STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, July 23, 2013

Huyu ndiye Hussein Javu mkali wa mabao wa Mtibwa Sugar

Javu wa tatu toka kushoto akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar
Jamaa nouma, Ona alivyuowaacha akina Himid katika pambano baina ya timu zao
Hapa akijifua katika timu ya taifa, Taifa Stars
moza
Akiwajibika uwanjani na kikosi cha Stars
Akitokelezea kibrazamen akiwa home
INGAWA anadai amefunga magoli mengi kiasi hakumbuki idadi yake kamili, lakini Husseni Javu anasema mabao aliyowafunga Yanga katika pambano la duru la kwanza la Ligi Kuu msimu uliopita ndiyo matamu asiyoyasahau kwa urahisi.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Sept. 19, mwaka jana, mshambuliaji huyo nyota wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, alifunga magoli mawili yaliyotosha kuipa Mtibwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Yanga na kusababisha aliyekuwa kocha wa timu hiyo ya Jangwani, Tom Saintfied kutimuliwa klabuni hapo akiwa na siku 77 tu.
Javu anasema kwa jinsi alivyoyafunga kiufundi na kuzima ngebe za wapinzani wao waliotamba kushinda kabla ya pambano hilo ndiyo inayomfanya asiyasahau.
"Kwa yeyote aliyeyaona atakubaliana nami yalikuwa ya ufundi na kubwa zaidi ni kukata kilimilimi cha Yanga kwa kuwalaza mabao 3-0 licha ya tambo zao kwamba wangetuchapa Jamhuri," anasema.
Javu shabiki mkubwa wa Manchester United na anayemhofia beki wa zamani wa Simba aliyetua Coastal Union, Juma Nyosso anasema hata hivyo pambano gumu kwake lisilofutika kichwani ni lile la Mtibwa na Mgambo JKT.
Anasema anaikumbuka mechi hiyo ya duru la pili lililochezwa Mkwakwani Tanga kwa sababu ya kuchezewa vibaya na beki aliyekabana naye asiyemkumbuka jina kiasi cha kumtia hasira na kulimwa kadi ya njano kabla ya kocha wake Mecky Mexime kumpumzisha ili kumwepusha na kadi nyekundu.
"Sijawahi kukutana na mechi ngumu kama ile ya Mgambo JKT hasa beki yake iliyokuwa inacheza kwa vurugu hadi nikapewa kadi ya njano na kumfanya kocha anitoe nje,"anasema.
Anasema licha ya vurugu hizo anashukuru Mtibwa walishinda bao 1-0 kupitia Salvatory Mtebe.

YANGA
Javu aliyeanza soka tangu akisoma Shule ya Msingi Turiani-Kilimanjaro, Morogoro na chandimu akikipiga Mwembeni Stars, amekuwa akitajwa kutua Yanga kwa msimu ujao, japo mwenyewe ameziruka taarifa hizo.
Mkali huyo ambaye hajaoa japo ana mchumba na watoto wawili kati ya watatu aliyokuwa nao baada ya mmoja kufariki, anakiri Yanga na Simba zilishamfuata kumtaka ajiunge nazo, ila hajasaini kokote.
"Sijasaini kokote kwani Simba na Yanga ziliponifuata nilizieleza nina mkataba na Mtibwa hivyo wazungumze na viongozi ili waafikiane," anasema.
Anadai tangu baada ya hapo hajajulishwa chochote na kushangaa kudaiwa  ameshamwaga wino Jangwani, huku akizushiwa pia ni majeruhi wa kudumu.
"Taarifa hizi zinashangaza wakati ni juzi tu tumemaliza ligi na kuichezea Mtibwa karibu mechi zote sasa majeraha hayo yametoka wapi," anahoji.
Anadai taarifa hizo zimempa usumbufu kwa kocha na daktari wake wakidhani aliumia kwenye 'ndondo' wakati hazina ukweli.
Javu anayependa kula chakula kizuri kwa afya na kunywa juisi , anasema kama Yanga na Mtibwa wamekubaliana juu yake, yeye hajajulishwa.
Hata hivyo anasema kama Yanga imemtaka kweli wamalizane na uongozi wake anaodai anauheshimu kwa kumtoa mbali kisoka tangu alipotua timu ya vijana enzi za kocha anayemsifia 'King' Abdallah Kibadeni.
"Hakuna asiyependa kuzichezea timu kubwa hivyo Yanga wakimalizana na Mtibwa nami nikaridhishwa na masilahi sitakuwa na tatizo lolote, soka ni ajira yangu na kokote nacheza,"anasema.
Javu (kulia) akiwa na jamaa yake Bakar Seblungo 'Beka'

