STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, May 23, 2013

Shinji Kagawa aipa taji Borussia Dortmund

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg6qnMGGtEdfljwGsrw8rCwj7Az3DybB28VZLR1sfi1mmYGfENc0OAMvIk91kA-UOfpfSkxBVypEs7biZVLGjf9QjGPv1VGFTXYprResinbb3klLzzYOUfYrXyXIVyyW2YP87McxG1lYi4/s1600/Shinji+Kagawa+wallpapers.jpeg
Shinji Kagawa katika uzi wa Manchester United

 

http://ballsybanter.com/wp-content/uploads/2012/06/Cologne-v-Borussia-Dortmund-Shinji-Kagawa-cel_2739644.jpg
Shinji Kagawa alipokuwa akiichezea Borussia Dortmund

 

KIUNGO wa kijapani anayeichezea Manchester United, Shinji Kagawa ametoa turufu yake kwa klabu yake ya zamani Borussia Dortmund kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika fainali itakayochezwa Jumamosi nchini Uingereza.

Kagawa aliyetua Manchester United msimu uliopita akitokea Dortmund kwa dau la Pauni Milioni 12, alisema anadhani Borussia wataifunga Bayern Munich kwenye fainali za michuano hiyo itakayochezwa katika uwanja wa Wembley.

Pia mchezaji huyo alisema mafanikio iliyopata Dortmund msimu huu kwenye michuano hiyo ya Ulaya licha ya kupoteza ubingwa wa ligi ya Ujerumani, itawachochea Man Utd kufanya vyema kwa msimu ujao wa Ligi hiyo ya Mabingwa Ulaya.

Pamoja na kupoteza taji la nyumbani Dortmund wamekuwa na mafanikio makubwa katika michuano hiyo ya Ulaya licha ya wali kutopewa nafasi kubwa kama klabu nyingine zilizong'olewa au kama ilivyo kwa mahasimu wao Bayern Munich.

Kagawa aliyecheza kwa mafanikio makubwa katika klabu hiyo ya Ujerumani, alisema Dortmund inacheza kwa kujituma na ina wachezaji ambao wanajua wajibu wao uwanjani, licha ya kuimwagia sifa pia Bayern akidai ni timu kubwa na yenye bahati katika soka.

Rio Ferdinand asaini mkataba mpya Man Utd



BEKI mahiri wa Manchester United, Rio Ferdinand amesaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea klabu hiyo na kuzima tetesi kwamba huenda angeachana na klabu hiyo.
Rio mwenye umri wa miaka 34 alinukuliwa akisema kuwa anapenda kuendelea kuichezea timu hiyo na ndiyo maana amesaini mkataba huo mpya wa mwaka mmoja.
"Nimesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja," alisema.
Alihoji ni mchezaji gani ambaye asingependa kucheza kwenye klabu kubwa kama Manichester ambayo kila wikiendi zaidi ya watazamaji 74,000 wanakuwepo uwanjani kumshangilia.
Beki huyo aliteua Old Trafford mwaka 2002 akitokea Leeds kwa mkataba uliovunja rekodi wa Pauni Mil 30 na kwa kipindi chote ametwaa mataji 14 tofauti akiwa na kikosi hicho ambacho kinampoteza kocha wake kipenzi na aliyeiweka kwenye kilele cha mafanikio, Sir Alex Ferguson aliyetangaza kustaafu hivi karibuni.

Hali bado tete Mtwara, wananchi wasakwa nyumba kwa nyumba


Mwandishi wetu aliyepo Mtwara ametueleza kuwa hivi sasa baadhi ya wananchi wa eneo la Magomeni mkoani mtwara wamekimbilia katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara Lugula wakihofia usalama wao kutokana na vurugu za kuchomwa kwa nyumba zao pamoja na vibanda vya biashara zilizotokea leo asubuhi katika eneo hilo.

Maduka maeneo ya Magomeni yamechomwa moto ikiwamo pia mali za Askari Magereza . Mwanafunzi wa CHUNO amefikishwa hospitali Ligula na majeraha ya risasi mguuni.  
Mwanamke mwingine anayekadiriwa kuwa na miaka 25 mjamzito ameuawa kwa kupigwa risasi maiti ipo Ligula.




