STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, February 16, 2013

Yanga wamtambikia Didier Kavumbagu



Didier Kavumbagu (kushoto)

Na Adam Fungamwango
WANACHAMA, mashabiki na wapenzi wa Yanga tawi la Mwananyamala, walipata fursa ya kutembelewa na mshambuliaji kipenzi Didier Kavumbagu kwenye tawi la klabu hiyo liitwalo Green Stone maarufu kama 'Uturuki'.
Kwa siku mbili mfululizo, mshambuliaji huyo mwenye magoli tisa Ligi Kuu, alilitembelea tawi hilo la Uturuki na kupata fursa ya kukutana na mashabiki, wanachama na wapenzi wa klabu ya Yanga na kubadilishana nao mawazo.
Mwenyekiti wa tawi hilo, Lumole Matovola maarufu kama 'Big' amesema kuwa wamefurahi kutembelewa na mchezaji huyo na kitendo cha kushikwa mikono na kukumbatiwa na wanachama ni kama tambiko kwa mchezaji ili azidi kuifanyia makubwa Yanga.
"Unajua mchezaji mkubwa kama huyu tena wa kigeni, kuja uswahilini kama huku na kuzungumza na wanachama ni kama tambiko, hivyo tunaamini itampa chachu ya kuona kumbe anapendwa na azidi kutufungia magoli," alisema Big na kuendelea.
"Tumekaa na umebadilishana naye mawazo, kusema kweli amefurahi sana kwa sababu amekuja kwa siku mbili hapa na Jumatano iliyopita akapiga bao lake la tisa, huu ni mfano wa kuigwa kwa nyota wengine, wakipata ruhusa ya kupumzika watembelee wapenzi wako matawini," alisema.
Wakati hayo yakiendelea, Big amesema tawi lao limepokea msaada ya viti sita kutoka kwa mwanachama mwenzao Yusuph Mhandeni na kufanya tawi hilo kuwa na viti nane na kusisitiza wanachama wengine kusaidia tawi hilo kwa hali na mali.

MARUFUKU WAGOMBEA KUFANYA KAMPENI-TFF


SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) limepiga marufuku kwa wagombea uongozi wa Shirikisho hilo kufanya kampeni kwa sasa na atakayebainika kufanya hivyo kamati ya uchaguzi itamuondoa kwenye kinyang’anyiro hicho. 
 Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema kwamba kampeni bado zimesimamishwa hivyo hairuhusiwi mtu yoyote kufanya kampeni mpaka itakapoangazwa. 
Msemaji wa TFF, Boniface Wambura
“Tunapenda kuwakumbusha wale waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali  za uongozi TFF kutoendesha kampeni kwa sasa mpaka watakapopewa barua za ruhusa hiyo na yeyote atakayekiuka kamati ya uchaguzi inamamlaka ya kumuengua katika kinyang’anyiro hicho. 
Hivi karibuni, kamati ya uchaguzi ya TFF chini ya mwenyekiti wake Deo Lyatto ilitangaza kusitisha kampeni za wagombea wa uchaguzi wa viongozi wa TFF uliopangwa kufanyika Februari 24 pamoja na ule wa bodi ya ligi uliopangwa kufanyika Februari 22. 
Aidha, kumekuwa na sintofahamu juu ya uchaguzi huo baada ya hivi karibuni kuwepo kwa shinikizo la kutaka kurejeshwa kwa aliyekuwa mgombea nafasi ya Urais wa TFF,Jamal Malinzi ambaye jina lake lilienguliwa na kamati ya Rufaa. 
Kitendo cha kuenguliwa kwa Malinzi kimeibua hisia tofauti kwa wadau wa soka ambao kwa nyakati tofauti wameinyooshea kidole TFF juu ya suala hilo kwa madai kwamba imeingiza mkono katika hilo, huku wakipanga kwenda kuzuia uchaguzi huo magakamani iwapo hatarejeshwa kwenye kinyang’anyiro hicho. 
Kama hiyo haitoshi, mmoja ya wagombea aliyeenguliwa katika kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Michael Wambura naye ameitaka TFF kuifuta kamati ya Rufaa kwa madai kuwa si halali, huku akipendekeza uchaguzi huo kufanywa kwa kufuata kanuni za zamani.