TUZO
Hussein Omar Javu, alizaliwa Februari 16, 1988 Turiani Morogoro akiwa mtoto wa pili kati ya sita wa familia yao na alisoma Shule ya Msingi Turiani Kilimanjaro kabla ya kubobea jumla katika soka.
Anasema wakati akiibuka katika soka alikuwa akiitwa Hussein Masha, bila kujua sababu, ingawa anamkumbuka nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kutamba na Pamba, Simba na Taifa Stars.
"Mtaani walikuwa wakiniita Masha, cha ajabu Masha alikuwa kiungo mimi tangu utoto nacheza ushambuliaji ila nililizoea jina hilo,"anasema. 
Anasema wakati akiichezea chandimu aliumia tumboni na kumfanya baba yake amzuie kucheza kwa miaka mitatu kabla ya kubembelezwa wadau wa soka kijijini kwao wakiongozwa na Mzee Hamis Cheza na kurejea tena uwanjani.
"Kama siyo Mzee Hamis sidhani kama ningecheza tena kwani baba hakutaka kusikia habari za soka akihofia ningeumia tena, niliporuhusiwa nilijiunga Kingstone." anasema.
Mkali huyo anayeitaka serikali kuwekeza katika soka la vijana kwa kuboresha shule za michezo hasa kuzisaidia 'academia' zilizopo ili kuibua na kukuza vipaji, anasema baada ya kuichezea Kingstone katika Ligi Daraja la Tatu alihamia kwa mahasimu wao Docks na kuongeza uhamasa mkubwa mpaka sasa.
Alipokuwa Docks alifuatwa na Alphonce Modest kumshawishi ajiunge Mtibwa iliyokuwa ikisaka vijana wa kuunda timu ya vijana ambapo hata hivyo alikataliwa kabla ya Kibadeni kumkingia kifua na kumbakisha akishajiliwa mwaka 2007.
Akiwa na timu ya vijana walishiriki michuano ya Uhai na kufanikiwa kuibuka  Mfungaji Bora akiifungia timu yake iliyomaliza nafasi ya tatu jumla ya mabao 7.
Javu anasema kabla ya tuzo hiyo alishanyakua tuzo nyingine kama hiyo katika michuano kadhaa ya mchangani mjini Morogoro na ameendeleza moto wa mabao hata alipopandishwa timu ya wakubwa ya Mtibwa aliyonayo mpaka sasa.
Anasema japo hajapata mafanikio makubwa katika soka, anashukuru amenunua kiwanja, kutwaa tuzo na mataji kadhaa kama ya Tusker na Mapinduzi akiwa na Mtibwa mbali na kumudu maisha na familia yake.
Ndoto za Javu ni kucheza soka la kulipwa na anasema analizwa na kifo cha mwanae huku akiwataja King Kibadeni, wazazi wake, rafikie Bakari Seblungo na kaka yake Mrisho Javu kama waliomsaidia kufika alipo.
Javu anayewataka wachezaji wenzake kupendana na kuzingatia nidhamu anadai anaimani kubwa Stars kufuzu fainali za CHAN kwa mara ya pili baada ya zile za mwaka 2009.

Rais JK akutana na Tony Blair Ikulu Dar es Salaam

 Rais Jakaya Kikwete akiwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair na mkewe Cherrie Blair alipokutana nao Ikulu jijini Dar es salaam leo. (PICHA NA IKULU)



Majanga: Msafara wa mazishi ya wanajeshi waliouwawa Darfur wapata ajali

 Picha mbali mbali za ajali ya gari iliyokua katika msafara wa maziko ya wanajeshi waliouawa Darfur iliyotokea Mwanakwerekwe sokoni umbali wa mita 300 kutoka Makaburi ya Mwanakwerekwe ambapo ndiko walipozikwa Wanajeshi hao.(Picha na Haroub Hussein).