Kwa sasa ( jioni  hii) inaelezwa kuwa katika baadhi ya mitaa hali imetulia na ni idadi ndogo ya wananchi ndiyo inayoonekana wakitembea mitaani isipokuwa eneo la Magomeni ambako mabomu yanaendelea kusikika huku huduma za kijamii katika mji huo zikiwa zimesimama zikiwemo usafiri, huduma za kibenki na shule
Credit:Mpekuzi Huru pia unaweza kuchungulia www.mtwarakumekucha.blogspot.com kwa updates za kinachoendelea Mtwara.

Yanga yatahadharishwa Kagame Cup

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEj-wNTiS0urUo8wOMFwqWJ0vzpBnDlo2yooX-52M-cZ5UN2JNHrVtVLvE9KyyG8N_z649s5etRc43ySwdL5fZJVU8TBWcKPLFKt3GK_S7QVhss2NUWcUH1s8wiZjlN8jn6zPGsIdMulOxo/s1600/Yanga+4.jpg
Mabingwa watetezi wa Kagame, Yanga wakishangilia taji lao la mwaka jana
MABINGWA watetezi wa michuano ya Kombe la Kagame, ambao pia ni mabingwa wapya wa soka nchini Tanzania, Yanga wametahadharishwa kufanya maandalizi ya kutosha iwapo wanataka kutetea taji la michuano hiyo ambaya kwa mwaka huu itafanyika nchini Sudan.
Yanga imepangwa kundi C pamoja na timu za Express ya Uganda, Vital'O ya Burundi na Port Djibout na itaanza kibarua chake siku mbili baada ya kuanza kwa michuano hiyo kwa kuumana na Express.
Kutokana na ugumu wa michuano hiyo itakayoanza Juni 18 hadi Julai 2, wanachama wa Yanga wameanza kutahadharisha mapema viongozi na wachezajiu wao kwamba wajiandae vyema kwa ajili ya kuzidi kuwapa raha katika ushiriki wao nchini Sudan.
Ramadhani Kampira, aliyewahi kuichezea timu hiyo na kuongoza Chama cha Soka wilaya ya Kinondoni (KIFA) alisema kwa kuiangalia michuano hiyo ya Sudan ni wazi itakuwa migumu, hivyo Yanga wanapaswa kujiandaa vyema na wachezaji kwenda 'kukaza' ili warejee Tanzania na taji.
Kampira alisema, yeye binafsi anaamini Yanga ina kikosi kuzuri kinachoweza kuwapoa raha, lakini bila kujipanga ni wazi inaweza kuwasononesha wanayanga ambao wanachekelea taji la 24 la Ligi Kuu Tanzania.
"Yanga wanapaswa kufanya maandalizi mazuri, tuna hamu ya kuona klabu yetu inatwaa taji kwa mara ya tatu mfululizo na kwa mara nyingine tena nje ya ardhi ya Tanzania baada ya mara mbili kunyakua Uganda," alisema.
Kampira, alisema tahadhari hiyo haipo kwa Yanga tu, bali hata kwa watani zao Simba ambao wana rekodi ya kunyakua taji hilo mara 6 pamoja na AFC Leopards ya Kenya kwa sababu nao ni wawakilishi wa Tanzania.
"Wawakilishi wetu wote wanapaswa kujipanga, wasitarajie mteremko Sudan, klabu zilizopo kwenye michuano hiyo siyo za kubeza nazo zinahitaji taji kama ambavyo Yanga na Simba zitakuwa zikilitamani,' alisema.
Jumla ya timu 13 zinatarajiwa kuchuana katika michuano hiyo ya kusaka Klabu Bingwa wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambapo Simba wenyewe wamepangwa kundi A na timu za APR Rwanda, Elman ya Somalia na El Merreikh.
Kundi jingine la michuano hiyo ni lile la B lenye timu za Super Falcon ya Zanzibar, El Hilal na El Ahly Shandi za Sudan na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini.

Majambazi wajeruhi na kupora Mil 40 Dar

 Pichani ndio matundu ya risasi zilivyorindima kwenye kioo cha dereva (risasi tatu) ,mara majambazi hayo kufanikiwa kumjeruhi dereva sehemu ya bega na kufanikiwa kunyakua begi linalosadikiwa kuwa,lilikuwa na kiasi cha fedha shilingi milioni 40 na kutokomea nazo.
Pichani kulia ni Askari Usalama barabarani akichukuliwa maelezo yake kutokana kushuhudia tukio la ujambazi lililofanyika maeneo ya Sayansi mataa-Kijitonyama jijini Dar mapema leo mnamo majira ya saa tano kasoro.
 