BUNGE LAFYATA! LAKUBALI VIKAO KURUSHWA LIVE


JAMHURI YA MUUNGANO WATANZANIA

BUNGE LA TANZANIA

__________

TAARIFA MAALUM KUHUSU BUNGE NA KAMATI


Ofisi ya Bunge imepokea kwa masikitiko taarifa kuhusu tafsiri ya kusitisha matangazo ya Shughuli za Bunge na Kamati, kinyume na jinsi ilivyoakisiwa katika mazungumzo ya pamoja kati ya Wanahabari na Katibu wa Bunge. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, Bunge la Jamhuri ya Muungano halina mpango wa kusitisha matangazo ya Bunge wala Kamati zake, ambazo kwa mahitaji ya sasa nazo zinapaswa kurushwa moja kwa moja kama sehemu ya mpango kabambe wa kuwapasha Wananchi yanayojiri katika Uendeshaji bora wa Shughuli za Bunge.Dhamira ya Bunge ni kuhakikisha kuwa mpango kabambe uliopo ni kumfikia kila Mtanzania alipo na kwa uwezo alionao aweze kupata na kushiriki katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. 


Hivyo Mpango mkakati uliopo utakuwa kuboresha mawasiliano ya kawaida kupitia Teknolojia ya Mawasiliano TEKNOHAMA, kwa wale watakaokuwa na uwezo wa kupata huduma za mtandao, na tayari tumeanza kurusha live video striping kupitia tovuti ya Bunge, na hata wale watakaopenda kujua zaidi, basi wanaweza kupitia majadiliano ya Bunge kwa nyakati tofauti. Aidha, kwa wale watakaokuwa na uwezo wa kushika mawimbi ya Radio, basi wataweza kufuatilia majadiliano ya Bunge katika Radio ya Bunge inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni katika masafa yanayoweza kupatikana nchi nzima, hii ikiwa ni jitihada za ziada kwa kuwa kuna Radio zinazotoa huduma hiyo ya moja kwa moja vizuri hadi sasa, kama vile RTD,BBC, STAR etc. Aidha, kwa wale watakaoweza kuwa na uwezo wa kumudu Luninga, basi Bunge limejipanga kuwapatia huduma hiyo moja kwamoja kupitia katika mtandao wake mpya utakaokuwa ukirushwa masaa 24, baada ya mitambo mipya ya kunakili majadiliano Bungeni na katika Kamati kusimikwa.

Hivyo basi utaratibu uliopo sasa utaendelea kutumika ambapo vituo vyote vya Television vitapewa fursa ya kurusha matangazo kwa utashi wao bila kuwekewa mipaka ya aina yoyote sambamba na matangazo yatakayotolewa na mitandao ya Bunge. Utaratibu huu unatokana na uamuzi wa pamoja kati ya Bunge na Tume ya Mawasiliano, ambapo vipindi vyote vya Bunge vitakuwa vinarushwa bila kudhaminiwa na taasisi yoyote zaidi ya mamlaka tajwa juu ya mawasiliano TCRA. Hivyo basi kwa maelezo hayo ni dhahiri kuwa Bunge halina mpango wa kusitisha matangazo ya TV wala yale ya Radio au Teknohama, bali linatarajia kuboresha upatikanaji wa huduma kwa utaratibu ulio rahisi na unaoweza kusimamiwa na pande zote, yaani Bunge na Wananchi. Aidha, kwa utaratibu uliopo sasa,Bunge halirushi matangazo ya aina yoyote, bali hutoa nakala ya majadiliano hayo kwa mtu yeyote atakaye au TV na Radio yoyote kupitia katika mitambo yake. TV zote zinazorusha matangazo ya Bunge hupata feed toka katika mitambo ya Bunge, na pale wanapoona yafaa basi huomba kutumia mitambo yao na hivyo kutumia fursa hiyo kuingiza Camera na Wanahabari ndani ya ukumbi wa Bunge kwa minajiri hiyo. Kuzingatia mabadiliko tajwa, utaratibu huo umepewa ukomo, ili sasa hapatakuwa na fursa ya kuingiza Camera ndani ya Kumbi za Bunge, bali wote watakaotaka kurusha matangazo ya Bunge kwa utashi wao, watapata clear feed toka katika mitambo ya Bunge na hivyo kurusha live vipindi vyote vya Bunge bila kuhaririwa kama ilivyonakiliwa katika makala mbalimbali.