                                            Gari lililopata ajali

Lililoua mdogo wake kwa mibangi lanaswa na Polisi

JESHI la polisi mkoa wa Singida limefanikiwa kumkamata Elibariki Alphoce (21) mkazi wa kijiji cha Kizega wilaya ya Iramba, anayetuhumiwa kumuua mdogo wake Mariam (9) mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Kizega.

Elibariki anatuhumiwa kumuua mdogo wake Mariam Julai 16 mwaka huu katika kijiji cha Kizega kwa kumkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili na kisha kuteganisha kichwa na kiwiliwili.

Ilielezwa kuwa Elibariki ni mtumiaji sugu wa madawa ya kulevya aina ya bangi.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida ACP Geofrey Kamwela, amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa Julai 18 mwaka huu akiwa amejificha kando kando ya mto Ruruma wa kijiji cha Ruruma tarafa ya Kiomboi.

Polisi Dar wayanasa majambazi 8 na silaha 7 lakana Mnyika kukoswa na bomu

IMG_9423
Baadhi ya askari polisi wakionyesha kwa waandishi wa habari silaha zilizokamatwa kutoka kwa watuhumiwa wa matukio ya ujambazi.

IMG_9432
DCP Mlege akitoa taarifa ya mafanikio ya Jeshi hilo kwa waandishi wa habari ambapo akizungumzia suala la Mh. Mnyika amesema askari No. E. 5340 D/CPL Julius aliyekuwa ndani ya gari la polisi PT. 1902 alikuwa anasogeza boksi lenye mabomu ya kutoa machozi ya kurusha kwa mkono, kwa bahati mbaya bomu hilo lililipuka ndani ya gari hilo na halikuleta madhara yeyote kwa askari polisi wala raia waliokuwa eneo la uwanja wa Sahara uliopo Mabibo ambako chama cha CHADEMA kilikuwa kifanye mkutano wa hadhara tarehe 21 Jula 2013 kinyume na utaratibu.

Jeshi la Polisi Kanda maalum Dar es Salaam limefanikiwa kukamata sila 5 ikiwemo SMG moja, Shortgun mbili, Riffle Mark 3 tatu, Pisto moja, Risasi 56, Maganda ya Risasi 17 na Majambazi 8.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishna wa polisi kanda hiyo, DCP A.M. Mlege amesema zoezi hilo lilifanyika Julai 18 mwaka huu katika maeneo ya Magomeni wilaya ya Kinondoni.

Amesema pia Jeshi hilo limeweza kukamata magari ya wizi matano, Injini tatu za magari, Vipande vya magari yaliyokatwa spea na wezi watano wa magari.

Katika hatua nyingine Jeshilo limekanusha habari zilizotolewa katika vyombo vya habari kuwa mbunge wa Jimbo la Ubungo Mh. John Mnyika kukoswa na bomu na kumjeruhi mmoja wa wafuasi wake.

Aidha limeomba siku zingine kabla ya kutoa habari ni vizuri likaulizwa ili kuthibitisha au kukanusha.

DCO Mlege amesema pia Jeshi la polisi Kanda maalum Dar es Salaam limemkamata tapeli hatari anayetumia namba tofauti za mitandao ya simu na majina ya watu maarufu anajulikana kwa jina la Mfaume Omari maarufu kama ‘Mau’.

