kinachohusiana na fainali hizo ikiwamo zawadi za washindi kikiwa kimekamilika," alisema Kafwinga.
Kafwinga alizitaja timu ambazo zitashiriki fainali hizo na mikoa yao ikiwa kwenye mabano kuwa ni Blue Leaf (Lindi), Yakwetu (Pwani), Billiard (Mwanza), New Stend (Shinyanga), Topland (Kinondoni), Absome (Tanga) na Corner Kasarani (Manyara).
Nyingine ni Mashujaa (Ilala), Tiptop (Tabora), Bilele (Kagera), Mboya (Kilimanjaro), Mpo Afrika (Temeke), Anatory (Morogoro), Delux (Dodoma), Ngija Point (Iringa) na Break Point (Mbeya).
Kafwinga alisema bingwa wa fainali kwa upande wa timu atajinyakulia fedha taslim Sh. milioni 5, kikombe na medali 10 za dhahabu, wakati kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume) bingwa atazawadiwa Sh.500,000 na bingwa kwa upande wa wanawake ataondoka na Sh.350,000.
Naye nahodha wa mabingwa watetezi wa fainali hizo, Topland ya Kinondoni, Patrick Nyangusi akizungumza baada ya kuwasili mkoani hapa alisema lengo lao ni kutetea ubingwa wao na kurejea nao tena Dar es Salaam.
Nyangusi ambaye pia ni bingwa wa Afrika kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja (wanaume), alisema hakuna timu ya kuwazuia kuchukua tena ubingwa huo kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
"Tumekuja kutetea ubingwa wetu na tuna imani ya kurudi nao tena Kinondoni. Hakuna timu ya kutuzuia tumejiandaa vizuri, hivyo wadau wetu wa Kinondoni waondoe shaka tutawawakilisha vizuri na kurejea tena na ubingwa wetu," alisema Nyangusi.
No comments:
Post a Comment