STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, August 25, 2013

Man City yachinjwa Cardiff, Saldado akiendelea kuibeba Spurs

Hero: Fraizer Campbell's goals could prove vital all season for the newly-promoted side
Campbell (10) akishangilia moja ya mabao yake na wachezaji wenzake wa Cardiff
WAKATI Roberto Saldado akiendelea kuibeba Tottenham Hotspur kwa kuipa ushindi wa pili mfululizo katika Ligi Kuu ya England vijana wa Manuel Pellergrini, Manchester City jioni hii wameonja kipigo toka kwa Cardiff.
Man City wamejikuta wakizodolewa kwa kulazwa mabao 3-2 na waliopanda daraja Cardiff katika pambano lililojaa upinzani mkubwa.
Mabao mawili  ya lala salama yaliyofungwa kwa kichwa na Fraizer Campbell yalitosha kuwazima Man City waliokuwa ugenini na kuwapa wenyeji ushindi wa kwanza Cardiff.
City walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Edin Dzeko muda mchache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili baada ya dakika 45 za awali timu hizo kushindwa kutambiana.
Hata hivyo bao hilo lilirudishwa na Cardiff dakika ya 60 na Aaron Gunnarsson kabla ya Campbell kufunga mabao yake dakika za 79 na 87 na City kuambulia bao jingine dakika ya 90 lililofungwa na Alvaro Negredo.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyotangulia kuchezwa, Tottenham ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wageni wao Swansea City kwa bao la penati iliyofungwa na Saldado ambaye ni bao lake la pili baada ya wiki iliyopita kuifungia pia Spurs bao la penati iliposhinda ugenini.

Rage nouma! Asaka ITC za Warundi na kuzipata watashuka dimbani Jumatano kuikabili Oljoro

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

Kifaa kipya cha Simba Gilbert Kazze ambaye ITC yake imeshatua na ataanza kibarua Jumatano jijini Arusha

Tambwe Amissi nyota wa mabao anayetarajiwa kuanza kazi na JKT Oljoro
  TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 
MWENYEKITI wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, leo mchana amefanikisha upatikanaji wa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC), kwa wachezaji wawili wa klabu hiyo kutoka nchini Burundi -Amissi Tambwe na Gilbert Kaze. 
Wachezaji hao wawili ambao pia ni tegemeo la timu ya soka ya taifa ya Burundi (Intamba Murugamba), hawakucheza katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania iliyochezwa jana kutokana na kutokamlika kwa uhamisho huo, jambo lililoleta usumbufu mkubwa kwa benchi la ufundi, wachezaji wenyewe, uongozi na wapenzi na washabiki wa  klabu. 
Rage aliondoka jijini Dar es Salaam jana usiku na imechukua chini ya saa 24 kuweka kufanikisha suala hilo. Katika taarifa yake kwa wana Simba, Mbunge huyo wa Tabora Mjini alisema amelazimika kuingilia kati suala hilo kwa sababu lilihusu baadhi ya taratibu muhimu za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na ukweli kwamba viongozi wa Vitalo, klabu waliyotoka wachezaji hao hawakuwa mjni na hivyo kuchelewa kwao kungeigharimu Simba. 
"Kila walipokuwa wakipigiwa simu kwa takribani siku tatu mfululizo walikuwa wakisema kwamba wako milimani. Sasa hawa watu wa Burundi wakikwambia wako miliman wanamaanisha wameenda kijijini kwao. Kuongea kwa simu pekee kusingetosha na ndiyo Kamati ya Utendaji ya Simba iliomba niende mwenyewe Burundi ili suala hili liishe," alisema. 
Hii ni mara ya pili kwa Rage, ambaye ana uzoefu wa kuongoza soka kwa zaidi ya miongo mitatu, kuingilia kati suala la uhamisho wa wachezaji wa kimataifa. Miaka miwili iliyopita, Mwenyekiti huyo alilazimika pia kusafiri kwenda nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kushughulikia uhamisho wa mchezaji Gervais Kago ambao nao ulikuwa na matatizo. 
Kutokana na kupatikana kwa ITC hizo, Kaze na Tambwe sasa wataruhusiwa kucheza katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya JKT OIljoro ya Arusha iliyopangwa kufanyika Jumatano ijayo mjini Arusha. Klabu ya Simba tayari imewakatia wachezaji hao vibali vya kufanya kazi hapa nchini. 
Wachezaji wengine wa kigeni wa Simba, Joeph Owino na Abel Dhaira, walicheza katika mechi ya jana kutokana na kukamilisha taratibu zote za uhamisho na kuwa na vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
 
