STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 24, 2013

VODACOM KUKABIDHI ZAWADI LIGI KUU BARA JULAI 3

Meneja Uhusiano wa nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalim (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza tarehe ya utoaji wa zawadi za ligi kuu ya Vodacom zitakazotolewa Julai 3 jijini Dar es Salaam.  Zawadi hizo ni za jumla ya Sh. milioni 200 zitakazotolewa kwa vipengele mbalimbali kwa timu za ligi hiyo.
WADHAMINI wakuu wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara Kampuni ya Vodacom imetangaza kuwa itakabidhi zawadi kwa washindi wa ligi hiyo Julai 3 jijini Dar es salaam.

Vodacom imesema ilikuwa ikisubiri kumalizika kwa hekaheka za timu ya taifa - Taifa Stars za kusaka nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil hali iliyochelewesha tukio la kukabidhi zawadi hizo kwa mabingwa pamoja na wote waliofanya vema katika msimu wa 2012/2013.
.
"Tulikuwa tukisubiri wakati mwafaka wa kufanya hivyo kwani tangu kumalizika kwa ligi mwezi uliopita mwelekeo wa taifa ulikuwa ni kuipa ari na nguvu timu yetu ya taifa katika kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil," alisema Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim.

Mwalim amesema maandalizi yote ya tukio hilo yamekamilika kwani hakukuwa na sababu nyingine ya kutokabidhi zawadi mara tu baada ya ligi kumalizika zaidi ya timu ya taifa - Taifa Stars.

Mwalim amesema hafla ya utoaji wa zawadi inahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali wa soka nchini wakiwamo wachezaji wa klabu ambao miongoni mwao wamo kwenye kikosi cha Stars, viongozi wa TFF na walimu wa timu ya taifa ambao wote hao kwa pamoja walikuwa na jukumu moja tu la kuhakikisha Stars inafuzu kwenda Brazil na hivyo isingekuwa vema kuingiza maandalizi ya jambo jingine katikati ya juhudi hizo.

Mwalim ametumia nafasi hiyo kuzishukuru klabu pamoja na Shirikisho la Soka (TFF) na kamati ya ligi kwa uvumulivu wao wakati wote ambapo Vodacom ilikuwa ikisubiri kupatikana kwa muda mwafaka wa kukabidhi zawadi.

"Tendo la kukabidhiwa zawadi ni moja ya matendo makuu kabisa kwa yeyote anayeshinda, tumeona uvumilivu mkubwa na wenzetu walituelewa wakati tulipowashauri kutoa nafasi kwa Stars bila kuharibu concentration ya taifa. Tumeonesha umoja wetu."
Vodacom itakabidhi zawadi za fedha taslimu takribani Sh. milioni 200 kwa mabingwa Yanga na Azam, Simba na Kagera Sugar zilizoshika nafasi ya pili hadi ya nne.

Mbali ya mabingwa timu ya Yanga ambayo itakabidhiwa fedha taslimu Sh milioni 70, wengine watakaotunukiwa ni wachezaji mmoja mmoja walioonesha umahiri kwenye maeneo yao.

Wengine watakaonufaika na zawadi za fedha ni kipa bora, mwamuzi bora, mwalimu bora, timu iliyoonyesha nidhamu na mfungaji bora, ambaye ni Kipre Tchetche wa Azam.

Vodacom imekuwa ikiidhamini ligi kuu ya soka ya Tanzania bara kwa zaidi ya misimu mitano sasa huku ikiiwezesha ligi hiyo kuimarika na kuwa ya ushindani kadri miaka inavyosonga mbele.

Balotelli kuikosa Hispania Nusu Fainali ya Kombe la Mabara

Mario Balotelli 'Super Mario'
MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya taifa ya Italia 'Azzurri' Mario Balotelli, atalikosa pambano la Nusu Fainali ya Kombe la Mabara dhidi ya Hispania siku ya Alhamis kutokana na kuwa majeruhi.
Balotelli aliumia na kutoka uwanjani wakati Italia ikichezea kichapo cha mabao 4-2 toka kwa Brazili Jumamosi iliyopita na kuungana na wachezaji wengine wa Azzurri watakaolikosa pambano hilo ambao ni  Andrea Pirlo na Riccardo Montolivo.
Kukosekana kwa Balotelli kunamfanya kocha wa timu hiyo ya Italia, Cesare Prandelli kuwa katika mtihani mkubwa katika pambano hilo dhidi ya Mabingwa wa Ulaya na Dunia, Hispania walioinyoa Nigeria jana usiku kwa mabao 3-0 na kumaliza mechi za makundi bila kupoteza mechi.
Mshambuliaji huyo mtukutu mwenye umri wa miaka 22 na anayeichezea AC Milan katika michuano hiyo amefunga mabao mawili mpaka sasa. na atakosa fursa ya kuisaidia timu yake iliyokumbana na kipigo cha aibu katika Fainali ya Kombe la Ulaya Euro Cup 2012 pale Hispania walipowanyoa kwa mabao 4-0.
Nusu Fainali nyingine ya michuano hiyo itachezwa keshokutwa kati ya Brazil ya Neymer na Uruaguay ya Luis Suarez ambao usiku wa kuamkia leo walitoa kipigo cha mabao 8-0 kwa Tahiti iliyoweka rekodi ya kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza ikifungwa mechi zote tatu za makundi na kufunga bao moja tu huku yenyewe ikiruhusu jumla ya mabao 24.

