STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, November 28, 2012

JB M'PIANA ATUA DAR, AAHIDI SHOO KALI IJUMAA LEADERS


JB Mpiana akizungumza mna Waandishi Dar es Salaam leo

MWANAMUZIKI nguli wa dansi Afrika, JB Mpiana ametua jijini Dar es Salaam juzi tayari kwa maonyesho kadhaa, likiwamo lile la uzinduzi wa albamu ya Mashujaa Band inayokwenda kwa jina la Risasi Kidole, litakalofanyika Ijumaa katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.
Kabla ya shoo hiyo ya Ijumaa, JB Mpiana ambaye amekuja na kundi lake zima la Wenge Musica BCBG, likiwahusisha wanamuziki wake za zamani na wapya, atauwasha moto jijini Arusha kesho kabla ya kufanya kweli jijini Mwanza Jumapili.
Akizungumza katika Hoteli ya Double Tree iliyopo Masaki, Dar es Salaam, JB Mpiana ameahidi kutoa shoo ya aina yake ambayo anaamini itakonga nyoyo za Watanzania.
Alisema kuwa amefurahisa sana kuja Tanzania kwa mara nyingine, ikiwa ni pamoja na mapokezi aliyoyapata, akiahidi kutoa burudani ya nguvu kwa Watanzania kuwalipa mapokezi waliyomwonesha.
 “Nina imani waandaaji wamefanya maandalizi ya kutosha, nimekuja na wanamuziki wangu wote 25, nimekuja na vifaa vyangu vyote vilivyopo katika kundi langu, ili kutoa burudani ya kutosha kwa Watanzania.
 “Nimewaletea albamu inayojulikana kwa jina la Biloko (chakula), watanzania wajiandae kula, yaani kupata burudani ya nguvu kutoka kwangu na kundi langu,” alisema JB Mpiana.
Kati ya wasanii aliokuja nao, alisema wapo wale wa zamani aliokuwa nao enzi hizo ndani ya kundi lake hilo lilipoanza kutamba katika anga ya muziki, na wengine wapya ambao wapo fiti.
Katika programu yake hapa nchini, amesema atapiga nyimbo zake za zamani na mpya ili kuwapa watanzania fursa ya kupata vionjo vya zamani na vipya, kuweza kupima ubora wa kazi hizo.
Akizungumzia muziki wa Tanzania, amewataka wasanii wa hapa nchini kujituma na kuzipenda kazi zao na kuiheshimu waweze kufanikiwa katika kazi zao hizo.
Juu ya kiongozi wa safu ya unenguaji, alisema safari hii inaongozwa na mwanadada Zambrota, ikiwa ni baada ya kufariki kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Monica.
 “Nimefurahi sana kuja Tanzania kwa mara nyingine, wapenzi wa burudani wajiandae kupata shoo ya nguvu kutoka kwa JB Mpiana,” alisema mkali huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya QS Muhonda, Joseph Muhonda, waratibu wa maonesho hayo, amesema kuwa ni matarajio yao wakazi wa Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, watafurahia shoo hiyo kutoka kwa JB Mpiana na Mashujaa kutokana na maandalizi ya nguvu waliyofanya, akiwataka wakazi wa maeneo hayo, kujitokeza kwa wingi.
Alisema kuwa katoka onesho la JB Mpiana jijini Arusha, atatumbuiza katika ukumbi wa Triple A kuanzia saa tatu usiku, wakati Desemba Mosi atakuwa katika ukumbi wa Villa Park kuanzia saa tatu usiku.
 “Maandalizi yote yapo sawa, kila kitu kimekamilika, tuliahidi JB Mpiana anakuja na kweli amekuja kama mlivyomuona,” alisema na kuongeza kuwa JB Mpiana atasindikizwa na wasanii wa Bongo Fleva kama H Baba, MB Doggy, Ney wa Mitego na wengineo.

