Mwenyekiti wa CHAMIJATA, Mohammed Kazingumbe |
CHAMA Cha Michezo ya Jadi Tanzania (CHAMIJATA) kimewaomba
wadau wa michezo kujitokeza kukisaidia chama hicho shilingi milioni 40 ili
kufanikisha mashindano ya Taifa ambayo yanatarajiwa kufanyika jijini Dar es
Salaam kuanzia Septemba 20 hadi 24 mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa CHAMIJATA Mohamed Kazingumbe
wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Alisema mashindano hayo ambayo yatashirikisha mikoa yote ya
Tanzania Bara na Visiwani ni moja ya utaratibu wa chama hicho kufanya michezo
ya jadi kila mwaka kwa lengo la kukuza tamaduni za nchi.
Kazingumbe alisema katika mashindano hayo wanatarajia kuwa
kutakuwa na michezo mbalimbali kama bao, kurusha mshale, mdako, mirela, kukuna
nazi na mingine mingi ambayo itakuwa ikitambulisha michezo ya jadi nchini.
“Tunatarajia kufanya mashindo ya michezo ya jadi ya Taifa
kuanzia Septemba 20 hadi 24 ila mpaka sasa changamoto kubwa ambayo inatukabili
ni fedha hivyo tunaomba wadau wenye kupenda michezo hii wajitokeze kusaidia,”
alisema.
Alisema hadi sasa ni mikoa michache imethibitisha kushiriki
ambayo ni Pwani, Simiyu, Lindi, Morogoro, Dar es Salaam pamoja na baadhi ya
taasisi za Serikali ila bado mikoa mingine inaendelea kuonyesha nia ya
kushiriki.
Mwenyekiti huyo alisema mikoa ambayo bado haijathibitisha
kushiriki inatakiwa kufanya hivyo hadi ifikapo Agosti 30 mwaka huu ambapo
maandalizi mengine yatakuwa yanendelea.
Kazingumbe alisisitiza kwa vyama vya mikoa na wilaya
kuhakikisha kuwa vinafanya mandalizi ya kutosha ili kuhakikisha kuwa ushindani
unakuwa mkubwa na kuleta tija.
Aidha alivitaja vyama vya michezo ya jadi na mikoa
kuhakikisha kuwa wanashirikiana ili kufanikisha mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment