STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, March 11, 2013

Simba yakana kuwasimamisha wachezaji wake
Na Ezekiel Kamwaga 
JANA na leo, zimetolewa habari tofauti kuhusiana na klabu ya Simba ambazo uongozi umeona ni vema uzitolee ufafanuzi kwa lengo la kuweka rekodi sawa. Ufuatao ndiyo ufafanuzi wa taarifa hizo.

1. SIMBA KUZUIWA HOTELINI
SAA mbili kabla ya mechi ya jana baina ya Simba na Coastal Union ya Tanga, mmiliki wa Saphire Court Hotel alitoa taarifa kwa uongozi wa Simba kwamba ataizuia timu isiondoke hotelini kwa vile anaidai Sh milioni 25 na anataka alipwe zote jana.

Ikumbukwe kwamba Simba imekuwa ikikaa hotelini hapo kwa muda mrefu sasa wakati inapoweka kambi. Pia, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba walifanya mkutano na wachezaji wote wa Simba katika hoteli hiyo usiku wa kuamkia jana.
Wamiliki wa hoteli hiyo hawakutoa taarifa yoyote kwa uongozi wakati huo juu ya dhamira yao hiyo.Wamiliki hao hawakutoa taarifa asubuhi ya mechi na walisubiri mpaka wakati timu inataka kuondoka ndiyo wakachukua hatua hiyo.
Kwa uongozi wa Simba, hatua hiyo ilikuwa ya ghafla mno. Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba ulikuwa umemlipa mmiliki huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika kipindi cha miezi 10 iliyopita.
Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya Angola, Saphire walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni kwamba klabu yetu ina utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu wasiolipa kama hatua hiyo ya wamiliki wa Saphire inavyotaka kueleza.
Uongozi wa Simba tayari ulitoa ahadi ya kumaliza deni lote inalodaiwa baada ya kulipwa fedha zake inazodai zinazotakiwa kulipwa wakati wowote mwezi huu au ujao.
Simba inadai zaidi ya Sh milioni 500 kwa wadai wake wawili (Etoile du Sahel ya Tunisia na Push Mobile) na inataraji kulipwa fedha hizo. Itakapolipwa fedha zake hizo, Simba itakuwa na uwezo wa kulipa madeni yake yote inayodaiwa na watu binafsi na makampuni bado ikabaki na fedha za kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.
Wakati ikisubiri ilipwe fedha zake inazodai, Simba itaendelea kulipa madeni yake taratibu kwa kadri itakavyoweza. Ifahamike kwamba kwa sasa chanzo kikuu cha mapato ya klabu ni fedha za mapato ya milangoni na za udhamini wa bia ya KILIMANJARO ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu.
Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na matumizi, Simba SC imeanza mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini kokote walipo duniani ili kuongeza mapato yake.
Tayari mawasiliano yameanza na wenzetu wa Sunderland ya England kupitia mradi wao wa Invest in Africa ili Simba nayo ifaidike. Simba SC inaomba pia umma ufahamishwe kwamba klabu ya soka kudaiwa si dhambi.
Iwapo klabu kubwa na tajiri duniani kama vile Manchenster United, Real Madrid na Liverpool zina madeni, inakuaje madeni ya Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati) yaonekane kama kitu kigeni?
Uongozi unaahidi kwamba utalipa madeni yake yote kwa kadri utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya kibenki, credit worthiness ya mteja inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa. Simba inapenda kusisitiza kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima kubwa na bado inavutia watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Simba ni CREDIT WORTHY INSTITUTION !
Hata hivyo, uongozi wa Simba unafikiria kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wamiliki wa Saphire Court Hotel kwa kitendo chake cha kuwazuia wachezaji na viongozi wa Simba hotelini kabla ya mechi ya jana. Simba inachukulia kitendo kile kama hujuma na kisheria kinaangukia katika kundi la FORCED IMPRISONMENT kwa wamiliki kuwazuia watu kinguvu hotelini kwao.
Wamiliki hawakutoa notisi kwa uongozi au taarifa yoyote ya mdomo au maandishi kabla ya kuchukua hatua hiyo. Lengo lilikuwa ni kuchafua heshima na hadhi ya Simba kwa hoteli ambayo imetoka kulipwa Sh. milioni 15 wiki mbili tu zilizopita.
Uongozi wa Simba SC unaapa kuilinda na kuitetea hadhi ya klabu yetu kwa nguvu zetu zote, akili zetu zote na maarifa yetu yote.