TENGA ASEMA TFF, SERIKALI KUKUTANA KUMALIZA UTATA WA TRA

Tenga


SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, wanatarajiwa kukutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kuzungumzia mustakabali mzima wa suala la makato katika michezo mbalimbali.
Hatua hiyo inafuatia TRA kuzifunga akaunti za udhamini wa ligi hiyo kama shinikizo kwa TFF  kulipa makato ya kodi kwenye mishahara ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’ tangu kipindi cha kocha Mbrazil Marcio Maximo kwa madai kwamba imekuwa haikatwi kodi za mishahara ya makocha na hivyo kufikia sh milioni 157,407.968.00.
Rais wa TFF, Leodger Tenga amesema leo kwamba kitendo walichokifanya TRA ni jambo la heri kwani kinaonyesha majukumu ya Serikali katika soka.
Alisema ukaribu uliopo sasa baina ya Serikali chini ya Rais Kikwete na soka ni mkubwa kutokana na ukweli kwamba  inachangia kwa kiasi kikubwa kulipa mishahara ya makocha wa timu za Taifa.
Alisema suala hilo linahitaji mazungumzo baina ya pande hizo ili kuweza kulipatia ufumbuzi na hakuna haja ya kuilaumu TRA kwa sababu inafuata taratibu zilinazostahili kwa mujibu wa kanuni.
 “Hawana njia nyingine ya kufanya hivyo ufumbuzi ni sisi ni kukutana na Wizara na TRA ili kulizungumza hili na katika siku mbili hizi tunarajiwa kukutana,”alisema
Tenga aliongeza kuwa TFF haina uwezo wa kulipa fedha hizo na kwamba hela zilizochuliwa si za Shirikisho hilo bali ni za ligi kuu Bara ambazo zimetolewa na wadhamini wake, kampuni ya simu za mkononi,Vodacom kwa maelekezo maalum.
 “Ni jambo nyeti na lazima lifanyiwe kazi, hatuwezi kumlamu mtu na nimatumaini tutakapoketi pamoja tutapata ufumbuzi,”alisema.
Aidha, Tenga alisema wanatarajia kuzungumzia suala la makato ya michezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na vilabu kwa muda mrefu.
 “Changamoto za namna hiyo tumekuwa tukizifanyia kazi kwa muda mrefu na ndiyo maana tangu mwaka 2005 asilimia ya makato ya TFF imekuwa ikipunguzwa, nadhani ni kuendelea kuwa na subira.

SIMBA WAMLILIA SHARO MILIONEA


Na Ezekiel Kamwaga
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa aliyekuwa msanii maarufu wa muziki na filamu, Hussein Ramadhani Mkiety, maarufu kwa jina la Sharo Milionea, kilichotokea jana usiku mkoani Tanga.

Kwa niaba ya klabu ya Simba na kwa niaba yake binafsi, Mwenyekiti anapenda kutuma salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu kutokana na msiba huu mkubwa sana si kwao pekee bali kwa taifa zima la Tanzania.

Sharo Milionea hakuwa msanii wa kawaida. Yeye ni miongoni mwa kizazi kipya cha vijana wa Kitanzania walioamua kutafuta maisha kwa kutumia vipaji walivyopewa na Mungu. Yeye alijitumbukiza zaidi katika uchekeshaji na baadaye akaonyesha uwezo mkubwa katika fani ya muziki.

Sharo alikuwa maarufu kiasi kwamba makampuni makubwa yalikuwa yameanza kumtumia kwenye matangazo yao ya kibiashara. Hii ilionyesha kwamba makampuni yalibaini faida itakayopatikana kwao kwa kumtumia msanii huyu ambaye bado alikuwa na heshima kubwa kwenye jamii kutokana na haiba yake na uwezo wake kwenye kazi alizokuwa akifanya.

Msiba huu umekuwa pigo kubwa kwa tasnia ya filamu ambayo bado inaomboleza vifo vya wasanii kama Steven Kanumba, Mlopelo na John Steven Maganga, waliofariki dunia mwaka huu pia.

"Ifahamike kwamba Sharo Milionea alikuwa miongoni mwa wasanii wa Kitanzania waliotuma maombi Simba ya kutaka kushiriki kwenye mchakato wa kutengeneza wimbo rasmi wa klabu ya Simba. Yeye alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiumizwa na ukweli kwamba klabu kama Simba inashindwa kufanya biashara ya kuuza nyimbo zake ilhali wanunuaji wapo," alisema Rage.

Kwa klabu ya Simba, namna pekee ya kumuenzi marehemu ni kufanyia kazi mambo ambayo alikuwa akitushauri kwenye eneo la biashara. Ni matumaini yetu kwamba iwapo tutafanya lile alilokuwa akitushauri, atakuwa mwenye amani huko alikotangulia mbele ya haki.

Rage amewaomba wasanii wa tasnia ya filamu na muziki kuwa watulivu na wenye subra kwenye kipindi hiki kigumu kwao. Kila kitu katika maisha ya wanadamu kinapangwa na Mwenyezi Mungu na ndiyo maana Waswahili wana msemo kuwa Kazi ya Mungu haina makosa.

Mola na ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu Hussein Ramadhani Mkeity

(Kamwaga ni Ofisa Habari wa Simba SC).

SUPER D APANIA KUPELEKA VIJANA WAKE OLIMPIKI 2016

Kocha wa Kimataifa wa Mchezo wa Masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' akiwa katika picha ya pamoja na vijana waliojitokeza katika mazoezi ya ngumi ufukwe wa GYKHANA Dar es salaam jana Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com


KLABU ya ngumi ya Ashanti Ilala imeota kuwa moja ya klabu itakayotoa wawakilishi katika michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2016  nchini Brazil.

Klabu hiyo ambayo kwa sasa inaundwa na chipkizi 18 pamoja na mabondia wakongwe imepania kufanya hivyo huku ikijitapa kuwa itaanza kufanya maajabu kupitia mashindano ya taifa ya mchezo huo yatakayofanyika Januari mwakani.