Chanzo - MOBLOG 

Rais wa Zanzibar aongoza mazishi wa wanajeshi waliouwawa Darfur

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, (wa tatu kulia) akijumuika na Vingozi na Waislamu wengine katika kuwaswalia  Merehemu Sgt. Shaibu Shehe Othman, na Cpl Mohammed Juma Ally katika Msikiti wa Nuru Muhammad, Mombasa mjini Unguja leo. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)
 Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wakibeba Jeneza la mwili wa Marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman, baada ya kuwasili mjini Zanzibar akiwa ni miongoni mwa wanajeshi 7 waliouwawa kwa kupigwa risasi Jimbo la Darfur nchini Sudan hivi karibuni.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, akitia udongo katika kaburi la Marehemu Sgt. Shaibu Shehe Othman, aliyezikwa leo katika makaburi ya Mwanakwerekwe mjini Unguja. 
 Baadhi ya Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania na Ndugu na Jamaa wa marehemu Sgt Shaibu Shehe Othman, na  Cpl Mohammed Juma Ally wakishiriki mazishi hayo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, (katikati) na Viongozi na Waislamu, wakiangalia  Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania, walipokuwa wakitoa heshima za mwisho kwa marehemu Sgt. Shaibu Shehe Othman, wakati wa mazishi yake katika makaburi ya Mwanakwerekwe leo.

SHIWATA watakiwa kuchangia ujenzi wa nyumba Mkuranga

Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Twalib 'Teacher' (kushoto)
Na Mwandishi Wetu
MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umewataka wanachama wake kuchangia ujenzi wa nyumba zao katika kijiji cha Mwanzega, Mkuranga ili kukamilisha mradi huo.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Caasim Taalib alisema jana Dar es Salaam katika mkutano wa wanachama wanaochangia ujenzi ambapo mpaka sasa nyumba 29 zimekamilika na wanachama 220 wamechangia ujenzi na jumla zilizokusanywa ni mil. 82.5.
Alisema SHIWATA haina fedha za kujenga nyumba za wanachama wake wala haina chanzo cha mapato kama si kwa njia ya kuchangishana na baada ya hapo kuwakabidhi wale waliokamilisha uchangiaji wa ujenzi wa nyumba hizo.
‘Ujenzi wa nyumba za wasanii utafanikiwa kwa kila mwanachama kuchangia nyumba yake kwa kujiaminisha kuwa hakuna utapeli wala biashara katika gharama za ujenzi wa nyumba hizo’alisema Taalib.
SHIWATA ambayo inaundwa na wasanii, wanamichezo, wanahabari na vijana wapatao 7,000 ilikuwa ikabidhi nyumba Agosti mwaka huu kwa mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Jellah Mtagwa na wasanii wengine 14 ambao wamekamilisha michango ya ujenzi  wa nyumba zao katika kijiji chao cha Mwanzega Kimbili, Mkuranga.
Wengine watakaokabidhiwa nyumba zao ni msanii maarufu nchini, Lumole Matovola ‘Big’ wa Bongo movie ambaye ni mwanachama wa SHIWATA wangine ni Mwandishi wa Habari, Josephine Moshi, Farida Ndimbo wa Jeshi la Magereza, Flora Kafwembe wa JKT Mgulani na Nyanza Kisadugwa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).  
Mpaka sasa SHIWATA imejenga nyumba 29 kwa ajili ya wasanii katika eneo la hekari 300 na wanajiandaa kulima shamba la hekari 500 walizonazo ili kujikwamua kimaisha.
              

Master Kinyogoli awafua mabondia Idd Mnyeke, Ibrahim Class

 Bondia Ibrahimu Class 'King Class Mawe' kushoto akipambana na Iddy Mnyeke wakati wa mazoezi yanayoendelea katika Kambi ya Ilala Amana CCM mabondia hao wanafanya mazoezi kwa ajili ya mashindano yao yatakayo fanyika baada ya kumarizika mwezi mtukufu wa Ramadhani 


Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hao watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani 

Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hawo watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani kulia ni kocha Mkongwe Habibu Kinyogoli 'Master' 
Bondia Omari Bai kushoto akisimamiwa kupiga begi na Kocha Kondo Nassoro wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kambi ya Ilala 
Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hawo watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani kulia ni kocha Mkongwe Habibu Kinyogoli 'Master' 
BONDIA IDDY MNYEKE AKIWA KATIKA POZI
Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hawo watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani Picha na BLOG YA SUPER D
Bondia Iddy Mnyeke  akipambana na Ibrahimu Class 'King Class Mawe' wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kamba ya Amana CCM Dar es salaam mabondia hawo watapanda ulingoni kuwakabili wapinzani wao baada ya kwisha kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani 
IDDY MNYEKE
BONDIA OMARI BAI AKIPIGA BEGI
Bondia Omari Bai kushoto akisimamiwa kupiga begi na Kocha Kondo Nassoro wakati wa mazoezi yaliyofanyika katika kambi ya Ilala