Ambapo kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwepo eneo la tukio wanaeleza kuwa majambazi hao walikuwa wapatao wanne wakiwa wamepanda piki piki,ghafla wakasimama na kulizunguka gari aina Vitz yenye usajili wa namba T929 CCX (pichani chini) kwa haraka,mmoja wao akiwa na mashine gun na wengine walikuwa na bastola.
 
Mmoja wao alifyatua risasi hewani kumtaka dereva asimame na ashushe vioo vya gari yake,kufuatia hali ya utata wa majibishano ya muda mfupi majambazi hao waliifyatulia risasi kadhaa gari hiyo upande wa dereva, bahati mbaya wakamjeruhi sehemu ya bega,ndipo wakafanikiwa kuondoka na begi kubwa linalosadikiwa kuwa lilikuwa na kiasi cha fedha shilingi milioni 40 (kwa mujibu wa dereva aliempeleka majeruhi hospitali).

Mara baada ya majambazi hayo kutimka wasamalia wema wakamchukua dereva huyo aliyekuwa akigugumia kwa maumivu ya jeraha lake na kumtafutia tax na hatimae kumkimbiza hospitali ya Kairuki kwa huduma ya haraka.
 Baadhi ya watu wakijaribu kubadilshana mawazo kwa kulitafakari tukio hilo la ujambazi.
 Gari iliyokuwa imevamiwa na majambazi ikikokotwa na gari la polisi mara baada ya kushindwa kuwaka.

Polisi Moro waapa kurudi tena Ligi Kuu


Kikosi cha Polisi Moro. Rambow (wa kwanza kushoto mbele)

MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya Polisi Moro, Mokili Rambow, amesema licha ya timu yao kushuka daraja, lakini wanaamini watacheza tena Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2014-2015.
Rambow, ambaye ni nahodha wa timu hiyo, alisema wamekubali matokeo kwa timu yao kushindwa kuhimili vishindo vya ligi hiyo waliokuwa wakiicheza kwa mara ya kwanza waliposhuka daraja msimu wa 2008-2009 akidai kuwa ilichangiwa na 'ushamba' wa ligi kabla ya kuzinduka duru la pili wakiwa wameshachelewa.
Akizungumza na MICHARAZO, Rambow alisema kushuka kwa timu yao ni pigo na jambo linalowaumiza karibu wadau wote wa klabu hiyo ikizingatiwa waliipigania kuirudisha ligi kuu kwa miaka kadhaa, hata hivyo hawana jinsi zaidi ya kujipanga upya ili kurudi katika ligi hiyo kwa msimu ujao.
Mchezaji huyo ambaye ameifungia mabao kadhaa timu hiyo akishirikiana na wachezaji wenzake, alisema Polisi kwa sasa wanafanya tahmini kabla ya kujiopanga kwa ligi Daraja la Kwanza msimu ujao ambapo aliapa kwamba ni lazima watarejea ligi ya msimu wa 2014-2015.
"Tunajipanga kwa ajili ya kurudi ligi kuu, tunajua ni kazi pevu lakini tutafanhya kila njia kurudi Ligi Kuu kwa kweli tumeumia mno kushuka tulipotoka," alisema Rambow.
Polisi Moro, imemaliza ligi ya msimu huu waliyoicheza baada ya kupanda toka daraja la kwanza, ikiwa na pointi 25 sawa na Toto Africans na kuungana na African Lyon waliotangulia mapema wakiwa na pointi 22 tu.
Katika duru la kwanza Polisi walitolewa nishai na kuambulia pointi nne tu ikiwa na kocha wao maarufu, John Simkoko kabla ya kuachana naye na kumpa jukumu hilo nyota wa zamani wa Yanga, Pan African na Taifa Stars, Mohammed Rishard 'Adolph' aliyeipa jumla ya pointi 21, lakini hazikuwasaidia kuwaokoa wasishuke.