Akizungumza na gaazeti hili Dar es Salaam jana, Kocha wa ngumi wa klabu ya Ashanti  pamoja na timu ya Mkoa wa Ilala Kimichezo Rajabu Mhamila 'Super D' alisema kwa sasa klabu yake imejikita katika maandalizi kabambe kuhakikisha inaingiza mabondia wengi katika timu ya taifa ambao baadaye wataingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi za kufuzu kucheza Olimpiki.


Alisema tayari jumla ya vijana 18 wanajifua katika Ufukwe wa Gymkhana Dar es Salaam kwa ajili ya mapambano mbalimbali ikiwemo ya ubingwa wa taifa ambayo yanaandaliwa na Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT).


Alisema vijana wengi waliopo kwenye klabu hiyo ni wenye umri chini ya miaka 12 na chini ya miaka 20 ambapo amewataja kuwa umri huo ni mzuri kwani kijana atakuwa mwepesi wa kuelewa kile ambacho atakuwa anafundishwa na makocha wake
Super D ambaye anafundisha kwa kutumia mbinu mbalimbali zikiwemo kwa njia ya DVD ambazo zinatoa mwanga kwa mchezaji kujua mchezo na kufahamu zaidi mbinu mpya zitumiwazo na mataifa mbali mbali Duniani.
Wakiwemo mabondia bingwa wa dunia kama Manny Paquaio,Floyd Maywether,Amir Khani, Mohamed Ali ,Mike Tayson na wengine wengi wanaotamba na waliotamba katika mchezo huo wa masumbwi Duniani
Super D ametoa wito kwa makampuni mbalimbali kujitokeza kutoa sapoti ya mchezo wa masumbwi kwani ndio mchezo pekee unaoweza kututoa kimasomaso watanzania tukafurahi

YOMBAYOMBA KUPAMBANA NA 'GOGO POA' KUCHANGIA WAGOJWA WA MOYO

 Saidi Omari 'Gogo Poa' .kushoto na Rajabu Mhamila'Super D' 
MABONDIA wa zamani walioiletea nchi Medali katika mashindano ya All Africa Games na Jumuiya ya Madola miaka ya 1998, Michael Yombayomba na Said Omari 'Gogo Poa' wamejitolea kupanda ulingoni na kutwangana kwa ajili ya kuchangia watoto wenye matatizo ya Moyo.





Yombayomba ambaye alitwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Jumuia ya Madola katika miaka hiyo ya 1998 na Gogo Poa wameamua kutwangana ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa watoto hao huku wakisisitiza wadau kuunga mkono tukio hilo.


Akizungumza na gaazeti hili Gogo Poa alisema pambano hilo litafanyika Januari 25 mwakani ambapo pia litasindikizwa na mapambano ya mabondia mbalimbali wenye viwango vya juu nchini.


"Tumeguswa sana na tatizo hili la watoto wanaougua ugonjwa wa moyo ambao wengi wao hukosa fedha kwa ajili ya matibabu hivyo sisi kama sehemu ya jamii tutahamasisha uchagiaji wa fedha kwa kujitolea kupanda ulingoni na chochote kitakachopatikana itakuwa ni sehemu ya mchango wetu,"alisema Gogo Poa.

Aliwaomba wadhamini na wadau mbalimbali kujitokeza kuzamini mchezo huo ambao una tija ya kuchangia watoto hawo kwani ata wao walikuwa watoto ndio mana wamekuwa katika afya nzuri na kucheza mchezo huo na kuiletea sifa taifa hili kwa kuleta Medali

Hivyo na watoto hawo wanatakiwa wawe na AFya njema ili wapate kuja kurithi nyayo zetu bila afya ya mtoto michezo yote akuna kwa kuwa vipaji vingi vinangaliwa ukiwa mtoto