Mzee Mandela hali yazidi kuwa tete

Mzee Mandela (kulia) akiwa na rais Jacob Zuma wakati hali yake ilipokuwa ikianza kutengemaa kabla ya kuelezwa imebadilika kiasi cha kuwa tishio
HALI ya Afya ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini na Mwanasiasa anayeheshimika duniani kote, Mzee Nelson Mandela inaelezwa kuwa tete.
Madaktari wanaomtibu Mwanaharakati huyo aliyeleta ukumbozi katika nchini ya Afrika Kusini, wamesema hali ya Mzee Mandela imekuwa siyo nzuri kwa saa 24 zilizopita na kwamba kwa sasa yu mahututi.
Habari hizo zimekuja kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais ya Afrika Kusini zikisema kuwa bado Mzee Mandela ameendelea kusalia hospitalini mjini Pretoria kwa siku ya kumi na sita akitibiwa mapafu yaliyosababisha tatizo kwenye mfumo wake wa upumuaji.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alimtembelea Rais Mstaafu huyo jana jioni na kuzungumza na jopo la matatibu wanaomtibia.
Baadaye Rais Zuma alirejea kauli yake ya kulitaka taifa na dunia kumuombea Mzee Mandela apate nafuu kwa hali aliyonayo.

Soggy Doggy Anter atangaza kuwania ubunge Jimbo la Segerea analoshikilia Makongoro Mahanga

Soggy Doggy Anter akiwajibika jukwaani

MSANII nguli wa muziki wa kizazi kipya nchini, Anselm Tryphone Ngaiza, 'Soggy Doggy Anter' ametangaza nia ya kugombea Ubunge wa jimbo la Segerea, Dar es Salaam kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.
Soggy Doggy ameweka bayana mipango yake hiyo ha kuwania kiti cha ubuinge cha jimbo hilo kinachoshikiliwa kwa sasa na Mhe. Makongo Mahanga kupitia akaunti yake ya Facebook ambapo aliandika;
"Shikamoo Mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga, imetosha sasa nadhani ni zamu yangu kuwatumikia wana-segerea 2015 kupitia CHADEMA" mwisho wa kunukuu. Pia kwenye ukurasa wake wa twitter imesomeka ivyo ivyo.
Msanii huyo alisema ameamua kujitosa kwenye siasa kupitia CHADEMA, kwa sababu ndicho chama pekee anachokiona kinachoweza kufanya mabadiliko kwenye jamii kwa sasa.

Azam waanza kujifua,10 pekee wahudhuria Morad kimyaaa

Wachezaji wa Azam walipokuwa wakijiandaa na mechi za Kombe la Shirikisho Afrika hivi karibuni
WACHEZAJI 10 pekee ndiyo waliohudhuria mazoezi ya timu ya Azam yaliyoanza leo kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo wachezaji wengi 16 wameshindwa kuhudhuria siku ya kwanza ya mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye uwanja wao wa Chamazi, kutokana na sababu mbalimbali huku beki Said Murad akiwa hana taarifa yoyote ya udhuru uliomfanya asiwepo mazoezini.
Taarifa hiyo imesema wachezaji walianza mazoezi asubuhi ya leo ni pamoja na Malika Ndeule, Brian Umony, Jabir Aziz, Waziri Salum, Gaudence Mwaikimba, Luckson Kakolaki, Samih Haji Nuhu, Seif Abdallah Karihe, Wandwi Jackson na Ibrahim Mwaipopo
Wachezaji wengine 16 wamekosekana kutokana na kuomba ruksa kwa matatizo waliyonayo ya kifamilia wakiomba kuanza mazoezi wiki ijayo ambao ni  David Mwantika aliye na matatizo ya kifamilia kama ilivyo kwa Omary Mtaki anayeuguza baba yake na Himid Mao aliyefiwa na baba yake mkubwa.
"Mchezaji pekee ambaye hakufika mazoezini na hakuna taarifa zozote juu ya kukosekana kwake ni Said Morad Mweda," taarifa hiyo inasomeka hivyo kuelezea kushindwa kujitokeza kwa beki huyo wa kati ambaye alisimamishwa na wenzake watatu kwa tuhuma za Rushwa kabla ya kusafishwa na TAKUKURU na kurejeshwa kikosi mwishoni mwa msimu uliopoita japo hakucheza hata mechi moja.
Moradi alisimamishwa na aliyekuwa nahodha, Aggrey Morris, kipa Deo Munishi na beki wa pembeni Erasto Nyoni.