2. WACHEZAJI, BENCHI LA UFUNDI KUFUKUZWA

KUNA taarifa zimeenezwa pia kwamba kuna wachezaji wa Simba wamesimamishwa au kufukuzwa kuchezea Simba.
Habari hizi nazo hazina ukweli wowote Ukweli ni kwamba, uongozi wa Simba umetoa ruksa kwa benchi la ufundi kupanga timu ambayo litaona inafaa kwa mechi husika.
Uongozi hautaingilia, kwa namna,njia au aina yoyote ile utendaji wa benchi la ufundi. Hakuna mchezaji yeyote aliyesimamishwa hadi sasa.
Pia uongozi unakanusha taarifa kuwa Daktari Mkuu wa Klabu, Cosmas Alex Kapinga, kuwa naye ameachia ngazi. Habari hizi hazina ukweli kwani daktari huyo ana ruhusa ya kikazi ya wiki mbili inayojulikana.

HITIMISHO
Katika namna ya kipekee kabisa, uongozi wa Simba unapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa washabiki wake waliojitokeza Uwanja wa Taifa na kuisapoti timu kwa asilimia 100.
Uongozi unathamini sana mchango wa wanachama wake na unaahidi kufanya kila unachoweza kuwarejeshea tena furaha mioyoni mwao.
Pia unatumia nafasi hii kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi ambao walicheza mechi ya jana katika mazingira magumu. Walicheza bila ya kufanya warm up na wakitoka kuwa wamezuiwa hotelini jambo ambalo lingeweza kuwaondoa mchezoni.

WAMILIKI WA TELEVISHENI WATISHIA KUSIMAMISHA MATANGAZO KISA VING'AMUZI

   Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi

WAMILIKI wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) wameitaka serikali kuacha mara moja utaratibu wake wa sasa wa kulazimisha matangazo yote ya televisheni nchini kurushwa kwa digitali kupitia ving'amuzi na badala yake irejeshe utaratibu wa zamani kwani hivi sasa wao wamekuwa wakipata hasara kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo, mwenyekiti wa MOAT, Dk. Reginald Mengi, ambaye aliambatana na wakurugenzi wa Sahara Communications (Star TV) na wa Clouds Media, alisema kuwa utaratibu wa sasa unaowalazimisha wananchi wote kupata matangazo ya televisheni kupitia ving'amuzi umekuwa ukiwakosha wengi matangazo hayo na matokeo yake, wao huathirika kwa kukosa pesa za kuendeshea shughuli zao kupitia matangazo ya kibiashara kama ilivyokuwa zamani.

Wamiliki hao wameitaka serikali kutoa uhuru kwa wananchi wote kupata matangazo kwa njia wanazotaka wenyewe za digitali na analojia (antena za kawaida) kulingana na utashi wao na pia uwezo wao kiuchumi badala ya ilivyo sasa ambapo wengi wamekuwa wakikosa uwezo wa kununua ving'amuzi na kuvilipia kila mwezi, hivyo kukosa matangazo yao na mwishowe kuwaingizia hasara wamiliki wa vituo vya televisheni.

Mengi ameongeza kuwa hadi sasa bado wanaendelea kufanya taratibu za kuisihi serikalini itekeleze yale wanayoomba na kwamba, wataendelea kufanya subira kwa miezi kati ya miwili hadi mitatu kuanzia sasa na wakiona kuwa bado serikali iko kimya, watakachokifanya ni kufunga vituo vyao vyote vya televisheni kwani ni bora waendelee na biashara nyingine kuliko ilivyo sasa ambapo kila uchao wamekuwa wakipata hasara.

Serikali ililazimisha kuanza urushaji wa matangazo kupitia ving'amuzi kuanzia Januari Mosi, 2013 na kuzima kwa awamu matangazo yote ya televisheni kupitia njia iliyokuwa ikitumika awali ya analojia isiyohitaji ving'amuzi bali antena za kawaida.

TFF YAMLILIA ATHUMANI KILAMBO

Athuman Kilambo (wa kwanza kushoto waliosmama) enzi za uhai wake akiwa na kikosi cha Pan African miaka ya 1980

Na Boniface Wambura 
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga, Pan Africans na Taifa Stars, Athuman Kilambo kilichotokea jana usiku jijini Dar es Salaam.
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Kilambo akiwa mchezaji, na baadaye kocha alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali alizochezea na kufundisha zikiwemo Pan Africans na Cargo, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Kilambo, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na klabu ya Pan Africans na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko ya kocha huyo aliyeinoa Pan tangu mwaka 1975 hadi 1984 akiisaidia kutwaa ubingwa wa Tanzania mwaka 1982 na kutetesha soka la Afrika yalifanyika jionio ya leo kwenye makaburi ya Kisutu mkoani Dar es Salaam ambapo TFF imetoa ubani wa sh. 100,000.
Marehemu Kilambo amefariki kutokana na kusumbuliwa kwa muda na ugonjwa wa Kansa ya Koo na inaelezwa marehemu ameacha watoto watano, watat wa kiume wakiwemo nyota wa zamani wa Yanga na Reli Ramadhani Kilambo na Athuman Kilambo.
Mungu aiweke roho ya marehemu Kilambo mahali pema peponi. Amina 

FIFA YATISHIA KUIFUNGIA TANZANIA, KISA SERIKALI

Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.
FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA. “Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake.
Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili kwanza.
“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.