Hata hivyo utaratibu huu wa kutumia Camera katika Kumbi utaendelea katika Kamati za Bunge, hadi hapo mitambo mipya ya mawasiliano itakapofungwa katika Kumbi zote za Kamati. Hivyo basi, ili kwenda sawia na taratibu hizo, Bunge litaendesha zoezi la kuwatathmini Waandishi wote wa habari za Bunge na kuwasajili kwa vigezo vitakavyoafikiwa kati ya Baraza la Habari,Idara ya Habari na Bunge lenyewe. Aidha ili kulinda heshima na maadili ya utangazaji, Bunge litatoa utaratibu (Code of Conducts for Media broadcasting) wa namna ya kunakili na kurusha matangazo ya Bunge bila kujali yanarushwa kwa utaratibu upi. Hili litasaidia kuweka misingi bora ya mawasilaino na hivyo kuwapa fursa Wananchi kujua hali halisi ya matukio yote ndani ya Bunge na katika Kamati, bila kuegemea upande wowote (Non Partisan). Hivyo basi, wakati zoezi la maboresho hayo likiendelea, Wananchi watajulishwa kila hatua na matarajio tajwa na kwamba tunaendelea kusisitiza tena, Wananchi wasiwe na hofu juu ya taarifa zilizopewa uzito usio stahili za kusitisha matangazo ya Bunge, ambao hazikuwa sahihi na pia hazikuainisha zoezi zima la maboresho ya upatikanaji na usambazaji wa habari za Bunge. Tunasikitika kwa usumbufu uliowasibu wote walioakisiwa na taarifa hiyo.


Dr. Thomas D.Kashililah

KATIBUWA BUNGE

Kemmy ana Nguvu ya Imani

Kemmy katika pozi

MSANII mkongwe katika fani ya uigizaji nchini aliyewahi kutamba na kundi la Kaole Sanaa, Juliet Samsom 'Kemmy' amevunja ukimya akiibuka na filamu mpya iitwayo 'Nguvu ya Imani'.
Akizungumza na MICHARAZO jana, Kemmy alisema filamu hiyo inayozungumzia maisha ya wafugaji na imani walizonazo ameifyatua kupitia kampuni yake iitwayo Giligali Entertainment.
Kemmy alisema filamu hiyo ambayo ipo katika hatua ya kuachiwa mtaani hivi karibuni ameigiza yeye akishirikiana na wasanii wengine kadhaa nyota akiwamo Simon Mwapangata maarufu kama 'Rado' na Jackson Kabigili.
"Najiandaa kutoka na filamu mpya niliyoitayarisha kupitia kampuni yangu baada ya kuwa kimya tangu nilipotoa kazi zangu za mwisho mimi kama mimi," alisema Kemmy.
Kemmy, aliyewahi kutamba na michezo ya kwenye runinga akiwa na Kaole mingi akiwa ameitunga yeye mwenyewe au kushirikiana na wasanii wenzake, alisema kazi hiyo mpya ni kati ya burudani aliojiandaa kuwapa watanzania baada ya kumkosa kwa muda.
"Huu ndiyo ujio mpya wa Kemmy, nimeanza na 'Nguvu ya Imani' na nyingine zipo njiani kwa sababu nimejipanga vema 2013," alisema Kemmy ambaye ni Mlokole.
Kabla ya kuwa kimya, Kemmy 'aliuza sura' katika filamu za 'Omtima', 'Joto la Roho', 'Mateka wa Moyo', 'My Daughter', 'My Life' na nyinginezo.