Bunge laahirishwa tena, kisa sakata la Mtwara

http://dewjiblog.com/wp-content/uploads/2013/02/8517823001.jpg
Spika wa Bunge, Mhe. Anna Makinda
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Anna Makinda ameliahirisha tena bunge leo asubuhi ili kupisha kamati ya uongozi ya Bunge iendelee kukutana ili kutoa maamuzi na tamko kuhusu vurugu za Mtwara.
Bunge hilo jana pia liliahirishwa kutokana na sakata hilo ambalo lilijitokeza mapema jana na kusababisha mtu mmoja kufariki dunia na uharibifu mbalimbali kutokea ikiwemo kuchomwa moto nyumba za viongozi wa serikali,chama cha mapinduzi na nyumba ya mwandishi wa habari wa TBC.
Pia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini umesimamishwa kwa muda mpaka ufumbuzi wa tatizo la vurugu hizo utakapopatiwa suluhisho.

Kesho bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Afrika Mashariki itajadiliwa.
 

Wanachuo Mwl Nyerere kutembelea yatima

UMOJA wa Wanafunzi Wanachama wa Umoja wa Mataifa Tawi la Mwalimu Nyerere (UNC MNMA) unatarajia kuwatembelea watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwenye kituo cha New Hope Familiy kilichopo Ungindoni Maweni, Kigamboni Jijini Dar es Salaam siku ya Jumapili ikiwa ni sehemu ya kuwaaga wanafunzi wanaomaliza chuo hicho hivi karibuni.
Hayo yamebainishwa na Katibu aliyemaliza muda wake hivi karibuni Selemani Msuya wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Alisema wanachama wa UNC wanaomaliza na wale ambao wanaendelea walikubaliana kwa pamoja juu ya kuwatembelea watoto hao ikiwa ni moja ya malengo yao kushirikiana na jamii iliyokaribu na chuo chao.
Msuya alisema moja ya malengo ya vijana wanachama katika umoja wao wao ni kuhakikisha kuwa wanashirikiana na jamii iliyokaribu nao ikiwa ni kwakushiriki moja kwa moja katika shughuli mbali mbali pamoja na kutoa msaada.
“Sisi vijana wanachama wa UNC kupitia chuo cha Mwalimu Nyerere tumeamua kufanya mahafali ya kuwaaga wenzetu kwa kushiriki chakula  cha mchana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwani tunaamini kuwa  tutakuwa tumefanya jambo nzuri kwetu na kwa watoto hao,” alisema
Katibu huyo aliyemaliza muda wake ambaye kwa sasa ni mjumbe wa kamati ya utendaji alisema katika ziara hiyo wanatarajia kushiriki chakula cha mchana, kutoa msaada wa vifaa vya shule na kusomea pamoja na kucheza pamoja.
Alisema wana UNC wamejitolea kuchangia kiasi kidogo kulingana na uwezo wao ili kuhakikisha kuwa wanafanya sherehe hiyo ya kuwaagana kwa kushirikiana na watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu.
Msuya huyo alisema tukio lingine ambalo litafanyika katika mahafali hayo ni kwa watoto hao ambao wanaishi katika mazingira magumu kuwapatia vyeti wahitimu ambao wanamaliza chuo hivi karibuni.
Katibu huyo ambaye amemaliza muda wake amewataka watu mbalimbali ambao wanatambua changamoto zinazowakabili watoto ambao wanaishi katika mazingira magumu kutoa misaada yao ili waweze kuunganisha na hicho kidogo walichonacho kuwapatia watoto hao.

Sheha amwagiwa tindikali Zanzibar

 
Sheha aliyemwagiwa tindikali na watu wasiojulikana akiwa hospitalini alipolazwa kwa matibabu
SHEHA wa eneo la Tumondo, visiwani Zanzibar, Mohamed Omary Said, amemwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana na hivyo kupata maumivu makali sehemu yake ya kifua na jicho kuumia pia.

Sheha huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Mnazi mmoja mjini Unguja ambapo alipatiwa matibabu ya dharura.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mukhadam Khamis, amesema chombo kilichotumika kumwagia tindikali Sheha huyo kilipatikana eneo la tukio na kwamba polisi imekichukua kwa kukichunguza kitaalam ili kugundua aliyekuwa akikitumia kwa kuangalia alama za vidole.

Sheha huyo alimwagiwa tindikali jana usiku wakati alipotoka nje ya nyumba yake kuchota maji na ndipo mhalifu huyo alipomwagia tindikali na kwamba hakuweza kumtambua.
Miezi michache iliyopita Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga naye alimwagiwa tindikali kabla ya imamu wa msikitini mjini humo kuuwawa kwa kukatwa mapanga sikui chachje baada ya matukio ya viongozi wa Kikristo kupigwa risasi na watu wasiojulikana.