STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, August 8, 2012

Azam yazidi kung'ang'ania Redondo yaionya Simba

WAKATI kiungo Ramadhani Chombo 'Redondo' akisisitiza kuwa, hana mkataba na klabu ya Azam na ndio maana ameamua kusaini kuichezea Simba, uongozi wa klabu ya Azam umeendelea kushikilia msimamo kwamba kiungo huyo ni mali yao na Simba 'imeliwa'. Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassor alisema wao sio wehu wakurupuke kung'ang'ania kwamba Redondo ni mali yao iwapo hawana mkataba nae na kudai Simba wanajisumbua na kuweza kuwakuta kama lililowakuta kwa mchezaji Ibrahim Juma 'Jebba' waliokuwa wakimng'ang'ania kutaka kumsajili. Nassor ambaye ni maarufu kwa jina la 'Father' alisema, Redondo ni mali yao kwa vile wana mkataba utakaomalizika mwakani mwezi Juni, na hivyo Simba kama wanamhitaji kiungo huyo ni wajibu wa kuzungumza nao ili wawape kwa utaratibu unaotakiwa. "Sio sio wajinga kumng'ang'ania Redondo, pia hatuwezi kumzuia iwapo anataka kwenda Simba, ila taratibu zinatakiwa kufuatwa kwa vile tunaye mkataba nae unaomalizika Juni mwaka 2013," alisema Nassor. Alisema kinachoendelea kwa Simba na Redondo hakutofautiani na sakata la Jebba ambaye Simba ilidai kumsajili na kwenda nae kwenye michuano ya Ujirani Mwema kabla ya kubaini kwamba walikuwa wakijisumbua kutokana na ukweli mchezaji huyo alikuwa na mkataba na Azam. Hata hivyo Redondo akizungumza na vyombo vya habari jana, alisema yeye hana mkataba na Azam kwa vile mkataka wake wa awali ulishaisha tangu Juni mwaka huu, pia akisema kilichomfanya aondoke ni kutoitwa na viongozi kupewa mkataba mpya. Pia alisema 'kifungo' cha miezi minne alichopewa na uongozi wa Azam kwa tuhuma za utovu wa nidhamu ni sababu nyingine iliyomfanya 'aipe' kisogo timu hiyo na kutua Simba ambayo aliichezea kabla ya kutua Azam misimu miwili iliyopita.

Safari ya Sikinde Marekani 'yaiva'

BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park 'Sikinde', imesema itaondoka nchini kwenda Marekani, kushiriki matamasha ya kimataifa mara baada ya sikukuu ya Idd inayotarajiwa kusherehekewa mwishoni mwa mwezi huu. Katibu wa bendi hiyo, Hamis Milambo alisema mipango ya safari imekamilika ikiwemo kurejea kwa viongozi na wanamuziki wao waliokuwa nchini humo kuweka mambo sawa. Alisema viongozi hao, Hassani Bitchuka 'Stereo' na Ally Jamwaka waliowawakilisha katika mazungumzo juu ya safari hiyo walisharejea na kusema kuwa kila kitu kimeenda sawa na kilichobaki ni kukamilisha mipango ya safari yao. "Kila kitu kimeenda sawa huko Marekani na viongozi na wanamuziki wetu wamesharejea na kwa sasa tunajipanga kwa ajili ya safari hiyo ambayo itafanyika baada ya kumalizika kwa sikukuu ya Idd," alisema. Aliongeza kuwa wakati wakijiweka tayari kwa ziara hiyo, pia bendi hiyo inaendelea na mipango ya kuzimalizia nyimbo mbili zilizosalia katika albamu ijayo sawia na kujiandaa na mpambano wao na watani zao, Msondo Ngoma. Msondo na Sikinde zinatarajiwa kuchuana katika maonyesho mawili yatakayofanyika katika miji ya Dar na Zanzibar wakati wa sikukuu ya Idd.

Rado awabeba 'Watoto wa Kanumba'

NYOTA wa filamu ambaye pia ni msanii wa muziki wa kizazi kipya, Simon Mwapagata 'Rado' ameachia filamu mbili mpya za 'Hatia' na 'Tamaa Yangu', huku akijiandaa kufyatua nyingine iitwayo 'Madduhu'. Alisema filamu hiyo imesharekodiwa ikiwa imewashirikisha wasanii chipukizi
walioibuliwa na marehemu Steven Kanumba katika filamu zake za 'This is It', 'Uncle JJ' na 'Big Daddy'. Alisema anaendeleza vipaji vya wasanii chipukizi ili kuenzi mchango na juhudi za Kanumba, aliyemtaja kama msanii aliyekuwa akimzimia na kuchangia kwake kutumbukia kwenye sanaa japo alisaidiwa na Jumanne Kihangale 'Mr Tues'. "Nimeingiza sokoni filamu zangu za 'Hatia', 'Tamaa Yangu' na 'XXL', wakati nikiwa nimesharekodi filamu yangu mpya iitwayo 'Madduhu' niliocheza na 'watoto wa Kanumba', kama njia ya kuendeleza vipaji vyao na kumuenzi," alisema. Rado aliwataja wasanii hao chipukizi alioigiza nao katika filamu hiyo aliyopanga kuitoa mwezi ujao kuwa ni pamoja na Hanifa Daudi 'Jennifer', Jamila Jailawi na Jalillah Jailawi. Alisema licha ya kuendekeza 'libeneke' kwenye fani ya uigizaji akifyatua kazi zake binafsi baada ya kipindi kirefu kuzifanya kazi za wenzake, pia anaendelea kukamua kwenye muziki kama kawaida. "Siwezi kuacha muziki, mie nagonga vyote kwani hivi ni vipaji ambavyo Mungu kanijali na siwezi kuzembea kuvitumia," alisema msanii huyo aliyepata umaarufu kupitia tamthilia ya 'Jumba la Dhahabu' enzi hizo akiwa na kundi la Fukuto Arts Proffesional.