Zahoro Pazi amfagilia Kim kuchezesha vijana Kili Stars

Zahoro Pazi (kushoto) akiwa uwanjani akichuana na Jerry Santo aliyekuwa Simba enzi hizo
MSHAMBULIAJI mkali wa Azam, Zahoro Pazi, amemfagilia kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen anayeinoa timu ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars katika michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Uganda, kwa uamuzi wake wa kuwaamini vijana katika kikosi cha timu hiyo.
Pazi, anayefahamika kwa jina la utani kama 'Cristiano Ronaldo', alisema kitendo kilichofanywa na Kim kuwapanga wachezaji karibu wote vijana ndio chachu ya ushindi wa mabao 2-0 iliyopata mbele ya Sudan na kuwataka watanzania wamuunge mkono kwani jambo hilo litailetea manufaa Tanzania siku za baadae.
Alisema kupewa nafasi kwa vijana kunawapa nafasi ya kupata uzoefu na kuondoka woga na hivyo kuweza kulitumikia taifa wakiwa Taifa Stars kama mashujaa wa Tanzania jambo ambalo limekuwa likililiwa kwa muda mrefu.
"Kwa kweli nimefurahishwa na uamuzi wa kocha Kim kuwapanga karibu vijana wote katika kikosi cha Kili Stars, kwani nadhani ndio chachu ya ushindi na pia italisaidia taifa kuweza kufanya vema zaidi kwani vijana hao ndio wanaoweza kuivusha Tanzania katika michuano mikubwa zaidi ya kimataifa," alisema.
Pazi, mtoto wa kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Idd Pazi 'Father' alisema kilichofanywa na Kim kinawatia moyo wachezaji vijana kama yeye ambao walikuwa wakipuuzwa Stars ilipokuwa chini ya Jen Poulsen aliyetimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Kim.
"Hata mimi ambaye nimekuwa nje ya timu ya taifa tangu Maximo alipoondoka nimepata moyo na kuamini nikijibidiisha naweza kurejea tena Stars," alisema.
Aliongeza kwa kuwataka Watanzania wamuunge mkono kocha huyo toka Denmark kwa madai anaonekana ni kocha mwenye mipango na maendeleo ya mbali kaa alivyokuwa Maximo hivyo aachiwe afanye kazi kwa raha zake na kwa muda mrefu ili Tanzania ivune matunda yanayoanza kuonekana.
Kilimanjaro Stars leo inatarajiwa kutupa karata yake ya pili katika michuano hiyo ya Chalenji kwa kuvaana na Burundi, ikiwa inachekelea ushindi iliyopata dhidi ya Sudan kwa mabao ya John Bocco 'Adebayor'.

Kivumbi cha Ligi ya England kuendelea leo, Aston Villa yaizamisha Reading

WAKATI vinara wa Ligi Kuu ya England, Manchester United ikitarajiwa kushuka dimbani leo kuvaana na West Ham ili kujihakikishia ufalme wa kileleni, Aston Villa yenyewe jana iliizamisha Reading kwa bao 1-0 huku kocha Harry Redknapp akianza kibarua chake QPR kwa kuambulia suluhu dhidi ya Sunderland.
Manchester itaavana na wagoinga nyundo hao kwenye dimba lao la nyumbani la Old Trafford, ikiwa ni siku chache tangu ilipoiizamisha QPR mabao 3-1.
Mashetani hao wekundu wapo kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 30, moja dhidi ya mabingwa watetezi, Manchester City ambao nao leo watashuka dimbani ugenini kuvaana na Wigan, huku LIverpool itakaribishwa na Tottenham na Arsenal kupambana na Eveton.
 Mechi nyingine zinazochezwa leo ni pambano la Southampton itakayovaana na Norwich City, Stoke City dhidi ya Newcastle United, Swansea City itakayopambana na West Bromwich na Clesea itakayoikaribisha Fulham.
Katika mechi zilizochezwa jana kwenye mfululizo wa ligi hiyo maarufu, Aston Villa iliizamisha Reading kwa kuilaza bao 1-0 lililotupiwa kambani na mshambuliaji wake, Christian Banteke katika dakika ya 80 kwa pasi ya Westwood.
Nayo QPR ikiwa chini ya kocha wake mpya, Harry Redknapp ililazimisha suluhu ugenini dhidi ya wenyeji wao Sunderland na kuifanya timu hiyo inayoburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo kufikisha pointi tano.
ratiba kamili ya mechi zinazochezwa leo katiika ligi hiyo ya England ni kama ifuatavyo:

 Chelsea v Fulham 19:45

  • Everton v Arsenal 19:45
  • Southampton v Norwich 19:45
  • Stoke v Newcastle 19:45
  • Swansea v West Brom 19:45
  • Tottenham v Liverpool 19:45
  • Man Utd v West Ham 20:00
  • Wigan v Man City
  • Wachezaji  Nathan Baker wa Aston Villa (kulia) na Jason Robert wakichuana katika pambano lao la jana.



Stars vitani na Burundi leo, Uganda yafuzu

Wachezaji wa timu ya Kilimanjaro wakitania kwenye mazoezi ya timu yao, ambapo jioni ya leo inavaana na Burundi