Kibadeni akana kumtimua Kaseja Msimbazi

Kocha King Abdallah Kibadeni
http://4.bp.blogspot.com/-3p3m1Z0fISo/TfhiEVIEefI/AAAAAAAAA4g/cuNaeynaWSA/s1600/JUMA_KASEJA%5B1%5D.JPG
Kipa Juma Kaseja
KOCHA wa Simba, Abdallah Kibaden 'King', ameibuka na kukanusha vikali uvumi kwamba ni yeye ndiye aliyemtimua kipa chaguo la kwanza wa timu hiyo na Taifa Stars, Juma Kaseja baada ya kumtema katika orodha ya nyota wanaotarajia kuwamo katika kikosi chake cha msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Badala yake, Kibaden ambaye pia ni mchezaji nyota wa zamani wa 'Wekundu wa Msimbazi' aliyewahi pia kuandika rekodi kwa kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho wakati akiifundisha mwaka 1993, amefichua kuwa Kaseja hakuwamo katika orodha ya wachezaji aliokabidhiwa na uongozi wa klabu yake hiyo.
Akizungumza na jana, Kibadeni, alisema wakati akikabidhiwa majina ya wachezaji wa timu hiyo ili aanze kuwanoa, jina la Kaseja halikuwamo na hivyo yeye hawezi kulirejesha kwa maamuzi yake binafsi.
"Sijamkata mimi, ila jina lake sikupewa. Hicho ndicho ninacheweza kukieleza... mambo mengine ni ya ndani ya klabu," alisema Kibaden, mshambuliaji nyota wa zamani wa timu hiyo aliyerejea kuwafundisha baada ya kuihama klabu aliyoiongoza msimu uliopita ya Kagera Sugar.
Alisema kwa sasa tayari ameshapata wachezaji 25 atakaokuwa nao katika msimu ujao wa ligi, huku akiwataja nyota wa kigeni kuwa ni wawili na wote wanatokea Uganda.
"Kikosi changu hakitazidi nyota 25, na wageni hadi leo (jana) ni kipa Abel Dhaira na beki Senkoomi (Samuel), mipango mingine ya ndani ni ya kiufundi. Mazoezi tunayoendelea nayo ni ya kawaida na wengi waliokuja kujaribiwa hawajanishawishi kuwachukua," aliongeza Kibaden.
Naye Kaseja ambaye aliwahi kusema kitambo kuwa hahofii kutemwa Simba, alisema kuwa hivi sasa anachofanya ni kuendelea kujiweka 'fiti' ili atumikie vizuri taifa kwa sababu yeye na wenzake wa kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars) wana kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa wanashinda katika mechi ijayo dhidi ya Uganda na kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa fainali zijazo za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN).
"Jamani kuhusiana na Simba siwezi kusema lolote kwa sasa... ila maisha ni popote," alisema nahodha huyo wa Taifa Stars ambaye wiki iliyopita alishuhudiwa akiwa katika mazoezi ya timu ya vijana ya Simba B, akishauriana na kocha msaidizi wa timu hiyo, Amri Said.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage hakutaka kueleza wazi suala la Kaseja na badala yake akasema kuwa hivi sasa, suala la nani asajiliwe na nani aachwe liko katika mamlaka ya kamati yao ya ufundi inayoshirikiana na benchi lao la ufundi.
Rage alisema vigezo vya kusajili mchezaji ni muhimu zaidi kutekelezwa na makocha na kisha kamati ya utendaji itakuwa ya  mwisho kwa lengo la kutoa baraka.
 