Kim atamba Stars imjeiva kuwang'oa Uganda The Cranes

Kim Poulsen
 Na Boniface Wambura
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwenye mechi ya marudiano ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayochezwa Jumamosi jijini Kampala.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo, Kim amesema tangu kikosi chake kimeingia kambini Julai 14 mwaka huu, wachezaji wamekuwa wakifanya vizuri kwenye mazoezi na wako tayari kwa ajili ya mechi hiyo.

“Uganda ni timu bora kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Mechi itakuwa ngumu, tunaamini tunakwenda kufanya vizuri. Tayari tunayo mikakati kwa ajili ya mechi hiyo, tunakwenda kuikamilisha Kampala,” amesema Kim.

Hata hivyo, Kim amesema licha ya mwitikio mzuri wa wachezaji kwenye mazoezi lakini wanakabiliwa na changamoto ya wengi wa wachezaji kuwawamefunga wakati wachezaji wanapokuwa kambini wanatakiwa kula, kunywa na kupumzika.

“Hiki ni kipindi kigumu kwa mpira wa miguu, na suala la kufunga ni la kiimani ambapo hatuwezi kuwazuia wachezaji kufunga. Karibu nusu ya wachezaji wanafunga, hii ni changamoto ambayo tunaiheshimu,” amesema Kim na kuongeza kuwa ni wazi kikosi chake cha kwanza kitakuwa na mabadiliko baada ya beki Shomari Kapombe kwenda kwenye majaribio nchini Uholanzi.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaondoka Mwanza kesho (Julai 24 mwaka huu) saa 7.25 mchana kwa ndege ya PrecisionAir na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe saa 8.15 mchana.

Wachezaji waliomo kwenye msafara huo ni makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.

Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.

Kampuni ya Isere Sports yagawa vifaa


Mkurugenzi wa masoko wa Kampuni ya Isere Sports inayoshuhulika na uagizaji na uuzaji wa vifaa vya michezo,Abbas Isere (kulia) akimkabidhi jezi Katibu Mipango wa timu ya Fresh Niga ya Kilwa Masoko ,Maulid Mtika maarufu Milulu zenye thamani ya Sh. 350,000.

Isere sports yatoa jezi kwa timu ya Kilwa Masoko
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Vifaa vya michezo, Isere Sports imetoa jezi seti moja yenye thamani ya sh. 350,000 kwa timu ya Fresh Niga ya Kilwa Masoko inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu wilaya ya Kilwa.
Katibu Mipango wa timu ya Fresh Niga, Maulid Mtika akipokea jezi hizo jana alisema msaada huo ni mfano wa kuigwa na wafanyabiashara wengine wenye uwezo wa kusaidia kuibua vipaji vya vijana kwenye soka.

Mtika ambaye ni maarufu kwa jina la Milulu alisema imefika wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litafute njia ili lishuke mpaka ngazi ya wilaya kujua matatizo yanawakabili timu ili kutafuta vipaji vya wachezaji watakaochukua nafasi ya waliopo Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

'Tunao vijana wenye vipaji vya kucheza soka kufikia ngazi ya timu ya taifa, kinachowanyima nafasi ya kuonekana ni vifaa vya michezo tunaomba TFF ishuke mpaka ngazi ya wilaya kuwasaidia vijana kukuza vipaji.
Alitoa wito kwa wadau wa michezo kujitokeza kusaidia timu ambazo hazina wafadhili lakini kuna vijana ambao wako tayari kuonesha vipaji vyao
Mkurugenzi wa Masoko wa Isere Sports, Abbas Isere alisema jana kuwa msaada huo ameutoa ili kukuza vipaji vya soka katika wilaya hiyo ambao wanahitaji misaada kama hiyo ili kuendeleza vipaji.