Azam kuvuna nini Afrika leo?


MSHAMBULIAJI John Bocco ataongoza safu ya ushambuliaji ya Azam FC ambayo leo inaikabili timu ya Al Nasri Juba ya Sudan Kusini kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika.
Bocco ambaye alikosa michezo kadhaa ya ligi kuu kutokana na kuwa majeruhi, amepona na leo atakuwepo uwanjani kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa kurejea uwanjani kwa mchezaji huyo ni faraja kwake kwa kuwa ataongeza safu ya ushambuliaji ya timu yake kwenye mchezo wa leo.
"Kwangu ni faraja kuwa na wachezaji wote muhimu kikosini kwa sababu mchezo wa kesho (leo) ni mkubwa na muhimu sana kwetu ukizingatia tunacheza kwenye uwanjawa nyumbani,' alisema Hall.
Aidha, alisema kuwa haifahamu timu hiyo ya Sudan Kusini hivyo watacheza kwa tahadhari huku wakiwa na lengo la kuibuka na uhsindi.
Alisema kuwa anafahamu wapinzani wao matokeo ya sare yatakuwa na faida kubwa kwao hivyo ni lazima wagangamale ili kupata ushindi.
Hall, alisema kuwa katika mchezo wa leo atatumia mfumo wa kushambulia na kulinda goli hili kutowaruhusu wapinzani wao kupata goli la ugenini ambalo litakuwa na faida kubwa kwao (Al Nasri).
Aidha, alisema kuwa kipindi cha kwanza cha mchezo wa leo kitakuwa kigumu zaidi kwa kuwa timu zote hazifahamiani.
"Siijui hii timu lakini kama imefika hapa ina maana ni timu nzuri, tutacheza kwa tahadhari zaidi katika kipindi cha kwanza na pamoja ya kuwa tuna lengo la kushambulia sana pia tutakuwa makini kwenye kulinda goli letu," aliongezea kusema Hall.
Aidha, alisema kuwa pamoja na ugeni wa timu hiyo, amekiandaa vizuri kikosi chake na anategemea kupata ushindi kwenye mchezo huo wa leo ambao ni wa kwanza kwa Azam FC kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa yanayoaandaliwa na Shirikisho la soka barani Afrika, CAF.

Wenger njia panda juu ya Wilshere FA

Kocha Arsene Wenger akiwa na Jack Welshere

LONDON, England
KIUNGO wa England Jack Wilshere ana uwezekano mdogo wa kupangwa na Arsenal katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Blackburn Rovers leo huku timu hiyo ikikabiliwa na mchezo wa nyumbani wa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich katikati ya wiki.
Mchezaji huyo mwenye umri wa chini yam iaka 21 amekuwa katika kiwango kizuri tangu apone jeraha kubwa la enka na aling'ara akiichezea England dhidi ya Brazili katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa wiki iliyopita kwenye uwanja wa Wembley.
Hata hivyo, kocha Arsene Wenger ana wasiwasi wa kuhatarisha uzima wa Wilshere baada ya kuumia paja katika katika mechi dhidi ya Sunderland ya ligi kuu ya Uingereza wiki iliyopita.
"Sintamhatarisha," Wenger alisema jana. "(Hii ni kwa sababu nina) nusu msimu nzima imebaki na nakumbuka kilichomkuta huko nyuma."
Beki Laurent Koscielny pia yuko shakani kucheza mechi hiyo ya raundi ya tano dhidi ya timu ya daraja la kwanza Blackburn kutokana na maumivu ya kiazi cha mguu.
"Wilshere na Koscielny watapimwa asubuhi hii na Thomas Vermaelen atakuwa amepona. Amefuzu vipimo leo," Wenger alisema. "Tuna watu wengi kwenye mazoezi leo ambao wanapimwa afya na tutaangalia wamepitaje."
Arsenal inakutana na Bayern Jumanne kwenye uwanja wa Emirates katika mechi ya kwanza ya hatua ya timu 16 bora.


