STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, August 12, 2014

Aisha Bui: Nilihatarisha maisha yangu kuwapa raha mashabiki wangu

NYOTA wa kike wa filamu nchini, Aisha Fat'hi 'Aisha Bui' amevunja ukimya na kuibuka na filamu mpya iitwayo 'Mshale wa Kifo' huku akiweka bayana kwamba alijitoa na kuhatarisha maisha yake kuiandaa filamu hiyo iliyotengenezwa porini.
Aisha alisema kuwa kutokana na maoni ya mashabiki wa filamu wanaolalamika kuwa filamu  nyingi za Bongo zimekuwa za mijini tu, huku baadhi ya matukio yakirudiwa kila katika sinema hizo hali hiyo ilimfanya abadilishe na kutoka kivingine.
Alisema hivyo aliamua kuhama mji na kwenda porini kuicheza filamu hiyo ambapo chupuchupu yeye na waigizaji wenzake kung'atwa na nyoka wakati wakiitengenza filamu hiyo.
“Nilijitoa na kuhatarisha maisha yangi kwa kuingia msituni ili tu kutengeneza filamu ambayo ikakata kiu ya mashabiki wasiovutiwa na filamu za 'sebuleni'. Ninajua nina deni kwa wapenzi wa kazi zangu, wanajua mimi ni bora hivyo lazima niwe bora kila mwaka,” alisema Aisha.
Filamu hiyo ya 'Mshale wa Kifo', imetengenezwa na kampuni ya Yuneda Entertainment ikiwashirikisha wakali kama Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’, Esha Buheti, Salim Ahmed ‘Gabo Zigamba’ na wasanii wengine.

Jennifer Mgendi akaribia kumtoa Mama Mkwe

MUIMBAJI nyota wa Nyimbo za Injili nchini ambaye pia ni muigizaji wa filamu, Jennifer Mgendi anatarajia kuiachia mtaani filamu yake mpya iitwayo 'Mama Mkwe' aliowashirikisha wakali wenzake wa muziki wa injili, Bahati Bukuku na Christina Matai.
Akizungumza na MICHARAZO Jennifer alisema filamu hiyo ipo njiani kuachiwa baada ya kukamilika kuhaririwa na kuwataka mashabiki wake wajiandae kuipokea.
Jennifer anayetamba na albamu ya 'Hongera Yesu', alisema filamu hiyo inayozungumzia mkasa wa mama mkwe anayelazimisha mwanae wa kiume kumzalia mjukuu ameigiza na wasanii kama Senga,Bi Esther, Christine Matai, Husna Chobis, yeye (Jennifer)  na wengine.
"Filamu yangu mpya ya 'Mama Mkwe' bado kidogo kabla ya kuachiwa mtaani ikiwa imechezwa na mimi mwenyewe, Bahati (Bukuku) Christine Matai, Senga, Bi Esther, Mussa Banzi na wakali wengine. Siyo ya kuikosa kwa jinsi ilivyo," alisema Jennifer.
Kabla ya filamu hiyo, Jennifer amewahi kutamba na filamu kadhaa kama 'Chai ya Moto', 'Joto la Roho', 'Teke la Mama', na 'Pigo la Faraja'.

Van Gaal awaonyesha Chicharito, Nani mlango wa kutokea Man United

Mlango u wazi kwenu kutimka Old Traffiord
SIKU chache kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya England na kufungwa kwa pazia la usajili katikia ligi hiyo, Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal amewaeleza wachezaji sita akiwamo beki wa kulia Rafael kwamba wanaweza kuchapa mwendo.
Marouane Fellaini, Wilfried Zaha, Nani, Shinji Kagawa na kinda yosso Will Keane pia wamevunja 'ndoa' na kikosi hicho cha Van Gaal na hilo limefanyika wakati United ikijifua katika Uwanja wa mazoezi wa  Carrington Jumamosi mchana.
Inaeleweka kuwa Mholanzi huyo amewaambia Fellaini, Zaha, Nani na Keane klabu hiyo itasikiliza ofa kwao baada ya kuwaweka sokoni rasmi.
Rafael, alishangaa kusikia jina lake likiwa katika orodha hiyo na kwamba pia anaweza kulazimisha kuondoka wakati huu klabu hiyo ikisaka beki wa kulia. Kagawa atatumika lakini kaelezwa ataanzia benchi nyuma ya Ander Herrera na Juan Mata.
Kiungo Anderson na mshambuliaji Javier Hernandez pia nao tayari wanajua kwamba United itasikiliza ofa endapo zitawasili mezani kwao. Southampton, Inter Milan, Tottenham, Atletico Madrid na Juventus zote zimeonyesha nia ya kumsajili Mmexico huyo, wakati Napoli itakuwa tayari kumsajili Fellaini kama dili hilo litakubalika na United.
Newcastle inaongoza katika vita ya kumsajili Zaha, huku Crystal Palace, West Ham na Nottingham Forest nazo zikihitaji huduma yake.
Cardiff City imeulizia uwezekano wa kumsajili kwa mkopo Keane ambaye ni pacha wa beki Michael, lakini United inahitaji kumtazama zaidi kabla ya kukamilisha dili hilo.
Kwa sasa United ipo sokoni ikisaka mabeki wapya wawili baada ya kushindwa kumsajili beki wa kati wa Arsenal, Thomas Vermaelen ambaye juzi alijiunga rasmi na Barcelona
Mabingwa hao wa zamani wamejipanga kufanya vyema katika msimu huu baada ya msimu uliopita kuboronga na kumaliza kwenye nafasi ya katikati tofauti na mazoea yao.