Na Somoe Ng'itu, Kampala
WAKATI wenyeji Uganda jana walikuwa wa kwanza kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Chalenji baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Ethiopia, timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) itatupa karata yake ya pili katika mechi ya kundi B dhidi ya Burundi leo.
Goli pekee kutoka kwa Brian Umony liliwafanya Uganda kufuzu baada ya kufikisha pointi sita katika kundi A, huku Kenya ambayo ilishinda 2-0 mapema jana dhidi ya Sudan Kusini ikishika nafasi ya pili baada ya mechi mbili. Ethiopia pia ina pointi tatu lakini iko katika nafasi ya tatu kutokana na tofauti ya magoli. Katika mechi ya kwanza Uganda ilishinda 1-0 dhidi ya Kenya, wakati Ethiopia iliifunga Sudan Kusini 1-0 katika siku ya ufunzi wa michuano hiyo inayofanyika kwenye Uwanja wa Namboole hapa Kampala.
Baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Sudan katika mechi ya ufunguzi, Kilimanjaro Stars itashuka dimbani leo kuikabili Burundi kuanzia 12:00 jioni.
Burundi ndio kinara wa kundi hilo kutokana na kuwa na magoli mengi ya kufunga ambapo alipata ushindi wa 5-1 dhidi ya Somalia.
Akizungumza na gazeti hili jana baada ya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Makerere, Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, alisema kwamba wachezaji wake wako vizuri na amejipanga kuikabili Burundi na hatimaye kuibuka na ushindi.
Kim alisema kwamba Burundi ni timu inayotumia nguvu lakini wachezaji wake wamejiandaa kutumia kasi waliyonayo kuwatoka wapinzani wao ambao wengi wana miili mikubwa wakiongozwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Selemani Ndikumana.
Alisema kuwa mashindano ni magumu na hakuna timu ya kuidharau hivyo amewaandaa wachezaji wake kupambana kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
"Kila mchezo tutaingia na mbinu tofauti, nimewasoma Burundi wakati walipokuwa wanacheza na Somalia...naamini tutawafunga ili tuongoze kundi letu," alisema Kim ambaye hii ni mara yake ya kwanza kufika Uganda na kuongoza timu kwenye michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea.
Aliongeza kwamba anafurahishwa na kikosi chake kucheza kwa kuelewana na anaamini kitafanya vizuri mechi zote zinazofuata na kutimiza malengo ya kurejea nyumbani na ubingwa.
Nahodha wa timu hiyo, Juma Kaseja, aliliambia gazeti hili kwamba jitihada za kila mchezaji ndiyo zinafanikisha matokeo mazuri na anaamini watasonga mbele katika hatua inayofuata.
Kaseja alisema kwamba mashindano haya yana upinzani na wao wamejiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.
"Ni mashindano ambayo tunakutana wachezaji tunaofahamiana hasa Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda, yana ushindani na yanatufanya tujifunze zaidi kila mara, mwalimu aliiangalia Burundi hivyo ametupa maelekezo ya nini cha kufanya ili tufanye vizuri," alisema Kaseja.
Aliongeza kwamba ushindi walioupata katika mechi ya kwanza haukuwa wa kubahatisha na wanaamini mwaka huu watafika mbali.
Aliwataka mashabiki wa Tanzania waendelee kuwaombea ili wao wafanye kile walichotarajia na kurudi nyumbani na heshima.
Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) itakamilisha mechi za hatua ya makundi Jumapili kwa kuivaa Somalia kuanzia saa nane mchana kwenye uwanja utakaotajwa hapo baadaye.
Mchezo mwingine utakaochezwa leo mchana ni kati ya Somalia na Sudan ambazo zote zilipoteza mechi zao za kwanza.