RATIBA YA FA KWA LEO:

Ratiba ya mechi za Kombe la FA la Uingereza leo:
Luton Town    v Millwall
Arsenal        v Blackburn    (12:00)
MK Dons        v Barnsley
Oldham        v Everton


Real Madrid kibaruani tena La Liga kesho

Nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo

MADRID, Hispania
Rayo Vallecano imedhihirisha kuwa umasikini si kilema na kucheza soka maridadi zaidi kwenye La Liga msimu huu iliyoiwezesha kushika nafasi ya sita kwenye msimamo na inaweza kuangalia maendeleo yake wakati itakapoikabili timu tajiri ya jiji lake Real Madrid kwenye uwanja wa Bernabeu kesho.
Ushindi wa kustahili wa mabao 2-1 wa nyumbani dhidi ya Atletico Madrid iliyo katika nafasi ya pili mwishoni mwa wiki iliyopita ulizaa mazungumzo ya kuwepo kwa uwezekano wa kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao na kuimarisha sifa ya Rayo kama moja ya viboko vya vigogo nchini Hispania.
Klabu hiyo masikini, ambao ipo chini ya uangalizi maamulu kifedha na ambayo uwanja wake wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 15,000 una majukwaa matatu kutokana na upande mmoja kutumuika kwa matangazo, imebadilika kutoka timu iliyokuwa ikisota kwenye daraja la tatu la soka ya Hispania kati ya mwaka 2004 na 2008.
Ina mtihani mgumu nyumani kwa mabingwa watetezi Real, ambayo haijafungwa kwenye uwanja wa Bernabeu msimu huu wote lakini imekuwa ikionyesha mwendo wa kusuasua kwenye viwanja vya ugenini na ipo pointi nne nyuma ya Atletico na 16 nyuma ya viongozi Barcelona.
Barca ilipumzika wiki nzima baada ya mechi yake ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ya hatua ya 16 bora nyumbani kwa AC Milan ya Serie A kupangwa kuwa Jumatano inaweza kuongoza kwa tofauti ya pointi 15 juu ya Atletico kama itaifunga timu ya 14 Granada leo.
Atletico imeshinda mechi zote 12 za nyumbani msimu huu lakini imepoteza michezo yake miwili mfululizo iliyopita ya ugenini na ni mgeni wa Real Valladolid kesho. 

RATIBA KAMILI YA LEO LA LIGA:
Getafe        v Celta Vigo
Malaga        v Athletic
Granada        v Barcelona    (4:00) 
Osasuna        v Zaragoza

Kapombe, Mess kujaribiwa Sunderland ya England

Ramadhani Singano 'Messi'




WACHEZAJI wawili wa klabu ya Simba, Shomari Kapombe na Ramadhan Singano 'Messi' watakwenda Uingereza kufanya majaribio kwenye kituo cha vijana cha klabu ya Sunderland inayoshiriki ligi kuu nchini humo mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu ya Bara, imedaiwa.
Mwaliko wa wachezaji hao kwenda nchini humo umekuja kufuatia ziara ya mmiliki wa Sunderland Ellis Short na viongozi wa klabu hiyo waliyoifanya Desemba mwaka jana hapa nchini, imedaiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti Simba, Ismail Aden Rage, ambaye uongozi wake umelaumiwa kwa mwenendo mbovu wa timu katika mechi za karibuni alisema wachezaji hao wakiwa nchini humo watafanya majaribio kwenye kituo hicho.
Aidha, alisema kuwa wakati wachezaji hao wakitarajiwa kwenda nchini humo baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi, makocha wa Simba watakwenda nchini humo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali huku pia makocha wa klabu hiyo ya ligi kuu ya Uingereza watakuwa wakija nchini kutoa mafunzo mbalimbali kwa wachezaji.
Aidha, alisema kuwa kwa kuanzia kwenye mchezo wa kesho wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Reacreativo Libolo ya Angola, Simba itavaa jezi walizopewa na klabu hiyo ya Sunderland.
"Lakini pia tumekubaliana kuanzia msimu ujao tutakuwa tukipokea vifaa kamili kutoka kwa wenzetu wa Sunderland na tutakuwa tukivitumia kwenye michezo mbalimbali," alisema Rage.
Alisema kuwa jezi hizo walizopewa na Sunderland pia zitakuwa na nembo ya wadhamini wao wa nyumbani na kampuni inayoidhamini timu hiyo ya Ulaya ya Invest in Africa.