Mtanzania kuwania taji jipya la IBF/USBA

MTANZANIA Rajabu Maoja anatarajiwa kuwa bondia wa kwanza wa Tanzania kuwania taji jipya la IBF Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi, lililoanzishwa na Shirikisho la Kimataifa la Ngumi za Kulipwa, IBF/USBA. Kwa mujibu wa Rais wa IBF/USBA kwa nchi za Afrika na Ghuba ya Uajemi, Onesmo Ngowi, Mtanzania huyo atapamba ulingoni Septemba 1, mjini Windhoek, Namibia kupigana na bingwa wa nchi hiyo, Gottlieb Ndokosho. Ngowi alisema IBF/USBA limeanzisha taji hilo kwa nia ya kupanua wigo kwa mabondia wa Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuna ya Uajemi kujitangaza zaidi katika mchezo huo kupitia IBF/USBA. "Katika mpango kabambe wa kupanua wigo wa mabondia wa Bara la Afrika na wale wa Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi, IBF.USBA imezindua taji jipya litakalojulikana kama 'IBF Africa, Middle East and Persian Gulf Title'," alisema Ngowi. Ngowi alisema pambano la kwanza la taji hilo linalojulikana kwa kifupi kama IBF/AMEPG, litafanyikia nchini Namibia likimhusisha Maoja na Ndokosho. Alisema pambano jingine linatarajiwa kufanyika katika jiji la Accra, Ghana kati ya bondia Richard Commey wa Ghana anayejifua kwa sasa nchini Uingereza atakayepigana na bondia kutoka Qatar ambayo iko katika Ghuba ya Uajemi. Ngowi ambaye ni Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBC, alisema juhudi hizo za IBF/USBA zinakuja wakati shirikisho hilo limeanzisha programu ya 'Utalii wa Michezo' na kuziteua Tanzania na Ghana kama nchi za mfano kwa kipindi cha miaka mitatu. Aliongeza fura iliyojitokeza ni fursa nzuri kwa mabondia wa Tanzania kuzichangamkia nafasi hiyo kuweza kuwania mataji makubwa na kujitambulisha kimataifa. Ngowi alibainisha kuwa kwa sasa ni mabondia wachache sana wa Tanzania wenye viwango vya juu ukilingamisha na mabondia wa nchi za Ghana, Namibia, Afrika ya Kusini, Uganda, Nigeria na Misri. Aliahidi kuwapatia mabondia wa kitanzania nafasi za kugombea mataji haya kila panapotokea nafasi hizi ili kuweza kufika walipo wenzao. Mwisho

Kiiza 'awafunika' Okwi, Ssentongo Uganda

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa timu ya Yanga, Hamis 'Diego' Kiiza ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Uganda kwa mwezi Julai akiwafunika nyota wengine wa nchi hiyo mshambuliaji anayeichezea Simba, Emmanuel Okwi. Kwa mujibu wa mtandao wa habari za michezo wa Kawowo, Kiiza anayeichezea pia timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes' alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo ya Julai na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini Uganda, USPA. Mtandao huo ulisema kuwa, Kiiza alifanikiwa kupata jumla ya kura 520, pointi 100 zaidi na aliyeshika nafasi ya pili katika uwaniaji wa tuzo hiyo, kinda la timu ya taifa ya vijana U20, Julius Ogwang aliyevuna pointi 420. Imeelezwa Kiiza amefanikiwa kupata tuzo hiyo kutokana na kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame, kwa mara ya pili mfululizo, huku ikimfagilia kwamba licha ya kuibebesha klabu yake ubingwa, pia alinyakua kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora kwa mabao sita aliyoyafunga. Hata hivyo ukweli aliyenyakua tuzo hiyo ni Said Bahanunzi pia wa Yanga aliyeifunga idadi kama hiyo ya mabao sita akilingana na Taddy Etekiama wa AS Vita, wakati Kiiza alionekana idadi hiyo ya mabao sita kwa kuongezewa kimakosa bao la beki Stephano Mwasika. Mbali na Kiiza na Ogwang, mwingine aliyekuwa katika Tatu Bora ya waliong'ara mwezi Julai ni mchezaji wa mpira wa wavu, Lawrence Yakan wa mabingwa wa michuano ya kimataifa ya Wavu ya Kampala (KAVC), Sport-S, aliyepata kura 415. Mwisho