SHARO KUZIKWA LEO, NCHI NZIMA NI MAJONZI MATUPU

Sharo Milionea enzi za uhai wake
WAKATI salamu za rambirambi zikiendelea kumiminika kufuatia kifo cha msanii wa vichekesho nchini, Hussein Mkiety maarufu kama Sharomilionea, aliyefariki dunia katika ajali ya gari juzi usiku, nyota huyo atazikwa leo saa 10:00 jioni.
Kwa mujibu mjomba wa marehemu, Omar Fundikira, Sharo atazikwa nyumbani kwao katika kijiji cha Lusanga wilayani Muheza mkoani Tanga.
Sharo alifariki dunia alifariki kufuatia ajali ya gari iliyotokea eneo la Maguzoni, Songa, Muheza.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa mkoa wa Tanga, Constatine Masawe, Sharo alikuwa peke yake garini wakati ajali hiyo ikitokea na mwili wake uko katika hospitali ya Teule, Muheza.
Kamanda Masawe alisema Sharo akiwa anaendesha gari namba T478 BVR Toyota Harrier akitokea Dar es Salaam kwenda Muheza na alipofika eneo hilo gari lake liliacha njia na kupinduka mara kadhaa na kusababisha kifo chake.
Taarifa za kifo chake kilianza kuzagaa kwa watu kutumiana ujumbe wa simu kabla ya kuthibitishwa na Kamanda Constantine.
Umati wa watu ulikusanyika katika hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza kujaribu kuushuhudia mwili wa muigizaji huyo aliyepata umaarufu mkubwa kutokana na vibwagizo vyake vya "Umebugi meen!", "kamata mwizi meen!" na "Ooh mamma!"
Mwandishi wetu ambaye alifika katika chumba cha maiti katika hospitali hiyo alishuhudia umati wa watu ukisubiri kuingia ndani ya chumba hicho kuuona mwili wa msanii huyo aliyeumia vibaya kichwani na kifuani.
Kutokana na hali hiyo mhudumu wa chumba cha maiti aliyejitaja kwa jina la Mhusa na daktari wa hospitali hiyo aliyejitaja kwa Kibaja walipata wakati mgumu kuwazuia watu waliofurika wakiwamo wanafunzi wanaosomea udaktari katika hospitali hiyo.
Baadaye mwandishi wetu alifika nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Lusanga ambapo alikuta vilio kutoka kwa ndugu na jamaa huku umati wa watu ukiwa umefurika nyumbani hapo pia.
Miongoni mwa wasanii waliokuwapo nyumbani hapo akiwamo mkongwe aliyekuwa akifanya naye kazi nyingi, Amri Athuman maarufu King Majuto, alisema kuwa amesikitishwa mno na msiba huo.
Majuto alisema anakosa maneno ya kusema kutokana na ukubwa wa msiba huo kwake kwa kumpoteza kijana aliyemsifu kuwa ni mchapakazi aliyekuwa na usongo wa mafanikio.
Mkogwe huyo huyo alisema kifo cha Sharo ni pigo kwa wasanii wote hususan yeye mwenyewe ambaye alikuwa ni meneja wake katika kazi zao za kila siku.
“Kusema kweli sioni wa kuziba pengo hili… ni mtu ambaye nilimzoea sana na sijui ni kipi cha kusema ila Mwenyezi Mungu anajua zaidi yetu,” alisema Majuto.
Rambirambi pia zilitoka katika serikali wilayani Muheza ambapo ilisema imeshtushwa mno na kifo cha Sharo kutokana na umahiri wake na kuifanya kazi ya usanii kuwa ajira kama zilivyo ajira nyingine.
Mkuu wa wilaya ya Muheza, Subira Mgalu alisema kuwa kimsingi msanii huyo amekuwa mfano wa kuigwa na wasanii wengine nchini kutokana na kuithamini na kuipenda  kazi yake na hivyo kuwa mbunifu siku hadi siku.
"Kwa kweli marehemu Sharo alikuwa ni mbunifu katika kazi yake na aliifanya sanaa kuwa ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, kweli huu ni mfano wa kuigwa na vijana na kupitia yeye wengi wameweza na wanaweza kujitambua kuwa wana vipaji ambavyo wakivitumia vitawaondoa katika umasikini. Inasikitisha kwamba ametutoka mapema sana kipindi ambacho wapenzi wa sanaa na watoto walishamzoea kumwona na kumsikia," alisema Mgalu.
Naye mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa msanii huyo.
Katika taarifa yake iliyotolewa na afisa habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, Rage alisema kwa niaba ya klabu ya Simba na kwa niaba yake binafsi, anapenda kutuma salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote wa marehemu kwa kuwa na msiba huu ni mkubwa sana si kwao pekee bali kwa taifa zima la Tanzania.
Taarifa hiyo ilisema: "Sharo Milionea hakuwa msanii wa kawaida. Yeye ni miongoni mwa kizazi kipya cha vijana wa Kitanzania walioamua kutafuta maisha kwa kutumia vipaji walivyopewa na Mungu. Yeye alijitumbukiza zaidi katika uchekeshaji na baadaye akaonyesha uwezo mkubwa katika fani ya muziki.
"Sharo alikuwa maarufu kiasi kwamba makampuni makubwa yalikuwa yameanza kumtumia kwenye matangazo yao ya kibiashara. Hii ilionyesha kwamba makampuni yalibaini faida itakayopatikana kwao kwa kumtumia msanii huyu ambaye bado alikuwa na heshima kubwa kwenye jamii kutokana na haiba yake na uwezo wake kwenye kazi alizokuwa akifanya.
"Msiba huu umekuwa pigo kubwa kwa tasnia ya filamu ambayo bado inaomboleza vifo vya wasanii kama Steven Kanumba, Mlopelo na John Steven Maganga, waliofariki dunia mwaka huu pia.
"Ifahamike kwamba Sharomilionea alikuwa miongoni mwa wasanii wa Kitanzania waliotuma maombi Simba ya kutaka kushiriki kwenye mchakato wa kutengeneza wimbo rasmi wa klabu ya Simba. Yeye alikuwa miongoni mwa wasanii waliokuwa wakiumizwa na ukweli kwamba klabu kama Simba inashindwa kufanya biashara ya kuuza nyimbo zake ilhali wanunuaji wapo."
Taarifa hiyo iliendelea: "Kwa klabu ya Simba, namna pekee ya kumuenzi marehemu ni kufanyia kazi mambo ambayo alikuwa akitushauri kwenye eneo la biashara. Ni matumaini yetu kwamba iwapo tutafanya lile alilokuwa akitushauri, atakuwa mwenye amani huko alikotangulia mbele ya haki."
Aidha, Rage amewaomba wasanii wa tasnia ya filamu na muziki kuwa watulivu na wenye subra kwenye kipindi hiki kigumu kwao akisema kila kitu katika maisha ya wanadamu kinapangwa na Mwenyezi Mungu na ndiyo maana Waswahili wana msemo kuwa Kazi ya Mungu haina makosa.