NIPASHE

CHADEMA yafichua njama nzito dhidi yao

Mussa Tesha aliyemwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo wa Igunga
Viongozi Wakuu wa CHADEMA (kulia) Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuna mpango mchafu wa kuwabambikizia viongozi wakuu wa chama hicho kesi ya kumwagiwa Tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Musa Tesha.
Viongozi wanaoandaliwa mpango huo ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, Mnyika alisema mpango huo unafanyika kwa lengo la kukidhoofisha chama chao kinachowapa wakati mgumu CCM.
Alisema hivi sasa baadhi ya makachero wa polisi wamekuwa wakiwakamata vijana na kuwalazimisha kukiri kwa kuandika au kuandikiwa maelezo kuwa viongozi hao waliwatuma kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Mnyika alisema wafuasi wao waliokamatwa na polisi kwa kuhusishwa na tukio hilo wameshinikizwa kusema Mbowe, Slaa, Lissu na yeye ndio waliowatuma kummwagia tindikali Tesha.
Alisema jambo hilo linaendeshwa kisiasa, ambapo wafuasi wanne wameshatiwa mbaroni na kuwalazimisha kuwataja viongozi wakuu wa CHADEMA kuhusika na uhalifu huo.
Mnyika aliwataja waliokamatwa ni pamoja na Evodius Justinian, aliyeshikiliwa kwa siku mbili mjini Bukoba, na baadaye akapelekwa Mwanza kabla ya kufikishwa Dar es Salaam.
Alisema zoezi hilo lilifanyika kwa kificho na mtuhumiwa huyo baadae alifikishwa Igunga.
Alibainisha kuwa taarifa za kada huyo kupelekwa Dar es Salaam  zilikuwa za kificho kwani wakili wake, Nyaronyo Kicheere aliyeongozana na ndugu wa mtuhumiwa huyo walipofika Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam walielezwa amepelekwa Makao Makuu.
Mnyika alisema mara baada ya Evodius kuonana na wakili wake, Kicheere, siku hiyo alieleza unyama aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na Dar es Salaam.
Katika maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate Nyombi, Evodius alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri bila ndugu zake kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila kuruhusiwa kuonana na wakili wake.
Kada huyo akisimulia unyama aliofanyiwa alisema:  “Nimepigwa na polisi Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wakati naletwa huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme nilifanya nini Igunga na kama najua mkanda wa Lwakatare.
“Nikiwa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia pamoja na mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa, niliomba kuwa na wakili wakanikatalia.”
Aliongeza kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya Lwakatare. Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick, lakini akapigwa makofi na askari wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
“Waliposimama kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video ni yangu. Ninaumwa sana tumbo la kuhara damu, natumia dawa nilizonunuliwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Kagera tarehe 4 Aprili,” alisema.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa pili aliyeteswa ili akubali kuandika kuwa Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika walimtuma akammwagie tindikali Tesha ni Seif Kabuta aliyekamatwa Mwanza.
Alisema Kabuta baada ya kukataa kukiri kuwa viongozi wake wanahusika na matendo hayo, walimfungia katika chumba maalumu wakamleta mke wake, mama yake na mkwe wake na kumtesa mbele yao ili akiri kuwa Mbowe na wenzake walimtuma kummwagia Tesha tindikali.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa tatu aliyekamatwa kuhusishwa na tindikali ni Oscar Kaijage wa Shinyanga mjini, ambaye awali alipokamatwa aliambiwa ni kwa sababu kuna pesa zimepotea kwa njia ya simu, na yeye alikuwa anajishughulisha na uwakala wa pesa kwa njia ya mitandao ya M-pesa na Z-pesa.
Alisema mtuhumiwa huyo alipokutanishwa na makachero wa polisi makao makuu, naye alilazimishwa aseme kuwa Mbowe, Slaa, Lissu na Mnyika walimtuma akammwagie Tesha tindikali.
Mnyika alisema mtuhumiwa wa nne ni Rajab Kihawa, aliyetumiwa wasichana kuitwa akiwa Dodoma, ambaye aliombwa akubali kupewa shilingi milioni 30, kama alivyolipwa Ludovick ili aseme kuwa Mbowe na wenzake waliwatuma kummwagia tindikali Tesha.
Mtuhumiwa wa mwisho ni Henry Kilewo, Katibu wa CHADEMA wa Wilaya ya Kinondoni, na Katibu wa Makatibu wa CHADEMA Kanda Maalumu ya Dar es Salaam anayeshikiliwa na polisi.
Polisi wanamtuhumu Kilewo kummwagia tindikali Tesha wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Kilewo alishikiliwa na polisi kuanzia Ijumaa iliyopita na baada ya kuhojiwa alichukuliwa kwa kificho kupelekwa Mwanza kwa ndege ili aweze kuunganishwa katika kesi hiyo ya Igunga leo.
Mnyika alisema Kilewo amesafirishwa bila wakili wake kuwa na taarifa kuwa amepelekwa Mwanza, wala mke wake aliyeambiwa ampelekee  chakula, lakini alipofika polisi aliambiwa mume wake hayupo.
Mmoja wa mawakili wanaokwenda Igunga kuwatetea Kilewo na wenzake, Profesa Abdallah Safari alisema wameshitushwa kusikia wateja wao wamelazimishwa kutoa maelezo ili kuwahusisha viongozi wakuu wa CHADEMA.
Alibainisha kuwa kutokana na kesi hiyo kuonekana kujaa masuala ya kisiasa, atashirikiana na mawakili wenzake ambao ni Peter Kibatala na Gasper Mwalyela na kama itakapolazimika watawaongeza Mabere Marando, Kicheere, Method Kimomogoro na Lissu.
Aliongeza kuwa imefika hatua itabidi atumie kifungu cha sheria cha 102, ili kujenga dhana ya kutiliwa shaka kwani viongozi wote wa CHADEMA sasa wamefunguliwa kesi katika maeneo mbalimbali nchini, huku wale wa CCM wakiachwa.
Profesa Safari alitolea mfano Mbunge wa Tabora mjini, Ismail Aden Rage, ambaye alipatwa na hatia katika uchaguzi wa Igunga na alipaswa kufungwa miaka mitatu bila fidia, lakini DPP amekalia faili lake hadi sasa.
Aliongeza kuwa mambo hayo yanajitokeza kutokana na CHADEMA kumtaja ofisa wa usalama anayeitwa Shaali Ally kuwa ndiye aliwatafuta vijana wa chama hicho akiwemo Ahmed Sabula na wenzake.
Alibainisha kuwa Machi 29, mwaka huu vijana hao waliitwa na Shaali katika chumba cha hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam, akiwataka wakubali kutumika kwa kutoa taarifa za vikao vya CHADEMA, kuwasilisha kwake nyaraka za kamati kuu na kueleza mipango ya chama katika kesi ya Lwakatare.
Kwenye mpango huu, ofisa huyo wa usalama wa taifa ambaye Marando alisema anamfahamu vizuri, alimuahidi Sabula kiasi cha sh milioni 30 na kwamba fedha hizo angelipwa kama ujira kwa kukubali kutoa ushahidi dhidi ya Lwakatare.