Imetolea na
 
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
SimbaSC

CHAMIJATA chatembeza bakuli kusaka Mil 40

Mwenyekiti wa CHAMIJATA, Mohammed Kazingumbe
CHAMA Cha Michezo ya Jadi Tanzania (CHAMIJATA) kimewaomba wadau wa michezo kujitokeza kukisaidia chama hicho shilingi milioni 40 ili kufanikisha mashindano ya Taifa ambayo yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 20 hadi 24 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CHAMIJATA Mohamed Kazingumbe wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Alisema mashindano hayo ambayo yatashirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ni moja ya utaratibu wa chama hicho kufanya michezo ya jadi kila mwaka kwa lengo la kukuza tamaduni za nchi.
Kazingumbe alisema katika mashindano hayo wanatarajia kuwa kutakuwa na michezo mbalimbali kama bao, kurusha mshale, mdako, mirela, kukuna nazi na mingine mingi ambayo itakuwa ikitambulisha michezo ya jadi nchini.
“Tunatarajia kufanya mashindo ya michezo ya jadi ya Taifa kuanzia Septemba 20 hadi 24 ila mpaka sasa changamoto kubwa ambayo inatukabili ni fedha hivyo tunaomba wadau wenye kupenda michezo hii wajitokeze kusaidia,” alisema.
Alisema hadi sasa ni mikoa michache imethibitisha kushiriki ambayo ni Pwani, Simiyu, Lindi, Morogoro, Dar es Salaam pamoja na baadhi ya taasisi za Serikali ila bado mikoa mingine inaendelea kuonyesha nia ya kushiriki.
Mwenyekiti huyo alisema mikoa ambayo bado haijathibitisha kushiriki inatakiwa kufanya hivyo hadi ifikapo Agosti 30 mwaka huu ambapo maandalizi mengine yatakuwa yanendelea.
Kazingumbe alisisitiza kwa vyama vya mikoa na wilaya kuhakikisha kuwa vinafanya mandalizi ya kutosha ili kuhakikisha kuwa ushindani unakuwa mkubwa na kuleta tija.
Aidha alivitaja vyama vya michezo ya jadi na mikoa kuhakikisha kuwa wanashirikiana ili kufanikisha mashindano hayo.

Yanga, Ashanti wavuna Milioni 102

Na Boniface Wambura
MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Ashanti United iliyochezwa jana (Agosti 24 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 102,856,000.

Watazamaji 17,744 walikata tiketi kushuhudia mecchi hiyo namba moja ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa mabingwa watetezi Yanga kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 24,400,102.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 15,689,898.31.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 12,406,831.75, tiketi sh. 4,453,890, gharama za mechi sh. 7,444,099.05, Kamati ya Ligi sh. 7,444,099.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 3,722,049.53 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,894,927.41.

Msondo Ngoma yatumbuiza kwa mara ya kwanza bila Gurumo

Baadhi ya wanamuziki wa Msondo Ngoma wakitumbuiza kwa mara ya kwanza baada ya mwanamziki mkongwe wa bendi hiyo Muhidini Gurumo kustaafu. Kutoka kushoto ni Shabani Lendi, Hamisi Mnyupe, Saidi Mabera, Juma Katundu na Shabani Dede.
Wanamuziki wa Msondo Ngoma kushoto ni Shabani Lendi,Hamisi Mnyupe,Saidi Mabera,Juma Katundu na Mustafa Pishuu wakitumbuiza bila gwiji, Muhidin Gurumo aliyetangaza kustaafu muziki.
Wanamuziki wa Msondo, Abdul Ridhiwani, Eddo Sanga, Athuman Kambi na Juma Katundu wakionyesha manjonjo yao katika onyesho lao la jana.
Wanamuziki Abdul Ridhiwani, Eddo Sanga, Athuman Kambi, Juma Katundu na Mustafa Pishuu wakitumbuiza.
Wasanii Hamisi Mnyupe kushoto na Romani Mng'ande wakiwajibika jukwaani

Golden Bush Veterani, Mwanza United Veterani ngoma droo


Golden Bush Veterani
 TIMU za Golden Bush Veterani na Mwanza United zimeshindwa kutambiana leo baada ya kutoshana nguvu na kutoka sare ya mabao 4-4 katika pambano kali la kusisimua lililochezwa kwenye uwanja wa Kinesi.
Mwanza United Veterani iliyosheheni wakali kama Henry Joseph, George Masatu, Aaron Nyanda, Albert Sengo, Bakari Malima na wengine walidhihirisha kuwa hawakuja Dar kushangaa 'maghorofa' kwa kuweza kuwabana wapinzani wao wanaosifika kwa kutoa vipigo kwa timu wanazocheza nao.
Katika mechi hiyo ya leo, wageni walipata mabao yao kupitia kwa Henry Joseph na Aaron Nyanda waliofunga mabao mawili kila mmoja, huku wenyeji wakipachika yao kupitia Shija Katina aliyefunga mawili, Rashid Ziada 'KR Mullah' na Abuu Ntiro waliotupia kila mmoja bao moja na kufanya hadi mwisho matokeo yawe mabao 4-4.
Uongozi wa Golden Bush umesema baada ya mechi hiyo wanajiandaa kwa pambano jingine kali siku ya Jumapili dhidi ya timu ya TASWA Fc.