ALIIBIWA KILA KITU
Watu wasiojulika waliiba kila kitu kutoka kwa msanii huyo baada ya kupata ajali ya gari na kufariki papo hapo.
Wezi hao walimuibia msanii huyo vitu vyote na kumbakisha na pensi ya ndani ambayo alikutwa nayo na polisi katika sehemu ya tukio akiwa tayari ameshakufa.
Ripoti zinasema kuwa baada ya kufa, vibaka wa eneo hilo la kijiji cha Maguzoni walimuibia viatu, mkufu, nguo, fedha.
Wakizungumza na NIPASHE mashuhuda katika eneo la tukio walisema kuwa walisikia kishindo kikubwa cha gari hiyo kuanguka kabla ya vijana ambao hawakutambulika kulivamia na kuanza kupora bila ya kutoa msaada kwa msanii huyo hadi watu walipojaa na kusaidia.
Hii ni ajali ya pili kwa Sharo kupata mwaka huu baada ya Januari 5 kunusurika katika ajali ya basi alilokuwa amepanda likitokea Burundi kuelekea Dar es Salaam kupinduka katika eneo Mikese, Morogoro saa 2:30 asubuhi.
Sharo ambaye alikuwa amekaa kwenye siti ya mbele kabisa alipoteza simu tu katika ajali hiyo ambayo ilijeruhi abiria wengine vibaya.
Kifo cha Sharo kinafuatia vifo vya wasanii wengine wawili wa filamu nchini ndani ya wiki moja, Mlopelo aliyetamba na kundi la Kaole na John Maganga aliyetamba na filamu ya 'Mrembo Kikojozi' aliyocheza na Aunt Ezekiel. John Maganga alizikwa jana mchana kwenye makaburi ya Kinondoni. Vifo hivyo pia vinakumbushia msiba wa Steven Kanumba, ambaye pia alifariki ghafla mwaka huu pia katika kilichodaiwa kuwa ni ugomvi wa kimapenzi.
Sharo atakumbukwa kwa ubunifu wake katika uigizaji akitoka kama mchekeshaji msafi tofauti na wachekeshaji wengi waliomtangulia ambao waliamini vichekesho ni lazima kuvaa kama katuni, kujaza nguo tumboni ili kuonekana na matumbo makubwa ama kujipaka masizi.
Akipendeza kwa mavazi nadhifu, Sharo Milionea alipata umaarufu kwa msemo wake wa "kamata mwizi meeen" na "Ooooh mamma!" huku akijipangusa mabega katika pozi za 'kibrazameni'.
Katika siku za karibuni amekuwa akitawala vioo vya televisheni kutokana na kushiriki tangazo la kampuni ya huduma za simu ya Airtel akiwa na mchekeshaji mkongwe King Majuto, ambapo msemo wake mwingine wa "umebugi meen!" umetawala hasa midomoni mwa watoto.
Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mbando, alisema jana kuwa wameshtushwa na kusikitishwa na kifo cha ghafla cha Sharo ambaye waliingia naye mkataba hivi karibuni ili kutangaza huduma za kampuni hiyo.
"Tunaungana na familia, ndugu na jamaa na wadau wa burudani kutokana na kifo cha Sharomilionea. Alikuwa ni kijana mdogo, mchangamfu na aliyekitumia vema kipaji chake cha sanaa na tulikuwa bado tunamtegemea," alisema Mbando.
Wasanii wengine waliowahi kufanya kazi na msanii huyo walisema kuwa wanashindwa kuamini kama amefariki.
Mchekeshaji mwenzake maarufu kwa jina la Kitale alisema siku tatu zilizopita alipigiwa simu na Sharo akimtaka aende nyumbani kwake.
"Nilipofika akaniambia hii ni 'suprise' huku akinionyesha ufunguo wa gari, aliniambia amenunua gari mpya na akanipa Sh.200,000 huku akiniambia kwamba kuna 'dili' ameniunganishia ya kwenda naye nje ya nchi kufanya kazi ya sanaa," alisema Kitale.
Muigizaji Masai Nyota Mbofu alisema itamchukua muda mrefu kumsahau Sharo aliyetamba naye kwenye filamu na kipindi cha 'Vituko Show' wakati wakiwa katika kampuni ya Al Riyamy.
Naye mtayarishaji wa filamu nchini Mustafa Wazir 'West' alisema atamkumbuka daima kwa kipaji Sharo wakati mchekeshaji mwingine aliyekuwa akiigiza na Sharo, Ally Boffu 'Man Bizo', alisema hadi sasa haamini kama amefariki.

VIPAJI TELE
Sharo alikuwa ni msanii mwenye vipaji vingi na aliyejitambulisha pia kama "bonge la rapa" na muimbaji wa Bongofleva.
Baada ya kukosa mafanikio kwa nyimbo zake za awali za awali kabisa za 'Nahesabu Namba' na 'Tusigombane', Sharo ambaye alianza sanaa ya kikazi kipya tangu mwaka 2004, alirekodi nyimbo nyingine za 'Tembea Kisharobaro', aliurekodi katika studio ya Andrew Music ya jijini Tanga na 'Sondela' alioupika katika studio ya Ally's Records ya Tanga pia.
Aliiambia NIPASHE katika mahojiano enzi za uhai wake kwamba pamoja na kumudu miondoko mbalimbali ya muziki kama kwaito, hip hop, na kadhalika, aliamua kugeukia kuimba.
"Nimeamua niimbe kwa sababu naona wengi wananikubali zaidi ninapoimba," alisema msanii huyo ambaye aliliacha jina la Sharobaro na kuhamia Sharomilionea.