Chanzo:TANZANIA DAIMA

Mwanamke Iringa ateketeza watoto wa jirani yake kwa wivu wa mapenzi

Picha hii haihusiani na habari hii, ila inaonyesha taswira ya nyumba iliyoteketea kwa moto
 MWANAMKE mmoja anayefahamika kwa jina la Taraji Muenzi, 31, mkazi wa kijiji cha Mwatasi, wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, anashikiliwa na jeshi la Polisi mkoani humo kwa kosa la kuichoma nyumba ya jirani yake na kuwateketeza watoto wawili waliokuwa ndani mwake pamoja na vitu vyote katika nyumba hiyo kwa kilichoelezwa wivu wa mapenzi.
Habari kutoka mkoani humo zinasema watoto walioteketezwa wakiwa ndani ya nyuma hiyo ni Faraji, 6 na Jacob, 3 ambao walikuwa watoto pekee wa Subira Kisitu aliyekuwa akituhumiwa na mtuhumiwa huyo kuwa anatembea na mumewe.
Inaelezwa kuwa Taraji kwa muda mrefu alikuwa akimtuhumu jirani yake kumuibia mume na kumchimba mkwara kwamba atamfanyizia, kiasi cha uongozi wa eneo lao kuitisha kikao na kumtwanga faini ya Sh 10,000 aliotakiwa kuilipa juzi, Juni 22 siku aliyofanya tukio hilo.Inaelezwa uongozi wa kitongoji hicho kiliamua kumtoza faini baada ya wiki iliyopita kumvamia jirani yake nyumbani kwake na kumwagia mboga na kusisitiza kuwa kuna kitu atakachomfanyia ambacho hatasahau maishani kama siyo kwa kumuua kwa sumu basi kwa kumchomea moto nyumba yake.
Hata hivyo inaelezwa kuwa jana juzi usiku akiamini kuwa jirani yake yupo ndani na wanawe aliamua kuichoma moto nyumba hiyo, ila kwa bahati mbaya jirani zake alikuwa klabuni akipata kinywaji na hivyo watoto pekee waliokuwa wamelala ndani ndiyo waliougua na kufa pamoja na mali zote.
Kamanda wa Polisi wa Iringa, Ramadhani Mungi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza wanamshikilia mwanamke huyo ili kumfikisha mahakamani kwa kitendo alichokmifanya ambacho kimeacha gumzo kijiji cha Mwatasi, huku familia ya watoto ikiwa katika majonzi makubwa ya kupoteza watoto wao.