TFF yashitakiwa mahakamani Mwanza



Na Faustine Feliciane
ALIYEKUWA mgombea wa nafasi mbili za Rais na mjumbe wa Kamati ya utendaji katika uchaguzi wa Shirikisho la soka (TFF) uliopangwa kufanyika Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam, Richard Rukambula amefungua kesi Mahakama Kuu kanda ya Mwanza kuzuia uchaguzi huo akishinikiza kurejeshwa kwenye mchakato.
Rukambula amefungua kesi hiyo itakayosikilizwa keshokutwa katika Mahakamu Kuu kanda ya Mwanza kupinga mchakato wa kumuengua kwenye uchaguzi huo kwa madai kuwa hakutendewa haki katika kuengeliwa kwake kwenye mchakato huo.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana kutokea Mwanza, Rukambula alisema kuwa amefika hatua ya kusimamisha uchaguzi huo wa TFF ili suala lake lijadiliwe na haki itendeke kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Wakati Rukambula akifikia hatua hiyo, Katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema shirikisho halijapata taarifa hizo lakini akasema pindi watakapoitwa mahakamani, vyombo husika ndani ya TFF vitakaa na kufanya maamuzi.
Rukambula amefungua kesi hiyo akisistiza hakutendewa haki katika kumuengua kwenye mchakato wa uchaguzi huo kwa maelezo kuwa aliomba nafasi mbili badala ya moja tu, kama inavyotakiwa.
"Tayari hili jambo limeshafika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza na kesi imeshapangiwa jaji atakayesikiliza suala hili ," alisema Rukambula,
Aidha, alisema jalada la kesi hiyo lipo kwa Jaji Muruma.
"Leo hii (jana) nimemtuma mtu na anakuja huko Dar es Salaam na ndege ya jioni ili kuleta barua kwa TFF ya kuitwa Mahakamani kusikiliza kesi hiyo," alisema Rukambula.
Aidha, alisema ameiomba Mahakamu Kuu kuisikiliza kwa haraka kesi hiyo ili imalizike kabla ya siku ya kufanyika kwa uchaguzi wa TFF; ili ikiwezekana arudishwe kwenye mchakato huo wa uchaguzi.
Aidha, alisisitiza kuwa maombi aliyoyapeleka mahakamani hapo ni ya kusimamisha uchaguzi huo ili mchakato wa kusaili wagombea urudiwe tena.
Rukambula anasema kuwa kamati ya uchaguzi ya TFF ilimuengua kwa madai kuwa aliomba kugombea nafasi mbili tofauti kwenye uchaguzi huo kitu ambacho ni kinyume na kanuni za uchaguzi wa TFF.
"Mimi sikuomba kugombea hizo nafasi kwa kufuata kanuni hizo wanazozisema bali nilifuata tangazo lao la uchaguzi walilolitoa ambalo halikuelezea kikomo cha kuwania nafasi kwenye uchaguzi huo," alisema Rukambula.
Aidha, alisema kuwa kama ni kosa kugombea nafasi mbili ni kwa nini TFF walikubali malipo yake ambapo alilipia fomu ya kuwania Urais na ile ya Ujumbe na kupewa stakabadhi zilizofuatana?

 CHANZO:NIPASHE JUMAMOSI