CHANZO CHA SHARO-MILIONEA
Wakati akianza sanaa yake ya ucheshi, msanii huyu alijiita Sharobaro, jina ambalo pia ni la studio ya kurekodi muziki inayomilikiwa na msanii na mtayarishaji wa muziki, Bob Junior, aliyemtoa msanii Diamond Platinumz.
Lakini baada ya kilichoripotiwa kuwa ni bifu baina yake na Bob Junior, msanii huyo aliliacha jina la "Sharobaro" na kuanza kujiita "Sharo Milionea".
"Sina ugomvi na Bob Junior, ila watu wa pembeni ndio waliokuwa wakiongea vibaya kutaka kutugombanisha, ndio maana nikamweleza kwamba ni vyema nibadili jina, ndo nikaanza kutumia Sharomilionea, lakini hatuna ugomvi," alisema Mkieti katika mahojiano na NIPASHE wakati wa uhai wake.
Alitamba katika filamu kadhaa za ucheshi ikiwamo ya 'Sharobaro' na 'Mtoto wa Mama', ambamo alitoa msemo wake uliompa umaarufu mkubwa wa "kamata mwizi meeen" pale alipoibiwa simu na kibaka, ambapo badala ya kumkimbiza alionyesha kwamba yeye "brazameni" hawezi kukimbiza mwizi hiyo akiwataka wengine wamsaidie huku akitoa msemo huo.
Baadaye alitamba katika filamu ya kampeni ya kupambana na malaria ya 'Chumo' akiigiza pamoja na Yusuph Mlela na Jokate Mwegelo ambayo ilikuja baada ya filamu yake nyingine ya ucheshi ya 'Back From New York', ambamo aliigiza kama kijana aliyerejea kutoka Marekani na kujumuika na baba yake (wa maigizo) King Majuto, ambaye naye akamgeuza kuwa 'mzee Sharobaro' anayevaa 'kibrazameni' na anayetemba huku akidunda kama vijana wa mjini.
Sharo Milionea enzi za uhai wake akiwa kapigilia kanzu
Hussein Mkiety 'Sharomilionea', alizaliwa Machi 20, 1987 Muheza, akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu na amefariki akiwa mbioni kufyatua video za nyimbo zake mbili zilizokamilika hivi karibuni za 'Vululuvululu' alioimba na Tundaman na 'Changanya Changanya' alioimba na Ally Kiba.

PICHA ZA GARI ALILOPATA NALO AJALI SHARO MILIONEA NA WANANCHI NJE YA CHUMBA CHA MAITI



Gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR alilokuwa akiendesha msanii wa filamu na muziki Hussein Ramadhani Mkieti ‘Sharo Millionea’ kutoka jijini Dar es salaam kuelekea Kijijini kwao Lusanga Wilaya ya Muheza  mkoa wa Tanga. Sharo Millionea alikufa papo hapo na mwili wake kuhifadhiwa Hospitali ya Teule Muheza Tanga.

Baadhi ya watu wakiliangalia gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR alilokuwa akiendesha msanii wa filamu na muziki Hussein Ramadhani Mkieti ‘Sharo Millionea’ kutoka jijini Dar es salaam kuelekea Kijijini kwao Lusanga Wilaya ya Muheza  mkoa wa Tanga. Sharo Millionea alikufa papo hapo na mwili wake kuhifadhiwa Hospitali ya Teule Muheza Tanga.

Gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR alilokuwa akiendesha msanii wa filamu na muziki Hussein Ramadhani Mkieti ‘Sharo Millionea’ kutoka jijini Dar es salaam kuelekea Kijijini kwao Lusanga Wilaya ya Muheza  mkoa wa Tanga. Sharo Millionea alikufa papo hapo na mwili wake kuhifadhiwa Hospitali ya Teule Muheza Tanga.

Mbunge wa Jimbo la Muheza Hebert Mtangi akiwasili nje ya jengo la Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Hospitali ya Teule Muheza kwa ajili ya kushuhudia mwili wa msaniii Sharo Millionea aliyekufa katika ajali ya gari wakati akitoka Dar es Salaam kwenda Lusanga, Muheza mkoani Tanga, ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Kijiji cha Songa Kibaoni jana usiku.

Wakazi wa wilaya ya Muheza na maeneo mengine wakiwa wamefurika nje ya Chumba cha Maiti cha Hospitali Teule Muheza, kusubiri kushuhudia mwili wa Sharo Millionea, aliyefariki kwa ajali ya gari usiku wa jana. (Picha Zote na Ahmed Khatib, Tanga).

Sharo Milionea enzi za uhai wake. Anatarajiwa kuzikwa leo kwao

Chanzo:Francis Dande